Mvutano upinzani na dola mfitini ni katiba?

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Sep 20, 2021
3,216
3,585
Nyanja: Demokrasia/Utawala Bora

Ninaandika andiko hii nikijuwa wazi kabisa kuwa wapo watakaopingana nami jambo ambalo ni kawaida kabisa kwa ufahamu wangu, sijui wa kwao, lakini pia raha ya kujifunza ni kutofautiana kimantiki ya hoja, kwa sababu ni ustaarabu kukubaliana kutokubaliana (agree to disagree). Ninachoshauri ni kuwa, yule ambaye anakusudia kutokubaliana nami avute subira kidogo asome mwanzo hata mwisho wa andiko ndipo atathmini kutokubaliana kwake nami kwa sababu anaweza akazua maswali mwanzoni mwa andiko ambayo kumbe majibu yake yako mwishoni mwa andiko, hivyo akajikuta hanitendei haki na kutendeana haki ndiyo msingi wa utangamano.

Aidha nina hulka moja kuu kuwa siku zote huwa siandiki kabla sijasoma/sijafanya rejea ya yale ninayotaka kuandika. Ninapokosa fursa ya kusoma kwa mapana, kimo na kina huwa sichukui hatua ya kuandika. Ninalazimika kufanya hivyo kwa sababu ninajihisi kuwa na bahati mbaya ya kuishi kwy jamii ambayo utamaduni wa kujisomea umetupwa kwa miaka mingi sana. Ndiyo maana hata dira ya taifa kwy lengo lake namba mbili imebainisha tatizo la Watz kukwepa kujifunza ambako kungewasaidia kupata maarifa ya kuwawezesha kutekeleza dira hiyo kwa kukamata fursa ambazo masharti yake ni usomi (kuwa na tabia ya kujifunza) kwanza, kwa maana bila maarifa tutajikuta dira yetu ikifanikishwa na wasomi raia wa kutoka nje ya Tz ambao ndiyo watakuwa na fursa za ajira kutokana na sifa yao ya uweledi.

Hivi karibuni kwy medani za siasa za ndani ya nchi yetu Tz, kumekuwa na chagizo za kambi ya upinzani zenye kuashiria kuwa demokrasia inakandamizwa. Wakati nikiwa na mtizamo tofauti na wakati huo huo nikiwa na haki ya kikatiba ya kutoa maoni sawa na ibara ile ya 18 (kama ilivyorekebishwa 2005), ninatambua haki ya kikatiba (ibara ya 29 na 30) ya upinzani kukuwa, kuwepo na kutumia fursa zilizopo kufanya shughuli zao, lakini kwa msisitizo wa kuheshimu sheria, maelekezo na amri halali zitolewazo na vyombo na mamlaka halali kikatiba pia. Siyo tu Tz ambako wapinzani wanalalamika kutendewa ndivyo sivyo, bali sehemu nyingi za dunia hii na wala siyo bara la Afrika pekee na kwamba wanatofautiana tu kwa aina ya mazingira yao ya kuendeshea shughuli zao.

Aidha, wakati wapinzani wanadai kutekeleza matakwa ya kikatiba kwa kuitisha mikutano na maandamano, vyombo vya dola, msajili wa vyama vya siasa, polisi, serikali na labda mahakama nazo zinadai kutekeleza wajibu wao wa kikatiba dhidi ya harakati hizo za wapinzani na kwamba zipo kwa mujibu wa katiba hiyohiyo. Sasa sijui hapa tatizo ni wapinzani, msajili wa vyama vya siasa, bunge iliyotunga sheria hizo, polisi, serikali, mahakama au katiba hiyo tajwa?

Uchovu wa katiba iliyopo ulimfanya pia Mhe. rais Magufuli achukuwe hatua zinazolenga kusahihisha mapungufu ya katiba hiyo (hakuivunja wala hakuiandika upya), ndiyo maana wanasiasa wa wastani walikuwa wakiona kwamba katiba inavunjwa, katiba ambayo hata wao wanasiasa hawa hawaitaki ilhali walishiriki katika uandikwaji wake mwaka 1977 na mabadiliko yake makubwa 14 chini ya demokrasia ya chama kimoja ambacho na wao walikuwa wanachama wake, na wengine wao bado hata leo baada ya kuwa wapinzani wameendelea kumiliki kadi za CCM wanachokipinga, huku wengine wao walipitisha kwa kura ya ndiyo rasimu ya katiba pendekezwa na sasa wanakula sahani moja na wenzao ambao walisusa bunge maalum la katiba, kweli wakati fulani unaweza kusukumwa kuamini kuwa siasa ni tikiti ambalo lazima litobolewe kwanza ndiyo ujuwe ndani yake.

Hatua za Mhe. rais Magufuli wa awamu ya 5 zilidhihirisha kwamba katiba ilipoteza nguvu, haki na uhalali wa kujisimamia kwa sababu matamko yake yalifikia hatua ambayo yalikuwa hayaheshimiwi na hayatekelezwi, hii inamaanisha katiba ilikuwa nusu mfu, kwa sababu ilishindwa kulihuisha taifa na kuliokoa dhidi ya kuelekea kwy msambaratiko, ilibaki na uwezo wa kusimika viongozi madarakani bila kuwasaidia kusimamia nchi. Hivyo Mhe. rais Magufuli pia kama walivyo wengine hakupingana na marekebisho yake yaliyoasisiwa na mtangulizi wake. Mhe. rais Magufuli wa awamu ya 5 alikuwa mwanamabadiliko pia kama walivyo wanamabadiliko wengine. Hata hivyo ieleweke kwamba hakuna katiba Afrika ambayo imeandikwa na malaika na kwamba ni msahafu, hata ile ya Kenya ambayo inasifiwa kwa ubora wake duniani bado inalalamikiwa sana na watawala wenyewe tena wale ambao pia kama Tz, waliipitisha wakiwa kama wapinzani dhidi ya Democratic Party cha Mhe. rais Kibaki. Huu ndiyo unafiki na fitina ya vyama vya siasa barani Afrika.

Kabla ya Mhe. rais JPM wa awamu ya 5 kutamalaki nchi, katiba yetu ilikumbwa na gonjwa moja baya sana la kuhakikisha kuwa mambo mema ya umma yanabaki kuwa nadharia tu huku yale maovu ya kuneemesha wachache yanatimia kwa matendo halisi. Katiba ilikuwa ikitoa mwanya kwa ukengeufu na kuminya fursa ya utakatifu, ilishindwa kukemea maovu katika jamii. Mhe. rais JPM aliamua kuchukua hatua za makusudi kabisa za kuhakikisha taifa linaiishi katiba yake kwa matendo halisi na siyo kuiishi kwa nadharia tu.

Mhe. rais JPM alikaza buti, hakukubali yaishe kama alivyokubali Mhe. Mbeki na sasa wanatamani enzi yake ingerejea ambayo haiwezi tena kujirudia (labda apindue). Yuleyule Mhe. Zuma waliyemkaribisha kwa vigelegele huku wakimnanga Mbeki mithili ya Yesu alivyokuwa akiingia mjini Yerusalemu (sijui kwa kuwa alikuwa na shehena ya mikate?!) sasa wamemfikisha yeye Zuma kwa Pilato na wanashangilia anavyowambwa msalabani huku wakimkana kutomjuwa kabisa. Kule Yerusalemu walimshangilia pia punda aliyembeba Yesu hadi ndani ya hekalu wakimfananisha na shujaa aliyewaletea Mfalme Mwokozi, lakini siku punda yule aliporudi Yerusalemu alipigwa kama paka mwizi tena akiambiwa maneno ya dhihaka kabisa kuwa ni najisi, wanasahau kuwa walimkaribisha hadi ndani ya hekalu hapo awali na hawakuona unajisi wake bali macho yao yaliona mikate tu waliyoletewa na Yesu kwa kutumia usafiri wa punda yule.

Wanasiasa hawakuifahamu kinagaubaga falsafa ya Mhe. rais JPM ingawa ni Mwanafalsafa aliyetumia lugha nyepesi kueleweka kwa watu wa madaraja na makundi-maslahi mbalimbali. Kwa vile hawakutafuta kuifahamu falsafa yake, iliwawia vigumu pia kumfahamu yeye Mhe. rais kama nafsi na roho japo waliweza kuufahamu utu wake wa nje. Hii iliwagharimu muda kumfahamu yeye na falsafa yake na mwelekeo wa serikali yake na walipozinduka uchaguzi mwingine uliwadia.

Wakati wanasiasa walimsuta na kumtangaza rais kuwa alikuwa akiminya demokrasia, wahisani ambao ndiyo siku zote wamekuwa miungu ya siasa na demokrasia ya Afrika waliendelea kumpongeza na kumpa ushirikiano mkubwa kuliko wote uwao ule ambao Tz kama taifa imewahi kupata tangu nchi imekuwa jamhuri, na zaidi walifanya hivyo kwa matendo halisi na wala siyo kwa nadharia.

Hali hii ni tofauti sana na nazidi kusisitiza kuwa haijawahi kutokea tangu nchi imekuwa jamhuri kwa sababu taifa chini ya awamu ya Mhe. rais JPM lilipokea misaada ya thamani kubwa ndani ya miezi 8 tu tangu rais alipoitamalaki nchi bila hata yeye rais mwenyewe kwenda kuombaomba kama tulivyozoea huko nyuma. Hata USA iliyoahirisha misaada ya Millennium Challenge ilijirudi yenyewe viganja vikiwa vimeunganishwa kifuani kama ishara ya kunyenyekea huku kibindoni ikiwa na kitita kikubwa kwa ajili ya Tz ya Mhe. rais JPM.

Aidha viongozi wa kiroho katika taifa la Tz nao walichukuwa msimamo kama huo wa wahisani kwa kuendelea kumtia moyo mkuu Mhe. rais JPM kuendeleza jitihada na dhamira yake ya kuiponya nchi na kupambana kuiweka huru toka vifungo vya ufisadi, umasikini, utawala wa mwenye fedha mpishe/muabudu, uonevu nk.

Mhe. rais JPM wa awamu ya 5 alisema tangu siku yake ya kwanza kuwekwa wakfu kuwa watu wakiwamo makuhani wamuombee sana ili nchi ipone, sasa wanasiasa ambao waliwaambia viongozi wa kiroho wamkemee rais JPM walijitambua kweli? Waliwasukuma viongozi wa kiroho kuwa na unafiki wa imani, wapika majungu, waleta fujo, ndumilakuwili kwa kuwa wangeitika mwito wa wanasiasa basi wangekuwa wamekiuka nadhiri yao (ambayo hawajawahi kuitoa) na kiapo chao cha kumuombea Mhe. rais, lakini zaidi wangekuwa hawana dira na wangekuwa wapotofu hali ambayo ingewafanya hata waumini wao ambao wameponyeka na hatua ambazo Mhe. rais aliweza kuchukuwa dhidi ya kupotea haki zao na uonevu mwingine wote wapoteze imani na viongozi wao wa kiroho.

Tangu Tz kuwa jamhuri sijawahi kusikia wala kuona maandamano, mikutano ya hadhara ya siasa za upinzani zikipeleka madawa na vifaa tiba mahospitalini, wala vitanda vya wagonjwa, madawati, kujenga miradi ya maendeleo nk ilhali upinzani unapokea ruzuku, mfuko wa jimbo, ada za wanachama na wafadhili wa ndani na nje. Sijui labda kwa kuwa rasilimali zote za upinzani zina lengo moja tu, kumenyana kuingia ikulu lakini siyo kuchangia miradi ya maendeleo hata kama wapiga kura wao wana dharura wao wapinzani watatumia gharama kubwa kusambaza propaganda kuwa dharura na matatizo yoyote yale ni jukumu la serikali na chama tawala. Tena watatumia gharama kuelezea hayo kwy mikutano mikubwa ya hadhara kwa kuzunguka nchi nzima na kulipana posho.

Ili nchi hii ipone, ifikie utimilifu wa ndoto yake ya kufikia maziwa na asali na pia kufikia dira yake ya maendeleo ya 2025, tunahitaji kuheshimu muda na kuwekeza vya kutosha kwy muda na kupunguza kwy ratiba zetu mambo ambayo hayana tija kwa wakati tuliopo.

Unabii wa Mwl Nyerere kuwa mpinzani wa kweli atatoka CCM haujatimia ama kwa sababu hao waliotoka CCM kwenda upinzani ama siyo kiwakilishi cha upinzani wa kweli aliomaanisha Mwl Nyerere na kama ni hivyo basi upinzani walioukuta, ukiuunganisha na upinzani walioupeleka huko baada ya kutoka CCM basi unagundua ukweli kwamba tunahitaji kizazi kipya cha upinzani kitakacho ongoza kambi ya upinzani kuelekea kwy unabii wa Mwl Nyerere, ilhali hatua alizochukuwa Mwenyekiti wa 5 wa CCM taifa kukihuisha chama haikujulikana kama zingeweza kuzaa mpinzani ambaye unabii wa Mwl Nyerere ulimaanisha, yaani chama kikisafishwa nani mwenye dhamira njema atakihama? Labda wanafiki tu.

Naomba kura zote
 
Bongo-mpya,

Leo IGP wa JMT amekutana na Msajili wa Vyama vya Siasa jijini Dodoma kujadili ombwe la sheria kwenye dhana ya mikutano ya ndani ya kisiasa ni nini hasa? ifanyikeje? kwa sheria ipi? Role ya Polisi ni ipi hasa? Je, kuna tofauti ya mikutano ya ndani na ya nje (labda nje ya jimbo kwa mantiki na muktadha huo)?

Kongole Jenerali Sirro,
Uko professional, unatumia vizuri taaluma yako ya sheria na career yako ya Upolisi; uliyosoma chuo chenye heshima kubwa Udsm na uzoefu mkubwa sana wa kimataifa ulionao plus hofu yako kwa MUNGU ambaye sote tutapeleka hesabu zetu kwake siku zile za Dahari na Kiyama. Hakika Jeshi umelifikisha pazuri sana ambapo linapata credit za kimataifa.
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom