Kaseba ampiga ngwala Maugo, adundwa
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 18th April 2011 @ 08:09 Imesomwa na watu: 207; Jumla ya maoni: 0
Mwamuzi John Chagu (kushoto) akimuonya bondia Japhet Kaseba baada ya kumchapa ngwala mpinzani wake Maada Maugo kwenye raundi ya saba wakati wa pambano lao lisilo la ubingwa kwenye ukumbi wa PTA Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam. (Na Mpigapicha Maalumu).
BONDIA Maada Maugo Aprili 16 alikuwa mwenye furaha kupita kiasi baada ya kutangazwa mshindi katika pambano la masumbwi uzani wa kati lisilo la ubingwa dhidi ya Japhet Kaseba.
Kutokana na matokeo hayo, Kaseba naye ametangaza kustaafu mchezo wa masumbwi pamoja na ule unaohusisha ngumi na mateke ‘kickboxing' ili kutimiza ahadi yake aliyoiweka kwamba endapo angepoteza mchezo wake na Maugo angestaafu.
Katika pambano hilo lililofanyika ukumbi wa PTA kwenye Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, lilionekana kuwa na ushindani mkali tangu mwanzo, lakini lilikuja kubadilika raundi za mwisho na kusababisha vurugu kwa baadhi ya mashabiki.
Mwamuzi wa pambano hilo, John Chagu alilazimika kumtangaza Maugo mshindi kwenye raundi ya saba, ambayo haikumalizika kutokana na kutokea vurugu na mashabiki wa pande zote mbili kuvamia juu ya ulingo.
Hatua hiyo ilitokana na Kaseba kumpiga ngwala mpinzani wake, jambo ambalo haliruhusiwi katika masumbwi, hivyo mashabiki wa Maugo kupanda ulingoni kwa hasira na wale wa Kaseba nao kupanda ulingoni wakidai Maugo alimchezea faulo bondia wao na ndiyo maana alipanda hasira na kumpiga teke.
Vurugu hizo za mashabiki na wapambe wa mabondia wote zilichukua karibu nusu saa, huku polisi waliokuwepo kwenye ukumbi huo wakifanya kazi ya ziada kuweka hali ya ukumbi kuwa wa amani.
Lakini wakati mashabiki kadhaa wakiwa juu ulingoni Kaseba alivua gloves zake na kutaka kushuka, lakini baadhi ya wapambe wake wakimsihi aendelee kupigana, kwani ilikuwa imebaki raundi moja na wengine wakimtaka ashuke.
Pambano lilikuwa la raundi nane. Hata hivyo bondia huyo aliendelea kubaki ulingoni, huku Maugo naye akiwa ulingoni kila mmoja akiwa amezingirwa na wapambe wake na wengine walikuwa wakibishana kuhusiana na tukio la Kaseba kupiga ngwala.
Lakini baada ya muda, polisi walifanikiwa kuwashusha wote waliokuwa juu ulingoni, kisha mwamuzi akawataka mabondia wote waondoke kwenye kona zao na waende kwenye kona huru.
Baada ya mabondia wote kuitikia wito huo, Chagu ambaye ni mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania, alichukua kipaza sauti na kusema pambano lilikuwa likiendelea, lakini bondia mmoja tayari alishavua gloves na hakuwa nazo, hivyo kulingana na sheria za masumbwi hakuwa na sifa za kuendelea kupigana.
Kutokana na hali hiyo, Chagu alimtangaza Maugo kuwa mshindi wa pambano hilo na kuamsha shangwe kubwa kwa mashabiki wake waliokuwa wamejazana ukumbini hapo, huku wale wa Kaseba wakionekana kunyongea.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Kaseba ambaye amepata kuwa bingwa wa dunia wa kickboxing alisema ameamua kustaafu ngumi pamoja na kickboxing kwani aliweka ahadi hiyo kabla ya mchezo wa juzi kwamba kama akipoteza ataacha.
Hata hivyo alielezea kusikitishwa na namna Maugo alivyokuwa akimchezea faulo, hivyo naye kuamua kulipiza kwa namna nyingine, kwa vile yeye pia alifanyiwa faulo.
Katika pambano hilo lililokuwa linasimamiwa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), chini ya Rais wa oganaizesheni hiyo, Yassin Abdallah lilichangamka zaidi kadri muda ulivyokuwa unaenda.
Maugo alianza pambano raundi ya kwanza na ya pili kwa kupiga ngumi za jab, lakini Kaseba hakuogopa, alisonga mbele akijibu mashambulizi na kuachia ngumi iliyomkamata Maugo na kumpa mshituko.
Raundi hizo za mwanzo walikuwa wanasogeleana na kujibizana mashambulizi ya ana kwa ana.
Mambo yalianza kubadilika raundi ya tatu, ambapo Maugo alikutana na left hook ya Kaseba na kujikuta akianguka chini, ambapo alihesabiwa na kuendelea na mchezo.
Maugo alijaribu katika raundi ya tatu na nne kumweka mbali mpinzani wake, lakini Kaseba
hakutaka kumwachia hivyo kulazimisha ngumi za piga nikupige zitumike.
Raundi ya sita Maugo aliianza kwa kusukuma jab nyingi mwilini mwa, kisha aliachia left hook na right hook fupi na zilizomkamata Kaseba na kumyumbisha, kiasi cha kuonekana kama
mambo yalianza kumgeuka Kaseba, lakini alitulia na raundi ilimalizika salama.
Mchezo ulibadilika raundi ya saba, ambayo iligeuka kuwa ya faulo nyingi kwa mabondia wote, ambapo Maugo alianza kwa kumchezea mwenzake faulo ambayo ni ya kimchezo kabla ya Kaseba kujibu kwa staili iliyosababisha kelele kwa mashabiki.