Simba, Mtibwa hapatoshi
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 26th February 2011 @ 23:59 Imesomwa na watu: 64; Jumla ya maoni: 0
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, leo watakuwa na kazi nzito pale watakapomenyana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika harakati za kutetea taji lake.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kali na ya kusisimua kutokana na unyeti wa nafasi ilizo nazo timu hiyo kwenye msimamo wa ligi hiyo ambao kabla ya mechi hii, Azam ndio inaongoza kwa uwiano mzuri wa mabao baada ya kulingana pointi na Yanga inayoshika nafasi ya pili.
Timu hizo zina pointi 35 kila moja.
Simba iko nafasi ya tatu kwenye msimamo huo ikiwa na pointi 34, ikishinda itafikisha pointi 37 na hivyo kurejea kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi mbili.
Mtibwa Sugar iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 30, ushindi wa mechi ya leo utaifanya ifikishe pointi 34 sawa na Simba, lakini Simba itaendelea kushika nafasi ya tatu kwa uwiano wa mabao.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Toma Olaba aliliambia gazeti hili kuwa mechi hiyo ni muhimu kwake kushinda, kwani itamuwekea mazingira mazuri ya kumaliza katika timu mbili za juu mwishoni mwa msimu.
"Unaona pointi zangu na Simba, hazijapishana sana, Simba akishinda ataongoza Ligi, mimi nikishinda nitamfikia Simba pointi na hilo linanipa nguvu ya kuifunga Azam mechi inayofuata na kuwa na uhakika wa kumaliza ligi katika nafasi mbili za juu," alisema.
"Siwezi kufungwa Dar es Salaam, Simba haiwezi kunifunga tena, nimeshawaandaa wachezaji wangu kwa ajili ya mechi hiyo," alisema Olaba.
Katika mechi ya raundi ya kwanza iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Hata hivyo mechi dhidi ya timu hizi, haitabiriki, lolote linaweza kutokea kwa timu yoyote ile.
Mtibwa Sugar leo italazimika kumtumia kipa wake namba mbili baada ya namba moja, Shaaban Kado kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyooneshwa katika mechi dhidi ya Toto African iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza katikati ya wiki.
Kwa upande wa Simba, Mkurugenzi wake wa ufundi Patrick Phiri alisema hawana cha kupoteza kwani wanataka kuongoza ligi.
"Mechi yetu itakuwa ngumu najua, lakini sisi ndio mabingwa watetezi tunataka kurudi kuongoza ligi, ili tutetee ubingwa wetu," alisema.