Mlio wa risasi harusini

Mlio wa risasi harusini

Konzo Ikweta

JF-Expert Member
Joined
Oct 3, 2013
Posts
745
Reaction score
1,504
Na Robert Heriel

Alijitazama kwenye kioo kikubwa cha kabati akiwa chumbani kwake. Kila alipojitazama hakuona kasoro yoyote katika mwili wake. Aligeuka huku na huku akiendelea kujitazama. Macho yake yalimuambia yeye ni mrembo.

Ni kweli Wala macho yake wala hayakumdanganya. Ismaiya alikuwa mwanamke aliyeumbwa akaumbika. Ninaweza kusema alikuwa ni moja ya wanawake wazuri kuwahi tokea katika dunia hii.

Alikuwa na urefu wa futi sita kamili. Mwenye umbo matata ambalo lililaza na kulewesha mioyo ya kila mwanaume aliyebahatika kumuona. Uso wake wenye macho makubwa kiasi yaliyolegea yalizidisha maradufu uzuri wake. Pua iliyochongoka huku chini yake ikipokelewa na midomo minene kiasi ilizidi kumpa point muhimu katika urembo wake.

Kichwani alikuwa na nywele fupi zilizokatwa kwa ustadi mkubwa huku masikioni kukiwa na herini kubwa za duara. Kifua chake laini kilibeba maziwa madogo kiasi. Kiuno chake chembamba kilichoshikilia Makalio makubwa yenye Nyonga nene kiasi yalitesa kile kiguo alichokuwa amevaa. Huku mapaja yake laini yakimeta meta mithili ya bilauri ya Dhahabu.

Huyo ndiye Ismaiya Binti Ndosi. Mwanamke mwenye uzuri usiosemeka. Rangi yake ya kahawia alimaarufu kama maji ya kunde ilikoleza uzuri wake.

Pamoja na uzuri wote huo lakini Ismaiya hakuamini kabisa kwamba Rafiki yake Adele angeweza kumnyang'anya Mchumba wake. Sasa aliuona uzuri wake sio kitu tena. Alijilinganisha na Adele ambaye hakumfikia kwa lolote lile. Alimzidi kwa kila kitu.

Ismaiya bado akiwa kwenye lindi la mawazo alijiuliza. Ni kipi haswa Adele ananizidi. Alijiuliza huku uso wake ukitazamana na taswira yake iliyokuwa kwenye kioo.

"Au Adele ananizidi mambo ya kitandani" Alijiuliza akiangalia mapaja yake yaliyokuwa yamenona haswa.

Basi kama kuna jambo ambalo Adele alibobea ni suala la Kummudu Mwanaume kitandani. Adele alikuwa fundi msanifu wa masuala ya kitandani. Alijua ni vipi ammiliki mwanaume yeyote yule. Adele alikuwa na kipaji cha kukata mauno katika mkao wowote ule jambo ambalo wanawake wengi huwashinda. Kama hiyo haitoshi Adele alifuzu Mafunzo ya kumdumaza mwanaume akili kwa kumpa mahaba na kumdekeza.

Ismaiya alijua fika kuwa Adele kamzidi mbali sana katika suala la kummudu mwanaume kitandani.

Alijibwaga katika kitanda kama mzigo. Alikuwa amechoka. Katika chumba cha Ismaiya kulikuwa na Kabati kubwa lenye kioo. Karibu na kitanda kulikuwa na dressing table iliyosheheni Vipodozi na mafuta ya kila namna. Chini lilikuwepo zulia la manyoya. Kilikuwa chumba lilichobeba Choo na Bafu.

Ismaiya aliiangalia Saa ya ukutani iliyoonyesha ni saa mbili kasoro. Aliichukua tena ile kadi iliyokuwa kwenye dressing table. Aliitazama Kama mtu ambaye haamini. Alisoma majina tena yaliyokuwa kwenye Kadi. Majina yalikuwa yale yale Adele Kisena na Robert Gabriel. Aliposoma jina la mchumba wake kipenzi Robert alijikuta akitoa machozi.

Alikuwa akimpenda Sana. Robert alikuwa mwanaume ambaye aliuteka moyo wake sawia. Hakuwahi kufikiri kuwa siku moja ataachana na Robert. Hata hicho kifo chenyewe aliahidi kupigana nacho kama kingekuja kumchukua kipenzi chake. Kama alikuwa tayari kupambana na kifo sembuse mwendawazimu mmoja aitwaye Adele. Alitaka kumuonyesha Adele kuwa yeye sio mwanamke wa kuchezewa. Alitaka kumtumia Adele kama mfano kwa Wanawake wengine wenye tabia za kuiba waume na wachumba za watu.

Alinyanyuka na kuvaa nguo zake. Alishika simu yake na kubonyeza bonyeza kisha akaweka sikioni.
"Ndio natoka nyumbani" Ismaiya aliongea na mtu aliyeupande wa pili kisha akakata simu.

Kama kawaida yake alikuwa amependeza mno. Alivalia suruali nyekundu iliyochora umbo lake kikamilifu. Juu alibalia blauzi ya maua ua iliyoachia sehemu kubwa ya kifua chake ambapo kulikuwepo mkufu wa dhahabu aliouvaa shingoni. Huyo ndiye Ismaiya bhana. Binti ambaye kama angegombea umiss dunia angeshinda bila kupingwa.

****--******

Msafara wa magari ya harusi uliowabeba Adele na Robert ulikuwa upo njiani kuelekea ulipo ukumbi wa harusi. Ulikuwa msafara wa aina yake kutokana na Uwepo wa magari Mengi ya gharama. Magari hayo yaliongozwa na Polisi wa Barabarani ambaye alisimamisha magari ya watu wengine wasiohusika na harusi ile.

"pipipi..pipipi..pipipi..!" Ilikuwa ni honi ya magari yaliyotoa mlio unaofahamika kama harusi. Wapita njia walisimama kushangaa msafara huo wa aina yake. Baadhi ya watu waliacha shughuli zao ili waangalie msafara wa harusi ya Adele na Robert. Baadhi ya Watu wengine walikuwa wapo madirishani wakiangalia tukio hilo lililoibua msisimuko mkubwa kwa kila mtaa ulipopita.

Adele alifarajika sana kuona mpango wake wa kuoana na Robert umekamilika. Alichungulia dirishani akiwa ndani ya gari akaona jinsi watu walivyokuwa wakiutazama msafara wa magari ya harusi yake. Aliachia tabasamu jepesi huku akijisifu na kuona fahari kwa siku ile.

Alimkumba Rafiki yake Ismaiya aliyemuibia Mchumba wake. Alikumbuka siku ya kwanza kukutana chuoni wakiwa mwaka wa kwanza. Alikumbuka siku Ismaiya alivyokuja kwa mara ya kwanza na Robert ambapo alipomuona tuu Robert moyo wake ulimpasuka. Tokea siku ile aliapia asingeweza kumuachia Robert, Rafiki yake Ismaiya.

Mawazo ya Adele yalikatishwa na Mlango wa Gari alilolipanda kufunguliwa. Tayari walikuwa wamefika ukumbini. Alijiweka sawa akisubiri maelekezo ya namna atakavyotoka.

Ukumbi ulikuwa umepambwa ukapambika. Watu walikuwa wamefurika wakiwa wamependeza sana. Mbele alisimama Mshehereshaji ambapo kushoto kwake kulikuwa na Dj aliyekuwa akiweka miziki kuhakikisha tukio lile linavutia zaidi. Maputo yaliranda randa na Mapovu yenye rangi za kupendeza ya shampoo yalikuwa hewani.

