Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,809
- 15,438
Leo nina kisa kimoja very interesting kuhusiana na hilo bango hapo juu.Kwenye miaka ya mwanzoni mwa 1980, nikiwa shule ya msingi alitokea kijana mmoja ambaye alikuwa ni mtupu kabisa darasani. Elimu ya darasani kwa kweli ilimshinda,nadhani alikuwa na tatizo ambalo kitaalamu linajulikana kama dyslexia,(Nilikuja kujua baadaye sana katika tafiti zangu).
Hili ni tatizo la mtoto kushindwa kusoma kabisa au kuwa na uelewa mdogo sana wa masomo, ni tatizo ambalo linahitaji waalimu walioandaliwa katika kuwafundisha watoto wenye tatizo hilo ambapo kama wakifundishwa kwa kutumia mbinu zilizopendekezwa na wataalamu wa saikolojia huja kuwa wasomi wazuri huku mbeleni.
Kwa bahati mbaya sana miaka hiyo mfumo wetu wa elimu ulishindwa kukidhi mahitaji yawatoto wenye matatizo hayo, hata hivyo sijui kama siku hizi mahitaji hayo yametimizwa, sina uhakika na hilo.Huyu kijana aligeuzwa kuwa kama kituko pale darasani na hata waalimu walikuwa walimtolea mfano mbaya kwamba atakuwa na maisha magumu huko mbeleni kwa sababu ya kushindwa kusoma na kuandika wakati huo tukiwa darasa la nne.
Hakuwa ni mtu mwenye furaha kwa sababu pia hakuwa na marafiki na hata familia alimotoka ilikuwa ni ile ya wazazi wakulima vibarua na kuuza mboga pori za majani na kuni ili kumudu kujikimu, na yeye pia alikuwa akiwasaidia wazazi wake kulima vibarua na wakati mwingine alileta ubuyu au ukwaju na kuuza shuleni.
Mara kwa mara alikuwa akirudishwa nyumbani kutokana na kukosa sare za shule na ilikuwa inamchukua muda kupata sare na kurejea shuleni, alizidi kuanguka katika masomo na hakuna aliyeonyesha kujali si waalimu wala wanafunzi wenzie, sana sana tulikuwa tukimcheka kila alipokuwa akipata sifuri kwenye mitihani.
Ilitokea siku moja alipata mchafuko wa tumbo darasani akajisaidia palepale darasani nakujichafua, harufu ya kinyesi ilisambaa darasa zima akawa anatafutwa aliyechafua hali ya hewa na kwa Bahati mbaya mwalimu wa sayansi kimu alikuwepo darasana akifundisha.
Alishindwa kuvumilia hali ile ikamlazimu aulize aliyechafua hali ya hewa ni nani. Wanafunzi waliokuwa naye karibu wakamnyooshea vidole. Kilichotokea ni kwamba yule kijana alitoka mbio huku kinyesi kikidondoka sakafuni na sisi wanafunzi tukatoka mbio kumkimbiza huku tukimzomea.
Hakukimbilia kwao, bali alikimbilia upande ilipo reli na huko aliokota mawe na kuanza kuturushia, ikumbukwe kwamba kwenye reli kunawekwa mawe ili kuzuia reli isididimie ardhini.Tulipoona mashambulizi ya mawe yamezidi tukarudi darasani na kulazimika kusafisha darasana kipindi kikawa kimeisha.Ile ilikuwa ndiyo graduation ya kijana yule kwani alitoweka pale kijijini na hakuna aliyejua kaelekea wapi.
Hata wazazi wake hawakuonekana kujua alipokimbilia na hakuna aliyeonekana kujali.Tulimaliza darasa la saba na kile mtu akandelea na masomo kivyake kwa sababu wakati ule kutokanana uhaba wa shule za serikali kufaulu ilionekana kama vile ni miujiza au bahatinasibu, kwa hiyo wazazi wengi walilazimika kuwapeleka watoto wao shule za sekondari za kulipia.
Miaka ilisonga na maisha yaliendelea. Miaka20 baadaye nikiwa katika utafiti wangu wa tiba mbadala kwa kutumia mitishamba, nilijikuta nikiwa Morogoro vijijini, huko sikuwa na mwenyeji nilipanga tukufikia hata kwa mwenyekiti wa kijiji au katibu kata anipe japo hifadhi kwamuda nifanikishe utafiti wangu. Aliniambia atanipeleka kwa bwana mmoja ambaye angeweza kunipa hifadhi kwa kuwa ana nyumba kubwa.
