Mkasa wa kweli: Sitasahau nilipogeuzwa paka

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,451
65a80e661d5e2f4a00d43cc2ce914987.jpg

SEHEMU YA 01
Kweli maisha ni safari ndefu. Kama ilivyo safari ndefu yoyote ile, ina milima, mabonde, mbuga na misitu. Na waswahili wana msemo usemao "Kabla hujafa hujaumbika".Leo unaweza kujiona uko kamili lakini kesho au keshokutwa ukawa mlemavu wa aina yoyote ile.
Lakini kama ulemavu unaweza kuwa jambo la kumshangaza mwanadamu, ingawa tumezoea kuwaona walemavu kila siku, inakuwaje pale binaadamu anapobadilika umbile lake na kuwa na umbo la mnyama, mnyama kabisa asiyeweza kusema chochote na mwenye miguu minne na mkia!
Bila shaka hilo litakuwa ni la kushangaza zaidi lakini ndilo lililonitokea mimi. Amini usiamini niligeuka paka na niliiishi kama paka kwa siku kadhaa. Na hapo ndipo nilipojua adha wanazopata wanyama kutoka kwa binaadamu na pia ndipo nilipojua kuwa uchawi upo na laana zipo.
Ilikuwa wapi na lini? sasa fumbua macho yako uanze kutiririka katika kisa hiki ambacho nina hakika hutakisahau maishani mwako.
Jina langu ni Rajab Mgosingwa. Hilo jina Mgosingwa nilipachikwa na watu kwa sababu neno hilo linatumika katika kabila langu la Kizigua kumaanisha "Mtu mwanamume" kwa hiyo kwa vile nilikuwa mzigua na rafiki zangu wakanipachika jina hilo la Mgosingwa. Lakini mwenyewe nililikatisha na kujiita Mgosi ambalo nalo kwa kabila la Kibondei lina maana ileile ya mtu mwanaume. Wazigua na Wabondei ni jamii yenye asili moja.
Nilizaliwa katika Kijiji cha Songe,Tarafa ya Kwekivu, Wilaya ya Handeni. Nilipofikia umri wa kwenda shule wazazi wangu walinipeleka shule kuanza darasa la kwanza. Nilisoma mpaka darasa la nne ambapo baba yangu mzazi alifariki. Na mimi sikuendelea tena na masomo. Nikaachia darasa la nne.
Mara nyingi nilikuwa nikimsaidia mama yangu kazi za kilimo na mifugo kwani mimi nilikuwa mtoto wa pekee niliyezaliwa. Sikuwa na ndugu wa tumbo moja. Nilianmbiwa kwamba mama yangu aliharibu mimba (mimba zilitoka) mara tano kabla ya kuzaliwa mimi na nilipozaliwa nilikuwa ndiyo kitinda mimba.
Pale katika mtaa niliokuwa naishi palikuwa na msichana mmoja akiitwa Chausiku. Nilisoma naye darasa moja. Mimi nilipoacha darasa la nne yeye aliendelea hadi darasa la saba.
Tulianza uhusiano wa kitoto tangu tukiwa darasa la tatu. Tulivyofika darasa la nne ambalo mimi niliacha tuliahidiana kuwa tukimaliza masomo tutaoana. Pale kijijini kwetu ukifika darasa la saba ndiyo umesoma. Sekondari ilikuwa ni kama ndoto isiyotabirika. Kwa mwaka kijiji kinaweza kisitoe hata mwanafunzi mmoja kwenda Sekondari. Na kama kutatokea mmoja inakuwa ni kioja. Kijiji kizima kitajua. Katika miaka yangu minne niliyosoma katika shule ile ya msingi, sikumbuki kama kulikuwa na mwanafunzi aliyekwenda sekondari.
Miaka miwili baada ya kuacha masomo Chausiku akawa mchumba wangu.Tulipendana sana. Wakati huo uhusiano wetu ulipata nguvu kwa sababu nilikuwa ninajua kutafuta pesa na nilikuwa nikimsaidia sana.
Lakini uchumba huo ilikuwa nimsubiri amalize darasa la saba ndipo tuoane. Mwenyewe alishajua kuwa asingefaulu. Kwa bahati mbaya Chausiku alipokuwa darasa la sita mama yangu alifariki dunia. Nikawa sina mtu wa kuniongoza. Nikauzauza mifugo na nilipoona maisha yameanza kuwa magumu nikaondoka kwenda mjini Handeni kutafuta kazi.
Nikamuahidi Chausiku kuwa endapo nitafanikiwa kupata kazi, mwakani nitarudi kuoana naye twende tukaishi Handeni kwani nilijua kipindi hicho yeye atakuwa amemaliza darasa la saba.
Handeni nilifikizia kwa mjomba wangu aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni moja ya ulinzi. Nilimwambia kwamba nilikwenda kutafuta kazi akajitahidi kunisaidia. Baada ya kukaa kwa miezi miwili akawa amenifanyia mpango wa kazi ya ulinzi katika kampuni aliyokuwa anafanya yeye.
Kwangu mimi ambaye sikupata mafunzo ya mgambo ilikuwa kazi ngumu na ya hatari lakini kutokana na shida nilijikaza kiume nikijua kwamba sikuwa na elimu na nisingeweza kupata kazi rahisi.
