Ujasusi Wa BOSS Ndani Ya Amnesty
Mnamo mwezi Juni au Julai 1972 H. J alipokea telegramu kutoka BOSS iliyokuwa na ujumbe huu:
Stephen Bubb c/o 19 Gladwin Close, Wigmore, Gillingham, Kent yumo katika wale wanaolipwa na Amnesty kama mfungwa aliyehukumiwa Pietermaritzburg, mjini Natal mnamo mwezi wa Aprili, 1972. Pesa hizo anatumiwa na kundi la Amnesty International la mjini Towns. Tafadhali peleleza na pata taarifa zaidi.
BOSS pia lilimtumia H. J ujumbe mwingine uliodai na/ au kuwa na anuani ya kwamba:
Stella Joyce anaaminika kuwa ni wakala wa CIA akiwa kama mmoja wa wanaharakati wa kisiasa wa Afrika Kusini waliopo mjini London. Aliacha utumishi wa Amnesty International na kujiunga na mfuko unaojulikana kama Primitive Peoples Fund. Huyu ni yule Stella Sweetman, mfanyakazi wa Amnesty International ambaye sasa ameolewa na John Cavill, mwanaume wa kizungu ambaye ni mwanahabari anayeishi mjini London. Swali: Ni nani anayeeneza uvumi juu ya Stella Joyce kwamba ni wakala wa CIA? Atakuwa ni Barney Zackon, mwanaharakati kutoka Afrika Kusini ambaye sasa anaishi Mtaa wa 12 Kiddepore Gardens, London NW3. Pata taarifa zaidi juu ya uvumi huo.
Alivyofahamu H. J, BOSS lilikuwa na uhusiano fulani na idara ya Upelelezi ya Hispania(Spanish Security Police) mwaka 1972. Mwaka huo huo H. J aliombwa kufuatilia taarifa za mwanamke huyo katika idara hiyo ya Hispania. Ujumbe alioupokea H. J ulidai wazi wazi kuwa hapakuwa na uhusiano kabisa. H. J aliambiwa kwamba chochote kilichokuwa kikiwasilishwa ilikuwa ni kwa msaada wa jamaa zao fulani wa mjini Madrid. Hivi ndivyo BOSS ilivyomwambia H. J.
Mapema mwaka 1972, Bibi Thelma E. H Pahahi wa Mtaa wa 4, The Graylands, High Rickleton, County Durham, alikwenda kwa jamaa wa Amnesty International kuwaarifu kuwa alikuwa mbioni kuandika makala juu ya Gereza la Segoviya. Mwezi Februari, 1972, Amnesty International mjini London ikarejeshea majibu ambayo yalisema hapakuwa na sababu ya kuandika makala juu ya Gereza hilo, na kwamba habari zinazomuhusu mfungwa aliyeko kwenye gereza hilo anayeitwa Jose Sandoval, zisichapishwe. Katika barua hiyo hiyo kwa Bibi Pehahi, Amnesty International ilieleza jambo ambalo ni muhimu kidogo kulijua juu ya habari za Madrid. Nukuu halisi ya barua hiyo ni hii hapa:
Lakini, kwa sababu ya uhusiano maalumu uliopo kati ya Amnesty International na serikali ya Hispania ambao unawaruhusu wanachama wa Amnesty International kutembelea wafungwa kwenye magereza, ni muhimu kwa hivi sasa Amnesty isielezee chochote juu ya hali za wafungwa waliopo katika magereza ya nchi hiyo na hasa kuchapisha taarifa zitakazopatikana kufuatia ziara katika magereza hayo. Tukifanya hivyo, makundi ya watu yatajenga shauku ya kutaka kujua zaidi juu ya wafungwa wanaowahusu, tuwe waangalifu, tusieleze kuwa taarifa hizo zimepatikana kufuatia ziara katika magereza hayo. Hata hivyo, tunafikiria kuchapisha taarifa nzito juu ya magereza hayo siku za usoni hasa tutakapokusanya maelezo mengi kutoka kwa ndugu, marafiki na jamaa za wafungwa hao.
BOSS ilimtaka apeleke taarifa kwa njia ya ujasusi iwapo Amnesty International ilikuwa mbioni kuchapisha taarifa hizo nzito juu ya magereza ya Hispania. Maombi haya yalimshangaza sana kwamba, iwapo BOSS ilikuwa linapokea taarifa nzito na za mara kwa mara kutoka ndani ya Amnesty International, kwa nini ilikuwa ikimtaka afuatilie wakati ikijulikana wazi kuwa hakuwa na rafiki katika Amnesty International ambaye angempatia taarifa nyeti kuhusiana na mambo inayoyashughulikia?