Nilipofika alinitambulisha kwa jina langu la ukoo, yule bwana akaonekana kushtuka lakini hakusema kitu. Ni kweli yule bwana alionekana kuwa na uwezo pale kijijini, alikuwa na myumba mbili zilizoko karibu, ngombe wa kisasa kadhaa, mashine ya kusaga nafaka na kukoboa inayotumia mafuta, alikuwa na jenereta kubwa na magari mawili, Toyota Canter na Toyota Hilax na pale kwake kulikuwa na duka kubwa la jumla na rejareja akisaidia kuwauzia wafanyabiashara wa pale kijijini na vijiji vya jirani bidhaa.
Ukweli ni kwamba kwa viwango vya pale kijijini alikuwa ni tajiri mkubwa, usiku baada ya kupata mlo wa usiku tulikaa kibarazani kwake kupiga soga kidogo ilikufahamiana zaidi. Alinidadisi sana ninapotoka na alionekana kutabasamu kila nilipokuwa nikimueleza kuhusu kijiji nilipotoka.Baadaye alijitambulisha kwangu kwamba na yeye anatokea kijiji hicho hicho, naalinitajia jina lake halisi, kumbe jina alilokuwa akilitumia ni jina jingine kwa sababu alitoroka pale kijijini na kukimbilia Morogoro.
Alipofika Morogoro alibadilisha jina na kujiita Mikwambe. Na hata bishara zake zilijulikana kwajina hilo.Nilimkumbuka lakini sikusimulia kisa chake cha kujinyea darasani ingawa yeye alikisimulia kwa dhihaka huku tukicheka wote. Alisema kwamba ile kujinyea ndiyo ilikuwa cheti chake cha kumaliza masomo na sasa ameitumia elimu ile ya darasani yakukejeliwa, kudhihakiwa na kudhalilishwa kuonyesha uwezo wake wa kutafuta fedhana sasa ni tajiri pale kijijini.
Kwakifupi tu alinieleza kwamba mtaji wake ulikuwa ni nguvu zake mwenyewe, alianza kulima vibarua baadaye akawa anakodisha ardhi na kulima, akafanikiwa kuvuna mazao mengi kwa takribani misimu minne akafanikiwa kununua ardhi na kujiandikisha kama mwanakijiji na kuanza biasharampaka kufikia hapo alipofikia.
Alinisimulia kwamba wazazi wake walirudi kwao huko sambani na amefanikiwa kuwajengea nyumba nzuri na alifanikiwa kuwasomesha wadogo zake wote na wengine yuko nao pale wakimsaidia shughuli za biashara na wengine wako jijini Dar ni watumishi serikalini nammoja ni daktari hospitali moja ya wilaya mkoa wa Pwani.
Ukweli ni kwamba huyu kijana kwa asili wao walitokea shambani na baba yake alihamia kijijini kwetu Upareni kama manamba kufanya kazi kwenye mashamba ya mkonge ni baada ya zao hilo kukosa umaarufu ndipo baba yake akaanza kulima vibarua kwenye mashamba ya wenyeji pale kijijini ili kujikimu.Tuliongea mengi, lakini kubwa kuliko alitaka kujua wale tuliokuwa tukiongoza darasani wakati ule shuleni tunafanya kazi gani au tunafanya shughuli gani.
Nilimwambiaukweli kuhusu maisha yangu na kazi ninazofanya na nilimweleza kidogo kuhusu wenzanguwengi tuliokuwa vinara darasani kwamba wengi hawana maisha mazuri sana,wachache wameajiriwa kama mimi, wengine wamekuwa madereva wa mabasi na malorina maisha yao bado ni ya kubangaiza, na wengine ni walevi kupindukia tena mmoja ambaye alikuwa ni namba moja mpaka alipofika sekondari bado alikuwa na akili sana, alikuja kufeli kidato cha sita ikawa ndiyo graduation yake ya kuhitimu nakujikita kwenye pombe hadi sasa maisha yake si mazuri.
Alionekanakufurahi kupata habari za kijijini kwetu, alikiri kwamba hakuwahi kurudi pale kijijini zaidi ya kuwatumia wazazi wake fedha na kuwahamishia kijijini kwao huko shambani ambapo aliwajengea nyumba na kuwafungulia biashara pale kijijini kwao.
Kuna mengi ya kujifunza hapa nawakaribisha wenzangu mtoe mawili matatu kutokana na hii simulizi.
Karibuni