Hapatoshi Diamond kesho
Mwandishi wetu
BAADA ya huzuni na simanzi ya mateso na kifo cha Yesu Kristo kwenye vilima vya Golgotha, Jerusalum, kesho itakuwa siku ya kipekee kwa Wakristo wote duniani kutokana na ushindi wa mwana wa Mungu dhidi ya kifo, ikiwa ni alama ya ukombozi wa mwanadamu kutoka kwenye minyororo ya dhambi.
Alfajiri ya kesho, mfuasi wa kweli Yesu, Mariam Magdarena, na wenzake, wakiambatana hadi katika pango ambamo mwili wa Yesu Kristo ulikuwa umehifadhiwa, wakakuta mambo tofauti.
Baada ya kufika pale, walipigwa butwaa wasiamini walichoshuhudia, jiwe lililokuwa limeviringishwa katika kaburi, likiwa limesogezwa kando ukiwa ni utimilifu wa mpango wa Mungu kumleta Yesu duniani kuukomboa ulimwengu kupitia mateso na kifo, lakini siku ya tatu anafufuka.
Siku ile, Mariam Magdarena na wenzake, wakashuhudia sanda iliyokuwa imefungwa kwenye mwili wa Yesu, ikiwa kando.
Katika lindi la mshangao, anatokea malaika wa Mungu na kuwaambia, wanayemtafuta, amefufuka kutika wafu na amewatangulia Galilaya, hivyo Mariam Magdarena na wenzake kuwa mashahidi wa kwanza juu ya ufufuko wa Yesu.
Kwa kutambua uhuhimu wa siku ya Pasaka, Kampuni ya Msama Promotins ya jijini Dar es Salaa, ikaamua kutoa nafasi kwa wakristo na wengineo kuisindikiza siku hiyo kwa shangwe na furaha ya aina yake.
Zawadi pekee iliyoandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions chini ya Mkurugenzi wake Alex Msama, ni Tamasha la kimataifa la muziki wa injili ambalo litafanyika kesho kuanzia saa nane mchana kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo ambalo limekuwa gumzo kila kona ya jiji la Dar es Salaam, mgeni rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mkuu wan chi kuwa mgeni rasmi katika historia ya matamasha ya injili nchini.
Rais Kikwete akiwa mkuu wa nchi iliyojengwa kwenye misingi imara ya amani, utulivu na uhuru wa kuabudu, kesho ataungana na wakristo katika tamasha hilo akitambua maana, umuhimu na thamani ya Pasaka kwa Wakristo.
Kwa upande wa Msama, anasema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwani maandalizi yote yamekamilika kwa asilimi 100 na hasiti kutoa pongezi kwa Rais Kikwete kwa kukubali kuwa mgeni rasmi.
Msama anasema, kutokana na majukumu mengi yanayomkabili mkuu wa nchi, kitendo cha Rais Kikwete kukubali kubeba jukumu la kuwa mgeni rasmi, hakidhihirishi umuhimu wa Pasaka tu, pia upendo wake wa dhati kwa watu wote bila kujali dini.
Kwa hali hiyo, Msama anatoa wito kwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili na wananchi kwa ujumla wa jijini Dar es Salaa na vitongoji vyake, kujitokeza kwa wingi kuisindikiza Pasaka wakiwa na mkuu wa nchi.
"Kamati yangu imejitahidi kufanya kila iwezalo kuhakikisha tamasha hili linakuwa lenye kiwango cha ubora wa hali ya juu, hasa ikizingatiwa mkuu wa nchi ndiye atakuwa mgeni rasmi, hivyo nawaomba wadau wa muziki wa injili tujumuike Diamond Jubilee" anasema Msama.
Kuhusu waimbaji, Msama anasema wamejiandaa vya kutosha kutoa burudani ya hali ya juu kwa kadiri roho wa Mungu atakavyomjalia kwa sababu pamoja na maandalizi, baraka za Mungu zinahitajika na kuongeza kuwa, waimbaji wote wakiwamo kutoka nje ya Tanzania, wapo tayari kwa ajili ya kesho.
Waimbaji ambao kesho watapamba Tamasha hilo linalotarajiwa kuvuta maelfu ya wapenzi, mashabiki wa muziki wa Injili na wananchi kwa ujumla, ni Rose Muhando, Upendo Nkone, Christina Shusho, Martha Mwaipaja na Boniface Mwaitege.
Mbali ya hawa kutoka Tanzania, wengine Annastazia Mukabwa, Pamela Wanderwa, Geraldine Odour aliyeshiriki kwenye albam ya Haleluya Collection Vol 5 ambayo pia itazinduliwa rasmi hiyo kesho na Solomon Mukubwa wote kutoka Kenya.
Waimbaji wengine katika tamasha hilo ni Ephraem Sekeleti kutoka Zambia na Faraja Ntaboba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa upande wa waimbaji, Muhando mwimbaji bora wa mwaka 2009, kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), anasema kwa maandalizi ambayo kila mwimbaji ameyafanya, kwa uweza wa Mungu, litakuwa tamasha la pekee kabisa.
"Ndiyo unajua kila jambo lina wakati na baraka zake, kwangu Rose naamini tamasha la safari hii, litakuwa la tofauti kwetu waimbaji kwa sababu inaonekana kila mwimbaji amefanya maandalizi ya kutosha tukijua utofauti wa tamasha la safari hii na mengine yaliyotangulia," anasema Rose.
Je, ni utofauti upi huo, Rose anasema utofauti mkubwa ni wao kuisindikiza Pasaka pamoja na mkuu wa nchi (Rais Kikwete) na kukiri kuwa, amewahi kushiriki matamasha mengi, lakini la safari hii, litabaki kuwa la kumbukumbu kwake," anasema.
