Mwaka Mpya Na Miungu Ya Kisiasa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mwaka Mpya Na Miungu Ya Kisiasa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by X-PASTER, Jan 1, 2012.

 1. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #1
  Jan 1, 2012
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Mwaka Mpya Na Miungu Ya Kisiasa

  Watu wengi wana tabia ya kusheherekea siku ya kuingia mwaka mpya, wengi upatwa na furaha na kuingiwa na kiwewe cha kuiona siku na mwaka mpya, kwa kujiona kuwa wamefaulu kuuona mwaka mwingine. Lakini wanasahau kuwa miaka inakwenda, na umri ndio unapungua.

  Binadamu anapopitisha miaka yake hana maana kuwa ana furaha bali ahesabu kuwa siku zake zinazidi kupungua na kukaribia kuingia kaburini, kwa hiyo iwe ni masikitiko na sio furaha khaswa kwa yule ambaye hakujishughulisha kufanya mambo mazuri kwa jamii yake!

  Miaka itakuwa ni ya kufaulu pindi ikiwa siku zimetumika kwa mambo mazuri na yalio leta faida kwa jamii yake na yake binafsi bila ya kuwaathiri wengine kiufisadi na itakuwa ni ya huzuni ikiwa miaka hiyo itatumika kwa ufisadi au kuachia ufisadii ukitendeka bila ya yeye kuchukuwa hatua za kudhibiti ufisadi huo.

  Watu wengi upendelea kuweka maazimio (resolution) yaani kuweka lengo au malengo atakayoyafanya katika mwaka huo mpya, nayo yote ni mambo mazuri, lakini Mtu makini hawezi kufanya hayo ya kuweka lengo lake au malengo yake kila mwaka tu, bali uweka malengo kila siku, na juu ya hivyo sio lengo au malengo ya kipuuzi bali ni malengo ya kujirekebisha kuwa bora kuliko siku iliyopita.

  Siku zinatupita, masaa yanatupita na hali za watu wengi hazibadiliki kuwa bora kwa sababu wengi wetu tumejiweka mbali na harakati za kujikomboa.

  Wengi wetu tumekalia siasa za maji taka, kuchafuana, udini, ukanda na uchama ndio tumeweka mbele, lakini tunasahau kuwa wenye maisha bora ni hao wanasiasa ambao kila kukicha tunawatetea na kuwakumbati na kuwaona ndio mitume na miungu watu!

  Mfano mdogo tu, hivi ni wangapi ambao wamepinga posho za wabunge zilizo ongezwa hivi karibuni? Kwanini zisiongezwe posho za Walimu, madaktari, manesi na wafanyakazi wa kima cha chini?

  Kwanini Wabunge na si raiya wa kawaida... Kwanini hizo posho zisitumike kununulia vifaa vya mahospitalini, kama hazitoshi kwanini zisinunue madawati kwenye mashule au kwanini wasipewe wale wagonjwa wasio weza kujilipia matibabu na madawa wanayo andikiwa uko mahospitalini, kwa nini wao tu?

  Ni wagonjwa wangapi wanakosa dawa uko mahospitalini na hali hao viongozi wa kisiasa wakiumwa mafua wanapanda zao ndege na kuelekea Ughaibuni kutibiwa na wakirudi hapa wanasifia mahospitali ya wenzetu, na hali wanaona za kwao hazina hadhi na hata hawashtuki. Na sisi raiya wa kawaida hata hatuhoji wala kushtuka kuwa hayo wanayo yafanya viongozi wa kisiasa ni dhurma kwa raiya. Ni sawa na baba mwenye kuacha familia yake ikifa kwa njaa na yeye anakwenda kula hotelini, na akirudi familia nzima inamshangilia kuwa baba karudi na ameshiba vema. Hakika familia ya namna hii itakuwa na ugojwa wa akili si bure.