Bibi harusi aliingia akiwa na Bwana harusi kwenye lango kuu. Macho yote yaligeuka nyuma kuwatazama. Hakuna ambaye hakuona kuwa Bibi harusi na Bwana harusi walipendeza. Adele mara kwa mara alikuwa akitazama huku na huko tofauti na ilivyotarajiwa. Kwa kawaida Bibi harusi huinamisha uso wake chini akitembea mwendo kama wa kobe mzee lakini hii ilikuwa tofauti kwa Adele. Yeye alikuwa akiangalia huku na huko kama mtu anayekagua jambo fulani.

Robert alikuwa ameangalia mbele kama askari anayekaguliwa na amiri jeshi Mkuu.

Walifika na kupokelewa na Washenga wao. Hatimaye walifika katika sehemu zao walizoandaliwa. Ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe na chereko wakiwapongeza. Wakati wengine wakiwapongeza Washenga walikuwa wanakazi ya kuwafuta jasho maharusi. Washenga waliijua kazi yao vyema. Waliwahudumia maharusi kikamilifu.

Maharusi walikaa kwenye viti vyao. Adele alimuuliza mshenga wake.
" Usalama upo Ramla?"
"Kila kitu kipo kama tulivyopanga"
Ramla ambaye ndiye mshenga wa Adele alijibu huku akimfuta jasho kwenye uso.
"Vizuri.. Yule Malaya sijui huko yupo katika hali gani?"
Adele aliongea kwa sauti ya chini.
Hata hivyo Ramla hakumjibu.

Harusi iliendelea lakini jambo ambalo Adele hakulitegemea lilijitokeza. Adele moyo wake ulilipuka kwa hofu. Alipoteza utulivu. Ni kama hakuwa na uhakika na kile alichokiona.

Alishangaa kuona Mshenga wake akiwa kavaa saa ya Ismaiya. Iweje Ramla avae Saa ya Ismaiya. Aliitazama kwa umakini akajiridhisha kabisa ilikuwa ni Ile ile Saa ya Ismaiya waliyonunua wote Pale Mlimani City.

Adele akili ikamzunguka. Hofu ikamkumbatia. Alihisi kuna mchezo hauelewi. Akimtazama Ramla ambaye alikuwa akitazama walipo watu huku akiwa kwenye lindi la mawazo.

Punde Ramla alimgeukia Adele hali iliyomfanya Ashtuke.
Wote walitabasamu na Ramla akamfuta Jasho Adele.

Kitendo cha Ramla kucheka kilimtia hofu Adele. Adele aligundua jambo ambalo liliipindua akili yake. Aliona Mwanya kwenye Kinywa cha Ramla. Ramla hakuwa na Mwanya. Adele alikuwa akiwaza. Marafiki zake wote hawana mwanya isipokuwa Ismaiya.
Hapo hapo aligundua kuwa yule sio Ramla bali ni Ismaiya. Hakuamini kuwa jambo lile lingeweza kutokea. Alianza kumuogopa Ismaiya. Alijiuliza ni kwa kivipi Ismaiya acheze mchezo mgumu kama ule.

Hata hivyo alijiuliza kama huyu sio Ramla. Je Ramla yupo wapi?

Akiwaza na kuwazua huku moyo wake ukipoteza utulivu alishtuka kumuona Ramla halisi akiingia mlangoni akiwa kavaa nguo zake kawaida. Moyo ulimlipuka. Alihisi kijasho kikimtoka. Ni kama presha ilimpanda.

Aligeuka kumtazama Mshenga wake ambaye hapo mwanzo alijua ni Ramla kumbe siye bali ni Ismaiya.

Ismaiya alitabasamu.
"Game ndio imeanza Bibi harusi"
Ismaiya aliongea kwa sauti ya chini akimtazama Adele. Adele bado alikuwa ametekewa huku akihisi kuchanganyikiwa.

Nini kitafuata...
Simulizi linakwendwa kwa jina MLIO WA RISASI HARUSINI.

Tuombe uzima. Itaendelea panapo majaliwa

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
 
Kuna watu wanatukana humu Moderator wape ban. Bado nina hasira na ban mliyonipa juzi
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom