Wasanii, serikali usingizi mzito
Makuburi Ally
UKITAZAMA mara nyingi watendaji wa kazi za sanaa wamekuwa ni wa kulalamika tu, hali ambayo inaonyesha kwamba sanaa inaelekea kaburini ingawa ina mchango mkubwa wa maendeleo ya jamii.
Umuhimu wa sanaa katika maendeleo yoyote unatokana na kuwa ndiyo dira ya maendeleo ya jamii, kwa sababu asilimia kubwa ya matakwa ya jamii yanapitia katika sanaa kwa kiasi kikubwa.
Ndiyo maana watoto wengi wanajifunza masuala mengi kupitia sanaa, kwa sababu wanajifunza kupitia wasanii bila kujali ni sanaa ipi inayowasilisha jambo kwa hadhira.
Wasanii pia hutumika katika majukwaa ya siasa kwa ajili ya kuleta hamasa kwa hadhira ili wamsikilize mgombea wa nafasi ya uongozi bila kujali kama ni mwenyekiti wa kijiji ama rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lakini pamoja na msanii kuhitajika katika kampeni za kuwania uongozi, mgombea akifanikiwa kupata nafasi, thamani yake inapotea na kukosa mwelekeo hadi uchaguzi ujao, jambo ambalo badala ya kuinuka, wanaanza upya.
Ukitazama wasanii wa Tanzania wenye maendeleo yanayotambulika ni wachache lakini wenzangu na mimi ndio wengi, jambo ambalo linakatisha tamaa maendeleo ya tasnia hiyo.
Hali inayosababisha wasanii kuwa katika hali duni, inatokana na wengi wao kutojitambua katika mpangilio wa kazi zao.
Inaonekana hawatambui taasisi zinazohusika na kazi zao kama Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Chama cha Hakimiliki na Shiriki Tanzania (COSOTA) na wengineo wanaohusika na sanaa.
Inashangaza siku moja Mwanasheria wa COSOTA, Doreen Anthony, aliwahi kutamka kwamba kuna wasanii ambao hata zilipo ofisi za chama hicho hawapafahamu na wengine hata kitu COSOTA, hawakifahamu na shughuli za chama hicho pia hawazifahamu na hawataki kupata elimu kupitia hakimiliki na shiriki.
Sasa kama ni hivyo, inatia mashaka kwa safari ya maendeleo ya sanaa kutokana na kwamba wanaopigiwa chepuo wenyewe hawako tayari kwa mipangilio ya maendeleo.
Mshangao kama huo uliwahi kutolewa na mwanamuziki wa nyimbo za Injili, Stara Thomas, katika mkutano mmojawapo wa mikutano ya sanaa, alijaribu kutazama mwelekeo wao na wasanii wenyewe, alipatwa na kigugumizi.
Katika tamko lake kuhusu maendeleo ya sanaa alishindwa pa kuanzia na badala yake alisema, "Sijui wasanii wana tatizo gani, hatuna umoja ambao utakuwa na sauti itakayofikishia mambo yetu mbele."
Sasa wasanii wanatakiwa kugeuka nyuma na kutazama mienendo yao ili wasake njia mahususi ya maendeleo, badala ya kuendeleza ‘ubwana' ambao ndani ya kipindi kifupi unapotea.
Ukiitathmini sanaa ya Tanzania ina vyama, mashirikisho na asasi nyingi, ambavyo vyote vinapigania maendeleo ya wasanii lakini bado kuna kelele zisizokwisha.
Kwa maana nyingine, sisi wenyewe tutazame kasoro zetu ambazo ni ‘Umiminaizesheni' ambao hautusaidii katika maendeleo tunayohitaji yatufikishe tunakohitaji.
Ingawa katika mipangilio ya kupata maendeleo inatakiwa kila mmoja ajipange kivyake, lakini katika suala ambalo linahitaji umoja, basi lifanyike lakini si fulani anaanzisha wengine hawapendi.
Tubadilike na tusake maendeleo ili tufanane na baadhi ya nchi ambazo ziko juu kimaendeleo kupitia tasnia hiyo.
Tukitazama nchi kama Marekani, uchumi wake unashikiliwa na wasanii ambao pato la nchi kwa asilimia kubwa linatokana na kazi zao sambamba na michezo pia, jambo ambalo wasanii na serikali yetu hawajapeana mikakati ya ukweli ili kutekeleza maendeleo stahili.
Tuipe thamani sanaa yetu kwani kuna baadhi ya nchi wanatumia picha ya msanii mchongaji katika fedha zao, jambo ambalo linaonyesha jinsi wanavyojali sanaa zao.
Serikali pia inatakiwa iwe karibu zaidi hasa kwa kutoa maelekezo mbalimbali kuhusu sanaa kwa vyama kama COSOTA na BASATA ili wasaidie wadau badala ya kuwaacha wapotee kwa kuandaa semina ama vipeperushi ambavyo vitasaidia kutambulisha maendeleo yao.
Sababu za kutofahamika kwa vyama na mabaraza zinatokana na wahusika kuketi ofisini bila ya kusaka namna ya kutambulika kwa jamii, jambo ambalo linashangaza, kwa sababu wasanii wote wako chini yao.