Mwezi Februari 1972, BOSS ilimtumia ujumbe mrefu kuhusiana na John Martinus Ferus, ambao nao ulionesha kwamba Afrika Kusini pia ilikuwa na taarifa zote muhimu na ikizijua vyema shughuli za wanachama wa Amnesty International nchini Ujerumani.
BOSS ilimwambia:
Ferus, John Martanus, mwanaume chotara mtu mzima akifahamika pia kama Hennie aliyeishi Mtaa wa 14 Hamner, Worcester, Cape Province, ambaye alikuwa mwanachama wa Umoja wa Wafanyibashara (SACTU), ambaye aliwekwa kizuizini Oktoba 1, 1963 na tarehe 30, Desemba, 1963 akaachiwa kwa dhamana baada ya kuhusishwa na matukio ya hujuma dhidi ya maeneo ya serikali akiwa kama mwanachama wa ANC. Shitaka hilo lilifutwa na mahakama mwezi Januari 1964 bali aliendelea kukabiliwa na ile amri ya kupigwa marufuku kwa Chama cha Kikomunisti. Chini ya Agizo la Serikali Namba 9 Kifungu Namba 1 cha kanuni Namba 44 ya mwaka 1950 ukomunisti ulipigwa marufuku . Mwezi Aprili 1966 alikamatwa na kuteswa kwa kuvunja kanuni hiyo, maelezo zaidi juu ya suala hili ni muhimu kwa kuwa zipo taarifa kuwa yuko mbioni kuja Afrika Kusini kutembelea familia yake kupitia jamaa mmoja wa Amnesty International. Bado sheria ingalipo na ujaji wake hapa utakuwa kinyume cha kanuni hiyo. Ferus alikabiliwa na kanuni nyingine ya kuzuiliwa nyumbani kutokana na amri hiyo ya kukipiga marufuku Chama cha Kikomunisti.
Kisha BOSS ikatoa maelezo ya kina juu ya safari ya Ferus iliyoandaliwa na mwanachama huyo wa Amnesty International. Maelezo hayo yalisema:
Taarifa tulizonazo ni kwamba Herr Claus-Rudiger von Hertzberg, mwanachama wa Amnesty International, anapanga kumtembelea Ferus. Hakuna ombi rasmi lililofanywa kabla ya kuandaa ziara hiyo, kwa hiyo tungependa kujua lini Von Hertzberg anakusudia kusafiri kuja Afrika Kusini. Chanzo chetu kisicho cha moja kwa moja ndani ya Amnesty kimetilia shaka suala hili, kwa hiyo pokea maelezo haya muhimu ambayo yatakuongoza katika upelelezi wako, maelezo haya mafupi ni kukusaidia usiende kwa wasiohusika wakati ukifanya upelelezi huo.
Chanzo cha upelelezi wa habari juu ya kutembelewa Ferus kinasema ifuatavyo:
Wakati fulani, shirika la Amnesty International nchini Ujerumani (Group 4) lilishughulikia suala la Ferus lakini kabla ya kwenda mbali, Von Hertzberg, aliyekuwa akilijuwa vyema suala hilo akahamia kundi la Amnesty International Namba 208 lilipo mjini Wolfhagen, hivyo akalizima kinamna suala hilo, kwa kuwa ilionekana alikuwa na ukaribu sana na jamaa huyo. Kundi namba 208 lilifungwa mwezi Novemba 1970 pale Von Hrtzberg alipohamia mjini Munich pamoja na faili la jamaa huyo. Amekuwa na mawasiliano na mama yake Ferus na amekuwa akijaribu kumuunganisha mtuhumiwa huyo na kundi la Amnesty la nchini Sweden. Von Hertzberg vile vile alipanga na jamaa yake mmoja kwenda kwa mama yake Ferus kuandaa mipango ya baada ya Ferus kuachiwa kutoka gerezani. Jamaa huyo tunamfahamu na katika ziara hiyo mjadala uliofanyika ulihusu ni namna gani atakavyotoroshwa Ferus mara baada ya kutoka gerezani.
