Moto wateketeza maduka 200 sokoni jijini Mbeya

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
40,860
30,273

mwanjelwa(2).jpg

Vijana wakikimbia kuokoa baadhi ya bidhaa zilizokuwemo kwenye mabanda yao yaliyomo katika soko la Mwanjelwa lililopo eneo la Sido Jijini Mbeya ambalo lilikiteketea kwa moto jana asubuhi.


Moto mkubwa umezuka katika soko la Mwanjelwa lililopo eneo la Sido, Jijini Mbeya na kuteketeza vibanda vya maduka zaidi 200, pamoja na mali nyingine za wafanyabiashara na kusababisha hasara kubwa ya mamilioni ya fedha.

Watu walioshuhudia tukio hilo, wamesema moto huo ulianza jana majira ya saa 3:15 asubuhi na kusambaa kwa kasi katika vibanda vya wafanyabiashara, hali iliyowaweka katika wakati mgumu askari wa Kikosi cha Zimamoto walioshindwa kuudhibiti moto huo mkubwa.

Askari wa Kikosi cha Zimamoto waliowahi kufika katika eneo la tukio wakiwa na magari mawili, lakini walishindwa kuufikia moto huo ambao ulianzia katikati ya soko kutokana na

miundombinu mibovu ya barabara ambayo hairuhusu gari kuingia ndani ya soko.
Aidha, shughuli za uokoaji wa mali ziliingia dosari, baada ya askari wa Jeshi la Polisi waliochelewa kufika katika eneo la tukio kuamua kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya vibaka

waliokuwa wameanza kuvamia maduka ya wafanyabiashara na kupora mali.
Baadhi ya watu waliozungumza na NIPASHE kwenye eneo la tukio, wamelaani kitendo cha Polisi kufyatua mabomu ya machozi kwa kuwa kilisababisha hata waliokuwa wakiokoa mali zao kushindwa kuendelea na kazi hiyo, badala yake

kukimbia ovyo ili kujihami na moshi wa mabomu ambao unawasha machoni.
David Mwakisole, alisema alishindwa kuingia ndani ya kibanda chake kwa ajili ya kuokoa mali, baada ya askari kuwasili na kurusha mabomu ambayo yalisababisha kuwepo kwa moshi unaowasha machoni jirani na kibanda chake.

”Mali yangu imeungua na kuteketea yote ndani ya kibanda, nilikuwa na uwezo wa kuokoa mali japo kidogo, lakini mabomu ya hawa askari yamenifanya nishindwe kabisa kutoa vitu ndani ya kibanda,” alisema Mwakisole.
Aidha, askari Polisi pia walifika na kikosi cha mbwa ambao walikuwa wakitumika kutimua watu wasisogee karibu na mabanda yaliyokuwa yakiungua moto, hali ambayo baadaye ilisababisha eneo zima la tukio kugeuka uwanja wa vita baada ya vijana kuanza kurushiana mawe na askari.

Hali ilipokuwa mbaya zaidi, ilibidi askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokuwa wakiongozwa na askari wachache wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuingilia kati na kusaidia kurejesha amani katika eneo hilo.
Vurugu hizo zilisababisha watu kadhaa kujeruhiwa kwa mawe yaliyokuwa yakivurumishwa na vijana pamoja na kupigwa na askari wa JKT na wengine kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa matibabu.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Anaclet Malindisa, alisema moto huo ni mkubwa ambao haujawahi kutokea jijini Mbeya na kwamba umesababisha uharibifu mkubwa wa mali za wafanyabiashara wa eneo hilo.
Alisema Jeshi la Polisi limejitahidi kulinda amani katika eneo hilo na vurugu zilizotokea zilisababishwa na vijana waliokuwa wakikaidi amri halali ya Polisi ya kuwataka waondoke kwenye eneo hilo kwa sababu za usalama.

”Sisi tulikuwa tunachukua tahadhari kwa kuwa kama moto ungefika pale kwenye kituo cha mafuta, kungeweza kutokea maafa makubwa sana, lakini vijana walikaidi amri ya kuondoka na ndio sababu Polisi ikaamua kuwaondoa kwa nguvu,” alisema Malindisa.
Alisema pamoja na vurugu, hakuna mtu aliyepoteza maisha na kuwa hadi wakati akizungumza na NIPASHE, alikuwa hajapata taarifa za

kuwepo kwa mtu yeyote aliyeumizwa au kujeruhiwa na moto huo.
Alisema thamani ya mali na hasara iliyosababishwa na moto huo pamoja na chanzo chake bado havijafahamika na kuwa Jeshi la Polisi litafanya uchunguzi baada ya kazi ya kuzima moto huo itakapokamilika.

NIPASHE ilipokwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambako walikuwa wakipelekwa watu walioathirika kwa moto huo, ilielezwa na Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Humphrey Kiweru, kuwa alikuwa amepokea majeruhi watatu kutoka eneo la tukio.
Dk. Humphrey alisema majeruhi hao walikuwa wanapatiwa matibabu na kwamba wakati huo asingeweza kutoa taarifa zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Evance Balama, alisema tukio hilo ni kubwa na la kusikitisha, ambalo limesababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara.

Hata hivyo, alisema tukio la moto pamoja na vurugu zilizotokea visihusishwe na siasa kwa kuwa moto umetokea kwa bahati mbaya na vurugu hizo zinatokana na Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wake hawafi kwa janga ambalo lingetokea kama moto huo ungefika kwenye kituo cha mafuta kilicho jirani.
Hili ni soko la tatu kuungua jijini Mbeya. Desemba 2006, Soko Kuu la Mwanjelwa ambalo wafanyabiashara hao walikuwa wakifanyia biashara kabla ya kuhamishiwa eneo la Sido liliteketea kwa moto na Desemba mwaka jana, Soko Kuu la Uhindini pia liliteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabishara.

CHANZO: NIPASHE

 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom