Profesa Muhongo aalikwa Uswisi, Marekani
Atahutubia mikutano ya wasomi duniani
Na mwandishi wetu,
Waziri wa Nishati wa Tanzania Profesa Sospeter Muhongo amealikwa kuhudhuria mkutano unaoshirikisha viongozi na wataalamu kutoka mataifa mbali mbali nchini Uswisi.
Mkutano huo ujulikanao kama World Economic Forum unafanyika jijini Davos nchini humo. Aidha kutoka nchini Uswisi, Profesa Muhongo ataelekea nchini Marekani alikoalikwa na Serikali ya nchi hiyo kwenye mkutano mkubwa unaojadili masuala ya nishati ambapo yeye atakuwa mmoja wa watoa mada.
Akitoka nchini Marekani, Profesa Muhongo ataelekea nchini Italia ambako pia amealikwa kama mmoja wa wataalamu duniani. Wakati mataifa makubwa yakipigana vikumbo kuwasilisha mialiko kwa Profesa Sospeter kwa kuthamini na kuheshimu utalaamu wake, wanasiasa na wafanyabiashara hapa nchini wameendelea kupuuza utaalamu huo na kuwalaghai watanzania.
Kikundi hicho cha watu wenye kusaka madaraka wanaotafuta fursa ya kuiweka mkononi serikali ijayo, wamekuwa wakitumia vyombo vya habari kuchafua wataalamu na wasomi mahiri wanaoheshimika duniani kama Profesa Muhongo.
"Inasikitisha wapinga maendeleo hawa wanaotumiwa na mataifa yale yale yanayothamini utaalamu wa akina Muhongo, wameendelea kuwafanya watanzania wajinga wao wanaoweza kuwaburuza kwa propaganda na kuwchafua watu wema na wazalendo", ameeleza kwa masikitiko Bwana Swedi Mfanyabishara jijini Dar es salaam.
Aidha ameelezea kushangazwa na watu waliojipatia uheshimiwa ambao awali amedai walikuwa wezi na majambazi, wanavyoweza kuwa na ujasiri wa kuwatukana wataalamu kama Profesa Muhongo. "Umefika wakati sasa kwa wazalendo wa nchi hii kusimama imara kupambana na watu hawa ili kuwaokoa watanzania wasiangukie mikononi mwa mabepari na wezi wa rasilimali zao", amedai.
Wakati huo huo, Waziri Muhongo ameiagiza Bodi ya TANESCO ifuatilie miradi ya umeme ya makaa ya mawe ili kumaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa umeme nchini.
Aidha mradi wa umeme vijijini(REA) unatarajiwa kupeleka umeme kwenye vijiji 1,500 nchini kote na kwamba Waziri Muhongo ameagiza mikoa na wilaya kuhakikisha mradi huo unakamilika kabla ya Aprili 30 mwaka huu. ( Source; ALHUDA)