Hata hivyo, alipotoka gerezani Ferus alikataa kuondoka Afrika Kusini baada ya kushawishiwa na mpenzi wake mmoja. Msemaji wa kundi la Amnesty International nchini Sweden jamaa mmoja aliyeitwa Herr Stephen Rosentrom, mara kwa mara alikuwa akikutana na Von Hertzberg mjini Munich na walikuwa wakijadiliana kile ambacho BOSS wamekuwa wakikiita kama hatua zaidi zitakazochukuliwa kuhusiana na suala la Ferus.
Kwa mujibu wa barua iliyotumwa kwa Martin Enthoven wa Amnesty International mjini London, Februari 7, 1972 kutoka kwa Theresia Becker wa kundi la Amnesty International Namba 45 (75 Farmstrasse, Woldorf 6083, Ujerumani Magharibi), Herr Von Hertzberg na Herr Rosentrom waliendelea kulishughulikia suala la Ferus licha ya Ferus mwenyewe kutokuwa tayari kuondoka Afrika Kusini. Kwa wakati ule Von Hertzberg alisema angependa kukutana ana kwa ana na Ferus kabla ya muda mrefu kupita na angefanya hivyo wakati wa ziara yake Afrika Kusini. BOSS ilikusudia kumkamata Herr Von Hertzberg kama angalimtembelea Ferus. Hata hivyo, alifuta mpango wake huo baada ya jamaa mmoja kumuonya kuwa asijitie kitanzi mwenyewe.
Gordon anasema Mwaka 1973, BOSS ilimtumia ujumbe mwingine uliosema: Abraham, Eric Antony, mwanaume mzungu wa Afrika Kusini, mwanafunzi, umri miaka 19, alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana uliojulikana kama National Youth Action mwaka 1971 na mwanachama wa NUSAS katika Chuo Kikuu cha Cape Town. Kijana Tatizo kama BOSS lilivyombabatiza, kwa wakati ule alikuwa akifanya kazi katika kundi la Amnesty International mjini London. Kwa mara ya mwisho anuani yake ilikuwa: 42 Southfield Road, Oxford, simu namba 42602; na rafiki yake huko aliitwa David King. Baada ya kupokea ujumbe huo, Gordon alimuuliza mkuu wake mjini London nini maana ya kijana tatizo, akajibu ulikuwa msamiati uliotumiwa na BOSS kwa vijana wote waliokuwa wakikataa kuwa wapasha habari ndumakuwili (Double Agents). Baadaye Eric Abraham alizuiliwa nyumbani wakati aliporejea Afrika Kusini. Mara kwa mara BOSS ilikuwa ikitumiwa ama ujumbe au nakala za nyaraka ambazo dhahiri zilichomolewa kutoka katika mafaili ya Amnesty International mjini London. Nyingi ya nyaraka hizo zilichomwa moto zikabaki chache. Mojawapo ni nakala halisi ya barua iliyotumwa na Bibi Tracy Ulltvei Moe kwenda kwa Bibi Jean Etsinger mjini Rio De Jeneiro Brazil, ya tarehe 11 mwezi Februari 1972. BOSS ilikuwa na kawaida ya kutuma nyaraka za Amnesty International zilizogongwa muhuri wa siri kila mwezi. Jasusi anayesimulia kisa hiki (Gordon) amedai kuwa nayo moja ya nakala hizo (Namba 142) ambayo imeorodhesha watendaji wote wa Amnesty International mjini London. Aidha nyaraka hiyo inaonesha mambo waliyokuwa wakiyachunguza katika nchi mbali mbali kama vile Iran, Indonesia, Sudan, Tunisia, Morocco, Ugiriki, Uturuki, Paraguay, Cuba na Ireland ya Kaskazini. Aidha, BOSS ilimjulisha juu ya watendaji wote wapya wa Amnesty International na anuani zao kamili. Bado alikuwa na orodha ya watendaji wapya wa Amnesty International wa mwaka 1970 ikiwa na majina 49. Hilo laweza kuwa jambo litakalowastaajabisha wakuu wa Amnesty International wakizingatia umakini wao kiusalama. Watashangaa ni nani aliyefichua majina ya watendaji wa shirika hilo. Hiyo ilikuwa kazi ya BOSS!
Mwanachama wa Amnesty International Namba 233 aliorodheshwa kama Viktor Melleney mkazi wa Barabara ya 40 Grosvenor, Chiswick, mjini London W4. BOSS ilimpeleleza jamaa huyu iwapo ni yule aliyekuwa muigizaji na mtayarishaji mashuhuri wa michezo ya kuigiza Afrika Kusini, Viktor Mellene, au ni mmoja wa jamaa zake. Kwa kweli, hakuwa huyo.