Mungu wetu tupatie rais aliye safi

Mungu wetu tupatie rais aliye safi

Keykey

JF-Expert Member
Joined
Dec 1, 2006
Posts
3,251
Reaction score
751
Wakuu hii nimeikuta mahala nikaipenda naona niwawekee hapa jamvini.

MUNGU WETU TUPATIE, RAIS ALIYE SAFI

La mgambo limelia, tutangaze nia zetu
Tuache sasa kulia, tutetee nchi yetu
Wa kushoto na kulia, tuonyeshe nia zetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Tume imepangilia, sifa za Rais wetu
Vigezo vyaingilia, uhuru na nia zetu
Taifa laangalia, usafi wa nyendo zetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Hata waliofulia, watamani kiti chetu
Wazidi kushangilia, tamko la Tume yetu
Urais walilia, watawale nchi yetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Kama hatujatulia, kwa zile tabia zetu
Iweje tuje tulia, tukigusa Kiti chetu
Dogodogo twalilia, kuzikidhi haja zetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Jamii yashangilia, tusemapo nia zetu
Hasa tukiingilia, kuwakashifu wenzetu
Tume ikivumilia, tuchezeavyo wenzetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Wengine twachukulia, Urais haki yetu
Bila hata kutulia, kuchunguza utu wetu
Na pia kuangalia, maoni ya watu wetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Sifa tunajitwalia, toka kwa wapambe wetu
Mkaa wajipalia, tukikosa kiti chetu
Vyombo vyawaangalia, wapambapo sura zetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Ukija kuchungulia, undani wa sifa zetu
Waweza hata kulia, uchafu wa nafsi zetu
Ikulu twachukulia, kama vile nyumba yetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Wengine wafagilia, walopora mali zetu
Wezi wawapalilia, wanyonyao mali zetu
Mambo wayapangilia, ili wanyonye nchi yetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Umma unawalilia, walotosa nchi yetu
Watakao kimbilia, kutawala nchi yetu
Njia wakifagilia, wakirubuni wenzetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Mambo ukifatilia, katika chaguzi zetu
Ni kule kukimbilia, teua rafiki zetu
Na pia kushambulia, wapingao mambo yetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Kiti kuja kukalia, ndani mwa Ikulu yetu
Uwe umeshatulia, kuilinda nyumba yetu
Dua zikitangulia, mbele ya Muumba wetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Wale walotangulia, ongoza Ikulu yetu
Mengi walivumilia, kunusuru nchi yetu
Umoja wakililia, na amani nchini mwetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Wengi tunacholilia, heshima kwa nyumba yetu
Tusipate kuja lia, kwa yale makosa yetu
Akishakuikalia, Ikulu ya nyumba yetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Yupo aliyetulia, wamuandaye wenzetu
Naye akichungulia, kauli na mbio zetu
Kamati yamwandalia, atawale nyumba yetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Zidini kufatilia, tunanipo nia zetu
Msikose vumilia, kusoma habari zetu
Na pia kuchungulia, safari na dira zetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Umma unacholilia, hatima ya nchi yetu
Yule atayekalia, kiti cha Ikulu yetu
Usije kuja kulia, kwa yale makosa yetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Mungu tunakulilia, inua Taifa letu
Watu watashangilia, ubora wa Rais wetu
Hofu kuifutilia, machafuko nchini mwetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Misumari pigilia, toboa adui zetu
Washindwe kuingilia, amani ya nchi yetu
Twakuomba mwagilia, baraka Ikulu yetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Zipo twazifagilia, sifa za Rais wetu
Kikwete kaachilia, tuseme yaliyo yetu
Wapo watakaolia, aagapo nyumba yetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi

Moja nakishangilia, la huyu Rais wetu
Ni kutokufagilia, ukabila nchini mwetu
Kikwete amelilia, umoja wa watu wetu
Mungu Wetu Tupatie, Rais aliye safi
 
Back
Top Bottom