Mtazamo Wangu

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,810
Kuna mdau kanitmia hii habari nami nimeona si vibaya ku-share nanyi

Mtazamo Wangu: Saleh J


Ndugu zangu na wazawa Watanzania wenzangu naomba kuchukua muda mdogo mtu kuandike machache na nataraji kuna mawili au matatu tutafaidika nayo katika mchango wa kimawazo.
Mwaka wa juzi (2009) miezi ya katikati, kuna jamaa yangu mmoja (jina limehifadhiwa) alinipigia simu kwa kutaka kuniuliza mtazamo wangu juu ya hali ilivyo kuhusu uwanja wa taifa wa Dar es Salaam kwanini hauna wadhamini wa kuweza kuuangalia uwanja huo; na vipi mtazamo wa serikali juu ya jambo hili, ili akatengeneze ripoti na kuirusha katika vyombo vya habari.


Tulianza kuongea kuhusu mada mbalimbali za kijamii ambazo zisizohusiana na siasa na kwa ufupi sana nilizungumzia hoja kuhusu mada ya uwanja wa taifa wa Dar es Salaam na katika mafupi hayo nilisisitiza sana mambo matatu kabla ya kutengenezwa ripoti au habari hiyo:

  1. Kufanya utafiti (survey) ya nguvu kwa jamii na watu wenye mtazamo wa mbali au wenye mtamzamo tofauti juu ya jambo hili ili alijue nje ndani na marefu na mapana yake kabla halijarushwa hewani na kuwafikia jamii.
  2. Kuishirkisha serikali kwa kupitia ubalozi wetu hapa London (wakati huo wa Mhe. Mwanaidi) ili papatikane majibu ya kikamilifu kwa upande wa serikali kwani kunaweza kuwa na sababu kubwa ya uwanja huo kutokuwa na wadhamini (wakati huo), au pengine wadhamini walikuwapo lakini ndio walikuwa wapo katika harakati za ukandarasi na serikali au wizara husika, au pengine kunaweza kuwa na sababu muhimu ambazo zimeifanya aidha wizara au kitengo ambacho kimejishughulisha na uendelezaji wa viwanja vya mpira wa miguu kutohitaji wadhamini.
  3. Kurusha habari au ripoti hiyo pale atakaporidhika yeye kuwa sasa majibu yashapatikana kutoka kwa jamii hususan wenye fani ya mpira miguu, kutoka kwa watu wenye mitazamo mbalimbali na kutoka kwenye vitengo mbalimbali husika; na mwisho, kupima matokeo ya ripoti hiyo itachukuliwa vipi na jamii.
Kwani hakuna kitu hatari kama ujumbe uliotangazwa kwa njia yoyote ile na ukawafikia jamii ambao unaweza ukasababisha migongano na kutokuwa na hali ya usalama katika jamii.
Kwasababu kiujumla, urahisi wa kurusha ujumbe au kutoa habari ni kama kuandika alifu kwa kijiti; na urahisi wa kutoa tangazo au kuamrisha kitu katika halaiki ya watu ni kama kupiga mruzi urahisi wake, lakini ujumbe unapowafikia watu hauwezi tena kurudishwa nyuma na utasambaratika kama moto uliowashwa kwenye bahari ya mafuta ya taa.
Na hatari zaidi, hujui katika kundi la watu hao nani na nani wataichukua habari hiyo kama ilivyoikusudiwa, na nani ataichukua habari hiyo kinyume na ilivyokusudiwa na hata kuipindua habari hiyo na kuitafsiri na kuipeleka kwenye mkondo mwingine na watu kufuata mkondo huo na kusababisha hali ya kutokuwa na usalama.


Bila ya kumnyima Mwandishi wa habari haki zake na uhuru wake, lakini kama Mwandishi huyo ni raia mwema kwa nchi yake, au kama ni Kiongozi, ni Kiongozi mzuri na mwenye kuipenda nchi yake na usalama wa Watanzania wenzake hawezi kufanya kitu au kuandika ripoti au habari ambayo inaweza ikasababisha machafuko katika kijiji, mji au nchi nzima. Mtu huyo haifai nchi yake na hata hafai kutumikia Watanzania wenzake na kila Mtanzania mwenye kuipenda nchi yake kutokana na historia ya nchi yetu inavyojulikana kuwa ni nchi mojawapo yenye usalama na amani duniani, kila Mtanzania mzawa mwenye uchungu na nchi yake itambidi asimame na amwangilie mara mbili-mbili mtu kama huyu bila ya kuangalia anatoka chama gani au anatoka kabila gani au dini yake nini au rangi yake ipi au ni Mwandishi wa gazeti gani (bila ya kumnyima Mwandishi wa habari haki zake na uhuru wake), lakini mtu kama huyo hatufai kumpa madaraka au kuwa kiongozi wa nchi yetu, nchi ambayo hazina yake tumerithishwa tangu enzi ya wazee wetu kama Lulu kwenye chaza yake na chaza yenyewe ndio usalama na tusikubali mtu kutuchukulia usalama wa nchi yetu na hazina yetu kwa njia moja au nyingine.


Kama ni kiongozi au kiongozi mtarajiwa hawezi kusema iko siku atakula kiapo kama kiongozi wa nchi na kuilinda katiba ya nchi wakati katiba hiyo hiyo inasema pamoja na kuwa na uhuru, lakini lazima kuzingatiwa mambo fulani ambayo yako wazi katika katiba yetu katika namba 19 ibara ya 3 “…kwa ajili ya usalama wa jamii, amani katika jamii, maadili ya jamii na umoja wa kitaifa.” Na vilevile, bila ya kusahau namba 147 ibara ya 2. Ikiwa hayo yamekosekana basi mtu huyo anatupeleka pabaya na mtu huyo hatufai katika taifa letu.


Katiba:
Katiba ya Tanzania siyo Daftari La Mazoezi.
Kwanza kabisa nimefurahi kuona kuwa rais wetu Jakaya Mrisho Kikwete katika uongozi wake kachukua hatua ya kuanza sakata hili la kubadilishwa kwa katiba (bonyeza hapa) kwa kuheshimu demokrasia na kwa kusikiliza Wananchi na vilevile kusikiliza Waheshimiwa wa pande tofauti za vyama ikiwemo Chadema (ikiongozwa na Mhe. Freeman Mbowe na Mhe. Wilbroad Slaa), CUF (ikiongozwa na Mhe. Ibrahim Lipumba na Mhe. Maalim Seif) na viongozi wa vyama vingine ambao wanalisisitiza jambo hili liwe.


Wasiwasi wangu ni kuwa jambo hili ikiwa litachukuliwa kwa pupa, kuna hatari ya kuwa na mipasuko na machafuko zaidi huko tunapokwenda.
Sipingi kubadilishwa kwa katiba, lakini hao wanaoendewa mbio katiba hiyo ibadilishwe ambao bila ya shaka ni Wananchi, baadhi yao kama si wengi wao hata mstari mmoja wa katiba hiyo hawajawahi kuiona ingawa serikali imeweka wazi kwenye mtandao (www.sheria.go.tz).
Kinachotisha zaidi, ni kuwa Watanzania wazawa wenzangu wengi ndio wenye kuitaka katiba ibadilishwe bila ya kujua yaliyomo na yepi wanayoyataka kutiwa katika katiba hiyo ili yapatikane hayo mabadiliko na hapa ndipo inapokuja kwa mara ya kwanza maana ya Wengi inabadilika kuwa Wachache.
Kwasababu wasiwasi wangu ni kuwa katiba itakuja kubadilishwa kipupa pupa halafu ije kukaa kwenye intaneti au kwenye madroo ya ofisi na hakutakuwa na mabadiliko yoyote kwa Wananchi wa Watanzania.


Upo na mimi?


Pendekezo Langu:
Pendekezo langu kama tumeamua katiba ibadilishwe, basi hao wanaobadilishiwa ambao ni Wananchi waelimishwe kwa kufanya Warsha na Midahalo ana kwa ana na Wananchi kwa muda maalum na kwa kupitia tume maalum ambao wenye kutoka mikondo tofauti na ambao wamekomaa katika fani hii kwa kuchukua yale yatakayojenga na kuyaacha yenye utata na hata ichukuwe miaka 18 (kumi na nane). Katiba hiyo itakuwa imetengenezwa na Watanzania kwa Watanzania, lakini haraka ya nini?
Tujiulize haraka ya nini baada ya miaka yote hiyo iliyopita na mpaka sasa wengine wanasema kama katiba ni moyo wa nchi, moyo gani una matundu na viraka, si utakufa? Mimi nasema Katiba ya Tanzania siyo Daftari La Mazoezi la kuja kuandikwa na kufutwa kila mwaka.


Midamu serikali ya awamu ya nne imeshaanza kulivalia njuga jambo la katiba na ikaamua ‘ku-invest’ katika jambo hili, basi tufanye mabadiliko ya katiba yetu adhimu ya Tanzania kwa kuhusisha Wananchi mpaka vijijini, iwe ni historia ya mabadiliko ya katiba ambayo dunia haijapata kuona, na hii ndio demokrasia na namshukuru kiongozi wetu rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa radhi na jambo hili na kusikiliza matakwa na kulichukulia jambo hili kwa utaratibu na hekima kabisa.
Samahani ndugu zangu Watanzania wazawa wenzangu kama nimemkosea mtu yoyote basi mtanisamehe na mtaniwia radhi.


Ndugu yenu,


Saleh Jaber


11/01/2011
 
Back
Top Bottom