China na nchi za Afrika zimekuwa na uhusiano uliodumu kwa miongo kadhaa, na uhusiano huu unagusa maeneo mbalimbali ikiwemo elimu, biashara na uchumi, sayansi na teknolojia, ujenzi wa miundombinu, kilimo, na maeneo mengine mengi. Kupitia ushirikiano kati ya pande hizo mbili, nchi nyingi za Afrika kwa sasa zinajivunia miundombinu imara na ya kisasa iliyojengwa na China, ikiwemo barabara, reli, viwanja vya ndege na bandari.
Katika sekta ya kilimo, China imekuwa ikipeleka wataalamu wake katika nchi za Afrika ili kuwasaidia kuongeza mavuno ya mazao yao, na pia kufanya kilimo cha kisasa cha kibiashara. Katika sekta hii, China imetambulisha mbegu za aina mbalimbali za kisasa ambazo zinaleta mavuno mengi kwa wakulima, na hivyo kuongeza kipato chao.
Nchini Madagascar, mpunga chotara uliotambulishwa na wataalamu wa kilimo wa China umekuwa mkombozi kwa wakulima wengi, kwanza umesaidia kuongeza mavuno yao, na pili umesaidia kuongeza usalama wa chakula.
Femosoa Rakatondratsara ni mkulima wa mpunga nchini Madagascar. Anasema awali, ardhi yao ilikuwa inatoa mavuno kidogo ya kutosheleza mahitaji yao tu, lakini sasa, kwa mpunga chotara, sio tu wanapata chakula cha kutosha, bali pia wanauza ziada, na kupata fedha za kuwawezesha kununua ardhi zaidi.
Katika kijiji cha Anosiarivo, ambacho ni moja ya vituo vya mpunga chotara, mashamba ya mpunga yanaonekana. Ramboasalama Anolalaina Ratsina, mtaalamu kutoka Wizara ya Kilimo nchini Madagascar, anawaongoza wakulima wa huko katika kumwaga dawa za kuzuia wadudu. Baada ya kupata mafunzo ya upandaji mara mbili mkoani Hunan, katikati ya China, kwa sasa yeye ni mtu muhimu katika kutangaza mpunga chotara.
Anasema ujuzi wake wa kupanda aina hiyo ya mpunga unatokana na wataalamu wa Kichina, na kuongeza kuwa, kwa miaka mingi, wataalamu wa China nchini Madagascar sio tu wametambulisha mbegu zenye ubora, lakini pia wamehamisha uzoefu wao kwa kufanay kazi pamoja na wataalamu wa huko katika mashamba. Hivi sasa, mafundi kama Ratsina wanabadilishana uzoefu wao na wakulima wengine nchini Madagascar.
Mwaka 2017, China ilizindua mradi wa mfano wa mpunga chotara nchini Madagascar, ukiongozwa na Akademia ya Sayansi ya Kilimo ya Hunan na Mbegu za Ufundi wa Juu za Yuan. Mradi huu ulikuwa moja ya vituo 10 vya mfano vya teknolojia ya kilimo, ulioahidiwa katika Jukwaa la kwanza la Ushirikiano kati ya China na Afrika.
Hu Yuefang, mtaalamu wa kilimo kutoka China anasema, wakulima wa nchini Madagascar wanategemea huruma ya asili. Mbegu duni, ujuzi mdogo, na miundombinu duni imewafanya wakulima wengi kushindwa kulima mazao ya kuwatosheleza kwa chakula. Anasema changamoto ya kwanza katika kutambulisha mpunga chotara ilikuwa ni kuchagua mbegu sahihi. Ili kutambua aina zinazoendana na hali ya hewa na ardhi ya Madagascar, yeye pamoja na timu yake walibeba sampuli nyingi za mbegu kutoka karibu kila eneo linalolima mpunga katika nchi hiyo, na hatimaye kuendeleza aina tano zinazoendana na mazingira ya huko zinazoweza kutoa mazao mengi, kustahamili ukame na mafuriko.
Hivi sasa, kilimo cha mpunga chotara nchini Madagascar kimefikia jumla ya ekari 90,000, huku mavuno yakiwa ni tani 7.5 kwa eka moja, ikiwa ni mara mbili ama tatu zaidi ya aina za kawaida za mpunga, na kuifanya kuwa nchi inayozalisha mpunga mwingi chotara barani Afrika kwa eneo.