MKASA wa kweli uliomkuta Marijani Rajabu Almaarufu Jabali la Muziki Alivyompatia nauli mdada wa Kisukuma huko Mwanza ili aje Dar lakini hakutokea!

Uzalendo wa Kitanzania

JF-Expert Member
Mar 8, 2020
2,207
4,702
Naam. Jabali la muziki Marijani Rajabu aliachwa kwenye mataa na mwanamke mchana kweupee barabara ya Uhuru Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Kwa lugha ya mjini iliyotoholewa kutoka kwa mkasa kama huu uliomkuta marehemu Nico Zengekala basi mzee wetu Marijani Rajabu nae alikua ameachwa Solemba!!

Ilikuwaje hadi Jabali la Muziki kutumbukia kwenye fadhaa hiyo?

Jabali la Muziki na kikosi chake walitembelea Mwanza. Akiwa huko Mwanza ndipo Jabali akapata bahati ya kukutana na Mwana mama mmoja jina lake Aisha. Aisha alikua Aisha kweli hata Mwanameka kasingiziwa. Hata Mayasa hakufua dafu.

Kwa vijana wa kileo au kwa lugha za vijana Aisha alikua "Twiga" au "Mnyama". Wazee waliozoea vya kunyonga badala ya vya kuchinja wao huita "mvinje".

Basi ndio tuseme Aisha alikua mvinje,mwanamke wa shoka! Aisha alikua ana macho ya golori, shingo la upanga, na miguu ya chupa.

Kama aliteremshwa kutoka mbinguni au aliumbwa kwa kuzaliwa Kama binadamu wengine Hilo halikumhusu Jabali.

Kwa nyota yake na umaarufu wake Jabali alikua tayari kwa lolote hata kama Aisha angekua keshaolewa. Ndio eeh! Si nzi hufia kwenye kidonda? Kama ingebidi hata kufa Jabali alikua tayari lakini sio kumkosa Aisha.

Mwanaume yoyote mgeni angekutana na Aisha uso kwa uso lazima angepoteza "network". Hivyo Jabali hakuwa tayari kusikiliza la muadhini wala mnadi swala.

Kwa hali ya kawaida hivi wanaume wa Mwanza wangekua wazembe kiasi gani hata wamwache msichana kama Aisha au bachela.

Hivyo Aisha alikua na mshikaji au washikaji. Ilikua siri yake kama alikua mmoja au zaidi ya mmoja. Lakini nae aliingiwa na tamaa ya kuwa na mtu maarufu. Jabali hakua mtu mdogo. Alikua ni mtu ambaye jina lake lilikata anga na kuenea kila kona ya nchi na dunia. Aisha akashikwa na kisebusebu na kiroho kikiwa papo.

Akaona kwake pia ni fursa pengine ya kuzidi kuwa mtu maarufu kwa kuwa na Jabali. Hivyo Marijani alivyopanga karata zake vizuri na kutupa ndoano Aisha akala chambo na kunasa.

Aisha akakubali ombi la Jabali kwa mikono miwili. Ungeweza kusema hata na miguu miwili pia maana alionesha furaha na bashasha isiyo kifani ingawa rohoni alikua na kiroho au dukuduku hasa kwa simulizi mbalimbali za kusikia zingine zikitaja wanamuziki kuwa ni wahuni nk.

Hata hivyo mbele ya Jabali alijikuta akikubali kila kitu. Jabali akajipongeza kwa kuopoa "chuma cha nguvu" akaweka mategemeo ya "kumaliza mpira" siku tu Aisha atakapofika Dar es Salaam.

Kwa kuwa Jabali hakua na muda mrefu Mwanza wakakubaliana wiki mbili zinazofuata Aisha asafiri hadi Dar es Salaam wakamilishe furaha ya penzi jipya.