  Labda niseme tabia moja, tabia ambayo Watanzania wengi kama si nchi nyingi zinazoitwa dunia ya tatu tumeikumbatia, kiasi ya kututia upofu wa akili. Tanzania ni nchi ambayo waasisi wake wameibatiza kuwa ni nchi yenye kufuata misingi ya kijamaa, wengi tunaelewa kuwa nchi nyingi zinazofuata siasa za ujamaa zilikuwa ni nchi zilizotawaliwa na mfumo wa chama kimoja. Na kwa kuwafumba wananchi macho, tuliambiwa kuwa tuna demokrasia ya chama kimoja. Ndani ya mfumo huu chama tawala kiliinuliwa juu na kuchukua nafasi ya Mungu wa taifa.

  Ili kuhami nafasi hiyo, hapo ndipo zilipobuniwa semi au slogan za kudai chama na serikali havina dini. Wenye dini wako huru na dini zao, wenye taaluma wabakie na taaluma zao, wanawake wabakie jikoni, wanafunzi wabakie darasani, wafanyibiashara wabakie madukani mwao, wafanya kazi wawe huru na kazi zao na wakulima nao wabakie mashambani mwao, vijana ni taifa la kesho kwa hiyo wasijihusishe na siasa.

  Siasa ikabakia kuwa eneo nyeti na haki ya kundi dogo lililojifanya kama ndio wateule katika nchi na kwa sababu ya uteule wao basi hawapaswi kuchukuliwa hatua za kisheria wanapokuwa wametenda makosa ya jinai.

  Kwa kitambo watawala waliufaidi uhuru huo kwa sababu ulikuwa ni uhuru wa kufanya maovu pasipo kupingwa, huku wakiwa wamewaengua na kuwatenga kabisa wananchi wengine wasishiriki kwenye maamuzi muhimu ya kisiasa. Kwa kifupi ukawako utawala wa wachache, lakini utawala wao ukawa hauna mipaka na kwa hiyo wakawa na uhuru wa kuharibu kama wapendavyo pasipo kizuizi chochote. Na kama ilitokea mwanasiasa mmoja kwenda kinyume na wenzake, basi walimuondoa haraka sana, na kumpachika majina mabaya mabaya.

  Utawala wa hao wachache ulienda sambamba na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu. Sheria mbaya kama za kumweka mtu kizuizini pasipo hata kumfikisha mahakamani zikatungwa kwa makusudi ya kupambana na wale watakao thubutu kuleta upinzani.

  Watawala walikosa imani na mahakama kwamba zinaweza kutoa haki wanayoitaka wao ndiyo maana walikimbilia vizuizi kama kwamba hiyo ndiyo dawa pekee ya kuleta umoja wa kitaifa.

  Katika maeneo mengine ya maisha zaidi ya eneo la siasa pia kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa haki za watu kwa mfano katika eneo la uchumi serikali ndiyo iliyopanga bei za mazao ya wakulima, ndiyo iliyopanga viwango vya mishahara, na pia ndiyo iliyopanga viwango vya bei za vitu pasipo kujali uzalishaji wala nguvu za soko. Sheria nyingi za ukandamizaji zilipitishwa na Bunge la chama kimoja, huku viongozi wa chama na serikali wakijigeuza miungu.

  Wananchi katika ujumla wao walishirikishwa kwenye siasa kama wateja tu wa kununua hicho ambacho wanasiasa wamekitengeneza katika mipango yao kila walichokipika.

  Watu walishirikishwa kwenye maandamano ya kuunga mkono maamuzi ya serikali au chama, lakini wale wachache wenye kuelewa mara walipothubutu kufanya maandamano yao kudai hiki au kile, ama maandamano ya kuelezea hisia zao, ilidaiwa ni maandamano haramu na waandamanaji walipata vipigo vya mbwa mwizi.

  Hali hii inaendelea mpaka leo, hakuna hata mwanasiasa au mbunge mmoja ambaye amethubutu, kuwauliza wananchi wake walio mchagua ni nini wanataka akipeleke bungeni. Na hao wanaojaribu kuhoji vyama vyao, wamebandikwa lebo ya waasi au wenye kutaka kuleta machafuko kwenye vyama husika.

