Julio kuiponza Tanzania CAF
Amteua Ngasa kikosi cha U-23
na Mwandishi wetu
KATIKA hali inayoonekana kama uzalendo, lakini hatari kwa soka ya Tanzania, mshambuliaji Mrisho Ngassa wa timu ya Azam FC, ameitwa kikosi cha vijana wa chini ya miaka 23.
Kama vile utani, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo, jana aliongeza nyota saba wapya katika kikosi chake akiwemo Ngassa, aliyetua Azam FC msimu uliopita akitokea Yanga kwa kitita cha sh mil. 59.
Ingawa si rahisi kujua mara moja Ngassa alizaliwa lini, lakini katika hali ya kawaida, nyota huyo aliyewahi kukipiga Toto Africa na Kagera Sugar, si chini ya miaka 23.
Hata hivyo, Ngassa ameitwa katika kikosi hicho kwa ajili ya kuwakabili Cameroon katika mechi ya marudiano ya kampeni ya kuwania tiketi ya kucheza michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwakani mjini London, England.
Katika mechi hiyo, Tanzania inapaswa kushinda kuanzia bao 1-0 ili kusonga mbele baada ya wiki iliyopita kufungwa mabao 2-1, mjini Younde, Cameroon.
Hatari inayoikabili Tanzania, kama Ngasa atachezeshwa na kubainika ni zaidi ya umri huo, ni kama ya mwaka 2004 pale timu ya vijana wa chini ya miaka 17, Serengeti Boys ilipoondolewa licha ya kufuzu.
Serengeti Boys chini ya Kocha Abdallah Kibaden ilipokwa tiketi hiyo ya fainali za Afrika kwa kumchezesha Nurdin Bakar.
Licha ya Tanzania kupata tiketi ya kucheza fainali zile ambazo zilipigwa nchini Gambia, kitendo cha kumchezesha Nurdin Bakar aliyekuwa amevuka umri, Tanzania ikaondolewa kwenye fainali zile na kuadhibiwa.
Pamoja na juhudi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Leodegar Tenga kukata rufaa Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), ilikuwa ni kazi bure.
Mbali ya Ngassa, wengine walioitwa jana kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Aprili 9 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ni mshambuliaji wa Yanga, Kigi Makasi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema Julio amewateua wachezaji hao ili kukiimarisha kikosi chake hicho.
Alisema, mbali ya Ngassa na Makasi, wengine ni Ali Lundenga, David Luhende wa Kagera Sugar, Jabir Aziz kutoka Azam, Kelvin Chale wa Simba na Juma Abdul kutoka Mtibwa Sugar.
Katika hatua nyingine, Wambura ametaja viingilio vya mechi hiyo itakayoanza saa
10:00 jioni ni shilingi 1,000 kwa watakaokaa viti vya kijani, bluu na rangi ya chungwa (orange), huku watakaokaa majukwaa ya VIP B na VIP C kiingilio kitakuwa sh 5,000 na VIP A watalipa sh 10,000.
Alisema tiketi za mechi hiyo, zitaanza kuuzwa leo katika vituo vya Oil Com Ubungo, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora/Ohio, Bigbon Msimbazi Kariakoo na Uwanja wa Uhuru. Mechi itaanza saa 10 kamili.
Tayari timu ya Cameroon imewasili nchini jana saa 5:20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways ikiwa na wachezaji 23 na kufikia katika Hoteli ya Paradise City Hotel, huku mwamuzi wa mechi hiyo ni Aime Ndayisenga akisaidiwa na Desire Gahungu, Jean-Claude Birumushahu na Athanase Niyongabo, wote kutoka Burundi na Kamishna wa mchezo huo ni Charles Masembe, kutoka Uganda.