Mtwara si Wendawazimu

Mtwara si Wendawazimu

katumbwalala

Member
Joined
Jan 17, 2013
Posts
27
Reaction score
20
Mtwara si wendawazimu|​
Paschally Mayega
RAIS wangu, walioliona jua kabla yetu wanasema kwenda mahakamani si kushinda kesi. Leo tunaambiwa wana wa Mtwara ni wa choyo. Wanataka gesi ya Tanzania iliyopatikana Tanzania sehemu ya Mtwara iwe yao peke yao! Na kwamba Watanzania wengine ambao hawakuzaliwa Mtwara hapana!

Gesi hiyo si yao! Simjui nani kaliumba neno hili kwani limejaa unajisi! Kama kweli wamesema hivyo na kwamba kilichowekwa ardhini na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Watanzania wote, wao wanataka kiwe chao peke yao, basi wala hakuna shaka wana wa Mtwara wamepata uendawazimu!

Lakini ndugu rais, inawezekana vipi wana wa Mtwara wote, wawe wendawazimu ghafla? Wakuamini hivyo lazima kwanza mwenyewe awe muumini wa nguvu za giza! Serikali wala isikalipie tu! Iwaambie Watanzania wote, wana wa Mtwara wakiwamo sababu zinazoifanya gesi ya Mtwara kutendewa tofauti na rasilimali nyingine za nchi hii. Almasi ya Mwadui inachimbwa Mwadui na kinu chake kiko Mwadui! Dhahabu ya Geita na kwingineko vinu vyake vimejengwa hukohuko Geita na kwingineko.

Hata sangara na sato viwanda vyake viko hukohuko wanakovuliwa, si Dar es Salaam. Kama ni kweli iweje gesi ya Mtwara kinu chake kijengwe Dar es Salaam? Kwanini kinu cha gesi ya Mtwara kisijengwe hukohuko Mtwara inakochimbwa? Suluhisho hapa si kutisha watu, ni kuwaeleza sababu. Za msingi zitakubaliwa, za kipuuzi zitapuuzwa!

Rais wangu wana wa Mtwara si wendawazimu wa kutaka gesi isitoke! Mwenyezi Mungu ni kweli. Kupotosha kweli ni kuwa mtumwa wa shetani. Anayepotosha madai ya wana wa Mtwara ndiye mwendawazimu. Ole wake mtu huyu! Ulimi wake ugandamane na taya zake, kwasababu ingelikuwa bora kwake kama angezaliwa bila sauti.

Niliandika huko nyuma kuwa mwanangu hajawahi kuniambia baba unasema uongo hata pale niliposema uongo wa dhahiri kwa makusudi. Husema tu, ‘Ah! Baba!' Nami sisemi wakubwa wetu wanaopotosha ukweli na kwamba wanasema uongo; nasema tu, Ah! Baba!. Rais wangu waliosoma kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu wataona kuwa gesi yetu ya Mtwara inafanana na kiwanda cha Msauzi.

Kama ambavyo kiwanda cha Msauzi kilivyosababisha harakati za ukombozi kwa watu wa Kumwitu kutoka katika makucha ya watawala wao waliokuwa wala rushwa kupindukia, tukio la Mtwara litazamwe kwa tahadhari kubwa! Kwa wale ambao hawakusoma kitabu hicho ni kwamba Msauzi alijenga kiwanda chake katika chanzo cha Mto Luzi. Mto pekee uliokuwa tegemeo la wananchi wa sehemu ile kuwapatia maji, samaki wa kitoweo na biashara na shughuli nyingine. Kiwanda hicho kikawa chanzo cha uharibifu mkubwa wa mazingira katika sehemu ile. Maisha ya wananchi yakaathirika vibaya na hali ya nchi pia.

Moshi mnene, mweusi mara nyingi uliifunika shule ya msingi ya Kumwitu. Ukaathiri kwa kiasi kikubwa masomo, wanafunzi, walimu na majirani. Sababu hiyo ikamfanya mwalimu mkuu kujitoa mhanga kuikabili serikali ikiondoe kiwanda kile. Lakini kwakuwa karibu kila kiongozi alikuwa amekula hongo nyingi kutoka kwa Msauzi serikali ilijibu kwa pamoja kwa maneno yaleyale yanayotamkwa hata leo kuwa mwekezaji ni mtu muhimu sana. Hivyo kwa viongozi Msauzi aliitwa mwekezaji na mwalimu mkuu akaitwa mchochezi.