  Watu wanashirikishwa kufanya neno lile ambalo chama kinataka lifanyike, lakini yanayohusu uendeshaji imekuwa ni mwiko. Siasa imebakia eneo maalum kwa ajili ya watu maalum. Kwa namna inayofanana na mchezo wa kuigiza, eneo la siasa linafanywa kama eneo takatifu na wote walioko ndani yake wanahesabiwa kama ni watakatifu, na ndio sasa hatuoni wapenzi wa vyama vya kisiasa wakiwahoji viongozi wao kwa kila jambo linalopita kwenye vyama vyao au uko bungeni. Na ndio miaka nenda rudi, ni wale wale tu, yaani hakuna kustaafu.

  Tanzania kuna pengo kubwa sana kati ya wanasiasa na wananchi, yaani vyama vimetekwa na wanasiasa wachache, miaka nenda rudi. Vyama vyote vinatenda mambo yake kama vyama vya kidola au vyama vya kiserikali vya enzi ya ujamaa (Ukomunisti). Kauli zote za vyama vikiwemo vyama vyote vya siasa vikiongozwa na chama tawala, ni vyama vyenye kutoa kauli za kibabe dhidi ya wananchama wake wa kawaida, na kauli hizo wala siyo kauli za wananchi. Kwa ufupi wananchi wamefumbwa vinywa na wanalazimika kuishi kwenye kibano na kabali ya vyama vyao au dola.

  Sambamba na hilo wasomi na wanataaluma nao wanakandamizwa kwa kulazimishwa kuwa chini ya uongozi na utawala wa mambumbumbu wa wanasiasa, ili tu kuhakikisha taaluma zao hazi-operate kwa uhuru.

  Kutokana na hali hiyo ya viongozi kujifanya miungu na kuchukua nafasi ya Mungu wa taifa ambao ni raiya wa kawaida, basi inatakiwa ili Mungu wa kweli aweze kuchukua nafasi yake, inapaswa, na kwa hakika ilibidi mifumo ya aina hii ianguke, isambaratike, na kutokomea kabisa. Lakini wanasiasa wanajuwa kucheza mchezo wao, wamekuja na slogan ya neno mageuzi.

  Yaani wametubana kweli kweli, tena kila kona, hata uko kwenye mageuzi tunakotaka kwenda tutakuwa nao tu. Wengi tunaamimini kwamba kauli ya wengi ni kauli ya Mungu, neno ili laweza kuwa na ukweli ndani yake au ikawa si kweli, inategemea na tafasiri ya mtumiaji. Lakini kwa wale wenye kuiamini hiyo kauli ukiangalia kwa undani yaani kwa jicho la rohoni utaona ya kwamba mageuzi ya kusambaratisha mifumo dhalimu hayakutoka kwa shetani bali yametoka kwa Mungu, kwani shetani hawezi kupigana na mifumo yake mwenyewe.

  Uko mashariki ya kati tunashuhudia wananchi wakiingia mitaani kudai haki zao za msingi, na yote hayo ni kwa sababu za wanasiasa uchwala ndio walioshika vyama tunavyo vishabikia.

  Bwana Yesu katika kuuelezea utawala wa Mungu, aliufananisha na upepo kisha akasema upepo huvuma kwenda kule utakako wala hatuwezi kuuzuia lakini sauti yake twaisikia.

  Katika tafsiri halisi upepo au kimbunga kilichoiitikisa mifumo ya mataifa mbali mbali ya dunia ndani yake kuna nguvu ya Mungu, ndiyo maana watawala pamoja na ujanja wao, ubabe wao, na nguvu zao za kidola hawakuweza kuzuia wala kuzima wimbi la mageuzi.

  Sehemu nyingine ya mafundisho yake, Bwana Yesu alisema yule mtu mwenye kulishika neno langu atafanana na mjenzi mwenye busara ambaye alijenga nyumba yake juu ya mwamba, hata upepo wenye nguvu ukaja ukaipiga nyumba ile lakini isitikisike, kwa sababu ilijengwa juu ya msingi imara, bali mwenye kuyapuuza maneno haya ni sawa na mjenzi mpumbavu ambaye alijenga nyumba yake juu ya mchanga, upepo wenye nguvu ulipokuja ukaipiga nyumba ile nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.

