Mrema ampongeza Mutungi kusuluhisha CUF

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
MWENYEKITI wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema, amempongeza Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kwa jitihada za kusuluhisha mgogoro wa uongozi uliokuwepo ndani ya Chama cha Wananchi (Cuf).

Amewasihi viongozi wengine wa vyama vyote vya siasa nchini kuzingatia Katiba za vyama vyao, misingi ya demokrasia na sheria za nchi, ili kuepusha na kuondoa migogoro ndani ya vyama au kati ya chama kimoja na kingine.

Amesema hakuna kiongozi wa kisiasa aliyekamilika kwa asilimia 100 kwakuwa , kila mmoja ana udhaifu wake. Mrema alitoa pongezi hizo jana Dar es salaam kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari. Sehemu ya taarifa hiyo ilisema, " TLP inampongeza Msajili na ofisi yake kwa kutatua mgogoro huo kwa kuzingatia sheria za nchi, sheria ya vyama vya siasa na pia, imezingatia misingi ya demokrasia ambayo ni nguzo ya mfumo wa vyama vingi vya siasa".

Alisema chama hicho kinaamini kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haikupendelea upande wowote kama baadhi ya watu wanavyodai, bali imefanya kazi yake kwa kuzingatia sheria ya vyama vya siasa ambayo kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa Msajili na sheria hiyo kukifuta chama chochote cha siasa nchini, endapo kitakwenda kinyume cha sheria hiyo, pamoja na kusuluhisha migogoro.

Alisema kwa vile ofisi ya Msajili imeshatoa maelekezo kwa chama cha Cuf, ni vyema wanachama wote wa chama hicho wakatulia na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na ofisi hiyo, ili kupata suluhisho la kudumu kwa manufaa ya chama chao na kwa manufaa ya taifa.

Alitumia muda huo kuwataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuzingatia Katiba za vyama vyao, misingi ya demokrasia na sheria za nchi ili kuepusha na kuondoa migogoro ndani ya vyama au kati ya chama kimoja na kingine au Serikalini.

“Nasema hivyo kwa sababu wapo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamekuwa mstari wa mbele kumlaumu Rais John Magufuli kwamba anavunja Katiba ya nchi pia, wanadai kwamba anavunja sheria za nchi na misingi ya demokrasia wakati wao wenyewe ndio vinara wakuvunja Katiba za vyama vyao na sheria za nchi pamoja na misingi ya demokrasia,” alisema.

Alitoa mfano chama kimoja cha siasa ambacho kiliendesha vikao vya kitaifa, lakini idadi ya wajumbe wa vikao hivyo haikulingana na uwiano halisi wa idadi ya wanachama wa chama hicho waliokuwepo kwenye pande mbili za muungano.

Mrema alisema kutokana na pongezi hizo wapo watakaosema kwa nini yeye (Mrema) apongeze ilhali alisababisha migogoro ndani ya vyama vya NCCR – Mageuzi na TLP? Akitetea, alisema hakuna kiongozi wa kisiasa aliyekamilika kwa asilimia mia 100, kila kiongozi anaudhaifu wake, lakini hata hivyo hakuwahi kufanya makosa makubwa kama wanayofanya wenzake.

“Sijawahi kuitisha vikao ambavyo idadi ya wajumbe hailingani na uwiano halisi wa wanachama wa chama changu waliopo Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema na kuongeza kuwa hajawahi kubadilisha Katiba ya chama chake kinyemela ili aweze kuendelea kubakia madarakani.

Alimtaka Msajili asikubali kuyumbishwa au kushinikizwa na kikundi chochote kile kwa manufaa au maslahi ya watu fulani, huku akimhimiza kuendelea kulinda sheria ya vyama vya siasa na misingi ya demokrasia na kwamba asisite kukichukulia hatua zinastahili chama chochote kitakachokiuka mambo hayo kama ambavyo ofisi hiyo ilivyopewa mamlaka kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa.


Chanzo: Habarileo
 
Back
Top Bottom