dubu
JF-Expert Member
- Oct 18, 2011
- 3,502
- 3,486
MJASIRIAMALI anayefuga mende kwa ajili ya chakula cha kuku na samaki anaowafuga na kuwauza kibiashara, Lucius Kawogo amesema ameanza kuzidiwa na oda za wateja wanaonunua mende kwa lengo la kuanza ufugaji.
Kawogo ameyasema hayo wakati akizungumzia na gazeti hili kuhusu mwitikio wa alioupata tangu gazeti hili toleo la Januari 7, mwaka huu, kuripoti jinsi anavyonufaika na ufugaji wa mende mkoani Njombe.
“Watu wananipigia simu kweli kweli na wengine wanaweka oda ya mende wengi, mpaka ninawazuia huku wengine wakilipia kabisa,” alisema Kawogo.
Tangu habari hizo zichapishwe, watu mbalimbali wamekuwa wakipiga simu katika ofisi za gazeti hili kutaka kujua namna ya kuwasiliana na mjasiriamali huyo ili waweke oda na kujifunza ufugaji huo.
Kawogo alisema: “Ninawashukuru sana HabariLeo. Tangu hizi habari zitoke kwenye gazeti lenu, nimepigiwa simu nyingi sana hata kutoka ofisi kubwa kubwa.” Kuhusu kuwazuia wengine wasinunue mende wengi, alisema:
“Wengine wanataka mende wengi mpaka ninawazuia kwa sababu ndiyo kwanza wanakwenda kuanza hivyo, wakianza na wengi kisha wakazaliana kabla hawajajua namna nzuri ya kuwadhibiti, watawashinda na kusambaa halafu itakuwa shida.”
Aliongeza: “Ndiyo maana ninawahimiza wanunue mende wasiozidi 100 kwa kuanzia na bahati nzuri, wananielewa maana wengine wamelipia kabisa ingawa wamepata tabu kujua namba zangu na wengine, imebini waulizie ndugu zao wanaonifahamu huku Njombe…”
Alisema wengine wanaompigia simu wanataka kujua namna alivyoanza ufugaji wa mende, faida, changamoto, chakula chao na namna anavyowadhibiti sambamba na usafi huku wakionesha ari ya wao kuanzisha ufugaji huo. Mmoja wa wateja waliolipia mende hao ili Kawogo amtumie ni Kassim Watanda wa Mbezi Malambamawili Dar es Salaam aliyesema jana kuwa, ataendesha mradi wa mende maeneo ya Kimara Bonyokwa jijini humo.
“Katika ufugaji huu, mimi niko kibiashara zaidi na malengo yangu ni biashara… Nimeagiza boksi moja litakalokuwa na mende 100 wazazi hata leo (jana) nimewasiliana naye, anaandaa boksi na usafiri kutoka Njombe hadi wanifikie hapa Dar,” alisema Watanda.
Kuhusu mtarajio alisema: “Natarajia faida nono maana kama yai moja linatoa mende watoto 50 nategemea kwa mende 100 kwa mwezi nitakuwa na mende 5000 na hao wakiuzwa kila mmoja shilingi 500, ni karibu shilingi 2,500,000 ninatazama baada ya miezi sita, licha ya changamoto na matumizi mengine muhimu, nitakuwa mbali.”
“Nimesukumwa na hamasa ya Rais John Magufuli kuwa tutumie akili na juhudi zetu kujikwamua kiuchumi. Hizi ni fursa na huyu ndugu yetu (Kawogo), amekuwa muwazi na mungwana kutuvutia na kutuita nasi tufanye kazi hii; amefanya jambo zuri na nyie (HabariLeo).”