Sehemu ya barua aliyoandikiwa mwalimu mkuu kutoka serikalini ilisomeka hivi: "Chama chetu kitukufu na serikali yetu tukufu vimeweka sera safi na iliyo wazi kabisa. Sera ya uwekezaji. Sera inayosaidia serikali yetu tukufu kupambana kwa nguvu zote na umaskini. Mwalimu mkuu gani wewe usiyeelewa hata sera ya uwekezaji, ubinafsishaji, ubia, ubabaishaji na sera nyingine kama hizo?

Mwekezaji ni mtu muhimu sana kuliko mtu yeyote katika nchi hii. Amekuja kuboresha maisha yetu. Huyu ni mtu wa kulindwa sana!"
Mwalimu mkuu aliwaambia wanafunzi wake na jamii iliyoizunguka shule yake kuwa, hakuna nguvu yoyote duniani inayoweza kuishinda nguvu ya wananchi waliokata tamaa na kuamua kuwa sasa basi! Liwalo na liwe! Nguvu ya wananchi wenye haki hushinda vita yoyote duniani.

Alipopiga yowe mwangwi wake ulisikika nchi nzima. Waliokuwa kwenye machimbo walisimama wakapambana na wezi wa madini yao.
Waliokuwa kwenye mbuga za wanyama walisimama wakapambana na waliokuwa wakiwasafirisha wanyama hai na kufanya ujangili mwingine. Wavuvi haramu na wezi wa mali ya umma walishughulikiwa sawia. Mwalimu mkuu alifanikisha ukombozi wa wanafunzi wake na wa nchi nzima lakini ni baada ya yeye kung'olewa meno bila ganzi na kuteswa sana!

Sasa wanatuambia Mtwara imetulia. Imetulia vipi wakati watu wengi wapo mahabusu? Itatulia vipi huku risasi zingali katika miili ya wananchi? Watu wamechomewa nyumba, wameporwa mali zao, wamebakwa na wengi wengine bado wanaugulia majeraha yao, useme kumetulia? Waziri Mkuu aliwahi kusema Mtwara imetulia, kumbe haikutulia. Na sasa amewaahidi mbingu!

Gesi ya Mtwara ichukuliwe kwa tahadhari isije ikawa muamsho kwa wale waishio sehemu ambazo serikali imejipanga kuwapa wawekezaji uchimbaji wa urani? Nao wakisema urani haitoki itakuwaje? Haliwezi likawasisimua waishio kuizunguka migodi yetu? Wakisema hatukubali kuporwa madini yetu, itakuwaje? Na wale wanaowaona wanyama wetu wakisafirishwa wakiwa hai je?
Rais wangu, si wana wa Mtwara tu, bali Watanzania wote kama taifa waliambiwa kuwa mchakato mzima wa kutoa kibali cha kutafuta na kuchimba gesi Mtwara uligubikwa na rushwa. Wakaambiwa kuwa waliohongwa, mamilioni yao wameyaficha katika mabenki ya Uswisi.

Aliyeanzisha hili alidai kuwa majina ya watumishi waliohongwa anayo. Ingawa sasa hivi yuko kimya lakini aliyowaingizia vichwani mwao Watanzania, wana wa Mtwara wakimo, bado yangali. Katika vifua vyao mchezo mzima wa gesi unachezwa kirushwa rushwa tu!

Kama Mtwara imetulia hao wana Mtwara karibu mia moja waliokamatwa wengine bila makosa wamemalizana nao vipi? Atuambie yule mama mjazito aliyekuwa ndani mwake alikosa nini mpaka wamuue kwa kumpiga risasi tumboni? Na kile kiumbe cha Mwenyezi Mungu kilichokuwa tumboni kiliwakosea nini askari katili wale?

Rais wangu, serikali lazima ieleze kwanini polisi walichoma moto nyumba tatu za raia na vibanda vya maduka kadhaa na kupora vilivyokuwa ndani! Kwa nini maeneo ya Magomeni, Chikongola, Nkanaledi na Mikindani askari walikuwa wakiingia kwenye nyumba za watu na kumkamata mtu yeyote hususan wanaume?

