Mikasa ya ajabu niliyoishuhudia kwa macho yangu

LwandaMagere

JF-Expert Member
Mar 15, 2020
264
2,471
Habarini za kutwa wanajamvi ,bila shaka wote mko bìèn!.

Kwanza kabisa nianze kwa kusema ninayo mikasa miwili ambayo nimewahi kuishuhudia kwa macho yangu na kuifanya kwa mikono yangu mwenyewe,mkasa wa kwanza ulituhusu mimi na ndugu zangu ambapo wakati huo nikiwa nina miaka 14 - 15 mwaka 2000 - 2001 huko mkoani Mara,wilaya ya Tarime,nchini Tanzania.
Mkasa wa pili unanihusu mimi mwenyewe pia,huu mkasa niliufanya wakati ambapo nishakuwa mtu mzima,hii ilikuwa kuanzia mwaka 2012 - 2018,mkasa huu unahusu maisha ya kitajiri yaliyohusisha nguvu za giza.
Kuna nyuzi kadhaa humu nimekuwa nikizisoma za watu mbalimbali kusimulia visa na mikasa ya maisha yao au jamaa zao ambayo waliwahi pitia. Hivyo nami nikaona sasa ni muda muafaka wa kuleta simulizi nilizo pitia maishani ili kuwafundisha na kuwaonya vijana wenzangu wote wenye tamaa ya kutafuta mali kwa njia niliyoifanya mimi waache mara moja kwani Mwisho wake unaweza kuwa kifo mikononi mwa shetani,ingawa mimi niliponea chupuchupu.


MKASA WA KWANZA - MWAKA 2000 - 2001.


Sehemu ya 1.


Nilizaliwa mwaka 1986 wilayani Tarime,mkoa wa Mara,nchini Tanzania.Wazazi wangu walinipatia Jina ambalo nisingependa niliweke wazi,ila jina maarufu au a.k.a nafahamika kama Lwanda Magere,kwenye tumbo la mama yangu tulizaliwa watoto 4,mtoto wa kwanza ni dada yetu mkubwa,mtoto wa pili ni kaka yangu ambaye alimfuatia dada yangu kuazaliwa,mtoto wa tatu ni dada yangu mwingine ambaye ndiye niliyemfuatia katika uzao,na mwisho kabisa nilizaliwa mimi.Elimu yangu ya msingi niliipata kwenye shule mbili tofauti,kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu,nilisoma shule ya msingi Sabasaba,hiyo ilikuwa mwaka 1997 - 1999;Darasa la nne mpaka la saba nilisoma shule ya msingi Turwa,hiyo ilikuwa mwaka 2000 - 2003.

Mimi na ndugu zangu pamoja na wazazi wangu tulikuwa tunaishi wilaya ya Tarime,mitaa ya Bomani,(wenyeji wa Tarime wanaielewa vizuri hii mitaa) sisi hatukuwa wenyeji wa Tarime ila mama na baba walienda huko kikazi miaka ya nyuma, hivyo tukajikuta tumekuwa wenyeji wa huko,ndugu zangu walionitangulia katika uzao,wao walizaliwa mkoani Mwanza,ila mimi pekee ndiye niliyezaliwa Tarime.Wazazi wangu kikabila ni Wasukuma,mama yangu alikuwa mwenyeji wa wilaya ya Kwimba,akitokea kijiji kimoja kinaitwa Sumve;Baba yangu yeye alikuwa mwenyeji wa wilaya ya Misungwi.Baba yangu alikuwa ni mtu wa kusafiri sana kikazi na mama yangu yeye kazi alikuwa anazifanyia pale mjini,japo pia walikuwa wakitoka kikazi mikoani,anaweza kukaa hata miezi 6 hajarudi nyumbani,mama alikuwa akifanya kazi kwenye kampuni ya ujenzi,hivyo nadhani zile pilika pilika za ujenzi pia zilimfanya kuwa bize sana.Baba yangu yeye alikuwa akifanya kazi kwenye shirika lisilokuwa la kiserikali,kwa wakati huo kwakuwa nilikuwa mdogo sikuweza kufahamu hilo shirika lao lilikuwa likijihusisha na kitu gani.