Nilivyoonekana ni kijana na nina nguvu mara nyingi nilipangiwa kwenye malindo ya usiku. Silaha niliyopewa ni kirungu na sime, isitoshe hatukuwa tukipewa makoti ya kuzuia baridi. Kama ulihitaji koti ilikuwa ni juu yako mwenyewe kulinunua. Na pia kama watakuja majambazi wenye bunduki katika lindo lako wakati wewe una sime na kirungu pia ni juu yako mwenyewe kuokoa maisha yako. Kilichotakiwa pale uhakikishe eneo unalolinda liko salama hadi kunakucha.
Siku za mwanzo mwanzo kabla sijalipwa mshahara wangu wa kwanza nilikuwa nikiteseka kwa baridi. Niliwahi kwenda na shuka nzito nikawa najifunika. Lakini mara nyingi ninapojifunika shuka na usingizi nao unakuwa jirani. Mjomba wangu alinishauri kwamba ukifika usiku wa manane nichome moto na vipande pande vya miti. Akaniambia nipendelee kuchoma majani ya mti wa mwarobaini kwani moshi wake unafukuza mbu.
Tangu mjomba aliponiambia hivyo nikawa nawasha vipande vya miti ili kuota moto kisha nachoma majani ya muarobaini kwa ajili ya kufukuza mbu.
Unapofika usiku mwingi ninaacha moto unawaka peke yake mimi mwenyewe ninapanda juu ya mti uliokuwa mbele ya ghala nililokuwa nikilinda na kujilaza kwenye matawi ya mti huo. Ule moshi wa muarobaini unaendelea kufuka na kufika juu ya ule mti hivyo mbu hupungua.
Siku moja wakati nikiwa juu ya mti mvua ikanyesha, ule moto ukazimika. Mvua ilipokuwa inazidi nikaona nishuke kwenye ule mti kwani nilikuwa natota na sikuwa na koti. Wakati nataka kushuka nikaona gari aina ya Land Rover iliyokuja hadi mbele ya lile ghala ikasimama. Nilipoiona gari hiyo niliacha kushuka nikawa naitazama.
Gari hiyo ilisimama mbele ya ghala hilo kwa kiasi cha dakika kumi hivi bila mtu yeyote kushuka. Nikapata wazo kwamba nishuke niende nikamuulize dereva wa gari hilo anataka nini, lakini wazo jingine likanikataza kwa kushuku kwamba wanaweza wakawa ni watu wabaya.
Baadaye kidogo akashuka mtu mmoja akasimama kando ya gari na kuangalia kila upande kisha akaulia kwa sauti ya juu.
"Nani analinda hapa?........nani nalinda hapa!"
Mimi sikujibu kitu. Nikaendelea kubaki kimya. Alipoona hapakuwa na jibu wala mtu yeyote anayetokea akasema.
"Tokeni"
Hapo hapo wakashuka watu watano kutoka katika gari hilo, mmoja alikuwa ameshika bunduki na wengine walikuwa na silaha za kijadi ikiwemo mitaimbo na koleo kubwa la kuvunjia makufuli. Hapo nikajua kuwa watu hao walikuwa majambazi.
Baada ya kutoka kwenye gari walilizunguka lile ghala kisha watano wakaenda kwenye lango la ghala hilo na mmoja aliyekuwa na bunduki alisogea kwenye ule mti, akawa amesimama akiangalia huku na huku.
Nikasikia kufuli moja likivunjwa kisha jingine na jingine tena. Makomeo ya chuma yaliyokuwa kwenye lango hilo yaling'olea kama mchezo. Wale jamaa walikuwa wanaume kweli kweli.
Wakati huo mvua ilikuwa inaendelea kunyesha na watu hao walikuwa wanatota lakini hawakujali mvua. Mimi ndiyo nilikuwa nimetota chapa chapa lakini kutokana na lile tukio, kule kutota pia sikukujali. Nilikuwa nikifikiria jinsi ambavyo ningeweza kuokoa mali iliyopo kwenye ghala hilo isiibiwe. Tatizo lililokuwa hapo si idadi ya wale watu. Kwa vile nilikuwa na sime watu sita ningeweza kupambana nao, nilikuwa nikijiamini. Lakini ile bunduki ndiyo iliyonitisha.
Usiku huo ndipo nilipogundua kwa vitendo matatizo ya kazi hizi za ulinzi wa usiku. Kwa vyovyote vile ilinipasa ninyamaze kimya na niwaache wavunje na kuchukua kila walichokuwa wanakitaka kwani nilijua nikijitia ubabe nitapoteza roho yangu.
Lakini kama wataiba na kuondoka nini kitatokea? nikajiuliza na kujipatia jibu mwenyewe, kwamba atakayeshitakiwa ni mimi na kuhusishwa na wizi huo. Angalau majambazi hao wangenikamata na kunifunga ningekuwa na utetezi.
Sasa nifanye nini? nikawa najiuliza lakini wale watu walishaingia kwenye ghala hilo.Baada ya nusu saa watakuwa wameshasafisha kila wanachokitaka na kuondoka kwa gari lao. Wao watafaidika kwa mali ya wizi, mimi ndiyo niingie kwenye matatizo.
