Msiwakamate Slaa na Mbowe, kamateni roho zao | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Msiwakamate Slaa na Mbowe, kamateni roho zao

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by bagamoyo, Jan 14, 2011.

 1. b

  bagamoyo JF-Expert Member

  #1
  Jan 14, 2011
  Joined: Jan 14, 2010
  Messages: 4,533
  Likes Received: 2,114
  Trophy Points: 280
  Mwandishi :padri Privatus Karugendo wa Gazeti Raiamwema
  12/Januari/2011​

  NINAJUA kwamba Rais Jakaya Kikwete ana washauri wake, hivyo sina haja ya kusema ninamshauri; inawezekana wanamshauri yeye anakataa kuwasikiliza, maana si lazima kufuata kila unachoshauriwa, lakini inawezekana pia kwamba anashauriwa vibaya kwa nia mbaya au kwa bahati mbaya.

  Damu inapoanza kumwagika watu wanapigwa na kuumizwa kiasi cha kukiuka haki za binadamu kumpiga mja mzito na watu kufa, hatuwezi kukaa pembeni na kuangalia yanayotokea kana kwamba tunaishi nchi ya jirani; sote tuna wajibu vinginevyo historia itatuhukumu wakati ukifika na tuna la kusema mbele za Mwenyezi Mungu.

  Kwa vile mimi ni Mtanzania na nina uchungu na Taifa hili, nashindwa kujizuia kutoa ushauri wa bure kwa Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM): Msiwakamate Slaa, Mbowe na wanachama wa CHADEMA; kamateni roho zao.

  Mwili ni mapambo tu kwenye uhai wa mwanadamu. Mwili unakufa na kuzikwa; hivyo kuutesa na kuufanyia mambo ya kinyama kama walivyofanyiwa kule Arusha, ni aibu kubwa kwa mtu yeyote mwenye akili timamu. Kwa nini kupoteza muda na nguvu kushughulikia kitu kinachopita na kukiacha kile cha muhimu kama vile roho?

  Kuwapiga, kuwaua na kuwaweka ndani viongozi wa CHADEMA ni vitendo vya kinyama vinavyofanywa na binadamu asiyefikiri. Maana mtu anayefikiri vizuri hawezi kumpiga binadamu mwenzake kwa nia yoyote ile; ukimpiga unaumiza mwili wake na roho yake inabaki salama, ukimpiga risasi akafa, unakufa mwili, lakini roho yake inabaki salama.

  Hadi leo hii tuna roho za watu waliokufa, wako kaburini lakini roho zao ziko salama na zinaishi miongoni mwetu. Roho ya Baba wa Taifa bado tunaishi nayo; roho ya Mkwawa bado tunaishi nayo, roho za mashujaa wote waliokufa wakitetea heshima na maisha ya Watanzania bado tunaishi nazo; wao walikufa ili sisi tuweze kuishi kwa uhuru na salama. Hivyo hivyo na sisi lazima tufe tukipambana kulinda uhuru na usalama wa vizazi vijavyo, kinyume na hapo tutakufa na miili yetu na roho zetu!

  Tumeshuhudia kwenye vyombo vya habari jinsi watu walivyopigwa kinyama kule Arusha na wengine kupoteza maisha yao. Tunaambiwa kwamba wengine bado wamelazwa hospitalini na wengine wanaomboleza waliokufa. Lakini Viongozi wa CHADEMA walipopelekwa mahakamani, watu walijazana mahakamani bila kuogopa virungu na risasi za polisi.

  Maana yake ni kwamba pale walipopigwa, jana yake walipigwa miili yao na roho hazikuguswa. Nina imani hata kesho CHADEMA wakiitisha maandamano mjini Arusha, watu watajitokeza kwa wingi. Ni kwamba Serikali ya Kikwete, haijafanikiwa kuzishika roho za watu wa Arusha na kuzifunga.

  Sitaki kuamini kwamba Rais Kikwete hakusoma historia. Hakuna popote duniani ambao risasi iliweza kupambana na wananchi. Watawala wote walioshughulika kuitesa miili ya wapinzani wao na wakati mwingine kuwaua, mwisho wao ulikuwa mbaya sana.

