Habari hii hapa
MwanaHALISI lashinda kesi
na Mwandishi wetu
KESI ya kukashifu, iliyokuwa ikilikabili
gazeti la MwanaHALISI, imetupiliwa
mbali na mdai ametakiwa kulipa
gharama zote za kesi. Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya
Kisutu jijini Dar es Salaam, Warialwande
Lema, katika hukumu yake Jumatano,
alisema ili maneno yawe, au yaonekane
kuwa ya kashfa, sharti yawe ama si ya
kweli au yawe ya uongo. Alisema kwa mujibu wa ushahidi
uliotolewa mahakama haikuona chochote
kile kilichothibitisha madai ya kashfa. Juma Jaffari Nyaigesha, Mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa wa Msewe, jijini Dar es
Salaam ndiye alilishtaki gazeti akidai
kuwa kwa habari na makala
zilizochapishwa katika matoleo yake
matano, alikashifiwa na kuvunjiwa heshima mbele ya jamii. Mdai alimshtaki mhariri wa gazeti, Jabir
Idrisa, mshauri wa gazeti, Ndimara
Tegambwage, Stella Kajuna mkazi wa
Msewe, mhariri mkuu, kampuni
inayochapisha gazeti, Hali Halisi
Publishers Limited, kampuni ya uchapaji ya Printech na kampuni nyingine ya
uchapaji, Tanzania Standard Printers
Limited. Nyaigesha alidai kuwa matoleo matano
ya MwanaHALISI yalikuwa na taarifa
zilizomkashifu na kumwondolea hadhi
mbele ya jamii. Aliyataja matoleo hayo kuwa yale ya 10,
12, 24, 31 Oktoba 2007 na 14 Oktoba
2008. Katika matoleo hayo kulikuwa na habari
na makala juu ya madai ya kuwepo
vitendo vya uhalifu Msewe, ukosefu wa
amani na matumizi mabaya ya madaraka
ambavyo Nyaigesha alidai vilikuwa
vinaelekezwa kwake. Katika hukumu yake, hakimu Lema
alisema kwanza mdai hakuleta hata
shahidi mmoja kuthibitisha madai yake
na kwamba yeye mwenyewe hakuweza
kuthibitisha kuwa amekashifiwa. Hata takwimu za kura za uchaguzi
alizopeleka mahakamani, zilionyesha
kuwa hata baada ya kuandika yaliyokuwa
yakitokea Msewe, katika uchaguzi
uliofuata alipata kura nyingi, jambo
ambalo lilikinzana na madai ya kukashfiwa. Hakimu alisema Jaffari ni kiongozi na
kile walichofanya waandishi kilikuwa ni
mjalizo halali na wa haki juu ya kiongozi
na uongozi wa umma na siyo kashfa. Alisema ameridhika na ushahidi
uliotolewa na walalamikiwa, ushahidi wa
maandishi kutoka kwenye kata na hata
kauli ya mdai kuwa mmoja wa
walalamikiwa alipigwa na kwamba yote
hayo yalidhihirisha umuhimu wa kilichoandikwa. MwanaHALISI ilikuwa ikitetewa na wakili
maarufu, Mabere Marando, wakati
Tanzania Standard Printers Ltd,
iliwakilishwa na wakili Audax
Kahendaguza Vedasto wote wa Dar es
Salaam. Kuhusu wachapaji wa gazeti, hakimu
alisema hawakuwa na hatia kwa kuwa
hawakutenda kashfa yoyote, kwa vile
hakuna kashfa iliyothibitishwa. Aidha hakimu alikubaliana na hoja
kwamba mchapaji anayefanya kazi
aliyopewa na kuirejesha kwa mhusika,
hawezi kuwa ametenda kashfa. Alipoulizwa Mkurugenzi Mtendaji wa
HaliHalisi Publishers, Saeed Kubenea, juu
ya hatua anayojiandaa kuchukua, alisema
hajakaa na wakili wake kupanga hatua
inayofuata.