HATIMAYE leo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inatekeleza azimio ililoliweka mwezi Desemba mwaka jana la kuzifungia simu feki.
Hatua hiyo itakwenda na matakwa ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, ambayo inataka kutekelezwa kwa mfumo wa Rajisi ya Namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi.
Kifungu cha 84 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, kinataka kuwepo kwa mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa Vifaa vya Mawasiliano vya Mkononi, ambayo inatakiwa ihifadhiwe na kuendeshwa na TCRA.
Pia sheria hiyo inawataka watoa huduma wa mawasiliano, yanayotumia vifaa vya mkononi kuweka mfumo wa kudumu wa kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mkononi, vinavyotumika kwenye mitandao yao.
Mfumo huu wa kielektroniki, ulizinduliwa rasmi Desemba 17 mwaka 2015 na unahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi (IMEI) kwa lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango (bandia) vya matumizi katika soko la mawasiliano.
Namba tambulishi za vifaa vyote vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano, havitaruhusiwa kuunganishwa kwenye mitandao ya watoa huduma baada ya simu hizo kuzimwa leo usiku wa saa sita.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema mpaka juzi uchambuzi uliofanywa unaonesha mabadiliko chanya ya idadi ya namba tambulishi, ambazo zilikuwa hazina viwango kupungua kutoka asilimia 3 hadi kufikia asilimia 2.96, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zikipungua kutoka asilimia 2 hadi kufikia asilimia 0.09. Vilevile, idadi ya namba tambulishi za simu halisia zimeongezeka kutoka asilimia 85 mpaka asilimia 96.95.
Matokeo hayo yanaonesha mwitikio mzuri wa wananchi juu ya uelewa wao katika suala zima la uzimaji wa simu ambazo hazikidhi viwango.
Matokeo hayo yanatoa picha nzuri hadi uzimaji wa simu bandia leo hii. TCRA pia imewataka mafundi wote wa simu nchini, kuanza mchakato wa kupata leseni ya kutengeneza simu, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwaorodhesha wanaoleta simu zao kutengenezwa ili kuepuka kuwa sehemu ya mtandao wa wizi wa simu.
Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa mfumo huu wa kielektroniki wa Rajisi, ambao utahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi, una lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano.
Endapo mtu atapigiwa simu na kutapeliwa fedha, mfumo huo utaweza kutambua namba tambulishi ya simu ambayo imetumika na mtu aliyeisajili. Ni rahisi kufuatilia mtu mwenye simu halisi ; na ni ngumu kwa mtu mwenye simu feki.
Pia mfumo huo utasaidia kuondoa tatizo la wizi wa simu, kwani mtu aliyeibiwa akitoa taarifa za kupotelewa kwa simu yake, simu hiyo itafungwa; na ikishafungwa haitaweza kutumika na mtandao wowote wa simu hapa nchini, kwa maana nyingine aliyenunua simu hiyo ya wizi atabaki na ‘toy’ (mwanasesere).