Madrid yashikwa lyon, Chelsea Yatesa Copenhagen
Send to a friend Wednesday, 23 February 2011 20:01
LONDON, England
TIMU ya Real Madrid ilishindwa kuitambia Lyon baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 huku timu ya Chelsea ikiichapa bao 2-0 FC Copenhagen na kukaribia kuingia hatua ya robo fainali.
Alikuwa mshambuliaji wa Lyon, Bafetembi Gomis aliyeondoa furaha ya Real Madrid baada ya kuisawazishia timu yake bao katika dakika ya 83 wakati Real Madrid ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 lililokuwa limefungwa na Karim Benzema.
Benzema alifunga bao hilo baada ya kuwatoka mabeki watatu wa Lyon katika eneo la penati na kumchambua kipa wa Lyon, Hugo Lloris.
Kwa matokeo hayo, klabu ya Lyon imeendeleza rekodi yake ya kutofungwa na Real Madrid katika mashindano hayo ya Klabu Bingwa barani Ulaya katika mechi saba walizowahi kukutana.
"Wanao wachezaji wazuri, kocha mzuri na mwenye uzoefu barani Ulaya, hivyo mechi ya pili itakuwa ngumu zaidi, nadhani nimechangia Real kufanya vizuri katika mechi hii kwa sababu ilikuwa ni mechi ngumu iliyokuwa na mpambano wa kweli na zilitengenezwa nafasi chache,"alisema kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho.
Kwa upande wa Chelsea ambayo haijawahi kushinda taji kubwa barani Ulaya, yenyewe ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Copenhagen, mabao ambayo yalifungwa na Nicolas Anelka.
Ushindi huo umemsaidia kocha wa Chelsea ambaye alikuwa akilalamikiwa kushindwa kuipa ushindi timu hiyo baada ya Chelsea kutolewa katika mashindano ya kombe la FA wikiendi iliyopita.
"Hii ni soka, unatakiwa ufanye mambo mazuri haraka kama ulipata matokeo mabaya, unatakiwa usitoke nje ya mtazamo wako mzuri, wachezaji wangu walijituma sana, walicheza soka nzuri sana na matokeo ni mazuri,"alisema kocha wa Chelsea, Carlo Ancelotti.
Naye kocha wa Lyon, Claude Puel alisema,"Nimeridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na vijana wangu, pia bado ipo mechi ya marudiano ambayo tunaweza kuitumia vizuri."
Alisema,"bado tuna nafasi ya kufuzu na hilo ni jambo la msingi, itabidi tuwe imara katika mechi ijayo, kwa sababu katika mechi hii tulipata nafasi nzuri, lakini hatukuzitumia vizuri."
Katika mechi ya Chelsea dhidi ya Copenhagen, mshambuliaji mpya wa Chelsea, Fernando Torres alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kufunga bao, lakini alishindwa kutumia nafasi alizozipata.
Lakini katika mechi hiyo aliyetamba alikuwa Nicolas Anelka ambaye alifunga bao la kwanza katika dakika 17, ambapo alifunga bao la pili katika dakika ya 54 pia.
Akimuongelea Torres, kocha wa Chelsea, Carlo Ancelotti alisema,"Jambo la msingi katika mechi hii lilikuwa ni kazi ya mshambuliaji kama alivyoifanya Torres, lakini hakuwa na bahati ya kufunga ingawa alicheza mchezo mzuri sana."
Akizungumzia pambano hilo kocha wa Copenhagen, Stale Solbakken hakulalamikia kichapo alichokipata ambapo alisema,"Walikuwa imara kutuzidi sisi na tulifanya makosa mengi ya kiufundi, walikuwa wana kasi na wepesi, ila wapo wachezaji wangu waliocheza vizuri sana na wengine walijitahidi."
"Labda hatukuwa wazuri kama Chelsea, lakini siku moja tutawakaribia, kwa swababu hivi sasa tumekubali Chelsea wametufunga bao 2-0,"alisema Stale Solbakken.
Timu hizi zitarudiana tena Machi 16.