Kwa niaba ya waimbaji wenzake, Rose anasema kesho ni siku ya furaha kuu kwani wanafurahia ushindi wa Yesu Kristo dhidi ya dhambi wakiwa na Rais na kusema, kwa Wakristo, ni kitu cha thamani kubwa.
Zaidi ya yote hayo, kwake (Rose) siku ya kesho ni zaidi ya tamasha kwani anakumbuka siku ya ubatizo wake, hivyo atafurahi kujumuika na waimbaji wengine wakiwemo kutoka nje ya nchi kuifurahia Pasaka.
"Nashukuru kupata nafasi hii ya kuimba kwenye tamasha kubwa la Pasaka, ni nafasi ya kipekee kwangu kujumuika na waimbaji wengine kufurahia ushindi wa Yesu Kristo pale Msalabani," alisema Mwaitege kwa njia ya simu.
Kuhusu maandalizi, Mwaitege amesema tayari amejipanga kwa kwa lengo la kutoa burudani ya kutosha kwa kadIri Mungu atakavyomjalia kwa sababu yote hutoka kwa Mungu, mwanadamu unaweza kupanga hivi, lakini ikawa vile.
Naye Upendo Nkone ambaye ni kati ya waimbaji watakaopamba jukwaa la Diamond Jubilee mbele ya Rais Kikwete, anasema ni furaha kubwa kwake kujumuika na waimbaji wengine.
Naye Nkone, anasema: "Nashukuru sana kupata nafasi hii ya kujumuika na waimbaji wengine na wananchi kufurahia ushindi wa Yesgu Kristo dhidi ya kifo, kama nitaifikia siku hiyo, nitarukaruka kwa furaha kubwa kwenye Ukumbi wa Diamond," anasema.
Anasema pamoja na malengo mengine ya uwepo wa tamasha hilo kwa mfano sehemu ya kile kitakachopatikana kuwafariji yatima, wajane na wengine wenye shida, anatoa wito pia kwa kila atakayefika Diamond Jubilee, autumie nafasi hiyo kusamehe wengine.
"Natoa wito kwa wote watakaofika Diamond Jubilee, kuwa na furaha pamoja na ufufuko wa Yesu Kristo kwa kungua mioyo yao wakiwasamehe wengine hata waliowakosea kwa sababu mungu anasema mpende jirani yako kama nafsi yako.
Christina Shusho kwa uopande wake, hakuna na mengi ya kusema isipokuwa amewawataka wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili wasikose kwenda ukumbi wa Diamond Jubilee kupata baraka za Mungu kupitia uimbaji.
Viongozi wa kiroho, pia hawakubaki nyuma kulizungumzia tamasha la leo na mengine yatakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na lile la keshokutwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Askofu wa Kanisa la Mungu mkoani Dodoma, Donald Mhango anasema tamasha la leo na mengine, yamenekana kuwagusa wengi kwani mbali ya kueneza ujumbe wa neno la Mungu, pia sehemu ya kile kitakachopatikana kusaidia wenye shida.
Anasema, kusaidia wenye shida kama vile yatima, wajane, ni jambo jema linalopaswa kuungwa mkono na kuwataka wapenzi na mashabiki wa nyimbo za Injili kujitokeza kwa wingi.
Kauli ya Askofu Mhango, inatokana na mpango wa Kampuni ya Msama Promotions kuahidi kutumia sehemu ya kitakachopatikana watoto yatima, wajane na waathirika wa milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto ambayo ilitokea Februari 16, mwaka huu.
Kiongozi mwingine wa kirogo, ni mchungaji wa kanisa KKKT mkoani Dododoma, Timothy Holela ambaye mbali ya kumpongeza Msama na kamati yake, amewataka wapenzi na wadau wa muziki wa injili kujitokeza kwa wingi.
Mchungaji Holela anasema kama watu watajitokeza kwa wingi katika ukumbi wa Diamond, uwanja wa Jamhuri na Kirumba, itakuwa faraja kwa waandaaji wa matamasha hayo kufikiria kuendelea na huduma hiyo yenye maana kubwa.
Je, baadhi ya mashabiki wa wadau wa muziki wa injili wanasemaje? Luckresia Rainer na Angel Deodatus wa Yombo-Kigilagila,
kwa nyakati tofauti wanasema wamekuwa wakisubiri kwa hamu kubwa Tamasha la Pasaka, hivyo kesho watakuwa kati ya maelfu watakaokwenda Diamond Jubilee.
Mwingine aliyelisubiri kwa hamu kubwa tamasha hilo, ni Annastazia Ferdinand Kobelo pia wa Kigilagila ambaye kwa maoni yake, uwepo wa Muhando na Mukabwa kumemvuta zaidi hasa baada ya kuimba vizuri kwenye albamu ya Kiatu.
Kwa upande wa kiingilio, Msama anasema, kiingilio katika tamasha la kesho, tiketi za viti vya kawaida, zitauzwa sh 4,000; viti vya maalumu (B) sh. 10,000 na viti maalumu (A) sh 20,000.
Aidha, kwa tiketi za viti maalumu vya VIP A zitakazokuwa kama meza za familia, wenye kuzitaka wapige simu 0713 383838, 0786 383838 na 0786 373737 kwa ufafanuzi zaidi kwani hazitapatikana getini.
Kiingilio cha matamsha mengine mawili ya Jamhuri- Dodoma na CCM Kirumba, Mwanza, kitakuwa ni cha aina moja yaani shilingi 3000 kwa lengo la kuwezesha wengi kupata nafasi ya kushuhudia uhondo huo wa nyimbo za injili kutoka kwa waimbaji mahiri kutoka ndani na nje ya nchi.