  Ingawaje watawala wanajitahidi sana kuficha, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba taifa letu halikujengwa juu ya mwamba imara ambao ni katiba iliyokubaliwa na wananchi wote badala yake nchi imejengwa juu ya maneno ya wanasiasa wachache, ambao wameingiza maneno ya kipuuzi, maneno yasiyokuwa na ukweli wala umakini wowote na baya zaidi nchi imejengwa katika misingi ya ushirikina na imani isiyoeleweka kama ni imani ya Mungu au imani ya shetani. Ndiyo maana nasema wote wenye kumcha Mungu (Waislam, Wakristo, Wenye dini za jadi) tusiukubali tena upumbavu wa kusema tusichanganye dini na siasa kwani huo ni uwongo, hawa wanasiasa wamekuwa kama mashetani ambayo kila kukicha wanatutenganisha na ukweli halisi wa maisha yetu.

  Mimi binafsi naami kwa kutumia imani zetu, tunaweza kuwachaguwa wanasiasa wa kweli wenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na si wenye kuogopa thamani ya vyeo vyao.

  Kuogopa uku thamani ya vyeo vyao, ndio kunawapelekea kuwa waongo, mafisadi na kupapia mali kwa sababu wanachuma ili kujiwekea ngome ambazo zitawalinda kesho na kesho kutwa. Na hata pale wananchi tukija kushtuka usingizini tutakuwa tumekwisha chelewa na wao wamesha jijengea himaya yenye nguvu kubwa kiasi ya kutoweza tena kutetereka.

  Enzi za ujamaa tulielezwa kwamba ujamaa ni imani hauna budi kujengwa na watu wanaoamini na kufuata kanuni zake. Imani iliyo elezwa katika ujamaa ule haikuelezwa wazi nini tofauti yake na imani za dini, wala haikuelezwa kwamba mhusika ama huyo mwananchi auamini ujamaa kwa kutumia nini. Je kwa kutumia akili yake, au mwili wake ili asije akachanganya imani ya ujamaa, na imani ya dini yake kama ni Uislamu, Ukristo, Uhindu au dini za jadi!

  Wanasiasa kwa vinywa vyao wanahubiri dini isichanganywe na siasa yao lakini katika uhalisi wa mambo na kwa matendo yao wao wanachanganya siasa yao na dini yao ya ufisadi.

  Kisha kwa ujanja wanasema siasa zetu si sawa na siasa za mataifa mengine, wametutengenezea mkorogo wa kuchanganya imani ya kisiasa na imani ya kidini kidogo, kutokana na ukweli kwamba mtu asingeweza kuigawa imani yake iliyoko rohoni mwake kwenye matabaka mawili yaani awe na imani kwa ajili ya siasa, na imani nyingine kwa ajili ya dini.

  Wengi tumewaona wakitumia vifungu kutoka vitabu vya dini, pale tu wanapo ona maslahi yao yapo hatarini, na kukemea udini pale viongozi wa dini wanapowakemea na kuwataka kuwa wasichanganye dini na siasa.

  Watanzania tumeishi katika udanganyifu huu kwa miaka mingi huku wanasiasa waongo wakitaka tuyaamini maneno yao kama vile tunavyoliamini neno la Mungu, mbaya zaidi wakaufanya uwongo wao (ambacho ni kitu cha binafsi) uwe ni sehemu ya siasa hadi watu wengine wakafikia kusema siasa ni uwongo.

  Hadi leo hii wengi wanaamini hivyo kwamba siasa ni uwongo na ndiyo maana hawataki siasa ichanganywe na dini lakini hiyo ni imani na misimamo yao potofu kwani siasa kama ulivyo uchumi, biashara, na sayansi nyingine yoyote ile inataka ukweli na uaminifu, kitu ambacho wanasiasa wetu hawana. Kwa sababu hawafuati kile kinachokatazwa na dini zao, zikiwa za kiislamu, kikristo au hata dini za jadi.

  Kwa sababu dini zote hizo zinakataza wizi, ufisadi na uongo, na zinaimiza tutendeane mema na kupendana. Sasa kwa wanasiasa kwa kutumia mbinu zao wameweza kutushawishi kiasi ya kwamba tukiwabada kwa mujibu wa dini zao, wanatubana kwa kutuambia kuwa tusichanganye dini na siasa.

  Basi mwaka huu wa 2012 uwe mwaka wa maazimio ya mabadiliko ya kila Mtanzania, maana tukiwaachia wanasiasa, na kuendekeza ushabiki usio na maana, hatutakuja ona mabadiriko hata baada ya miaka 100 ijayo.

  Mafunzo ya dini yanasema, ukiona jambo baya liondowe kwa mkono wako, kama huwezi basi lisemee watu wasikie kama hili baya, Jambo la mwisho kama hayo yote uwezi basi angalau lichukie kwenye moyo wako na hili la kuchukia ni katika Imani dhaifu sana isiyotakiwa na Mungu.

  Na kuna kauli moja inasema hivi, dalili za mtu mnafiki ni tatu, anaposema anaongopa, anapotoa ahadi hatimizi/anaivunja, anapoaminiwa na amana hufanya khiyana. Na dalili zote hizo zipo kwa wanasiasa wetu. Je tunashindwa kuondoa ufisadi na ukiritimba kwenye vyama vyetu kwa mikono yetu, na kubakia kuchukia tu!?


  Haya basi tusichnganye dini na siasa... ah ah ah ah ama wametupata kweli kweli.
   
 2. M

  Mkandara Verified User

  #2
  Jan 1, 2012
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  X - Pastor,

  Makala yako nzuri sana na nashukuru umegusia sehemu nyingi sana zenye umuhimu wa kutambua UTU wa binadamu unatokana na yepi?..
  Kitu kimoja tu ambacho binafsi nakitazama tofauti ni pale unaposisitiza DINI na SIASA kuingiliana kwa sababu ya mapungufu ama makosa yanapoingia... Mkuu haramu ni haramu haina siasa wala dini maana ukitazama miiko na maadili ya viongozi na wananchi ktk siasa zimetokana na mtazamo mkubwa wa imani za dini zetu iwe Waislaam, Wakristu au Wahindu. Hivyo unapomsikia Padre ama Sheikh akilaani kitu sii kwamba hakilaaniwi kisiasa pia, bali yule unayemkosoa ndiye kakiuka miiko na maadili kama unavyomlaani shetani kwa mtu alofanya kufur ktk imani za dini..

  Kwa hiyo siasa zinaweza kabisa kusimama peke yake bila Dini kwa sababu siasa zinatakiwa kusimamia yale mazuri ya UTU wa binadamu na kwa imani tofauti, yaani pale tunapokutana sote na kuunda UMOJA wetu bila kujali imani za dini maana msingi wa maisha yetu tayari umeisha jengwa na imani hizi..Muislaam bora au Mkristu mbora hawezi kufanya siasa haramu hata kidogo ukiona mtu anafanya hivyo basi hata imani yake ya dini tayari imekwisha haribika, hivyo huyu mchungaji au Sheikh anatakiwa kuzungumza na mtu huyu anapokuja kanisani/ msikitini kusali..

  Kwa nini hawa Mapadre na Masheikh wetu wanashindwa kuzungumza na viongozi hao hao wanapokuja makanisani au misikitini na kuwaambia mabaya wanayofanya kinyume cha imani zao za dini?.. Kwa nini wachukue jukwaa la siasa kuwa ndio uwanja wa mafundisho yao ili hali hawa watu hukutana kila siku au kila wiki sehemu za ibada?.. Kama una ujumbe wa kiimani unashindwa vipi kuusema kwa mhusika isipokuwa ktk magazeti kama sii kutafuta umaarufu ama kuutangazia Umma nguvu yako kwa jamii?..Ofisi yako iko kanisani au msikitini mbona huitumii unapomwona kiongozi akija sali..

  Tena hawa hawa viongozi wa dini ndio wapo ktk payroll ya hawa viongozi na kila wanapoona cheque haikufika wakati muafaka ndio huanza haya malumbano wakati misaaada ya mafisadi wanaipokea tena kwa furaha kubwa wakipiga na mapicha yaonekane magazetini, jamani dini sii imetufundisha unapotoa sadaka basi jaribu hata jirani yako asiuone mkono unaotoa iweje kanisa.msikitii wapokee sadaka za watu kwa shamrashara hali wakijua mtu huyu huyu ni kati ya waumini mafisadi wanatakiwa kulaaniwa..

  Mwisho, swala la Ujamaa.. Ujamaa haukuwa na ubaya wowote zaidi ya imani kama ilivyosema Kisiasa. Ni iliyataka mazuri yote ya UTU wa binadamu kama dini zinavyotutakia ktk ibada za kijamii kupendana na kutomtendea mtu yale usiopenda wewe utendewe. Na maadam ni imani leo hii wewe kama ni Muislaam au Mkristu huwezi kuona ubaya ikiwa mafundisho ya dini yako ndiyo pekee yanatumika kuwashawishi watu wafanye mema. Hili nina hakika nalo kabisa isipokuwa hatuwezi kufikiria hivyo kwa sababu sisi wote tuna dini tofauti lakini haiondowi imani na ki**** kwamba dini yako ndiyo yenye msingi bora wa maisa ya mwanadamu kuliko dini nyinginezo...

  Hivyo Nyerere kucuhua Ujamaa haiwezi kuwa haramu au mbaya kwa sababu hakuna binadamu ajuaye kwa uhakika kwamba Ujamaa ni mbaya kuliko Ubepari au kinyume lakini pia huwezi kuchukua yote ndivyo tulivyo fundishwa ktk imani za siasa. Aidha uwe Mjamaa au Bepari chagua moja... Kama vile huwezi kuwa Muiaslaam na Mkristu kwa wakati mmoja. Utengano baina ya siasa na dini ninkwamba DINI inamhesabu kila mtu mmoja mmoja kwa imani yake wakati Siasa ni za Taifa zima lichague... Hivyo Uhuru ulukuwa nao kuchagua dini moja ndio unakufunga wewe ktk kufuata mafundisho ya dini hiyo tu na huoni haramu zake sawa sawa na Siasa zinavyolifunga Taifa ktk imani moja pasipo kuona Uharamu wake..

  Sasa labda wewe nambie, toka tumeingia Ubepari kwa nini Mjamaa huonekana hana nafasi?.. iweje tulipokuwa wajamaa tuliyaona mabaya ya Ujamaa na haramu zake lakini leo ukizungumzia Ubepari na haramu zake ni makosa na wewe unaonekana huna mchawi?..Inakuwaje Ubebari unatumia nguvu ya wanyonge kuwatajirisha baadhi ya watu...

  Leo hii tunasema tunahitaji wawekezaji nchini kutoka nje kwa sababu hatuna uwezo, kwani tulipopata Uhuru hatukujua kwamba hatuna Uwezo na nini sababu ya kudai Uhuru ikiwa huna uwezo maana wakoloni walitutawala kwa misingi ya kwamba hatuna uwezo na wao wakatuletea maendeleo. Je Uhuru ulikuwa ni swala la kumwondoa Mkoloni IKulu na kumweka mtu mweusi japokuwa uwezo tulikuwa hatuna?.Hivi kweli hii ndio ilikuwa ahadi ya Uhuru?..

  Mwaka 2012 naukaribisha kwa hofu kubwa ya kupotea Tolerance, fikra za kubomoa msingi uliojengwa na waasisi wa Uhuru wetu kwa fikra mpya za Kibepari ambazo zinatawaliwa na UMIMI, utengeno, na kila mtu atabeba mzigo wake na kwa bahati mbaya sisi ni nchi maskini sana duniani...Na ipo mifano mizuri sana ya wapi tunakwenda.. Msingi mpya tunaoujenga unatupeleka wapi na mwisho wa siku tutafika huko tusijue imekuwaje..