Huu ni weledi gani wa polisi wa kutuliza ghasia kwa kuiba mchele, sukari, unga wa ngano na nguo kutoka kwenye maduka?
Paulina Idd kutoka Magomeni ‘A' anasema: "Majumba yetu yamechomwa moto, wanaofanya fujo ni polisi wenyewe halafu wanakuja wanatubaka na kuiba mali zetu mpaka simu. Tunateseka sisi, yaani tumechoka kabisa na serikali yenyewe." Ndugu Rais ‘serikali yenyewe', mbele ya wananchi ni rais mwenyewe!

Ndugu rais, sitaki Watanzania wafikie mahali wakadhani Mwenyezi Mungu aliwaumbia Waziri wa Mambo ya Ndani anayeweza kazi hiyo mmoja tu, Augustine Lyatonga Mrema! Na baada ya Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine na Edward Ngoyayi Lowassa kuwa hawapo tena eti kati ya Watanzania zaidi ya milioni arobaini hakuna hata mmoja wa kufanana nao kiutendaji! Mbona Waswahili wanasema Mungu aliumba watu wawili wawili?

Vipeperushi vya kuashiria vurugu hizo vilitolewa wiki nzima kabla ya tukio. Intelejensia ilikuwa wapi? Kwanini kungoja mpaka tukio litokee? Kama hatuwezi kuwaamuru waliopo katika nafasi hizo wapishe basi tupishe sisi! Rais wangu, Kingunge Ngombale - Mwiru amezushiwa kifo. Alipozinduka akasema ‘niko fiti'. Alisikitishwa na uzushi huo, lakini kwa mshangao wa wengi alianza kulilia Azimio la Arusha.

Alisema Azimio la Arusha lilipotangazwa yalianzishwa mashirika ya umma zaidi ya 400 ambayo yalisaidia pamoja na mambo mengine kutoa ajira kwa wananchi wengi wakiwamo vijana. Wakati Azimio la Arusha linaasisiwa Kingunge Ngombale - Mwiru akiwa kiongozi alishiriki na wakati linauawa pia alishiriki.

Leo anakiri kuwa wakati wa Azimio la Arusha haikuwa rahisi kukuta vijana wakiwa mitaani bila ya kuwa na kazi za kufanya, hivi sasa wimbi la ukosefu wa ajira limekuwa kubwa na kuwaathiri zaidi vijana. Anasema Azimio la Arusha lilitoa fursa kwa wananchi wengi wakiwamo vijana kupata ajira na kushiriki katika fursa mbalimbali za kiuchumi na kwamba uchumi wa sasa wa soko huria hauwezi kumaliza tatizo la ajira nchini hususan kwa vijana.

Rais wangu, ni vema na vizuri sana kuona mtu huyu analilia Azimio la Arusha sasa wakati anaziona siku zake zikifikia ukingoni.
Kama walivyosema wahenga kuwa majuto ni mjukuu, leo Kingunge Ngombale- Mwiru anasema bado anaamini Azimio la Arusha lilikuwa na maana kubwa kwa Watanzania. Ndugu rais, mzee Ngombale - Mwiru asiishie kujutia tu, bado ana nafasi ya kuongea na wazee wenzake, Ali Hassan Mwinyi, John Samwel Malecela, Salmin Amour na wenzao kuwarudishia Watanzania tunu hii. Hakuna atakayeishi milele hapa duniani.

Hawa wazee wetu wamechoka, siku zao za kuishi hapa duniani zinahesabika. Kama wataitaka thawabu ya Mwenyezi Mungu, wasemezane sasa warudishe walichowadhulumu watu wa Mungu, Azimio la Arusha! Kingunge Ngombale - Mwiru akizungumzia wana CCM wanaotaka kugombea urais mwaka 2015 kuanza kujitangaza na kupitapita kwa wanachama, alisema hilo si kosa. Alisema mwiko si mtu kutaka kugombea urais, mwiko ni kutofuata utaratibu.

Kingunge alisisitiza kwamba kama mwenyekiti wa chama amekwisha kusema ruksa kwa wanaoutaka urais kujipitisha alimradi hawavunji kanuni za chama kama kujenga makundi ya kuhasimiana, hakuna wa kutoa kauli nyingine, kwani ndiye msemaji wa chama.
Akitoa ruksa hiyo alipozungumza na wabunge wa chama chake, Mwenyekiti Kikwete alisema:

"Wabunge na mawaziri wenye nia ya kutangaza nia ya kugombea urais wawe huru, kwani hiyo ni haki yao, isipokuwa wafanye kwa wema bila kukivuruga chama na kuwagawa wana CCM katika makundi. Sioni tatizo watu kujipitisha. Sisi sote hapa tulijipitisha. Lakini tufanye hivyo kistaarabu bila kuvurugana."

