Ni hivi, kanuni ya asili (nature) vitu huenda na muda. Kwa kawaida vizazi hubadilika na kutokana na kubadilika huko kizazi huhitaji vitu vingine tofauti na kizazi kilichopita. Ukiingalia ccm ni taasisi ya kizazi kilichopita, kutokana na mahitaji ya nyakati kinajikuta hakina mvuto tena, sio kwamba Magufuli au ccm hawajafanya kitu, bali mahitaji ya kizazi hayahitaji tena ccm.
Ni bahati mbaya viongozi wa ccm wote kwa umoja wao, Magufuli pamoja na usalama wa taifa wanafumbia macho kanuni hii ya asili kwani madaraka ni sehemu ya wao kuepukana na umasikini. Ndio maana unaona ccm imefanya siasa yenyewe kwa muda wa miaka minne. Wamewafanyia wapinzani hujuma zote za wazi na za kificho ili upinzani ufe, lakini haufi na wananchi hawavutiwi hivyo na ccm. Udhibitisho ni watu kususia kujiandikisha mpaka imepikwa idadi, na sasa wapinzani wamejitoa na kuonekana kuungwa mkono, kiwaziwazi hata kwa kificho. Hiyo yote ni kwa sababu ya kanuni ya asili. Hapo ilipo hata ccm ifanye mazuri gani haiwezi tena kuendelea kutawala kwa kukubalika na walio wengi, na wakikosea tu wakatoa nafasi basi ndio mwisho wao.
Nakumbuka wakati mziki wa bongo fleva umeanza miaka ya mwishoni ya 90, ulipigwa vita kuwa hauna maadili, lakini vijana ambao ndio wengi walizidi kuupenda, ukaanza kupigwa kwenye vituo vya redio na TV za binafsi na kuvuta vijana wengi kusikiliza vituo hivyo vya binafsi, huku redio na TV ya taifa ikiendelea kupiga nyimbo za kina sikinde, Ottu jazz nk zenye maadili lakini zikisikilizwa na wazee tu. Leo hii hata redio na TV ya taifa inapiga sana miziki ya kizazi kipya kwani ndio yenye wengi, hiyo ndio kanuni ya asili. Hata hiki kinachoendelea sasa ni vyema Magufuli aambiwe hawezi kurudisha tena wananchi kwa mabavu kwenye siasa ya chama kimoja, sana sana atapelekea nchi kwenye machafuko.