  Hoja yangu katika makala hii, ni kulaani kwa nguvu zangu zote vurugu zilizotokea Arusha, watu wakafa, wakapigwa na kudhalilishwa. Tanzania nchi inayojisifu kuwa na Spika wa kwanza mwanamke; itazomewa na kulaaniwa na dunia nzima kwa kitendo cha Polisi kumpiga mama mja mzito aliyekuwa akifanya maandamano ya amani kudai haki za msingi za wananchi. Mama huyu alipigwa akiwa amefunga kitambaa cheupe mkononi kama ishara ya amani. Mbaya zaidi hata pamoja na yeye kuwaambia Polisi, kwamba yeye ni mja mzito waliendelea kumpiga. Pamoja na unyama huo, bado nina imani kwamba roho ya mama huyu hawakuigusa. Ataendeleza mapambano na mtoto atakayezaliwa atakuwa mpambanaji.

  Nalaani pia kuwashika na kuwaweka ndani Dk. Slaa, Freeman na Philemon Ndesamburo. Naishauri waachiwe maana kuwashika ni kazi bure. Wataitesa miili yao, lakini kamwe hawawezi kuzigusa roho zao
  .
  Leo CCM ikitaka kushindana na CHADEMA au Rais Kikwete akitaka kupambana na wapinzani wake, azikamate na kuzifunga roho zao! Kama Rais Kikwete anataka akumbukwe na Watanzania wote baada ya kutoka madarakani basi aanzishe mkakati wa kuzishika roho za Watanzania na kuzifunga. Lakini akiachia utamaduni wa kupiga watu, kuwatesa watu na kumwaga damu uendelee atashindwa kama wengine walivyoshindwa na dunia itamsahau kabisa!

  Viongozi wote waliofanikiwa kuongoza vizuri na kukumbukwa milele yote, ni wale waliofanikiwa kuzikamata na kuzifunga roho za wananchi wao. Mfano mzuri ni wa Mahatma Gandhi. Huyu hakuwa na serikali, hakuwa na jeshi, hakuwa na polisi; lakini kwa vile alifanikiwa kuzishika na kuzifunga roho za Wahindi, walimsikiliza na kumfuata na kuungana kupambana na mkoloni bila kumwaga damu.

  Hawakushika silaha kupambana, walifanya maandamano, waliendesha migomo na kususia bidhaa za Wazungu kama vile nguo na chumvi. Wafuasi wa Mahatma Gandhi, walipigwa na kuumizwa na polisi wa wakoloni, lakini walisonga mbele. Walifungwa na kuwekwa magerezani, lakini walisonga mbele.

  Yeye alikuwa akifungwa usiku na mchana, lakini alisonga mbele kutetea haki na kuleta uhuru wa watu wa India. Daima aliwaambia wafuasi wake, kwamba polisi wa wakoloni watapiga miili yao, lakini hawatazigusa roho zao.

  Filamu inayoonyesha maisha ya Mahatma Gandhi, inaonyesha vizuri kitu ninachojitahidi kuelezea kwenye makala hii.

  Mfano mwingine ni wa Yesu wa Nazareti. Huyu hakuwa na mali, hakuwa na nyumba, hakuwa na serikali, hakuwa na majeshi; lakini kwa vile alifanikiwa kuishika mioyo ya wafuasi wake na kuifunga, walimfuata kila alikokuwa akienda na walikuwa tayari kupoteza maisha yao kwa kufanya kazi yake. Ukiondoa ujambazi ulioingizwa Kanisani na Mfalme Constantine, watu waliingia kwenye imani ya Ukristu kwa mvuto; si risasi na upanga, bali kwa kuvutwa; kwa mtindo wa kuzishika roho na kuzifunga. Bahati mbaya viongozi wa Kanisa waliofuata walishindwa kutengeneza mfumo mzuri wa kulifanya Kanisa liwavute waumini. Dini ya Ukristu ilienezwa kwa upanga na kumwaga damu kinyume kabisa na mafundisho ya Yesu.

  Ingawa mfano wa magaidi si mzuri kuutumia katika makala hii, lakini kwa vile ni kitu kinachotokea kila wakati na sasa hivi nchi zote zimekuwa na mifumo ya kujikinga na magaidi, si vibaya kuutaja hapa. Nina imani wale wanaowaandaa magaidi si kwamba wanawafunga na kuwatesa ili kuwashawishi kukubali kujilipua. Kinachofanyika ni kushika roho zao na kuzifunga. Hata hivyo dunia nzima imekataa kukaa chini magaidi hawa kuongea na hao na kusikiliza matatizo yao. Kufikia hatua ya kujilipua, si kitu cha kudharau, wakisikilizwa mtu atashangaa kugundua kwamba hata magaidi ni watu wanaopigana kwa njia hiyo kutetea uhai wao na uhai wa vizazi vyao.

