Nizar azuiwa kujiunga Stars
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 23rd March 2011 @ 23:59 Imesomwa na watu: 622; Jumla ya maoni: 1
ZIKIWA zimesalia siku mbili kabla ya timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars kumenyana na wenzao wa Jamhuri ya Kati, kiungo tegemeo wa Stars, Nizar Khalfani amezuia kujiunga na timu hiyo.
Khalfani anayecheza Vancouver Whitecaps ya Canada alitumiwa tiketi ya ndege Machi 22 ikionesha kuwa alitakiwa kuwasili nchini Machi 23 tayari kwa mechi hiyo ya awali kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwakani.
Habari za uhakika zilizopatikana kutoka katika Shirikisho la Soka nchini (TFF) zilisema kuwa uongozi wa Vancouver umekataa kumruhusu Khalfani kujiunga Stars, kwa vile Shirikisho hilo halikufuata utaratibu unaostahili.
"TFF ilishatuma tiketi kwa Nizar kwamba aje leo (jana) lakini uongozi wa timu yake anayochezea umesema unafahamu kama mchezaji huyo anatakiwa kucheza mechi hiyo na mara kwa mara humruhusu lakini safari hii hawatafanya hivyo kwani taratibu hazijafuatwa," alisema mmoja wa maofisa wa TFF.
Akifafanua, Ofisa huyo alisema, tatizo lililojitokeza ni kwamba TFF iliwasiliana moja kwa moja na mchezaji mwenyewe baada ya kuwasiliana na uongozi wa klabu yake.
Hata hivyo, uongozi wa Vancouver haujafunga milango kwa TFF kutuma maombi ya kumtaka mchezaji huyo. Mechi kati ya Stars na Jamhuri ya Kati imepangwa kuchezwa keshokutwa.
"Wamesema kama TFF inamhitaji Nizar iombe, lakini sijui kama itawezekana maana muda wenyewe umeshakwenda, sidhani kama itawezekana," alisema ofisa huyo.
"Utaratibu huwa klabu inaandikiwa barua ya kumuomba mchezaji, ikishajibiwa ndio inatuma tiketi, sasa hilo halikufanyika, Shirikisho limetuma tiketi kwa Nizar tu moja kwa moja na kutuma nakala kwa uongozi wake ndio maana tumekataliwa," alisema ofisa huyo.
Aidha akiwasiliana kwa facebook na gazeti hili, Khalfani alikiri kupata tiketi na kusema kuwa atashindwa kujiunga na Stars kwa vile uongozi wake haukuombwa.
"Kweli tiketi niliipata, na viongozi waliniita na kuniambia kuwa hawataweza kunipa ruhusa kwa vile hawakuandikiwa barua yoyote kutoka TFF, ndio inabidi nisubiri kuona watalitatua vipi suala hilo," alisema.