Vituko Na Mikasa Vya Mirungi Na Walaji Mirungi
(Kama inavyoitwa petroli dhahabu nyeusi, Mirungi inaitwa na walaji wake dhahabu ya kijani).
Matukio yafuatayo hapa chini ni ya kweli yamewahi kutokea na hakuna kilichozidishwa; yanathibitishwa na walaji katika sehemu hizo:
1. Mmoja wa wasagaji Mirungi alipohandasika alitundika koti lake pale alipo nzi ukutani akidhani ni msumari, na la kushangaza zaidi, ni pindi nzi yule aliporuka kuhamia kwengine, bwana yule alimfuata pale anapotua na kujaribu kutundika koti lake kwa mara ya pili.
2. Mwengine alijigonga kwenye mti wa stima barabarani na kuuomba msamaha akidhani amemgonga mpita njia mwenzake.
3. Dereva mmoja wa Taksi huko Arusha alikuwa amembeba abiria mzungu aliyekuwa akielekea kituo cha ndege cha KIA (Kilimanjaro International Airport) ambacho kipo katikati ya mji wa Arusha na Moshi, kwa kupandwa na Handasi, alijikuta akikipita kituo hicho na kufika Moshi mjini. Akaanza kuuliza kituo kiko wapi pamoja na kwamba anakijua kilipo kituo ila ni ulevi wa Mirungi umempoteza-, akaulizwa Kwani wewe umetokea wapi? Akajibu, Arusha, akaambiwa, Mbona kituo umekipita huko nyuma kabla hujaingia Moshi?
akachanganyikiwa na kuanza kurudi kwa kasi, hata alipofika kituoni, Abiria keshakosa ndege!!
4. Na huko Australia: Bwana na Bibi McDavitt wa huko Perth (Australia) walipewa zawadi ya mmea na rafiki yao wa Kiafrika ili wauoteshe katika bustani yao kubwa nzuri iliyopo mbele ya nyumba yao. Mti ulikuwa mkubwa na mzuri wa kuvutia. Mti ulipokuwa mkubwa kiasi, rafiki yake wa Kiafrika aliomba apunguze (pruning) majani na matawi ya huo mti huo ili uendelee kuwa mkubwa na wa kuvutia. Mtindo huu uliendelea mara kwa mara na kila mara mti unapoanza kuchipuwa vizuri, yule rafiki Mwafrika akawa anakuja na kuomba kupunguza matawi na majani kama ilivyo kawaida yake. Lakini siku moja, Bwana na Bibi McDavitt walishtuka walipoona watu wengine wa Kiafrika (na sio rafiki yao wa kila siku) wakikata matawi bila ya rukhsa yao. Hapo ndipo walipopatwa na wasiwasi kuhusu mti huo. Na baadaye wakagundua ya kuwa mti huo ni mti wa Mirungi! Wakaamua kuukata.
5. Na Djibouti: Tani kumi za Mirungi hupelekwa kila siku kwa ndege kutoka Ethiopia kuelekea Djibouti. Katika uwanja wa ndege, hakuna mgeni anayengojewa kwa hamu kama mgeni huyo (Mirungi). Zaidi ya magari 300 yanakuwa tayari kwenye kiwanja cha ndege kumpokea mgeni huyo wa thamani. Wafanya biashara wa Mirungi wanaitwa Masultani wa Qaat. Ilitokea siku moja watu kushikwa na kiwewe kiwanja cha ndege walipopata habari ya kwamba huenda Mirungi isiwasili siku hiyo kwa sababu fulani fulani. Ilitokea fujo katika nchi na ilikuwa ni siku ya huzuni na watu waligoma kuondoka kiwanja cha ndege. Punde si punde, ndege iliwasili na watu walipopata habari hiyo, basi walikumbatiana kwa furaha na kupeana mikono kama vile ni Siku Kuu. Djibouti imekataa kupiga marufuku mirungi kwa sababu inaingiza serikalini kila mwaka faida ya dollar 15,000,000.- Kwa hivyo, umefanya mkataba wa Kiserikali baina ya Djibouti na Ethiopia kuhusu kutochelewesha mirungi hata siku moja.