Haitawezekana! nikajiambia kijasiri. Nikashuka taratibu kwenye ule mti bila kusababisha sauti kusikika.
 
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA 2
ILIPOISHIA
Wakati huo mvua ilikuwa inaendelea kunyesha na watu hao walikuwa wanatota lakini hawakujali mvua. Mimi ndiyo nilikuwa nimetota chapa chapa lakini kutokana na lile tukio, kule kutota pia sikukujali. Nilikuwa nikifikiria jinsi ambavyo ningeweza kuokoa mali iliyopo kwenye ghala hilo isiibiwe. Tatizo lililokuwa hapo si idadi ya wale watu. Kwa vile nilikuwa na sime watu sita ningeweza kupambana nao, nilikuwa nikijiamini. Lakini ile bunduki ndiyo iliyonitisha.
Usiku huo ndipo nilipogundua kwa vitendo matatizo ya kazi hizi za ulinzi wa usiku. Kwa vyovyote vile ilinipasa ninyamaze kimya na niwaache wavunje na kuchukua kila walichokuwa wanakitaka kwani nilijua nikijitia ubabe nitapoteza roho yangu.
Lakini kama wataiba na kuondoka nini kitatokea? nikajiuliza na kujipatia jibu mwenyewe, kwamba atakayeshitakiwa ni mimi na kuhusishwa na wizi huo. Angalau majambazi hao wangenikamata na kunifunga ningekuwa na utetezi.
Sasa nifanye nini? nikawa najiuliza lakini wale watu walishaingia kwenye ghala hilo.Baada ya nusu saa watakuwa wameshasafisha kila wanachokitaka na kuondoka kwa gari lao. Wao watafaidika kwa mali ya wizi, mimi ndiyo niingie kwenye matatizo.
Haitawezekana! nikajiambia kijasiri. Nikashuka taratibu kwenye ule mti bila kusababisha sauti kusikika.
SASA ENDELEA
Yule mtu aliyesimama kando ya mti akiwa na bunduki alikuwa amenipa mgongo na bunduki aliishika kwa mkono mmoja akiwa ameielekeza chini. Mara kwa mara alikuwa akifuta maji ya mvua kwenye uso wake ili aweze kuona vizuri.
Nilipofika chini ya mti huo nilichomoa sime yangu nikaipunga na kuanza kumnyatia mtu huyo kwa nyuma. Kutoka shina la mti na mahala aliposimama yeye kulikuwa ni hatua tano. Nikapiga hatua ya kwanza...ya pili...ya tatu...ya nne. Sikutaka kumfikia karibu kabisa. Nikainua sime juu kisha nikaishusha kwenye kiganja cha mkono wake ulioshika bunduki.
Nukta mbili baadaye kiganja na bunduki vikawa chini. Mtu huyo aliruka na kugeuka nyuma akiwa ameushika mkono wake nilioukata. Nikamkabili na kuipunga sime kwa mara ya pili, nikamchanja kwenye bega. Akageuka na kwenda mbio huku akipiga kelele. Nikainama na kuchukua ile bunduki.
Wenzake waliposikia kelele walitoka haraka kwenye ghala na kumulika tochi. Walimuona mwenzao akikimbilia kwenye gari lao huku damu inamtoka. Wakaniona na mimi nimeshika ile bunduki nikiwaelekezea. Watu hao wakashangaa. Nikafyatua risasi kwenye lango la ghala. Jambazi mmoja alianguka palepale, wenzake wengine walitoka mbio kukimbilia kwenye gari.
Sikutaka kufyatua risasi nyingene kwa sababu sikujua bunduki ile ilikuwa na risasi ngapi kwani haikuwa aina ya bunduki za kijeshi zinazokaa risasi nyingi.Ilikuwa bunduki ya kiraia ambayo aghalabu hukaa risasi mbili tu.
Hivyo niliona nikifyatua risasi ya pili na kama bunduki yenyewe ilikuwa na risasi hizohizo mbili nitakuwa nimejimaliza mwenyewe.Majambazi hao kwa kujua kuwa nimemaliza risasi zilizokuwemo wanaweza kunivamia kwa hasira na kunikatakata kwa mapanga na kupata nafasi ya kuendelea na ujambazi wao.Kufa kwa mwenzao mmoja niliyempiga risasi na kumkata mwenzao mwingine kwa sime kusingewazuia wasiendelee na uporaji huo.
Majambazi hao walijipakia kwenye gari lao haraka haraka na kuliondoa kwa kasi.
Mvua iliyokuwa inanyesha nayo ikaacha.Kwa nukta kadhaa nilisimama nikiliangalia gari hilo lilivyokuwa linakwenda mbio bila kuamini kuwa niliweza kuwasambaratisha majambazi hao waliotaka kuniharibia kitumbua changu.
Sikuweza kuamini kuwa nilikuwa nimewashinda. Na ndani ya moyo wangu sikuona fahari juu ya ushindi huo kwani nilifikiria mengi. Kwanza nilifikiria kwamba nimeshaua na nimeshamkata mmoja wao kiganja cha mkono. Kitendo cha kuua mtu na kumkata mtu kiungo cha mwili vilinitia hofu kwa vile katika maisha yangu sikutarajia kuwa ningekuja kutenda vitendo kama hivyo.
Lakini hili linaweza kuonekana si jambo la msingi sana kunitia hofu. Pengine jambo la msingi ni kufikiria kwamba wale majambazi wanaweza kurudi tena wakiwa na bunduki nyingine kwa ajili ya kulipa kisasi.
Wazo hilo ndilo hasa lililonitia hofu. Hata hivyo nilijikaza kiume nikaenda pale alipoanguka yule mtu niliyempiga risasi nikamuangalia na kuona alikuwa ameshakufa, risasi niliyoifyatua ilikuwa imempiga kifuani. Koti alilokuwa amevaa lilikuwa limetapakaa damu.
Nikarudi tena kwenye ule mti nikauegemea na kusimama hapohapo huku macho yangu yakitazama kwa kila upande.Nikajiambia nikiona gari linakuja nitakimbia na kwenda kujificha mahali penye giza .
Laiti kama kituo cha polisi kingekuwa karibu na hapo ningekimbia mara moja na kuwaita polisi lakini kituo kilikuwa mbali na hapo. Vilevile hapakuwa na mlinzi wenzangu aliyekuwa karibu.
Nikaendelea kusimama kwa muda mrefu.Nilipochoka nilikaa chini kwenye tope. Muda ulizidi kwenda mpaka nikaona kumekucha. Ghala ninalolilinda linalindwa usiku na mchana.Wakati mimi ninalinda usiku kuna mwenzangu mwingine anayenipokea zamu saa kumi na mbili asubuhi lakini anachelewa kufika. Badala ya saa kumi na mbili anaweza kuja saa moja au saa moja na nusu.
Siku ile ilikuwa ni bahati, aliwahi kuja.Kwanza alishangaa kunikuta nimeshika bunduki kisha akaona lango la ghala limevunjwa na kuna maiti iliyolala katikati ya lango hilo huku damu ikiwa imesambaa chini.
“Mgosi vipi tena?” mlinzi mwenzangu aliyekuwa akiitwa Mbwana aliniuliza akiwa ameshituka “Naona umeshika bunduki na ghala limevunjwa na kuna maiti hapa!”
“Jamaa wamekuja kuvunja usiku”
“Halafu ikawaje?”
Nikamueleza na kumuonyesha kile kiganja cha mkono wa jambazi nilichokikata kwa sime.
“Kumbe palipita patashika!”
“Ni patashika kubwa.Hivi nilikuwa ninakusubiri ili nikimbie ofisini kutoa taarifa halafu tukatoe taarifa polisi”
“Yaani mimi ndiyo nibaki na hii maiti?”
“Ndiyo baki nayo” nikamwaambia na kuchapuka kuondoka katika eneo hilo .
Nilifika katika ofisi yetu iliyopo katikati ya mji wa Handeni. Afisa wetu alikuwa tayari ameshafika. Nikamueleza kilichotokea. Akaniambia.
“Hebu twende”
Tukaondoka tena kurudi katika eneo la tukio.Baada ya afisa wetu kujionea mwenyewe hali ilivyokuwa akaniambia,
“Twende polisi haraka”
Tukaenda kituo cha polisi huku njia nzima akinimwagia sifa kwa kuokoa mali zilizokuwemo kwenye lile ghala.
Tulipowapa taarifa polisi, polisi watatuwakatupakia kwenye gari na kwenda nao katika eneo la tukio.Hapo nilihojiwa maswali na nikajibu kila nilichoulizwa.Baada ya hapo polisi hao waliichukua ile maiti na ile bunduki ya majambazi pamoja na kile kiganja. Wakaniambia nirudi nyumbani lakini saa tatu nifike kituo cha polisi kuandika maelezo.
Polisi hao wakaondoka na ile maiti.Afisa wetu akaniruhusu niende nyumbani kubadili nguo kwani zilikuwa zimetota na kujaa tope.Nikarudi nyumbani.Nilimueleza mjomba kilichotokea.Akanipa moyo kwa kuniambia.
“Hayo ni matukio ya kawaida katika kazi zetu lakini umefanya kitendo cha kijasiri”
Ilipofika saa tatu nikawa kituo cha polisi.Nilikuwa nimeshaoga na kubadili nguo isipokuwa si kunywa chai kwa sababu ya wasiwasi.
Nikiwa kituo cha polisi niliingizwa katika ofisi ya afisa upelelezi ambaye alichukua maelezo yangu.Baada ya kumaliza kuchukua maelezo yangu alinipongeza kutokana na ujasiri wangu.
Tukio hilo la ujambazi lilisababisha nipande cheo kazini kwangu.Nikavalishwa v mbili begani. Pia ukawa ndiyo mwanzo kwa walinzi wa usiku wanaolinda sehemu nyeti kupewa bunduki. Kwa vile mimi nilikuwa sijapata mafunzo ya kutumia bunduki nilipewa lindo jingine la mchana kwa wiki nzima huku nikipewa mafunzo ya jinsi ya kutumia bunduki na kulenga shabaha.
Je nini kitatokea?
 
SEHEMU YA 03

ILIPOISHIA
Tulipowapa taarifa polisi, polisi watatu wakatupakia kwenye gari na kwenda nao katika eneo la tukio.Hapo nilihojiwa maswali na nikajibu kila nilichoulizwa.Baada ya hapo polisi hao waliichukua ile maiti na ile bunduki ya majambazi pamoja na kile kiganja. Wakaniambia nirudi nyumbani lakini saa tatu nifike kituo cha polisi kuandika maelezo.
Polisi hao wakaondoka na ile maiti.Afisa wetu akaniruhusu niende nyumbani kubadili nguo kwani zilikuwa zimetota na kujaa tope.Nikarudi nyumbani.Nilimueleza mjomba kilichotokea.Akanipa moyo kwa kuniambia.
“Hayo ni matukio ya kawaida katika kazi zetu lakini umefanya kitendo cha kijasiri”
Ilipofika saa tatu nikawa kituo cha polisi.Nilikuwa nimeshaoga na kubadili nguo isipokuwa si kunywa chai kwa sababu ya wasiwasi.
Nikiwa kituo cha polisi niliingizwa katika ofisi ya afisa upelelezi ambaye alichukua maelezo yangu.Baada ya kumaliza kuchukua maelezo yangu alinipongeza kutokana na ujasiri wangu.
Tukio hilo la ujambazi lilisababisha nipande cheo kazini kwangu.Nikavalishwa v mbili begani. Pia ukawa ndiyo mwanzo kwa walinzi wa usiku wanaolinda sehemu nyeti kupewa bunduki. Kwa vile mimi nilikuwa sijapata mafunzo ya kutumia bunduki nilipewa lindo jingine la mchana kwa wiki nzima huku nikipewa mafunzo ya jinsi ya kutumia bunduki na kulenga shabaha.
SASA ENDELEA
Baada ya wiki moja nikawa tayari ninajua kutumia bunduki.Nikarudishwa kwenye lindo langu lilelile la usiku.
Nimekieleza kisa hicho kwa sababu kilikuwa chanzo cha mimi kufahamiana na msichana mmoja anayeitwa Msekwa. Nilikutana na msichana huyo sokoni. Sote tulikuwa tunachagua nazi. Msichana huyo wa Kiruvu akanisalimia kwa kutabasamu kisha akaniambia.
“Ninakufahamu”
“Tulikutana wapi vile….?” Nikamuuliza huku nikijaribu kuvuta kumbukumbu.
“Ninakufahamu tu”akaniambia
Nikawa sikumuelewa. Alipoona ameniacha njia panda akaniambia.
“Wewe si ndiye uliyemkata jambazi mmoja kiganja cha mkono ukachukua bunduki yake.....?” hakumaliza sentensi yake akacheka kisha akaondoka. Nikabaki nimesimama nikimuangalia.
Kitu ambacho sikukijua ni kwamba habari zangu zilizungumzwa sana pale Handeni jinsi nilivyowasambaratisha wale majambazi.Wakati nikipita kwenye mitaa watu walikuwa akinisema na kuninyooshea kidole.Yule msichana alikisikia kisa changu na kuniona nilikuwa kijana shujaa. Kwa kweli alinipenda.
Siku nyingine nilikuja kukutana naye wakati ninaenda kazini. Akanisalimia na ndipo nilipogeuka na kumuona.Tukaulizana hali. Akanieleza anapoishi kisha tukaachana. Kutoka siku ile tukawa tunakutana mara kwa mara na kuzungumza. Bila kutegemea tukaja kuwa marafiki na mwisho akawa mchumba wangu.Nikaja kuoana naye.
Tayari nilikuwa nimepangisha chumba changu kwenye nyumba ya mzee mmoja iliyokuwa jirani na mahakama ya mwanzo.Nikaendelea na maisha nikiwa na mke wangu ambaye tulipendana sana. Miaka mitatu ikapita.
Siku moja wakati naenda kazini mchana,nilisikia sauti ya msichana akiniita nyuma yangu. “Rajabu….Rajabu….” nikageuka nyuma na kumuona Chausiku yule mchumba wangu wa kwanza ambaye tulipanga kuoana nikipata kazi lakini nilipopata kazi nikamsahau na kuoana na msichana mwingine.
“Oh! Chausiku ni wewe? Sikukujua, samahani”
“Najua hukunijua.Habari za siku?”
“Nzuri, za Songe au hukai Songe siku hizi?”
“Niko Songe nakusubiri wewe uje unioe, naona kimya tu”
Nikajidai kucheka.
“Mbona mimi nilishaoa”
“Kumbe ulishaoa?” akaniuliza kwa sauti ya fadhaa.
“Nilishaoa mwenzako”
“Sasa kwanini hukuja kuniambia kama umebadili mawazo?”
“Kwa hilo nakuomba unisamehe.Najua nilikosea”
“Basi nimeshakusamehe.Ndoa ni riziki, kama haikupangwa haiwezi kuwa. Sasa unafanya kazi wapi?”
“Ninafanya kazi ya ulinzi. Si unaniona nilivyovaa?”
“Unafanya wapi?”
Nikamuelekeza zilipokuwa ofisi zetu.
“Sasa wewe utakuja lini Songe?”
“Nikipata likizo mwaka huu nitakuja kuwatembelea”
“Sawa, basi mimi huwa ninakuja mara kwa mara kuuza
vyungu. Nikimaliza kuuza ninapanda gari ninarudi”
“Basi ukija nitembelee ofisini kwetu. Si umesha pajua?”
“Nimeshapajua”
Baada ya hapo tukaagana. Akaenda zake na mimi nikaenda kazini kwangu.
Kumbe kile kitendo cha kumwambia nitembelee ofisini kwetu kilikuwa kosa.Baada ya wiki mbili wakati nimerudi nyumbani jioni kutoka kazini,nikasikia mtu anabisha mlango wa chumba changu.Mke wangu alikuwa uani.Nilipofungua mlango nikamuona mfanyakazi mwenzangu amefuatana na Chausiku.Nikashituka.
"Karibuni" nikawaambia huku nikitoa tabasamu la uongo kuficha mshangao wangu.
"Ahsante" mfanyakazi mwenzangu ndiye aliyejibu na kuongeza "Huyu msichana alikuja ofisini kukuulizia.Anasema anatoka Songe,alikuja kuuza bidhaa zake hapa mjini lakini amechelewa gari.Ametuambia wewe ni kaka yake"
"Ndiyo, tunatoka kijiji kimoja" nikasema na kumtazama Chausiku.
"Kumbe leo ulikuja na umechelewa gari?" nikamuuliza.
"Gari limewahi kuondoka na sina pa kulala ndiyo nikaja kukuulizia kazini kwako ili unipe msaada wa mahali pa kulala hadi kesho asubuhi nirudi kijijini" Chausiku akasema kwa ufasaha na kujiamini kama vile alijua mimi nina chumba cha wageni wakati chumba changu kilikuwa kimoja tu.
Kadhalika sikuufurahia ugeni wake nyumbani kwangu kwa sababu ya vile nilivyomuacha kwenye mataa na kuoa mke mwingine.Sikutaka kabisa wakutane na mke wangu lakini ndiyo alikuwa ameshaletwa nyumbani. Sikuwa na la kufanya zaidi ya kumkaribisha.
"Basi mimi ninarudi kazini" mfanyakazi mwenzangu aliniambia.
Nikaagana naye akaenda zake.
Mke wangu aliposikia sauti za watu akaja haraka kwenye mlango, akamuangalia yule msichana.
Nikamtambulisha kuwa ni binti wa shangazi yangu anayeishi Songe kisha nikamueleza tatizo lililomleta kwangu jioni ile.
Mke wangu Msekwa kwa kudhani ni wifi yake alimkaribisha chumbani.Wakazungumza sna kwa furaha na vicheko.Jua likawa limekuchwa. Nikamfuata mama mwenye nyumba na kumuomba amruhusu mgeni wangu alale chumbani kwa binti yake kwa siku moja.
Mama mwenye nyumba akanikubalia.Jioni ile tulipika wali kwa sababu ya mgeni.Wenyewe tulikuwa tupike ugali.Baada ya kula tulikaa nje tukazungumza mpaka saa nne usiku tulipoingia ndani kulala.
Asubuhi kulipokucha Chausiku aliondoka mapema sana ili kuwahi gari la saa moja.Nilishukuru kwamba katika kukaa kwake pale nyumbani mke wangu hakumgundua kwamba alikuwa mchumba wangu wa kwanza.
Baada ya wiki mbili ulitokea ugomvi kati yangu na mke wangu. Kisa cha ugomvi huo ni mke wangu kuchelewa kupika. Siku hiyo nilirudi kutoka kazini saa kumi na moja jioni. Kwa kawaida ninakuwa sili mchana siku nikiwa kazini. Ni mpaka jioni ninaporudi mke wangu anakuwa ameniwekea chakula cha mchana.
Siku hiyo sikukuta chakula na njaa ilikuwa inaniuma. Nilimkuta mke wangu amelala. Nikamuuliza "Vipi?"
Akanijibu kuwa alikuwa amechoka baada ya kurudi kutoka katika harusi ya jirani yetu.
Kawaida yetu ni kuwa ninaporudi kutoka kazini huniuliza kuwa aniwekee chakula au maji ya kuoga. Lakini siku ile hakuniuliza chochote. Ikabidi nimwaambie mwenyewe.
"Nimwekee chakula"
"Sikupika" akanijibu haraka.
"Hukupika kwa nini?"
"Si nilikwenda harusini?"
"Ukenda harusini ndiyo hupiki?"
"Ah! nimechoka bwana, nimerudi sasa hivi!"
"Sasa kama wewe umekula harusini mimi nikale wapi?"
"Lakini si umeniruhusu mwenyewe niende?"
"Hilo sio swali langu. Nimekuuliza kama hukupika mimi nikale wapi?"
"Lakini uliniruhusu mwenyewe!"
"Kwamba usipike?"
"Niende harusini"
"Lakini sikukuambia nenda harusini lakini usipike. Kama umesharudi huko harusini kwanini hukupika?"
