Muungano na Katiba mpya

mito

JF-Expert Member
Jun 20, 2011
10,513
10,404
WanaJF, hii nimeinasa kwenye blog ya Michuzi nikaona inafaa kuanikwa hapa pia!

Samahani sana Anko, naomba uweke hii hoya yangu kwenye libeneke lako ili niweze ku-share mawazo yangu na watanzania wenzangu popote walipo. Nimeshindwa kuvumilia kukaa na mawazo haya moyoni mwangu kutokana na jinsi hali ya Muungano wetu inavyojadiliwa na kuhusishwa na Katiba mpya ambayo mchakato wake umeanza kushika kasi.
Kama alivyowahi kusema Mh. Zitto “idadi ya wapinga muungano inazidi kuongezeka siku hata siku. Ukiwauliza kwa nini hawataki muungano wanasema aah, basi tu. Kama ni Mzanzibari atasema Tanganyika wanatutawala. Kama ni Mtanganyika atasema Wazanzibari wamezidi kelele, tunataka Tanganyika yetu. Lakini ni lazima tuurekebishe Muungano huu. Ulivyo sasa utavunjika tu. Kuulinda muungano ni kuufanyia marekebisho makubwa”. Kusema kweli hoja yangu kubwa iko hapa, na inatokana na sababu kubwa mbili zinazofanya nikose imani kabisa na wanasiasa wetu. Moja, ni hii tabia ya wanasiasa wengi kutosema ukweli kuhusu kwanini wazanzibari wengi hawataki muungano. Sijui kama ni kweli kwamba hawajui wazanzibari wanalilia nini hasa? au hawajafanya utafiki wa kutosha kujua kwanini wazanzibari wengi wanapinga huu muungano?

Jamani, tatizo kubwa la wazanzibari si udini kama baadhi wanavyodhani, si wabara wanaoishi au kufanyakazi Zanzibar, si wakristo wanaopenyeza ukristo Zanzibar, si uwiano wa nafasi za ajira katika taasisi na mashirika ya umma, na wala si mafuta kama wengine wanavyofikiria. Haya na mengine ambayo sikuyataja ni geresha tu, ila shida kubwa ya wazanzibari ni UTAIFA. Wazanzibari wanaona kwamba kuwa kwao ktk muungano kumeua kabisa nchi yao. Wanataka wajulikane na mataifa mengine kama nchi. Wanaamini wakijulikana kama nchi na mataifa mengine watapata fursa nyingi ambazo wamekuwa wakizikosa kwa kuwa ndani ya muungano. Tena ukiongea na wazanzibari kuhusu marekebisho ya muungano, watakwambia wanataka muungano kama wa nchi za Ulaya au kama ule wa EAC (shirikisho) ambapo kila nchi inajulikana kama nchi ndani ya muungano. Kwa hiyo shida kubwa ya wazanzibari iko hapa! Na ukitaka kutimiza kiu ya wazanzibari maana yake utavunja muungano wa sasa (kitu ambacho serikali ya JK haiku tayari kukiona), halafu sasa ndo mkae mjadili kuhusu hilo shirikisho.

Sababu ya pili ya msingi wa hoja yangu, ni kuhusu marekebisho ambayo wanasiasa wetu wanapendekeza yafanyike ili kuulinda muungano. Kusema kweli hapa ndo nachoka kabisa, maana mapendekezo yao mengi yanaangalia zaidi maslahi yao binafsi na ya vyama vyao kuliko wananchi wanaowaweka katika madaraka. Wabara wengi, Chadema, CUF n.k wanaamini kwamba hoja ya kuwa na serikali tatu ndo itakuwa suluhisho la matatizo ya muungano. Binafsi nasita kuamini hilo kwa sababu hoja ya serikali tatu itakuwa haijategua kitendawili cha utaifa wa wazanzibari, hivyo wataendelea kuupinga tu muungano. Kwa maana hoja hii itakuwa ni mzigo bure kwa serikali katik kuziendesha hizi serikali tatu, na utakuwa ni ufujaji wa pesa za walipa kodi. Isitoshe ni hoja yenye kulenga kuwapa ulaji wanasiasa kwa kuwatengenezea nafasi nyingi za kisiasa.

Ngoja nimalizie hoja yangu kwa kutoa angalizo. Mchakato wa katiba mpya umeanza. Serikali imeishaahidi kuwa itahakikisha mchakato unamalizika kwa wakati ili katiba mpya iweze kutumika katika uchaguzi mkuu ujao. Hizi zinaonekana kama habari njema sana kwa vyama vya upinzani na watanzania kwa ujumla ambao wamekuwa wakilalamikia mapungufu yaliyomo katika katiba ya sasa katika kuhakikisha demokrasia ya kweli inatendeka katika kuchagua viongozi wetu wa kisiasa. Lakini nyuma ya pazia kuna hili! Watu binafsi, vyama vya siasa, na taasisi mbalimbali vinashauri baada ya kuandaa rasimu ya katiba mpya basi ipelekwe kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni (referendum). Huu ni ushauri mzuri lakini kutokana na hali ilivyo nashawishika kusema uchaguzi ujao unaweza kufanyika kwa kutumia katiba ya zamani, unajua kwanini? Kuna kila dalili kuwa wananchi wengi hasa wa Zanzibar hawawezi kupitisha rasimu ya katiba mpya ambayo haitatambua utaifa wao. Kwa maana hiyo kuna uwezekano mkubwa wa katiba mpya kukataliwa na wananchi. Je hali hii ikitokea itakuwaje? Kumbuka uchaguzi mkuu utakuwa umekaribia, je itabidi rasimu ikafanyiwe marekebisho kwanza halafu irudi tena kwa wananchi kupigiwa kura ndo uchaguzi ufanyike? Au itabidi uchaguzi ufanyike tu kwa katiba ya zamani? Au je itabidi serikali iliyopo madarakani iendelee tu hadi katiba mpya itakapopatikana ndo uchaguzi ufanyike?
Wadau nawasilisha!

Binafsi naona hizi points zina mashiko! Tuziangalie kwa mapana na marefu yake!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom