Wakali wa milima ya Uluguru wanataka kurejea Ligi Kuu
Ghisa Abby
BAADA ya kutwaa ubingwa wa mkoa wa Morogoro katika michuano ya ligi ya taifa ngazi ya mkoa, kazi iliyobaki kwa timu ya soka ya Tumbaku FC, ni kujipanga vizuri zaidi, ikiwa ni safari ya kucheza Ligi Kuu bara.
Timu hiyo ya Tumbaku FC, inayomilikiwa na kampuni ya Tumbaku ya TTPL, hivi karibuni, ilinyakua ubingwa huo wa mkoa kwa kuibuka kinara na kujitwalia sh 100,000 na kombe.
Kwa mujibu wa kocha wa timu hiyo, Experious Mchonde ‘Super,' mafanikio hayo hayakuja kama mvua, bali yaliandaliwa na kujengwa kwa takribani mwaka mmoja.
"Kabla ya kuanza kwa ligi hii, nilihakikisha ninawandaa vizuri vijana ili kuwa na timu shindani na ndivyo ilivyotokea, nashukuru sana, nawapongeza wachezaji na kampuni ya Tumbaku kwa sapoti," anasema.
Mchonde anasema, kutokana na maandalizi hayo mazuri, licha ya kukutana na timu zenye uwezo mkubwa kisoka, vijana wake walijitahidi kupata matokeo mazuri, hadi mwisho wa siku, wakaibuka mabingwa.
Je, ni timu gani ilikuwa tishio katika michuano hiyo? Mchonde anasema zote zilitoa upinzani mkubwa, lakini Alliance One ndio walikuwa wagumu zaidi hasa ikizingatiwa walikuwa wakitetea taji.
"Timu hii nayo ilijiandaa vizuri, kwa sababu walikuwa wakitetea ubingwa wao, lakini tunashukuru tumezima ndoto yao ya kutaka kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo," anasema Mchonde.
Ni mara ya ngapi timu yake kucheza mashindano hayo? Mchonde anasema ni zaidi ya mara nne bila mafanikio, hivyo safari hii wakaamua kujiandaa vizuri ili kupata mafanikio makubwa kuliko miaka iliyotangulia.
"Safari hii tuliweka malengo ya kutwaa ubingwa, hivyo kwa jitihada, malengo na sapoti kutoka kwa uongozi wa kampuni, tumefanikiwa."
Kocha Mchonde ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya Tumbaku anasema, anamshukuru Mungu kwani matunda hayo yamekuja ukiwa ni mwaka mmoja tu tangu aanze kuinoa.
Mbali ya mashindano hayo, Mchonde anasema timu yake imewahi kushiriki mara mbili mashindano ya Shirikisho la Michezo, Mashirika ya Umma na Makampuni binafsi (SHIMMUTA), na mashindano ya Mei Mosi waliyoshiriki mara tatu.
"SHIMMUTA tumeshiriki mara mbili na mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka jana, ambapo tulitwaa ubingwa, mashindano ambayo yalifanyika mkoani Tanga," anasema.
Aidha, timu hii imewahi kushiriki mashindano ya Mei mosi na kutwaa ubingwa mwaka jana, hivyo safari hii watashiriki wakiwa mabingwa watetezi.
Akizungumzia matarajio ya timu yake katika Ligi ya Taifa, Mchonde anasema kazi kubwa inayowakabili ni kujiandaa vizuri, ili kutimiza azma ya kurejea Ligi Kuu ya bara waliyowahi kushiriki kabla ya kushuka.
Anasema, timu hiyo ni kati ya vigogo vya soka vilivyowahi kutikisa soka ya Tanzania wakati huo ikicheza Ligi Kuu hadi katikati ya miaka ya 1980.
Anasema, tangu iliposhuka, timu hiyo ilikaa muda mrefu bila kushiriki mashindano yoyote kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi wa kiwanda.
"Kwa sasa uongozi wa kampuni uliopo madarakani unapenda sana masuala ya michezo, ndio maana tunafanya vizuri katika kila mashindano," anasema.
Pamoja na timu hii kumilikiwa na kampuni ya Tumbaku ya TTPL, bado inakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo upungufu wa vifaa vya michezo kama viatu, mipira na jezi.
Kocha huyu, anatoa wito kwa wadau wa michezo mkoani Morogoro kuisaidia kwa hali na mali, ili timu hiyo iweze kuleta sifa katika mkoa huo.
Aidha, ameuomba uongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Morogoro (MRFA), kuonyesha ushirikiano katika kukabiliana na mashindano yajayo.
Mchonde anasema siri ya mafanikio ya timu, ni maandalizi hivyo timu hiyo inapaswa kuandaliwa vizuri ili iweze kuwa shindani kwa maslahi ya soka ya mkoa huo na taifa.
Anasema, lengo ni kuuwakilisha vizuri mkoa, hivyo wanaelekeza nguvu katika mazoezi ili kuwa shindani katika Ligi ya Taifa ngazi ya taifa.
Naye Buya Kassim ambaye ni mchezaji wa timu hiyo, aliyeibuka mfungaji bora wa ligi ya mkoa, anasema licha ya kutopatiwa zawadi kutokana na kutokuwepo kwa zawadi hiyo, kwake ni faraja kubwa.
Anasema zawadi ya kitu ni matokeo ya kufanya vizuri, lakini kutokabidhiwa zawadi rasmi ya ufanisi wa kazi, bado hakuondoi ufanisi wenyewe, hivyo ataongeza juhudi akijua ipo siku atapata zawadi.
"Licha ya kutotangazwa na kupewa zawadi ya ufungaji bora wa ligi, lakini kitendo cha kuwa kinara wa mabao katika ligi hii, kwangu ni zawadi tosha ambayo itakuwa changamoto ya mimi kujituma zaidi kukuza kipaji changu," anasema Kassim.
Anasema, juhudi zake binafsi pamoja na kuzingatia maelekezo ya kocha wake, ndio siri kubwa ya mafanikio yake dimbani akiifungia timu yake jumla ya mabao sita.
Naye Katibu Mkuu wa MRFA, Hamisi Semka, anasema timu hiyo ilitwaa ubingwa baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Alliance One katika mechi ya mwisho.
Anasema, wanashukuru kwa sababu timu yao imekuwa na mwendo mzuri tangu kuanza kwa michuano hiyo kwa kutofungwa, hivyo kumaliza wakiwa vinara kwa pointi 12.
Anasema kutokana na mafanikio hayo, timu hiyo itauwakilisha mkoa kwenye mashindano ya ligi ya Taifa ngazi ya taifa yatakayotangazwa baadaye na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF).
Katika michuano hiyo iliyofikia tamati hivi karibuni, timu ya Mitumba ilitwaa nafasi ya pili, hivyo kujitwalia kombe dogo na shilingi 50,000.
Aidha, katibu huyo amewashukuru wakazi wa mkoni hapa kwa ushirikiano mkubwa kwa kipindi chote cha michuano hiyo na kusihi moyo huo uendelee kwa maslahi ya timu hiyo na soka ya Mkoa wa Morogoro.