  Mfano mzuri sana ni nchi mbili Tajiri sana nza Kiafrika..Sudan na Nigeria hizi nchi zimetawaliwa Kisasa lakini dini ime play big role ktk siasa zake na wamekuwa Mabepari kabla hata ya Uhuru wao na inafurahisha sana kuona tofauti zilizopo nchi hizo ndizo zina ukaribu sana na mazingira yetu..nitakwambia kwa nini:-

  NIGERIA
  Hii ni nchi ambayo ni tajiri mkubwa wa mafuta pengine nchi ya tano duniani leo hii imegawanyika kutokana na dini na sababu kubwa ni ugawaji wa Utajri. North ambako wako Waislaam na yanakopatikana mafuta na utajiri wa nchi hiyo asilimia 70 ya wananchi wake ni maskini. South ambako kuna wakristu wengi na hakuna utajiri wana asilimia chini ya 30 ya maskini...Ina maana Utajiri wa nchi hiyo hauwafikii walengwa na wala kuwajali watu wa North na bahati mbaya maadam dini zimechanganywa na Siasa badala ya watu wa North kuitazama serikali hasira zao zinakwenda kwa Wakristu, kumbe utawala mzima wa nchi hiyo unawapa nafasi zaidi watu wa South bila kujali dini zao..Leo hii nchi bado maskini na wameanza kulana wenyewe kama wanyama...vita imeingia hadi sehemu za ibada.

  SUDAN:-
  Hawa nao ni matajiri wakubwa sana kwa rasilimali ile ile ya mafuta. Mafuta yako South kwa Wakristu lakini asilimia 80 ya masikini wako South hali North ambako hakuna mafuta asilimia chini ya 30 ndio maskini... Wamepitia mitihani kama ya Nigeria kwa miaka mingi sana mwisho siku ya siku imefika wamefikia kugawana na kuunda nchi mbili ili South (wakristu) wapate kunufaika na Utajiri waliojaliwa wakisdhulumiwa na North (waislaam).

  Sasa baada ya kuwekeana mipaka, hawa maskini wa south walokuwa asilimia 70 leo ni 100% swala lao wanataka kutajirika sasa nani kwanza?...Hivyo Udini umekwisha baina yao na Waislaam, sasa umeingia mdudu mwingine aitwaye Ukabila. Vita imefumuka baina ya wao kwa wao kugombania Utajiri uliopo na makundi yameanza kujitekeza baina yao kwa makabila na kila mmoja akitaka utajiri kwake kwanza, na huwezi kupata utajiri huo kama huongozi nchi.

  Kwa hiyo tatizo halikuwa dini, wala haikuwa jambo la kupatiwa suluhu kwa kutenganisha nchi isipokuwa haramu za Ubepari ambazo siku zote Ubepari huandamana na UFISADI..Na tuwaombee Mungu watu hawa watambue makosa yao kwamba Mali imelaaniwa hadi vitabu vya dini na pasipokuwepo na msingi bora wa kijamii kuhakikisha mgawanyo bora wa rasilimali hizo wanadamu hupoteza UTU wetu bila kujali dini, kabila wala Undugu.. Nigeria wakifikia kugawana nchi kama Sudan, hao North wataupoteza Uislaam wao na kuanza kupigana kwa makabila pia..Tatizo sio dini, kabila wala rangi bali UBAPARI usiokuwa na miiko na maadili..

  Nadhani nimeandika mengi ya kutosha na pengine umepata mwanga mkubwa juu ya tofauti zetu ktk misingi ya kiutawala. Binafsi sipingani na Ujamaa isipokuwa tu ktk mfumo wa kiuchumi pale serikali inapohodhi njia zote za uzalishaji - Hii haikuwa mfumo zmuri isipokuwa Freemarket economy ambayo serikali inatakiwa ku control na kutazama zaidi mgawanyo wa rasilimali zake na hawa viongozi kuwekea miiko na maadili kama kinga ya Tamaa na kibinadamu kama tunavyoaswa kutokuriba zinaa..
   
 3. J

  JokaKuu Platinum Member

  #3
  Jan 1, 2012
  Joined: Jul 31, 2006
  Messages: 12,781
  Likes Received: 5,021
  Trophy Points: 280
  Mkandara,

  ..I thought in Nigeria mafuta yanapatikana South kwa Wakristo kama kina Ken Sarowiwa, na Col.Chukwuemeka Ojukwu.

  ..Northern Nigeria ambako Waislamu wako wengi kuna rasilimali chache sana, isipokuwa wao wamejaaliwa kuwa na population kubwa.

  ..kwa msingi huo wa kuwa na population kubwa, na ku-dominate Jeshini, Maraisi karibu wote wa Nigeria wametokea North.

  NB:

  ..viongozi wa Nigeria ni hawa hapa: Alhaj Tafawa Balewa, Gen.Johnson Ironsi,General.Yakubu Gowon,Gen.Murtala Mohamed,Gen.Olusegun Obasanjo,Alhaj Dr.Shehu Shagari, Gen.Mohamad Buhari, Gen.Ibrahim Babangida,Gen.Sani Abacha, Gen.Abdulsalami Abubakar, Gen.Olusegun Obasanjo, Alhaj Umar Yar'Ardua,na Goodluck Jonathan. Kwenye rangi ya blue ni Waislamu.
   
 4. M

  Mkandara Verified User

  #4
  Jan 1, 2012
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  1. Yap kuhusu Mafuta kweli yapo South ukanda wa Delta... my mistakes shukran!

  2. Hapana mkuu wangu hapa ndipo nilipotaka sana kusema ya kwamba tusiwahukumu watu kwa dini zao au majina maana Babangida na Abacha ni wa South japokuwa waislaam hao wengine sijatazama kwa umakini lakini najua huwezi kufiiria kila Muislaam anatoka North na mkristu ni kutoka South hizi ni siasa mbaya sana za kuwagawa watu..Pia simuoni Azikiwe ktk list na Gowon sidhani kama alikuwa muislaam.. na kitu nachojaribu kulenga hapa ni hatari ya ile fikra ya kuwatazama watu kwa dini na makabila yao (dhana)ukifikiria itakusaidia wewe kupanda unapomshusha mwingine..Tufikirie zaidi Uzalishaji na kugawana mavuno badala ya mila na desturi yetu ya kugawana umaskini au mtaji (urithi).

  3. Marais ulowasema wengi ni wale ambao walikuwa viongozi wakati Nigeria inatawaliwa kijeshi. Na hawa viongozi japokuwa walikuwa waislaam sio wote wanatoka North ingawa majority yao walitoka North na utawala mzima kwa ujumla ulitoka Jeshini by ranks na mapinduzi, lakini Utajiri wa nchi hii ulibakia kusini wakati hawa ni waislaam wenye jamaa zao North.
  So kiongozi, being a Muslim au Mkristu haiondoi hulka ya binadamu ktk UFISADI..Fisadi anaweza kuwa ndugu yako Muislaam/mkristu kwa maana ya mifano tunayoiona Nigeria na Sudan nchi ambazo Udini uliwagawanya wananchi wakati viongozi wao wakii enjoy matunda ta utawala na sii dini zao.

  Nigeria tunaona marais wengi waislaaam kama ulivyosema lakini what have they done kwa watu wao ingawa wanaona wazi kwamba North maskini ni asilimia 70. Na wa kusini wanasema utajiri ni wao hivyo huko juu mtajijua kama ilivyokuwa Sudan watu kudai rasilimali zao na sii za Taifa kutokana na Ujenzi wa chuki za kidini..

  Mnafikri haya yalitokea kwa bahati mbaya? sidhani ni mpango wa kutugawa ili tutawaliwe na kwa habati mbaya sana tanzania leo watu wanajitazama kwa rangi zao.. viongozi wengi wanaanza kujitambulisha kwa dini zao hawakosi misikitini na makanisa kujijenga. Hii ndio hatari ya kule tunakoelekea yaani hata tuwe na mafuta kesho maadam dira yetu inaelekea kule kwa kina hawa Nigeria na Sudan basi ni swala la muda tu lini tutafika kuwa kama Nigeria au Sudan...
   
 5. R

  Ramso5 Member

  #5
  Jan 2, 2012
  Joined: Dec 13, 2011
  Messages: 63
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 13
  Mhhh....?
   
 6. Safety last

  Safety last JF-Expert Member

  #6
  Jan 2, 2012
  Joined: Mar 24, 2011
  Messages: 4,224
  Likes Received: 164
  Trophy Points: 160
  Mafuta mengi yapo south Nigeria, niger delta Sio North.
   
Loading...