Yanga bingwa 2010/11
Imeandikwa na Na Waandishi Wetu; Tarehe: 11th April 2011 @ 13:00 Imesomwa na watu: 441; Jumla ya maoni: 1
Mabingwa wapya wa Tanzania Bara mwaka 2010/11 timu ya Yanga ya Dar es Salaam.
YANGA ndiyo gangwe la soka Tanzania kwa mwaka 2010/2011.
Hatua hiyo inatokana na ushindi wa mabao 3-0 iliyoupata Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza dhidi ya Toto African ya mjini humo, hivyo kufikisha pointi 49 licha ya
Simba nayo jana kuifunga Majimaji ya Songea mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Simba kama ilivyo Yanga nayo imefikisha pointi 49, lakini Yanga ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, ambapo Yanga ina faida ya mabao 25, wakati Simba yenyewe ina faida ya mabao 24.
"Jamani Simba wenu huyo, jamani Simba wenu atatung'ata huyo, aah Simba mwenyewe kumbe koko… Simba kumbe ngedere, Simba kumbe ngedere," ndivyo mashabiki wa Yanga
walivyokuwa wakiimba jana baada ya kumalizika kwa mchezo wa Dar es Salaam na ule wa
Mwanza.
Ilikuwa raha kwa mashabiki wa Yanga, lakini ilikuwa karaha kubwa kwa mashabiki wa Simba waliokuwa na imani kwamba timu yao ingeibuka na ushindi katika mchezo huo. Yanga sasa itacheza michuano ya klabu bingwa Afrika mwakani, huku Simba ikicheza Kombe la Shirikisho.
Katika mchezo wa Dar es Salaam, Simba ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao mawili, ambapo moja lilifungwa na Shija Mkina dakika ya 11 na Emmanuel Okwi dakika ya 24, wakati la Majimaji lilifungwa kwa penalti dakika ya 42 na Kassim Kilungo.
Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi Alex Mahagi wa Mwanza, baada ya beki Meshack Abel
kumkwatua Mohammed Kijuso aliyekuwa anaelekea langoni. Kipindi cha pili Simba ilicheza kwa nguvu zaidi, lakini umaliziaji ulikuwa mbovu, ambapo ilipata bao la tatu dakika ya 68 mfungaji akiwa Mbwana Samatta, huku lile la nne likifungwa dakika za majeruhi.
Wakati mashabiki wakiamini matokeo hayo yangemalizika hivyo, Jerry Santo aliangushwa
ndani ya eneo la penalti, huku zile dakika za nyongeza zikiwa tayari zimeoneshwa, lakini shuti
la Okwi liligonga nguzo na kurudi uwanjani, hivyo kuwafanya mashabiki wa Simba kuduwaa na kuona kombe walilokuwa wakilishikilia likiwaponyoka.
Wachezaji wawili wa Majimaji, Paul Ngalema na Kulwa Mobi walioneshwa kadi nyekundu jana kwa nyakati tofauti kutokana na mchezo mbaya. Wote walikuwa na kadi za njano, hivyo walioneshwa njano ya pili na kutolewa nje. Katika mchezo wa Yanga na Toto African, mabingwa hao wapya walianza kushangilia bao dakika ya 47 mfungaji akiwa Nurdin Bakari kwa shuti la mbali.
Dakika ya 67 Mzambia Davies Mwape alifunga bao la pili kutokana na krosi ya Shadrack
Nsajigwa, wakati goli la tatu lilifungwa dakika ya 60 na Nurdin Bakari kutokana na krosi ya
Nsajigwa. Matokeo hayo yaliamsha shangwe kwa mashabiki wa timu, hasa baada ya kupata taarifa kuwa Simba ilikuwa imeshinda mabao 4-1, hivyo ilikuwa bado nyuma kwa uwiano wa mabao ya kufunga.
Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Azam iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-1, ambapo mabao ya
washindi yalifungwa na John Bocco na Mrisho Ngasa. Kutokana na bao hilo Ngasa amefikisha mabao 16 na kuibuka mfungaji bora wa ligi hiyo.
Mchezo mwingine ulifanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, ambapo Polisi Dodoma na JKT
Ruvu zilifungana bao 1-1. Bao la Polisi lilifungwa na Bantu Admin, wakati la JKT lilifungwa na Mwinyi Kazimoto. AFC Arusha na Majimaji zimeshuka daraja.
Jumla Maoni (1) Maoni habari leo mko juu sana kutoa habari za kueleweka jitahidini tena kwani ushindani ni mkubwa tupo pamoja daima kulijenga taifa letu la TANZANIA Thank you