Siku moja baba alipata safari ya kikazi kwenda mkoani Singida ambako alikaa kama miezi miwili, aliporudi alirudi na dada mmoja mwenye asili ya kiarabu(half cast)akiwa kama mfanyakazi wa ndani,kwa maelezo ya baba ni kwamba,yule dada alikuwa ni mfanyakazi wa ndani,nakumbuka mama yangu alimfokea sana baba akimtuhumu kwamba uenda yule mwanamke anaweza akawa mchepuko wake, ila baba anazuga kwamba ni mfanyakazi(siunajua tena mambo ya wivu).Baadae mambo yalikaa sawa,yule dada akawa mfanyakazi wa ndani pale nyumbani kwetu,Kiukweli alikuwa mzuri sana, kwasababu tulifundishwa nidhamu na heshima,tulimheshimu kama dada yetu na tukampenda pia.Siku zikasonga,hatimaye miezi nayo pia ikakata tukiishi kwa furaha,amani na upendo.
Wakati huo nakumbuka ilikuwa mwezi wa 12 mwaka 2000.Baba alihamishwa kikazi kupelekwa jijini Dar es salaam,hivyo pale nyumbani tukabaki na mama ambaye pia alianza kusafiri kikazi na kukaa hata miezi 5 au 6 hajarudi nyumbani, kilichokuwa kinafanyika ni kutumiwa pesa ya matumizi na kutupigia simu kutujulia hali.

Baada ya siku kadhaa kupita, siku moja usiku yule dada wa kazi, alituita sebuleni mimi pamoja na wale dada zangu akatueleza ya kwamba,yeye anawageni wake ambao ni ndugu zake watakuwa wanakuja kumtembelea kila mwisho wa mwezi,kwa kuwa tulifundishwa ukarimu, hivyo hatukuona taabu, ila alitueleza ya kwamba hao ndugu zake wanamashariti makali na inapaswa tuyaelewe ili watakapokuja tusipate taabu,hivyo sababu ya kutuita ilikuwa ni kutupa namna iliyo bora ya kuwapokea hao ndugu zake!.Kiukweli mimi nilipata mshituko kidogo, nilijiuliza maswaĺi kadhaa lakini sikupata majibu, tulikuwa tumezoea kuwapokea wageni mbalimbali siku zote na walikuwa wakija bila masharti!,sasa nikawa najiuliza hao ni wageni wa namna gani waliokuwa na masharti tena akasema ni makali na kila mtu anapaswa ayafuate si ombi bali ilikuwa ni lazima!.

Watu wote pale sebuleni tulikaa kimya,nilikuwa nikiziangalia sura za dada zangu zilibadilika ghafla na kuonyesha huzuni.Basi masharti yenyewe yakawekwa bayana kama ifuatavyo:-

1. Siku hiyo wote tutavaa nguo za kulalia(pajama)nyeupe.

2. Siku hiyo vyumba vya kulala vihakikishwe vinakuwa safi isionekane hata nukta ya uchafu.

3. Kabla ya kufika kwa wageni,ukihitaji kuoga basi hakikisha unaenda kuoga na sabuni ambayo alikuwa akiitumia yeye huyo dada wa kazi.

siikumbuki ile sabuni lakini ilikuwa na marashi makali sana na yenye harufu ya kupendeza.

4. Akawaambia dada zangu kwamba,siku hiyo ambayo wageni wake walikuwa wanakuja,endapo kuna mtu atakuwa kwenye siku zake za hedhi,basi hakutakiwa aonekane pale nyumbani maana angejuta!.


Hayo ndiyo yalikuwa masharti tuliyopewa siku hiyo.


Itaendelea.......................
 
tea.jpeg
 
MKASA WA KWANZA- Sehemu ya 2.


Inaendelea.............


Basi kwakuwa ilikuwa ni usiku tulipomaliza hicho kikao cha kumsikiliza dada wa kazi ilibidi kila mtu aelekee chumbani kwake kulala,ile nyumba ilikuwa kubwa,ilikuwa na vyumba 4 hiyo ni mbali na sebule,chumba cha kulia chakula,jiko,bafu na choo;Mimi nilikuwa nalala mwenyewe chumbani kwangu,dada yangu mkubwa alikuwa akilala chumba chake mwenyewe,yule mfanyakazi alilala na yule dada yangu niliyekuwa nikimfuatia mimi katika uzao, kilicho baki kilikuwa ni chumba cha wazazi wangu.
Yule kaka yangu ambaye yeye alikuwa akimfuatia dada yetu mkubwa katika uzao,alikuwa akiishi mkoani Mwanza kwa shangazi yetu wakati huo,hivyo hapo nyumbani niliishi mimi,wazazi wangu na ho dada zangu.

