Ndugu wananchi wazalendo wapenda maendeleo, naomba sana mnielewe na mnivumilie.
Awali ya yote, nawapa pole sana wananchi wenzangu kwa tabu mnazozipata kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili, hii ni changamoto kubwa kwetu sote. Nchi yetu tukufu na Taifa letu tukuka la Tanzania litatimiza miaka 50 ya uhuru mwezi Desemba mwaka huu, hiki ni kipindi kizuri kwetu sote kubadili msimamo na mtizamo dhidi ya watawala, kwamba badala ya kuwaachia kila kitu juu ya mustakabali wa nchi yetu, wakati sasa umefika wa kuwa na mawazo chanya juu jinsi ya kutuvusha kutoka hapa tulipo kuelekea nusu karne ijayo.
Tanzania ni Taifa huru, je wananchi wake ni watu huru?
Ndugu wananchi, tufunguke kifkra na kimatendo pia. Mimi nimechukua jukumu la kuongoza vuguvugu la mapinduzi ya kweli yatakayoleta ukombozi wa kweli wa mwananchi wa kawaida.
Nawaomba sana mniunge mkono ndugu zangu ili tujikomboe na tuweze kupiga hatua, kutoka kwenye hali ya Taifa huru lenye watu maskini na wanyonge ndani ya nchi yetu, na kuwa watu huru wenye matumaini ya kufaidi rasilimali za nchi yetu.
Tanzania ni nchi yenye vyama vingi vya siasa, ila wananchi wake wengi si wanachama wa vyama hivyo, nami nawakilisha kundi hili kubwa la wazalendo wapenda amani ambao hawafungwi na itikadi za chama chochote cha siasa.
Katiba mpya ya nchi yetu ni lazima izingatie demokrasia ya kweli, kwa kuruhusu wagombea huru wasiotokana na vyama vya siasa katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Nimalizie kwa kuwatakia ndugu zangu waislam swaum yenye wingi wa heri katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan, asanteni sana.