Kocha-Ni miujiza AFC kubaki Ligi Kuu Send to a friend Thursday, 10 March 2011 20:05
Sweetbert Lukonge
ZIKIWA zimebaki mechi nne kabla ya kufungwa kwa pazia la Ligi Kuu Tanzania bara, kocha wa AFC ya Arusha, Rashidi Chama amekata tamaa kwa timu yake kubaki kwenye ligi hiyo msimu huu.
Wakati klabu za Simba, Yanga na Azam zikipigania kusaka ubingwa wa ligi msimu huu upande wa pili timu za AFC, Majimaji, Ruvu Shooting pamoja na Polisi Dodoma zenye zimeanza kujiandaa kurudi ligi daraja la kwanza msimu ujao.
Akizungumza na Mwananchi jana Chama amesema kuwa hana matumaini ya timu yake ya AFC kubakia Ligi Kuu isipokuwa kwa sasa atahakikisha anatafuta heshima kwenye mechi zake zote zilizo bakia."Labda kwa muujiza ndiyo tunaweza kubakia Ligi Kuu kwani mpaka sasa uwezo wa kufanya vizuri katika mechi zetu nne zilizobakia ni ngumu.
"Kwani tunakabiliwa na mechi ngumu ikiwemo ya Jumamosi dhidi ya Simba ambayo kwa hakika itakuwa ngumu sana ukizingatia wapinzani wetu hao wanahitaji kushinda ili waweze kujiweka katika mazingira mazuri ya kunyakuwa ubingwa."Pamoja hilo, lakini tutahakikisha tunapigana kwa nguvu zetu zote ili tuweze kujiwekea heshima japokuwa kuwa tutashuka daraja," alisema Chama.
Kwa upande wa timu ya Majimaji ya Songea, kocha mkuu wa timu hiyo Peter Mhina amesema kuwa timu yake bado ina matumaini makubwa ya kubakia Ligi Kuu na inahitaji kufanya vizuri katika mechi zake zote zilizobakia.
Alisema jambo la msingi ni kwa wadau mbalimbali wa timu hiyo kushirikiana na uongozi katika kuiunga mkono kwa kila hali ili iweze kufanikisha ndoto zake kwenye michezo yake minne iliyobakia.
"Bado tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kuepukana na hatari ya kushuka daraja kwa sababu hatujazidiana pointi nyingi na wenzetu waliotangulia," alisema Mhina.
Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 41, ikifuatiwa na Yanga(39), timu zote zimecheza mechi 18.