  Hivyo kwa kiongozi anayetaka kuiongoza Tanzania, afahamu kwamba kuwapiga watu, kuwakamata na kuwafunga au kuwaua si msaada wa kumsaidia kuwaongoza vizuri. Njia hii imetumiwa na wengi na wameshindwa.

  Makaburu wa Afrika ya Kusini walimkamata Nelson Mandela na wenzake wakawatesa na kuwafunga lakini kwa vile hawakufanikiwa kugusa roho wafuasi wao waliendeleza mapambano hadi walipofunguliwa. Makaburu walifikiri kumfunga Mandela ni kumaliza tatizo, kumbe ilikuwa imepandwa na inakua kwa kasi ya kutisha. Pamoja na nguvu za jeshi la Arika ya Kusini, hawakufua dafu mbele za nguvu ya Umma.

  Kuwakamata Dk. Slaa na Mbowe, kutesa miili yao, hakutasaidia chochote kama roho zao zitabaki huru na nguvu ya kutisha; mkiwafungia Arusha, maandamano mengine yatatokea Mwanza, Mbeya, Karagwe, Kigoma na nchi nzima. Hata mkiwakamata wafuasi wa Mwanza na kuwaweka ndani; mkikamata wafuasi wa Sumbawanga na kuwaweka ndani, mkikamata wafuasi wa Dar es Salaam na kuwaweka ndani; wengine watachipukia kwingine. Mbegu ya mabadiliko imepandwa, imeanza kuota na kukua kwa kasi, kuiua kwa risasi na marungu ni ndoto za mchana.

  Arusha yalikuwa maandamano ya kupinga uchaguzi wa Meya, uliofanyika kwa mizengwe. Hivi karibuni yanakuja maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya umeme. Na haya yanaweza kuwa maandamano makubwa kuliko yote tuliyoyazoea. Umeme unagusa maisha ya watu wengi, kuupandisha ni kutaka kufanya maisha yawe magumu zaidi. Inawezekana yakawapo maandamano ya kushinikiza katiba mpya; pamoja na Rais Kikwete, kutoa ahadi ya kuunda Tume ya Katiba, wananchi wanalilia Baraza la Katiba. Inawezekana pia yakawapo maandamano ya vyuo vikuu kushinikiza mikopo na mengine mengi.

  Huwezi kuyazima maandamano yote haya yanayokuja kwa risasi na virungu. Kwani Tanzania tuna risasi ngapi? Tunazo milioni 40? Tuna polisi wangapi? Tunao milioni 40? Watanzania sasa hivi wanakimbilia milioni 40, wakishikamana hakuna la kuwafanya.

  Tumesikia laana kwa CHADEMA kwa kuendesha maandamano ambayo walijua watakutana na upinzani mkali wa polisi. Maandamano awali yaliruhusiwa, amri ya kuyavunja ilitoka Dar es Salaam dakika za mwisho. Hii si Tanzania ya 1945, kwamba watasema dakika za mwisho na watu wasikilize na kufuata amri! Maandamano ni mipango, si kukurupuka, kuna gharama zake kuyafuta gahfla kama ilivyokuwa huko nyuma si jambo rahisi, ilitakiwa polisi iyalinde kwa nguvu zile zile tulizoziona.

  Lakini pia maandamano ni haki ya kila mwananchi. Na niwajuavyo CHADEMA hakukuwa na mpango wa kuvurugika amani kama wanavyodai polisi. Yalikuwa ni maandamano ya amani na kazi ya Polisi ingekuwa kuyaongoza hadi mwisho wake, lakini sasa kinyume ndicho kweli.

  Ingawa vyote vinategemea, mwili na roho, lakini ukweli unabaki hapa hapa kwamba roho ina nguvu lakini mwili ni dhaifu. Basi sisi kama taifa tujishughulishe kutafuta dawa ya kutufanya tuwe watu wa kawaida.
  Source: www.raiamwema.co.tz 12/Januari/2011
   
Loading...