2. MAZISHI NDANI YA TEHRAN
Sehemu ya Kwanza.
Julai 23, 2011, saa kumi na nusu na nusu mchana (4:30 pm), watu wawili wenye bunduki wakiwa na pikipiki walitokea katika mtaa wa Bani Hashem kusini mwa Tehran, wakatoa silaha kutoka katika makoti yao ya 'leather' na kummiminia risasi mtu aliyekuwa katia harakati za kuingia nyumbani kwake. Wakapotelea kusikojulikana baada ya mauaji kitambo kabla ya polisi kufika. Aliyeuawa alikuwa Darioush Rezaei Najad, miaka 35, profesa wa fizikia, na mtu muhimu katika programu ya silaha za siri za nuclear za Iran.
Alikuwa kiongozi katika utengenezaji wa switch za kielektroniki kwaajili ya kuwahia kichwa cha bomu la nuclear.
Rezaei Najad hakuwa mwanasayansi wa kwanza wa Iran kukutana na mwisho mbaya.
Rasmi ilifahamika kuwa, Iran inatengeneza tecknolojia ya nyuklia kwa matumizi salama, na walisema kuwa kinu cha Bushehr, chanzo muhimu cha nishati kilochotengenezwa kwa msaada wa Urusi, ilikuwa ushahidi tosha wa nia yao njema. Ila pamoja na kinu cha Bushehr, vituo vingine visivyo rasmi vinavyojishughulisha na nyuklia vilishagundulika, vyote vikiwa na ulinzi mkali na visivyoweza kufikika kirahisi. Baada ya muda Iran ililazimika kukubali uwepo wa baadhi ya hivi vituo, japo walikataa tuhuma za kutengeneza silaha ndani ya vituo hivi. Ila kufikia hapo, tayari taasisi za kiupelezi kutoka mataifa ya magharibi na taasisi za siri za ndani zilishaweka wazi jinsi baadhi ya wanasayansi katika vyuo vya Iran walivyopewa dili la kutengeneza bomu la kwanza la nyuklia la Iran.
Ndani ya Iran, zile zilizoweza kujulikana tu kama 'taasisi zisizofahamika' ziliendesha vita kali ili kuzuia programu hii ya siri ya silaha za nyuklia.
Tarehe 29 ,mwezi wa kumi na moja, 2010, saa moja na dakika harobaini na tano asubuhi (7:45am), kaskazini mwa Tehran, pikipiki ilitokea nyuma ya gari la Dr. Majid Shahriyari, kiongozi wa kisayansi wa mradi wa nyuklia wa Iran. Wakati akilipita gari, mwendesha pikipiki aliyevalia kofia ngumu aligundisha 'kifaa' katika kioo cha nyuma cha gari. Sekunde chache baadae kile 'kifaa' kililipuka na kumuua yule mwana fizikia wa miaka 45 na kumjeruhi mkewe.
Vivyo hivyo, katika mtaa wa Atashi kusini mwa Tehran, mwendesha pikipiki mwingine alifanya vilevile kwa gari aina ya Peugeot 206 mali ya Dr. Fereydoun Abassi-Davani, mwanasayansi mwingine wa nyuklia. Mlipuko ulimsababishia Abassi-Davani majeraha pamoja na mkewe.
Mara moja serikali ya Iran ikawanyooshea Mossad kidole. Uhusika wa hawa wanasayansi wawili kwenye mradi wa silaha za atomi za Iran ulifahamika kwa siri, ila Ali Akbar Salehi, kiongozi wa mradi, alitangaza kwamba lile shambulio limemfanya Shahriyari kuwa 'shahidi' na limeondoa ua pendwa katika timu yake.
Rais Ahmadinejad, pia, alionyesha shukrani zake kwa hao watu wawili kwa namna ya kipekee kabisa. Mara tu baada ya Abassi-Davani kupona majeraha yake, Ahmadinejad alimteua kama makamu wa rais Iran. Watu walioshambulia hawa wanasayansi hawakuwahi kupatikana.
Januari 12, 2010 saa moja na dakika hamsini asubuhi (7.50am), Profesa Masoud Ali Mohammadi alikuwa akitoka nyumbani kwake katika mtaa wa Shariati, Gheytarihe, kaskazini mwa Tehran. Alikuwa njiani kuelekea kwenye maabara yake katika chuo kikuu cha tecknolojia cha Sharif. Alipojaribu kufungua mlango wa gari yake, mlipuko mkubwa ulitikisa mtaa huu uliotulia. Maafisa wa usalama waliowahi eneo la tukio walikuta gari ya Mohammadi iliyopasuliwapasuliwa na mlipuko na vipande vya mwili wake.
Aliuawa na mlipuko wa bomu lililofichwa katika pikipiki iliyokuwa kando ya gari lake.
Vyombo vya habari vya Iran vilitangaza kuwa Mohammadi aliuawa na Mossad.
Rais Ahmadinejad alitangaza kuwa,"haya mauaji yanatukumbusha mbinu za ki-zayoni".
Profesa Mohammadi, miaka 50, alikua ni mtaalam wa 'quantum physics' na mshauri katika programu ya silaha za nyuklia za Iran. Vyombo vya habari vya ulaya vilitangaza kuwa Mohammadi alikua askari wa jeshi la walinzi wa mapinduzi 'Revolutionary guards', jeshi lililoegemea mrengo wa serikali.
Ila maisha ya Mohammadi, kama tu kifo chake, yalijaa mafumbo na sintofahamu. Baadhi ya marafiki zake walisema kuwa alihusika tu katika tafiti za kinadharia, ila sio katika miradi ya kijeshi; kuna waliosema kuwa aliunga mkono wale wanaoipinga serikali na alishiriki katika maandamano ya kuipinga serikali. Ila ajabu ni kuwa, nusu ya waliohudhuria katika mazishi walikua wanajeshi wa jeshi la ulinzi wa mapinduzi 'revolutionary guards'.
Jeneza lake lilibebwa na maofisa wa 'Revolutionary Guards'. Uchunguzi uliofuata ulionyesha kweli kuwa Mohammad alijihusisha sana kuendeleza matamaanio ya nyuklia ya Iran.
Januari 2007, Dr. Ardashir Hosseinpour, inasemekana aliuawa na mionzi yenye sumu. Habari za mauaji yake ziliandikwa kwenye gazeti la 'Sunday Times' London, likionyesha taarifa zilizopatikana kutoka katika moja 'think tank' iliyopo Texas.
Maafisa wa Iran walizinanga hizo ripoti, wakidai Mossad haikuwa na uwezo wakufanya operesheni kama hiyo ndani ya Iran, na kwamba, "Profesa Hosseinpour alikufa kwa kukosa hewa baada ya kuvuta moshi uliosababishwa na moto kwenye nyumba yake".
Walisisitiza pia kwamba, profesa huyu mwenye miaka 44 alikuwa mtaalam wa kutukuka wa 'electro-magnetic' na hakuhusika na miradi ya nyuklia ya Iran kwa namna yeyote.
Ila ilikuja kufahamika kuwa Hosseinpour alifanya kazi katika kituo cha siri cha Isfahan ambapo uranium ilibadilishwa kuwa gesi. Hii gesi ilitumika kuongezea uranium ubora katika kinu cha Natanz, kilichokuwa mbali chini ya ardhi na chenye ulinzi mkali. Mwaka 2006, Hosseinpour alizawadiwa nishani ya juu kabisa ya sayansi na tecknolojia Iran; miaka miwili kabla, alikua amezawadiwa na nchi yake nishani ya kutukuka katika tafiti za kijeshi.
Itaendelea...
Usikae mbali..