Basi Jabali mzee wa watu akajikung'uta akiba yote ya matumizi binafsi aliyokua nayo mfukoni akampa Aisha kwa ajili ya kufanya nauli ya kuendea Dar es Salaam akampa na hela za matumizi yake binafsi.

Wakakubaliana Aisha akifika na kuteremka Mnazi Mmoja achukue tax hadi hotel ya Keys (Keys Hotel) iliyoko barabara ya Uhuru Kariakoo ambako ingekua rahisi Jabali kufika na kumuona kirahisi.

Hivyo Jabali akaondoka na kurudi Dar. Ilipofika siku ya ahadi ya Aisha kufika Dar, Jabali akiwa na shauku zote alijikokota na tumbo lake hadi hotel ya Keys akiwa kaulamba kiujana na suruali na shati vimepigwa pasi na kunyooka sawasawa!

Kwa mkwara au kutaka ujiko nae akachukua tax kuingia nayo pale wakati hakua mbali na ilipo hoteli. Lengo likiwa kutaka kumkoga Aisha kama angemkuta ametangulia kufika na kumsubiri ili amuone akiteremka na usafiri (tax lenye kibatari juu) ili Aisha azidi kumuona yeye Jabali ni bab kubwa na mtu wa mjini haswa.

Kama Marehemu Nico Zengekala alivyochomwa na jua toka asubuhi basi na yeye Jabali ndivyo ilivyomtokea.

Hakumkuta Aisha wala kivuli cha Aisha. Akauliza wahudumu pale na hata kuzungu kila kona ya hoteli hakumuona Aisha wake.

Vijana wanasema Jabali alikua amejiandaa "kuua" siku hiyo hasa jinsi Aisha alivyokua na umbile la kutamanisha. Basi Jabali akabaki na tamaa zake moyoni. Moyo ukafifia kila masaa yalivyozidi kwenda hadi jua likazama na giza kuingia ikawa usiku wa giza Totoro Aisha haonekani na wakati huo hakuna simu.

Jabali akili zikamzungua wakati mwingine zikimpa fikra labda Aisha aliwahi kufika mapema zaidi kabla yake isije kuwa mijanaume ya mjini ilimuona na "kumfaulisha" haraka haraka.

Akapiga moyo konde n kuamua tena kupanga arudi siku ya pili yake.

Kesho yake Jabali hakukata tamaa. Alifika tena pale Keys hotel tena alidamka mapema zaidi labda angebahatisha kumkuta Aisha maana ahadi yao ilikua ya uhakika na nauli alimpa.

Siku hiyo nayo ikapuyanga hadi jua likazama hola! Akili za Jabali sasa zikaamua kuwa Aisha amecheza mchezo mbaya wa udanganyifu. Akili zingine zikawa zinamwambia labda atakua amepata dharura.

Bahati mbaya zaidi ilikua maongezi ya kukutana barabarani juu kwa juu hakuwahi hata kujua Aisha alikua akiishi mtaa gani au nyumba gani huko Mwanza labda angeweza kufunga safari ya kurudi kumtafuta.

Marijani akaondoka hapo Keys hotel na kurudi nyumbani akiwa amenywea kama kuku aliyenyeshewa na mvua.

Hakusubiri hata wiki ipite au mwezi kichwa kikawaka moto akaamua kumtungia wimbo aliamini popote alipo Aisha ujumbe utamfikia.


Akjitahidi sana kuficha ghadhabu zake na kutoweka zaidi lawama mbele. Aliweka akiba pengine Aisha baada ya kusikia kilio chake hicho angeweza kurudisha moyo nyuma na kuja kutimiza ahadi.

Huyo dada Aisha inasemekana hadi miaka ya karibuni alikua akiishi nchini Marekani na anakadiriwa kuwa umri wa takribani miaka 60 au zaidi sasa.

*Ooh Mpenzi Aisha Masikini Jabali aliingia choo Cha like!!!

Inaendelea Part 6

(C) Sir. Katanga@2021
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom