Mwanasheria Mkuu: Ruksa Takukuru kuwahoji wabunge | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mwanasheria Mkuu: Ruksa Takukuru kuwahoji wabunge

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by MziziMkavu, Jul 13, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jul 13, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,615
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema.  Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, amevitaka vyombo vya dola kuwahoji wabunge wanaotoa misaada na zawadi kwa watu binafsi, lengo likiwa ni kuwashawishi wawapigie kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
  Jaji Werema alitoa kauli hiyo baada ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kumtaka kulitolea ufafanuzi suala la wabunge kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wanapokuwa wanakamilisha ahadi zao kwa wapigakura wao majimboni.
  “Nimepata malalamiko kadhaa kutoka kwa wabunge na kwa leo nimepokea mawili kuwa wakati wanapokuwa wakitekeleza ahadi zao majimboni mwao, wanavamiwa na Takukuru… Ni vyema Mwanasheria Mkuu baada ya utambulisho ukalitolea ufafanuzi hili,” alisema Spika Sitta.
  Akilitolea ufafanuzi jambo hilo, Jaji Werema pia aliwataka wabunge kujibu maswali wanapohojiwa na maofisa wa Takukuru baada ya kuwatilia shaka kuhusiana na misaada wanayotoa.
  Jaji Werema alisema kuwa afadhali angekuwa analishughulikia jambo hilo peke yake, lakini kuna vyombo vingine vinashughulikia mambo hayo.
  Alisema: “Katika sheria hii (Sheria ya Gharama za Uchaguzi), hata mimi ninayo mamlaka ya kukushughulikia,” alisema.
  Alisema wabunge wana wajibu wa kufuata sheria na kuepuka dhuluma, vitisho, ubabe, rushwa, uonevu na upendeleo na kufuata misingi ya demokrasia.
  Alisema Katiba inasema mbunge anakoma ubunge pale Bunge litakapovunjwa na kwamba Katiba ya nchi ndiyo inayojibu malalamiko hayo ya wabunge.
  Jaji Werema alisema wabunge wana haki ya kusukuma maendeleo ya majimbo yao kwa kutekeleza ahadi zao ambazo walishindwa kuzitimiza katika kipindi cha nyuma.
  Hata hivyo, aliwataka wabunge hao kusoma Sheria ya Gharama za Uchaguzi hasa ibara 21 kifungu cha 1(a), ili kuyafahamu mambo ambayo yamezuiwa na sheria hiyo wakati wa mchakato wa uchaguzi.
  Alisema kesi za wabunge kugawa vyerehani au vitu vingine zinatofautiana ambapo wengine wamekuwa wanakwenda kinyume cha kifungu hicho cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
  Akizungumza baada ya Jaji Werema kumaliza kujibu swali hilo, Spika Sitta, alisema Bunge linatarajiwa kuvunjwa rasmi Agosti Mosi, mwaka huu.
  “Kama umechelewa kutimiza adhadi zako umebaki mwezi huu tu,” alisema na kuikumbusha Serikali kuwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDEF), zilitoka mwezi uliopita na nyingine mwezi huu.
  Aliwashauri wabunge mambo watakayoyafanya kutokana na fedha za CDEF na mengine, kuzingatia suala la uwazi.
  “Wewe unafikisha cherehani usiku na Pick Up yako hakuna wananchi hata risala... Mbunge makini atahakikisha kuwa kunakuwepo na wananchi, risala na viongozi mbalimbali wanakuwepo wakati anakamilisha ahadi yake,” alisema.
  Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), John Komba, alihoji kama ni kosa kisheria wananchi kuwapokea wabunge wao wanaporudi kutoka bungeni kama ishara ya shukurani kuwa wamemaliza kazi waliyomtuma vizuri.
  Akijibu swali hilo, Jaji Werema alisema si kosa kwa wananchi kuwapokea wabunge wao wanaporudi majimbonni kwa sababu ubunge hautakoma Julai 17 mwaka huu.
  Alisema serikali itatangaza katika Gazeti la Serikali kuhusu kuvunjwa rasmi kwa Bunge.
  Hivi karibuni, kumekuwa na taarifa mbalimbali za wabunge wanaomaliza muda wao kuhojiwa na maofisa wa Takururu baada ya kugawa misaada na zawadi mbalimbali kwa wapigakura wao.
  Wakati huo huo, Spika Sitta, amewataka wabunge kuhakikisha wanakuwepo bungeni Ijumaa wiki hii wakati Rais Jakaya Kikwete atakapokwenda kuwaaga rasmi.
  Alisema Rais Kikwete atakutana na wabunge hao Ijumaa saa 10:00 jioni na kuongeza kuwa: “Hakutakuwa na shughuli nyingine, ila muwepo tu, Rais atakuja kuwaaga.”
  Aidha, aliwataka kuwepo hadi siku hiyo kwa kuwa fedha za mafao walizopewa awali sio za mwisho na kwamba Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, amewaambia kuwa kuna fedha nyingine.  CHANZO: NIPASHE
   
 2. Kaa la Moto

  Kaa la Moto JF-Expert Member

  #2
  Jul 14, 2010
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 7,666
  Likes Received: 166
  Trophy Points: 160
  Hivi hizi sheria zipo hapa JF? Nahitaji kuzijua kuna mtu anaweza kuniwekea hapa?
   
Loading...