MKURUGENZI MALINYI ATOA MIL 53 KWA AJILI YA VIJANA NA WANAWAKE

acer

JF-Expert Member
Apr 4, 2012
1,595
142
*_WANAWAKE, VIJANA MALINYI WAULA_*

*Halmashauri yawapatia Sh milioni 53 kutoka mapato yake ya ndani*

Na Mwandishi Wetu, Malinyi

HALMASHAURI ya Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro imetoa Sh milioni 53 kutoka katika mapato yake ya ndani ili kuyawezesha makundi ya wanawake na vijana kujikwamua kiuchumi.

Aidha halmashauri hiyo pia imetoa Sh milioni 36 kama asilimia 20 ya mapato ya ndani inayotakiwa kurudi vijijini kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Marcelin Ndimbwa alikabidhi fedha hizo kwa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo Nassoro Rashid na Msaidizi wake Silvia Samwel kwa niaba ya Baraza la Halmashauri hiyo.

Hatua hiyo imekuja kufuatia mpango kabambe uliowekwa na Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi wa kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo pamoja na mambo mengine inaziagiza halmashauri kutoa asilimia 20 ya mapato yake kusaidia wanawake na vijana kujikwamua kutoka uchumi wa chini kwenda wa kati.

Mkurugenzi Ndimbwa akizungumza katika tukio hilo alisema ; “Hatuwezi kusubiri ruzuku kutoka serikalini, tumeamua kutoa mitaji kutoka katika mapato yetu ya ndani, mpaka sasa tumeshaviwezesha vikundi 21.”

Alisema mbali ya fedha hizo, pia halmashauri hiyo imetoa Sh milioni 36 ambayo ni asilimia 20 ya mapato ya ndani inayopaswa kurudi vijijini kwa ajili ya miradi ya maendeleo vijijini hatua ambayo alisema itaharakisha katika kutatua kero za wananchi.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Nasoro Liguguda akizungumzia hilo alisema kiasi hicho cha fedha kilichotolewa ni kati ya Sh milioni 170 zilizotengwa na halmashauri hiyo kutoka katika mapato yake ya ndani kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 ili kuwasaidia wanawake na vijana.

“Tumeamua kutoa fedha hizo ili kuwawezesha akina mama na vijana kutoka katika mapato yetu ya ndani, pia katika vikundi vitatu vinavyojihusisha na kilimo ndani ya mradi wetu wa umwagiliaji tumewasaidia kuwapa mbegu bure na kuwapa baadhi ya pembejeo.

“Lazima tumuunge mkono Rais wetu (John Magufuli) katika kuhakikisha tunatokomeza umasikini katika Wilaya yetu ya Malinyi,” alisema Liguguda.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika Juma Mtego alishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli kwa kutilia mkazo agizo la halmashauri kutoa fedha za mikopo kwa wanawake na vijana.

“Tunashukuru kwa kupewa fedha hizi kwani haijawahi kutokea kwa vikundi vyetu kupata mikopo. Miaka yote tulikuwa tumezoea kupewa ahadi na wenye fedha ndio waliokuwa wananufaika na mikopo ya serikali lakini sio sisi watu masikini,” alisema Mtego.

*Source* _Habari Leo_ 03/12/2016
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom