JOHN ONDOLO CHACHA: Mtoto wa mwanamuziki aliyerithi soka
Makuburi Ally
INAWEZEKANA kabisa nyoka akazaa mjusi? Sidhani; mara nyingi nyoka huzaa nyoka. Lakini imetokea kwani nyoka amezaa mjusif Msemo huo unaweza kwenda sambamba na aliyekuwa mchezaji mahiri wa zamani, John Ondolo Chacha ambaye alicheza katika timu ya Lipuli ya Iringa msimu wa 1991-92 akitokea jijini Dar es Salaam.
Chacha ambaye alipachikwa majina ya Niva, Pembe ya Ndovu na Thobias Ocholla kutokana umahiri wake wa kucheza beki namba nne katika timu alizowahi kucheza, baba yake alikuwa ni mdau mkubwa wa sanaa.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii, anaanza kwa kuelezea tofauti iliyoko kati ya soka la sasa na la miaka waliyocheza wao.
Anasema, ilikuwa ni kwamba, wao walijituma katika mazoezi binafsi, kuliko wa sasa ambao ni wavivu.
Anaongeza kuwa, sababu ya uvivu wa mazoezi, inasababisha kupozesha mpira katika mashindano ya kimataifa, ambayo Watanzania wengi wanajitokeza kuwashangilia.
Chacha anasema, anashukuru elimu kubwa aliyoipata kutoka kwa Kocha Abdallah Kibadeni ‘King Mputa', ambaye mara nyingi alimpa mawazo mengi, ambayo yalimsaidia katika kucheza soka.
Anaeleza, katika safari yake ya soka, alipata elimu kutoka kwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, ambaye aliwafundisha wakiwa katika timu ya Shekilango huku Bendera akiishi katika ghorofa za Shekilango.
Pamoja na kupata elimu kutoka kwa makocha ambao wazoefu, lakini alitatizwa na suala la uvumilivu wa kukaa katika timu moja zaidi ya miaka minne.
Ananasema, alianza kusakata soka mwaka 1986-87 alipoajiriwa katika kiwanda cha Alminium Africa kilichopo Temeke, ambako alicheza msimu mmoja na kukutana na kocha Kibadeni katika timu ya Future, iliyokuwa na maskani yake Urafiki jijini Dar es Salaam.
Akiwa Alminium, alikutana na wachezaji wengi ambao baadhi yao walicheza Ligi daraja la kwanza (sasa hivi Ligi Kuu Tanzania bara), mmojawapo akiwa ni kiungo Suleimani Ally aliyewahi kucheza Yanga miaka ya 1987-88.
Hakudumu sana Alminium, akarejea timu iliyoko karibu na nyumbani kwao Shekilango ya Future, iliyokuwa na vijana wengi ambao walikuja kuwa tishio katika medani ya soka la Tanzania.
Alipokuwa Future, timu hiyo ilikuwa chini ya Kibadeni kipindi hicho, ambako alikuwa ni mfanyakazi wa kiwanda cha nguo cha Urafiki akiwa ametokea masomoni nchini Ujerumani kwenye kozi ya ukocha.
Kutokana na umahiri wake uwanjani, Kibadeni alimpeleka kiwanda cha Urafiki na kupata kazi kitengo cha ufundi wa magari, akiwa pia ni mchezaji.
Akiwa Urafiki, alifundishwa pia na Salum Madadi ambaye ni Ofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na kukutana na wachezaji wengine kama Wema Juma, Kenny Mwabulambo, Habibu Kondo, Muhesa Kihwelu, Jumanne Ucheche ambaye baadaye walihamia Lipuli ya Iringa na John Ngunde ambaye sasa hivi ni mmojawapo ya Maofisa Watendaji wa Mitaa jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo ilikuwa mojawapo ya timu ngumu katika ligi ya soka Mkoa wa Dar es Salaam, lakini iliishia ligi ya Kanda ya Dar es Salaam.
Kutokana na umahiri wa ufundishaji, Kibadeni alichukuliwa na Chama cha Soka Tanzania (FAT), sasa TFF kuifundisha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars', hapo Chacha akahamia Nyota Nyekundu yenye maskani yake Kariakoo Mtaa wa Congo jijini na kukutana na Faustine Kibingwa, Rosta Ndunguru, Ayoub Mzee na John Bosco, ambako aliendelea kupata uzoefu mkubwa, kwa sababu mara kadhaa timu hiyo ilicheza mechi za kirafiki na Taifa Stars.
Mara nyingi, Kibadeni alimweleza Chacha kwamba, kwa jinsi anavyocheza soka, atafika mbali zaidi ya Tanzania, ila kikubwa zaidi ni kuzingatia miiko ya mchezo huo na kuwa na uvumilivu.
Mwaka 1989, alichukuliwa na timu ya kiwanda cha Twiga Cement kilichopo Wazo Hill jijini Dar es Salaam, kutokana na umahiri akiwa uwanjani, akapewa ajira kiwandani hapo na kukutana na ofisa wa TFF hivi sasa, Idd Mshangama akiwa kocha.
Mwaka 1991, alihamia Lipuli ya Iringa baada ya kuonekana katika mashindano ya ligi daraja la pili ambako alikutana na akina Peter Lugenzi, Willy Komakoma, David Kika, Elisha John, Nurdin Gogola na Hassan Mwajeki.
Kipindi hicho kikosi cha Lipuli kilikuwa chini ya kocha Mzambia, Donald Phiri ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Zambia na Pascal Bella, ambako alikutana na viwango zaidi, kwa sababu alipata nafasi ya kucheza na timu kama Simba, Yanga, Coastal Union, African Sports na Milambo ya Tabora.
Pamoja na timu yao kuwa bora katika ligi daraja la kwanza, lakini anaikumbuka mechi waliyofungwa mabao 5-0 na Pamba ya Mwanza, ambayo ilikuwa na wachezaji mahiri kama Kitwana Seleman, Nteze John Lungu, Madata Lubigisa na wengineo.
Anasema, cha kushangaza baada ya mchezo huo uliochezwa jijini Mwanza, tajiri wa machimbo ya Mgusu aliialika timu hiyo kwa gharama zake kucheza na timu yake ya mgodini.
Katika mchezo huo, alikutana na mshambuliaji mahiri wa timu hiyo, Eliud Ngessa ambaye alicheza naye utafikiri wanawania nafasi ya kufuzu kombe la dunia, hadi mwamuzi wa mchezo aliwatoa nje kwa kadi nyekundu.
Anaongeza kuwa, cha kushangaza zaidi baada ya kutolewa wachezaji hao, mpira ulipooza sana, hali ambayo ilisababisha mwamuzi huyo kuwaita na kuwaamuru warejee kwa mara nyingine uwanjani, hali ambayo hakuelewa refa huyo alitumia sheria ipi, kwani mchezaji akitolewa nje kwa kadi nyekundu haruhusiwi kurejea uwanjani mara nyingine.
Kwa kuwa tamaa yake ilikuwa ni kucheza nje ya mipaka ya Tanzania, akatoka Lipuli na kurejea Dar es Salaam msimu wa 1992-95, ambako baadhi ya viongozi wa timu ya Konde ya Pemba, wakamtaka akachezee timu yao katika ligi kuu kisiwani humo.
Akiwa na wachezaji wenzake sita kutoka Dar es Salaam, Abdul Ramadhani ‘Mashine', Mohamed Mwape, Abdallah Mohamed, Omar Mbweza na Ramadhani Abdallah, baadaye timu hiyo ilifuzu kucheza ligi ya Muungano katika mashindano ya kila mwaka.
Wakati akiwa katika hatua za mwisho za mkataba wake, timu za Jamhuri na Kipanga ambazo zote ni za Jeshi la Wananchi zilimuhitaji, alikataa na kurejea Dar es Salaam, ambako alikutana na Kibadeni kwa mara nyingine, ambaye alimwelekeza kwamba, kutokana na umahiri alionao katika soka, asubiri kidogo atamtafutia timu.
Kwa kuwa hakuwa na uvumilivu, alielekea Kenya na kufanya majaribio timu za AFC Leopards, Kenya Breweries na Mumias Sugar ambako ndipo alipofanikiwa timu hiyo iliyokuwa ikifundishwa na kocha Dennis Munyendo na kukutana na nyota kama akina Mark Serengo na Nika Hammer.
Mwaka 1996-98 akajiunga na Posta ya Kakamega nchini humo, ambako akiwa katika timu hiyo, alipata hisia ya kumrejea Mungu kwa kenda chuoni kupata elimu ya dini katika chuo cha Mtakatifu Makarios cha Kenya na kufanikiwa kupata cheti cha uchungaji.
Anasema, kipaji chake katika soka, alikirithi kutokea kwa babu yake, aliyekuwa akiitwa John Alyango, ambaye aliwahi kucheza Kombe la Gossage.
John Chacha, ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya 12 wa marehemu Mzee Ondolo John Chacha, ambaye alikuwa ni mojawapo ya wadau mahiri wa muziki na sanaa hapa nchini, ambaye aliweka mikakati ya kukuza na kuendeleza sekta hiyo kwa kujenga kituo kikuu nyumbani kwake Shekilango jijini Dar es Salaam.
John aliyezaliwa miaka 45 iliyopita, hivi sasa ana mke na watoto wanne na ni mchungaji wa kanisa la Full Categro lililopo katika kituo cha Sanaa Shekilango jijini Dar es Salaam.
Anasema, mipangilio iliyopo kwa sasa ni kukuza na kuendeleza sanaa sambamba na michezo mignine kama soka na kuwa kituo cha kusaka vipaji na kuviendeleza kimataifa.
Anatoa wito kwa TFF, kufanya mabadiliko makubwa ya Kamati ya Ufundi, ambayo inaonekana kuelemewa na mzigo, kutokana na kwamba, hivi sasa Tanzania hakuna timu inayoeleweka ya Taifa.
Anapendekeza, Kamati hiyo inaweza kuongozwa na Watanzania kama Kibadeni, Adolf Rishard na Charles Boniface Mkwasa, ambao wana elimu ya kutosha ya kuifanya kazi hiyo.
Anatoa wito pia kwa mawakala, kuwaandaa wachezaji kisaikolojia ili wawe mfano bora katika timu za nje na kuwataka pia wachezaji wa sasa, kuacha uvivu na kumuiga Mohamed Ngulungu ambaye alicheza timu ya Taifa miaka 10 bila ya kupoteza uwezo wake.