Rais wangu, haya ni maneno makini ya kiongozi mwenye busara kubwa. Wanaosema busara hiyo hukuitoa wametumwa na nani? Huku ni kuwachanganya wanachama. ‘Bosi' ni nani? Anapotokea kiongozi wa chini kutoa kauli tofauti na kiongozi wake wa juu, kuna mawili. Au, hana nidhamu, au katumwa kinafiki na mwenyekiti mwenyewe! Kama katumwa na mwenyekiti, basi mwenyekiti ndiye chanzo cha fitina na unafiki ndani ya chama!

Karibu miaka miwili imepita tangu niandike kuwa, hata kama kwa hiari yao wenyewe, Rais wetu Kikwete na ndugu Edward Lowassa wangeamua kufarakana wasingeweza. Mazingira waliyoyatengeneza wenyewe yanawalazimisha kubaki pamoja. Kabla hajatoa ruksa hiyo, rais alitangulia kumsifia Edward Lowassa. Akasema kwa misuli ya Edward peke yake CCM itaupata udiwani wa kule jimboni kwake. Kumfagilia akatia, "Au siyo mzee?"

Rais wa nchi kuonesha hadharani kuwa anautambua uwezo mkubwa alionao Edward Lowassa kiuongozi, ni kumpamba mno! Amemtofautisha Edward kwa kiasi kikubwa na washindani wake. Akionesha kuona matokeo kwa mbali, rais alisema:

"Mnaweza kuchafuana leo, kesho mkapata mgombea mwenye nundu nyingi na mabandeji kila mahala, halafu mkapata shida kumnadi." Anauona na kukiri uwezekano wa huyu mtu kuibuka mshindi ndani ya chama chake. Ikatamkwa kuwa kilichopangwa na Mungu mwanadamu hawezi kupangua! Ni kwa sintofahamu hii ya watu wawili hawa CCM na serikali yake havijafanya lolote la kujivunia tangu mwaka 2008!

Rais wangu, kuuawa kwa Azimio la Arusha ndiko kulikosababisha watoto wa maskini kunyimwa elimu ya juu, kwa sababu tu ya umaskini wa wazazi wao; vijana kukosa ajira na kuwafanya baadhi ya viongozi wetu na familia zao kuwa na utajiri wa kutisha, huku umaskini mkubwa na ugumu wa maisha vikiwaandama Watanzania wakati Mungu wao aliwawekea kila aina ya utajiri juu na chini ya ardhi yao!

Kifo cha Azimio la Arusha ndiyo chanzo cha ufisadi uliokithiri serikalini na katika vyombo vyake kuruhusu wezi wetu wa madini na rasilimali za nchi yetu na hivyo kusababisha vurugu na mauaji kama haya ya Mtwara, sehemu mbalimbali za nchi yetu!
Walioliua Azimio la Arusha wana deni kubwa! Majuto, manung'uniko na laana za maskini wa nchi hii vitawashukia wasipotubu. Kuiona mbingu itakuwa ni mashaka kwao!

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere akimtazama Rupia aliyekuwa amekaa chini ya mkungu, alilia kwa uchungu akiita, "Paolo! Paolo! Paolo!" akamgeukia Edward Lowassa akasema: "Na nyinyi wengine, mkiliacha Azimio la Arusha, mtakuja kupata taabu sana baadaye." Na sasa yanatimia!

Naikumbuka vema siku hiyo kwani nilipiga picha na Mwalimu, picha inayonikumbusha machozi ya Baba wa Taifa kila niionapo! Taifa linaambiwa majeruhi wengi zaidi wa vurugu za Mtwara wana risasi za moto katika miili yao! Wananchi wanapigwa risasi kama swala! Ah! Nyerere baba! Uwakumbuke watu wako huko uliko!

Kuuawa kwa Azimio la Arusha kumevifanya vyama vya siasa kuweka masilahi ya chama mbele badala ya wananchama au wananchi kwa ujumla. Fukuto ndani ya vyama sasa, ni kinyang'anyiro cha kugombea madaraka. Viongozi wako ‘bize' kiasi kwamba hakuna tena muda wa kushughulikia matatizo yanayowakabili wanachama au wananchi kwa ujumla.

Taifa linaelekea katika kilindi chenye giza nene!
 
Back
Top Bottom