Habari za Michezo na Burudani
Nizar, Babi, Mrwanda wakwama
Imeandikwa na Betram Lengama; Tarehe: 25th March 2011 @ 11:05 Imesomwa na watu: 500; Jumla ya maoni: 0
Beki Nadir Haroub (kulia) akimpiga chenga mshambuliaji Athumani Machupa wakati wa mazoezi ya Taifa Stars katika Uwanja wa Karume kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati Machi 26 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. (Picha na Yusuf Badi).
NYOTA watatu wa ‘Taifa Stars' wanaosakata soka nje ya nchi, Nizar Khalfan, Abdi Kassim ‘Babi' na Danny Mrwanda, hawatokuwemo kwenye kikosi cha kesho kitakachocheza na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha wa Stars, Jan Poulsen, amesema mjini Dar es Salaam kuwa nyota hao wameshindwa kujiunga na wenzao kwa ajili ya mchezo huo wa kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (CAN) kutokana na kukosa ruhusa kwenye klabu zao.
Kushindwa huko kwa Khalfan anayechezea Vancouver Whitecaps ya Canada pamoja na Babi na Mrwanda ambao wapo klabu ya Dong Tam Long An ya Vietnam kunatokana na kuwepo matatizo ya mawasiliano kati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na klabu zao.
Licha ya kuwakosa wachezaji hao, Poulsen alisema hakuwezi kuathiri kikosi chake, kwani anaamini waliopo ni imara na wanaweza kufanya vizuri.
Poulsen aliita wachezaji sita wa kulipwa katika kikosi chake kwa ajili ya mechi dhidi ya timu hiyo inayoongoza Kundi D, ambalo lina timu za Tanzania, Algeria na Morocco, lakini wachezaji watatu wamejiunga na wenzao.
Wachezaji hao ni Athumani Machupa anayecheza timu ya Vasuland ya Sweden, Idrisa Rajabu anayecheza Sofapaka ya Kenya na Henry Joseph anayecheza Kongsvinger ya Norway.
Akizungumzia mchezo huo wa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Poulsen alisema Stars inahitaji ushindi wa udi na uvumba, ili ijiweke katika nafasi nzuri kwenye mbio za kuwania nafasi ya kufuzu fainali hizo zitakazoandaliwa kwa pamoja na nchi za Gabon na Equatorial Guinea.
"Pamoja na ukweli kuwa ninawafahamu kidogo tu wapinzani wetu ambao wanafanya vizuri katika kundi letu kwani wamewafunga Algeria na kutoka suluhu na Morocco, nina matumaini tutafanya vizuri katika mchezo wetu kutokana na maandalizi mazuri na endapo tutatumia vema uwanja wa nyumbani hasa kwa kuungwa mkono na mashabiki wote," alisema Poulsen.
Kwa upande wake kocha wa CAR, Mfaransa Accorsi Jules Francois alibainisha kuwa haijui kabisa Stars, lakini hilo sio tatizo kwani hali hiyo pia ilimkumba kabla ya kuumana na Algeria na Morocco na ataijua hiyo kesho uwanjani.
Wakati huohuo, TFF imeipatia jukumu la kuuza tiketi za mchezo huo wa Stars na CAR, kampuni ya Premier Sports Bingo ambayo inajishughulisha na michezo ya ubashiri wa matokeo mbalimbali ya mechi za soka na michezo mingine.