Nilipomuuliza hivyo alikunja uso akaguna. Jambo hilo liliniudhi nikakasirika.
Je nini kilifuatia baada ya hapo? Hebu endelea kufuatilia hadithi hii
 
SEHEMU YA 04

ILIPOISHIA
Kawaida yetu ni kuwa ninaporudi kutoka kazini huniuliza kuwa aniwekee chakula au maji ya kuoga. Lakini siku ile hakuniuliza chochote. Ikabidi nimwaambie mwenyewe.
"Nimwekee chakula"
"Sikupika" akanijibu haraka.
"Hukupika kwa nini?"
"Si nilikwenda harusini?"
"Ukenda harusini ndiyo hupiki?"
"Ah! nimechoka bwana, nimerudi sasa hivi!"
"Sasa kama wewe umekula harusini mimi nikale wapi?"
"Lakini si umeniruhusu mwenyewe niende?"
"Hilo sio swali langu. Nimekuuliza kama hukupika mimi nikale wapi?"
"Lakini uliniruhusu mwenyewe!"
"Kwamba usipike?"
"Niende harusini"
"Lakini sikukuambia nenda harusini lakini usipike. Kama umesharudi huko harusini kwanini hukupika?"
Nilipomuuliza hivyo alikunja uso akaguna. Jambo hilo liliniudhi nikakasirika.
SASA ENDELEA
Alipoondoka kitandani ili aende akapike nikamzuia.
"Basi endelea kulala......unakwenda wapi.....wewe si unajifanya jeuri!"
Lakini hakunisikia akatoka kwenda uani. Ilimchukua saa nzima kutayarisha ugali kwa mboga ya mrenda na perege wa kuchoma. Aliponiwekea kwenye meza nikaisukuma sahani ya ugali ikaanguka chini na kuvunjika.
"Unamuwekea nani?....kwenda zako!" nikamwaambia kwa ukali "Si nilikwambia basi, sitaki chakula?"
"Sasa ndiyo uisukumie chini sahani ya ugali?" akaniuliza naye akinionesha kukasirika.
"Tena ushike adabu yako, nitakupiga sasa hivi!" nikamwaambia kwa sauti ya ghadhabu huku nikinyanyuka kwenye kiti.
Mke wangu alipoona nimehamaki hakusema tena.Aliinama akauokota ule ugali ulioanguka pamoja na vipande vya sahani akatoka navyo uani. Na mimi nikatoka kwenda mtaa wa pili ambako kulikuwa na baraza ya kahawa. Nikakaa na kuzungumza na wenzangu.
Ilipofika saa mbili usiku nilikwenda kula kwa mamalishe kisha nikarudi nyumbani.Kwa vile nilikuwa nimekasirika sikuzungumza na mke wangu.Nilikwenda bafu kuoga kisha nikarudi kulala.
Asubuhi kulipokucha nilioga nikavaa nguo zangu za kazini.Sikusemeshana lolote na mke wangu.Nilimuachia pesa yake ya matumizi mezani kisha nikatoka.
Nilivyotoka kumbe na yeye alitoka kwenda katika kijiji kimoja kilichokuwa jirani. Alikwenda kumchukua dada yake aje atupatanishe.
Siku ile nilirudi usiku kutoka kazini. Kilichonifanya nichelewe kurudi ni kwamba mwenzangu aliyetakiwa kuja kunitoa katika lindo alipata dharura akachelewa. Isitoshe nilipotoka katika lindo nilipitia kwa mamalishe nikala chakula ndio nikarudi nyumbani.
Nilipofika nilimkuta mke wangu na dada yake Mkiwa. Tukaulizana hali. Akaniambia alikuwa arudi kijijini kwao jioni ile lakini kwa vile nilichelewa kurudi ilimbidi anisubiri.
Baada ya kuoga mke wangu aliniwekea chakula lakini sikukila. Sikukila kwa sababu kwanza nilikuwa nimeshakula na pili zile chuki za jana yake nilikuwa bado ninazo.
Msekwa alipoona sikukila kile chakula alitoka chumbani na kwenda kumuambia dada yake.Mara nikawaona wanaingia chumbani.
"Shemeji mbona hutaki kula?" Mkiwa akaniuliza
"Sitaki tu" nikamjibu.
"Si kawaida mtu kuwekewa chakula na mke wake akakataa bila
sababu,lazima ipo sababu.Mke wako ameniambia tangu jana umekataa chakula na hamzungumzi"
"Ni kweli lakini yeye atakueleza ni kwa kwanini nimekataa chakula na kwanini hatuzungumzi"
Mkiwa akamgeukia mdogo wake
"Msekwa hebu eleza kumetokea nini?"
Msekwa akaeleza yaliyotokea jana yake lakini hakuyaeleza sawasawa.Maelezo yake yalikuwa ni ya kunipa mimi lawama.
"Hebu sema ukweli mbele ya dada yako, niliporudi kazini nilikukuta wapi?" nikamuuliza
"Ulinikuta nimelala" akajibu
"Nilipokuuliza kuhusu chakula ulinijibu nini?"
"Chakula nilichelewa kupika kwa sababu nilienda harusini na nilikuaga"
"Ulichelewa kupika au uliniambia hukupika?"
"Si nilipika chakula ukakimwaga wewe!"
Hatua yake ya kugeuza geuza maneno ikaniudhi tena.
Nikamgeukia dada yake na kumueleza ukweli ulivyokuwa.Dada yake akaona mke wangu alikuwa na makosa.Kule kwetu wanaume ni watu wanaoheshimiwa sana.Ili kutusuluhisha Mkiwa akamgombesha sana mdogo wake na mwisho akamwaambia asingependa asikiye tena kuwa ameudia kosa kama hilo.
Msekwa akamjibu kuwa hatarudia.
"Sasa muombe msamaha mume wako" Mkiwa aliyeonekana kuwa mkali akamwaambia mdogo wake.
Mke wangu akaniangalia kisha akainamisha kichwa chini na kuniambia
"Nakuomba unisamehe mume wangu"
Hapo nikahisi moyo wangu unakunjuka na kinyongo nilichokuwa nacho kinaondoka.
"Nimekusamehe" nikamwaambia kwa sauti tulivu.
"Basi naomba ule hicho chakula" akaniambia.
"Nimeshakula chakula huko nilikotoka lakini kwa vile umeniomba nitakula tena"
Nikaosha mkono na kula kile chakula.
Ugomvi wangu na mke wangu ukaishia hapo.
Asubuhi kulipokucha Mkiwa akaniambia anasubiri ikifika saa nne ataondoka arudi kijijini kwao, nikamjibu vyema.Wakati huo nilikuwa ninajindaa kutoka niende kazini.Baada ya kumaliza kuvaa sare zangu niliwaaga mke wangu na dada yake, nikatoka.Lakini nikakumbuka kuwa nilitoka bila kumuachia mke wangu pesa za matumizi na mke wangu naye alisahau kuniuliza.Nilikuwa nimeshafika mbali nikaamua kurudi na kuingia chumbani mwangu.
Lakini nilipoingia humo chumbani, sikuamini macho yangu. Nilijifuta uso nikatizama tena.Mke wangu alikuwa amelala chini huku damu zikimtoka kifuani.Kisu chenye mpini wa nchi tano kilikuwa kimezama kifuani kwake. Wakati namuangalia ndio alikuwa anavuta pumzi za mwisho na kukata roho.Kwa kweli nilishituka sana.Nikajiuliza je nilikuwa naota? lakini akili yangu iliniambia haikuwa ndoto.Nilichokiona kilikuwa kweli.Mke wangu amechomwa kisu na kuuawa mara tu nilipotoka.
Nikainama pale alipolala ili nimuangalie vizuri na kuyasadikisha macho yangu kama alikuwa ni yeye kweli.
Mara nikasikia mlango unafunguliwa nyuma yangu, Mkiwa akaingia.Alikuwa anatoka kuoga.
"Samahani nilijua umeshatoka" akaniambia halafu akamuona Msekwa aliyekuwa amelala chini. Mimi nikanyanyuka na kumgeukia yeye.
"Kitu gani kimetokea hapa?" nikamuuliza.
"Ha! shemeji umempiga kisu mke wako?" Mkiwa akang'aka na kuongeza "Mimi nilijua ule ugomvi umekwisha kumbe umemuwekea kisasi mwenzako!"
Vile nilivyomgeukia alidhani nilitaka kumkamata, akakurupuka na kutoka mbio huku akipiga kelele.
"Jamani mdogo wangu ameuliwa na mume wake....."
"Mimi siye niliyemuua,nimerudi sasa hivi na kumkuta ameshachomwa kisu.Sijui ni nani aliyefanya ushenzi ule" nikasema huku nikiwa ninamfuata Mkiwa aliyekuwa amekimbilia uani.
Wanawake waliokuwa uani pamoja na mama mwenye nyumba wakatushangaa.
"Jamani kuna nini, mbona mnatushitua?" mama mwenye nyumba aliuliza kwa hofu.
"Msekwa ameuliwa,amepigwa kisu kifuani na shemeji.Nendeni chumbani mwao mumuone!" Mkiwa akasema huku akilia
"Sikumpiga kisu shemeji, hebu nielewe.Mimi nilikuja na kumkuta ameshapigwa kisu. Mbona unataka kunitia katika hatia?" nikamwaambia kwa ukali kidogo.
"Ni wewe shemeji, ndiye uliyekuwa naye huko chumbani.Ni chuki za jana hizo"
Wanawake wote waliokuwa uwani wakaenda ukumbini, wakaingia chumbani mwangu.Mimi nilikuwa nikiendelea kueleza kile nilichokishuhudia.Kila aliyeingia mle chumbani alitoka mbio huku akipiga kelele.
Wanawake wengine walikimbilia uani wengine walikimbilia nje.Mama mwenye nyumba alinifuata na kunishika mkono na kuniuliza "Kwanini umefanya kitendo kama kile mwanangu?"
"Sikumpiga kisu mimi mama"
"Ni wewe, shemeji yako amekuona.Unakataa nini" mama mwenye nyumba akanikata kauli.
Balaa hilo! Je nini kitatokea?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom