Miwa yailewesha Yanga
• Mashabiki wawashukia viongozi, wachezaji
na Ruhazi Ruhazi
WAKATA miwa wa Mtibwa Sugar ya Manungu Turiani, Morogoro jana walitibua rekodi ya Yanga ya kutopoteza mechi katika Ligi Kuu Bara baada ya kuichapa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Bao pekee lililoizamisha Yanga lilifungwa na mtokea benchi, Juma Javu, dakika ya 70, akiunganisha krosi ya Juma Abdu, aliyeambaa na mpira wingi ya kulia na kumimina krosi iliyowapita walinzi wa Yanga na kumkuta mfungaji.
Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya Yanga kuzinduka na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Mtibwa, lakini kukosa umakini na mbinu kwa washambuliaji wao kukawagharimu kushindwa kusawazisha.
Vincent Barnabas aliyeingia badala ya Ally Mohammed nusura aipigie Mtibwa bao la pili dakika ya 80 lakini shuti lake likambabatiza mlinzi wa Yanga, Chacha Marwa.
Mlinzi chipukizi wa Yanga anayecheza pembeni kushoto Zuberi Ubwa, nusura aipatie Yanga bao la kusawazisha dakika za lala salama lakini shuti lake la mita 30 lilipanguliwa na kipa Shaban Kado na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Hadi mwamuzi Alex Mahagi kutoka Mwanza anamaliza pambano hilo, ni Mtibwa Sugar waliotoka kidedea wakijikusanyia pointi zote tatu, huku mashabiki wa Yanga wakirusha maneno makali nje ya uwanja huo.
Huu ni mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu kwa Yanga kucheza chini ya Fred Minziro, baada ya Kocha aliyeifikisha hapo Kostadin Papic kuiacha timu hiyo wiki iliyopita.
Baada ya mechi hiyo kumalizika, mashabiki waliokuwa na hasira walitaka kumshusha kwenye gari la wachezaji, kiungo wao Godfey Bonny ‘Ndanje', kwa madai kuwa alikuwa akimnyima pasi za kufunga mshambuliaji Mzambia Davies Mwape, kabla ya Jerry Tegete kuokoa jahazi kwa kuwaambia kuwa watakwenda kuyamaliza wenyewe mambo hayo.
Baada ya kumkosa Bonny, mashabiki hao walimvaa Makamu Mwenyekiti, Davis Mosha ambaye alijifungia ndani ya gari lake aina ya Noah, ingawaje mashabiki hao walifanikiwa kuvunja kioo cha nyuma na kumtwanga jiwe akiwa ndani kabla ya gari hilo kuondolewa kwa kasi na kutoweka eneo hilo la uwanja.
Mashabiki hao, ambao walikuwa wamegawanyika makundi kila moja likilaumu baadhi ya viongozi, pia walimweka kati mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Mohammed Bhinda kwa madai hayo hayo ya kuwashawishi wachezaji kucheza chini ya kiwango, lakini alijitetea na kupona kupokea kibano.
Mosha akizungumzia hali hiyo, alisema itafika wakati wataachia Yanga hao, kwani anaona hakuna kitu kinachoendelea, ingawa yeye yuko hapo kwa ajili ya kutetea masilahi ya wanachama ambao ndio waliomchagua.
Vikosi Yanga, Nelson Kimathi, Fred Mbuna, Abuu Ubwa, Chacha Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro', Godfrey Bonny, Juma Seif, Jerryson Tegete, Davies Mwape na Kigi Makasi/Nsa Job.
Mtibwa Sugar, Shaban Kado, Juma Abdu, Yussuf Nguya, Obadia Mungusa, Salum Swedi, Julius Mrope, Faustin Lukoo, Omari Matuta, Ally Mohammed/Vincent Barnabas na Lameck Dayton/Yussuf Mgwao/ Hussein Javu.
Leo Simba inashuka katika dimba hilo kuvaana na African Lyon katika mfululizo wa ligi hiyo.