SoC03 Muuaji wa kimya aliezoeleka

Stories of Change - 2023 Competition

JenDa

New Member
Sep 13, 2022
1
0
Msingi wa mafanikio na maendeleo ya mtu mmoja mmoja mpaka taifa zima ni afya bora, hakuna shughuli yoyote ambayo binadamu anaweza kuifanya pasipo kuwa na mtaji namba moja ambao ni afya.

Katika jamii za kitanzania kumekua na mazoea mengi yanayohatarisha afya za watu lakini mazoea ya watumiaji wa tumbaku kuvuta kiholela katika maeneo ya umma hasa yaliyokatazwa ni tabia iliyokithiri na kushika kasi kwa watumiaji wa bidhaa hizo hasa sigara kuvuta sigara zao muda na mahali popote wanapojisikia au kuamua kufanya hivyo hasa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi.

Licha ya mazoea hayo mabaya kuwa hatari kwa uhai na afya za watu bado swala hili limekua likifumbiwa macho na kupuuzwa kwa kiwango kikubwa bila kujali wala kuzingatia sheria za uthibiti wa matumizi ya tumbaku zinazokataza uvutaji wa tumbaku kwenye maeneo yanayotumiwa na watu wengi.

Kwa mujibu wa taarifa ya TMDA (Tanzania Medicines and Medical devices Authority) ya 26/7/2021 iliyotolewa kwa UMMA chini ya kifungu cha 12 cha sheria ya udhibiti wa bidhaa za tumbaku ,sura 121 kimetafsiri maeneo ya umma kama mahali zitolewapo / kupatikana huduma mbalimbali za kijamii kama masokoni.

sehemu za usafiri wa umma na kadhalika ,licha ya sheria hiyo kukataza matumizi ya uvutaji wa aina yoyote ile ya bidhaa za tumbaku na kuelekeza alama na maneno yanayokataza kufanya hivyo katika maeneo hayo kuwekwa bado wahusika wanatumia bidhaa hizo kwa uhuru uliopitiliza mithili ya kutokuwepo na sheria yoyote wala mtu wa kuzisimamia sheria hizo.

Vilevile sheria hiyo iliweka bayana kuwa wavutaji wameruhusiwa kuvuta tumbaku katika maeneo maalum yaliyotengwa kwajili ya matumizi na kuweka bayana kuwa bidhaa zinazohusika na sheria hii ni zile zinazotambulika tu kisheria kama sigara, siga, tumbaku ya unga ,kiko n.k kupitia kifungu cha 13 cha sheria hiyo pasipo kuhusishwa kwa bidhaa za tumbaku zisizovutwa.

Licha ya sheria hiyo kuwepo uvunjwaji wa sheria hiyo umeshuhudiwa na kuendelea kwa kiwango kikubwa tena katika maeneo hayohayo yaliyokatazwa tena watu walio katika makundi maalum kama wazee,wajawazito na Watoto wakikumbana na kadhia hiyo hasa katika masoko na vituo vya usafiri wa umma huku wavunjaji sheria wakichukua fursa ya watanzania wengi kutojua madhara yaliyopo katika moshi unaotoka katika tumbaku iliyoungua hata kwa wavutaji wa daraja la pili ambao ni wale wanaovuta hewa yenye moshi wa tumbaku kutoka kwa wavutaji.

Ukiukwaji wa sheria ya udhibiti wa matumizi ya bidhaa za tumbaku ni tabia kongwe iliyoleta mazoea ya kuzipuuza kemikali takriban 250 katika moshi wa tumbaku zilizothibitika kusababisha madhara ya kiafya kwa binadamu kama maradhi ya moyo , kiharusi na matatizo ya mfumo wa hewa ,wakati kemikali Zaidi ya hamsini zilizopo katika moshi wa tumbaku zimethibitika kusababisha saratani ambayo ni ugonjwa unaotishia afya, uhai wa watanzania Pamoja na ustawi wa nchi kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya wagonjwa wapya wa saratani mbalimbali wanaoendelea kuripotiwa katika hospitali mbalimbali za umma na binafsi hapa nchini ,ugonjwa huo unajulikana si tu kwa kuwa hatari bali pia unaohitaji gharama kubwa za matibabu jambo ambalo halipaswi kuwa kwa kiwango kikubwa hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Uwepo wa nikotini katika moshi wa tumbaku huongeza na kuchochea uwezekano wa kupatwa na saratani hata kwa mtu asie mvutaji wa kwanza pekee bali hata mvutaji wa pili ambae ni mtu aliye karibu na mvutaji wa kwanza au anaefikiwa na moshi wa mvutaji wa kwanza na kuvuta hewa iliyochafuliwa na moshi huo.

Pamoja na madhara hayo miongoni mwa mengi yatokanayo na uvutaji holela wa tumbaku na sheria za kukataza tabia hiyo kuwepo lakini wavunjaji sheria hawakamatwi wala kuchukuliwa hatua yoyote kwa kukiuka sheria wala wananchi hawajaonesha kuchukua hatua yoyote ya kukemea swala hili kwa umoja Zaidi ya kushuhudia watumiaji wengi wa tumbaku wakiendelea kutamba na kuvunja sheria na wananchi kuizoea hali hiyo hatari kwao.

Hali hii inatoa tafsiri kuwa mamlaka husika zimeshindwa kuwadhibiti na kuwawajibisha wavunjaji hawa wa sheria na kwamba mamlaka hizo nazo zimeona ni kawaida kwa sheria hizo kuvunjwa pasipo mtu yoyote kuwajibishwa . Uwepo wa sheria hizo ni Ushahidi kwamba wapo wanaotakiwa kuhusika na kuzisimamia kwa kuwawajibisha wanaozivunja.

Ninapendekeza kuwepo na utaratibu wa kuwawajibisha wahusika wanaopaswa kuzisimamia sheria hizo ili nao waweze kuwawajibisha wahusika, uwajibishwaji huo usiishie katika maneno matupu tu ikiwa ni sehemu ya kuwafanya wawe makini kusimamia majukumu yao sambamba na utozwaji wa faini kubwa ama kifungo kwa wakiukaji wa sheria huku hatua hizi zikihusisha serikali kupitia wizara husika na jeshi la polisi kusimamia sheria hizi bila kukiuka haki za binadamu wakishirikiana na wananchi katika kukemea na kudhibiti swala hili.

Ili kuwapa motisha wananchi na serikali katika kutekeleza hili uwepo utaratibu wa kuwapongeza wananchi na watumishi wa serikali wanaofanikisha kusimamiwa kwa sheria hii kutoka katika tozo wanazotozwa wavunjaji sheria kupitia faini wanazolipishwa.

Nii italeta chachu ya kubadilika kwa mazoea haya mabaya na kupunguza idadi ya visa vipya vya saratani vinavyoongezeka kwa kasi kubwa na kukabiliana na changamoto ya kudhoofu kwa rasilimali watu ambayo ni nguvu kazi ya taifa Pamoja na fedha nyingi zinazoelekezwa katika matibabu ya saratani.

Vilevile sheria hazitungwi ili tu kuwekwa katika maandiko bali zifanikishe adhma ya uwajibikaji kwa pande zote mbili baina ya wanaopaswa kuzisimamia na wale wanaowajibishwa nazo kwa misingi ya maendeleo ya jamii.

kiko (2).jpg
 
Back
Top Bottom