SEHEMU YA 58
Watanzania wengi waliopenda umbeya muda huo walitaka kukesha kama popo, walikuwa wakilijadili jambo hilo kwa mapana zaidi kwani kwa kile kilichokuwa kimetokea, kiliwaumiza kwa sababu tu huyo Violeth alikuwa mwanamke aliyetulia na kujiheshimu ambaye hakutaka kufuatilia maisha ya mtu yeyote yule.
Muda huohuo Theo alikuwa hotelini akiendelea kula raha na Iyanya, moyo wake ulikuwa na furaha kubwa, kila alipomwangalia msichana huyo, kwa jinsi alivyoumbika na kiwowowo chake cha kizushi kikamchanganya zaidi.
Ilipofika majira ya saa sita usiku, wakamaliza hivyo kukaa kitandani na kuanza kupiga stori.
Mwanaume huyo alimwambia Iyanya ukweli wa moyo wake kwamba alimpenda, hakukuwa na mwanamke zaidi yake, alimpenda zaidi ya mke wake, alimpenda zaidi ya mtu yeyote yule katika dunia hii.
“Why don’t you divorce your wife and marry me?” (kwa nini usimpe talaka mkeo na unioe mimi?) aliuliza Iyanya.
“No! It that won’t happen,” (hapana! Hilo haliwezi kutokea)
“Then you don’t love me,” (basi hunipendi)
“I love you Iyanya! I really love you,” (nakupenda Iyanya! Nakupenda mno)
“Why don’t you want to diveorce your wife for me?” (kwa nini hutaki kumpa talaka mkeo kwa ajili yangu?) aliuliza msichana huyo.
“We are christians! Things don’t work that way.” (sisi ni Wakristo! Mambo hayafanywi hivyo) alisema Theo huku akimwangalia msichana huyo.
Akamsogelea na kumkumbatia. Alimwambia kwamba hata kama hatompa talaka mkewe bado angempenda mpaka kifo chake na kusingekuwa na kitu chochote kile ambacho kingemtenganisha kutoka katika ufalme wake.
Maneno hayo yakamfanya Iyanya kumpenda zaidi Theo, alijiona kuwa na thamani kubwa, mzuri hata zaidi ya Violeth ambaye muda huo alikuwa hospitalini akimuuguza mtoto wake.
Wakati wakijiandaa kulala ndipo simu ya Theo ikaanza kuita, akaangalia jina, alikuwa meneja wake. Hakutaka kuipokea lakini akaona siyo tatizo, alitakiwa kumdanganya kwamba alikuwa na mkewe hivyo ili hata kama alihitaji kumwambia amfuate, asitoke.