Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,508
- 911,249
- Thread starter
- #12,481
Tanzania inahitaji kocha kama Mourinho
Mwandishi wetu
Mwandishi wetu
Kocha yule alinitazama kama vile ndo kwanza ananijua, kisha akaniambia huenda mimi ni mwandishi pekee ambaye sijui kama jambo hilo ndilo linalotokea.
Nikataka ufafanuzi.
"Unatumiwa sms na kiongozi au mfadhili, ‘anapendekeza' first eleven ya siku hiyo. Unapata sms kama tano hivi za namna hiyo kutoka kwa watu tofauti, lakini wote wenye sauti ndani ya klabu, unategemea nini?"
Kwa mujibu wa kocha huyo, wakati wa kutuma sms hizo, huenda wako pamoja katika hoteli moja wakizungumzia mechi hizo.
Anasema wakati mapendekezo hayo yakitolewa, watatu kati ya watano hao hawajafika mazoezini zaidi ya wiki na hawajui maendeleo ya wachezaji.
Kipindi hicho, Simba na Yanga zote zilikuwa chini ya makocha wa kigeni. Nikamwuliza kama hata sasa bado walimu hao walikuwa wanapangiwa timu.
Akacheka na akanieleza vikosi vya kwanza vya Simba na Yanga siku za mchezo hujulikana siku mbili kabla na hupangwa katika mabaa na mahoteli. Alinipa mchapo huu.
"Mimi nina wachezaji kama wawili hivi wako Yanga niliwahi kuwafundisha nikiwa (anaitaja timu), baada ya kusikia listi ya mechi siku mbili kabla, nikawauliza kama wanafahamu jambo hilo, wakasema wamesikia na kocha wao ananung'unika kwa sababu hawampi nafasi ya kuchagua wachezaji anaowahitaji yeye."
Hili ni jambo lililopo na si porojo. Mfadhili au kiongozi aliyenunua mchezaji kwa fedha nyingi, asingependa kuona mchezaji huyo anakaa nje. Ndiyo maana kuna wachezaji wanaoitwa mchezaji wa fulani.
Inabidi acheze, vinginevyo uhusiano kati yake na kocha au benchi la ufundi unaharibika.
Hii ndiyo ambayo mara nyingi imepelekea wachezaji kuwa watovu wa nidhamu. Mchezaji anafikia kipindi eti anafokeana na kocha wake.
Anafanya hivyo kwa msukumo wa aliyemsajili kwa sababu anafahamu hawezi kuchukuliwa hatua zozote za kinidhamu.
Makocha wetu wanakubali hali hii kutokana na kukosa msimamo kunakochangiwa na ulofa wao. Wanahitaji fedha kwa ajili ya familia zao, ingawa mikataba yao inasomeka kuwa wao ndiyo watakaokuwa wa mwisho katika maamuzi ya timu kiufundi.
Wanaona ya nini bwana kugombana na watu wanaokupa kula kwa sababu ya mchezaji. Waache wachezaji wao wacheze, wakifungwa si wao. Kumbe hawaangalii wasifu wao utakavyosomeka hapo baadaye.
Moja kati ya vigezo vya kocha wa soka ni nini alikifanya hapo kabla. Kile cha wakati uliopita, kinatoa picha ya nini utakifanya hapo baadaye.
Jambo hili linanikumbusha kuhusu Jose Mourinho, kocha mwenye maneno mengi wa Real Madrid ya Hispania. Wakati huo akiwa Chelsea, hakuridhishwa na uamuzi wa mmiliki wa timu hiyo, Roman Abramovich kumleta kikosini mshambuliaji wa zamani wa AC Milan, Andriy Shevchenko.
Mkali huyo wa kutikisa nyavu raia wa Ukraine, hakuwa katika mipango ya Mourinho na alionyesha wazi hisia zake za kukataa ununuzi wa bei mbaya wa mchezaji huyo.
Lakini kwa kuwa bosi alikuwa ameamua kumnunua, hakuwa na jinsi, akasubiri afike katika maeneo yake, aweze kufanya vitu vyake. Na kweli, pamoja na uzuri wa Andriy, hakuweza kupata namba ya kudumu kikosini Chelsea.
Na kwa vile inasemekena Andriy na Roman ni marafiki, kitendo hicho kilimuudhi bilionea huyo, aliyeanza kutengeneza mazingira ya kumtimua Mreno huyo.
Kuna siku aliwahi kueleza hadharani: "Mimi ukinichukua leo kusimamia biashara za Roman, nitazifilisi haraka. Ndivyo ilivyo kwake, hawezi kuifanya kazi ya ukocha!"
Yalikuwa ni maneno ambayo si rahisi kutamkwa na mwajiriwa kuelekeza kwa mwajiri wake. Ni maneno ya kijasiri ambayo yanafaa kusemwa pia na makocha wa Kitanzania, ili kuweza kuisaidia soka yetu kusonga mbele.
Wao kama wanazipenda timu zetu na wana fedha, wazilete fedha hizo kwa uongozi, kisha viongozi wamuulize kocha anahitaji wachezaji gani ili wao wakamilishe masuala ya ununuzi.
Viongozi na wafadhili, hata kama tunawapenda vipi baadhi ya wachezaji walio katika vikosi vyetu, labda kwa kuwa wanajua kupiga kanzu au chenga, bado tumpe nafasi ya mwisho kocha atekeleze mipango yake. Hii itatusaidia kupata nafasi ya kuhoji uwezo wake kama timu zetu zitafanya vibaya.
Sasa mtu kama Sendeu au Ndimbo anapopanga timu badala ya makocha wao, zikianza kudorora watapata wapi ujasiri wa kuhoji uwezo wao?
Soka ni mchezo wa kitaalam, unaofundishwa na watu waliosomea. Si kila mmoja anaweza kuwa kocha, ingawa kwa Tanzania, mechi moja inaweza kuwa na makocha zaidi ya 20,000. Tubadilike.
PRINT