Kuishi hivi ndiyo ilikuwa desturi yetu na endapo wageni walikuwa wakitutembelea hapo nyumbani ilibidi yule dada yangu nilimfatia akiache chumba chake akalale na dada yetu mkubwa ili chumba chake wageni walale,na kama walikuwa wa kiume basi nililala nao kwenye chumba changu.Basi ilipofika jumapili,yule dada wa kazi aliwaambia dada zangu kwamba,kwa kuwa jumapili ni siku ya gulio(soko),ilitupasa kwenda kununua hizo Pajama alizotuambia siku ile ya yale masharti ya wageni wake,wenyeji wa Tarime nadhani watakuwa wanaelewa kila jumapili ilikuwa wanaita "siku ya soko" ilikuwa kama mnada,yaani siku hiyo wafanya biashara,wakulima wote wa ndani na nje(Kenya)walileta biashara zao kuuzwa hapo sokoni,,hivyo hata kama ungehitaji kitu gani cha bei rahisi basi ungekipata hapo gulioni siku hiyo,sijajua kama bado huu utaratibu upo mpaka leo au ulishabadilika maana nina muda mrefu sijarudi Tarime.

Gulio hili lilikuwa linafanyika karibu na shule ya msingi Sabasaba,ilikuwa nyuma ya jengo la ccm la wilaya,hivi viwanja nakumbuka vilikuwa vinaitwa viwanja vya Mwenge,kama sijakosea.Siku hiyo tulijiandaa wote na tukatoka kuelekea mjini,kwakuwa enzi hizo hakuna bodaboda tulitembea mpaka mjini na ilikuwa ni kitu cha kawaida kutembea tofauti na leo,umbali tuliotembea ingekubidi upande boda boda.Kila mtu alikuwa na shauku ya kuwashuhudia wageni wa dada wa kazi,basi tulifanikiwa kuzipata hizo nguo za kulalia (Pajama)nyeupe ingawa zangu zilikuwa kubwa sana ila niliambiwa zitapunguzwa na zitanifaa,japo haikuwa kazi nyepesi kuzipata ila tulifanikisha.

Safari ya kurejea nyumbani ilianza kama kawaida tuliuchapa mwendo wa miguu na hatukuona shida maana tulishazoea kutembea,kwa miaka hiyo haikuwa ajabu sana,mbali ya Pajama pia tulinunu nguo nyingine za kushindia,ilimradi kila mtu alifurahi kwa mitoko aliyoipenda.Nakumbuka hiyo ilikuwa katikati ya mwezi huo wa 12,na ilipofika kama siku mbili kabla ya mwezi kuisha,alituita tena baada ya kula na alitukumbushia tena yale masharti aliyotupatia kwenye kikao cha mwanzo,na alituambia kwamba kesho kutwa kwa kuwa ndiyo mwezi unaisha tujiandae kuwapokea ndugu zake!,sasi bila wasiwasi kila mtu alisema yupo tayari kwa mapokezi!.

Pale nyumbani nakumbuka tulikuwa na mlinzi ambaye mchana kutwa anakuwa kwenye shughuli zake na ilipokuwa ikifika jioni ya saa 12 ndiyo anakuja kwa kazi ya ulinzi,alikuwa mzee fulani hivi mnywaji wa pombe na kimuonekano alikuwa wa ajabu sana ila alikuwa na uwezo wa kuongea kiingereza,kifaransa,kireno na kikurya kwa ufasaha kabisa!,japo ulikuwa ukimuangalia huwezi amini,mama alikuwa akituambia kwamba,huyo mzee alikuwa amesoma sana,sema bangi na pombe zilimletea uwendawazimu,alikuwa akiitwa Mniko(Muniko)sijui kama nipo sahihi kwa namna linavyotamkwa,siunajua tena majina ya kikurya!,sisi tulipenda kumuita mzee Mniko.Basi yule dada wa kazi alimwambia dada yangu mkubwa amwambie mzee Mniko siku watakayo kuja hao ndugu zake asije akanywa pombe,alimwambia ambembeleze siku hiyo ajizuie kunywa,Yule mzee alikuwa mbishi sana,akawa anapayuka maneno ya kashfa kwamba,hakuna mtu wa kumzuia kunywa pombe kwasababu ni sehemu ya maisha yake!,tangu mwanzo huyu mzee Mniko na yule dada wa kazi walikuwa hawapatani kabisa,sijajua shida ilikuwaga ni nini,hivyo yule dada wa kazi kuliepuka shari la mzee Mniko ilibidi amtume dada mkubwa akaongee naye uenda angemuelewa,lakini mzee alibwata kwa ghadhabu kwamba hakuna wa kumzuia kunywa pombe na kama ni sheria basi huyo mdada wa kazi azipeleke huko kwao alikotoka!.

Basi kwakuwa yule mzee tulimzoea tulichukulia kawaida ila dada wa kazi alimsihi sana dada kwamba hata kesho yake pia aongee naye.Siku moja kabla ya tukio la kuwapokea wageni kila mtu alikuwa bize na ishu zake za hapa na pale ikiwemo usafi wa nguo pamoja na vyumbani,kiukweli hatukutaka kum-disapoint yule dada wa kazi kwani kila mtu alitii maelekezo bila shuruti!.


Itaendelea........................
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom