Miaka saba ya raha na karaha Chuo Kikuu Mzumbe

Ngongo

JF-Expert Member
Sep 20, 2008
18,920
31,161
KILIPOKUWA kikiitwa chuo cha Uongozi wa Maendeleo kikitoa masomo ya ngazi ya stashahada, sifa za ubora wa taaluma na wahitimu wake zilisambaa ndani na nje ya nchi.

Miaka saba baada ya kujibadilisha na kuanza kutoa shahada, Chuo Kikuu cha Mzumbe kimekuwa katika wakati mgumu mbele ya macho ya jamii.

Jambo kubwa linalowatatiza baadhi ya watu ni kuwepo kwa taarifa za mara kwa mara kuwa chuo hicho kina wahadhiri wasio na sifa ya kufundisha ngazi hiyo elimu ya juu.

Mfano mzuri ni taarifa ya hivi karibuni iliyotoka katika gazeti moja la kila siku kuwa chuo hicho kina wahadhiri wakuu wanane ambao vyeti vya masomo yao vina walakini.

Taarifa hiyo iliongeza kusema kuwa vyeti hivyo ama ni feki au vilitolewa na vyuo visivyokuwa na ithibati au ubora unaokubalika kimataifa.

Hata hivyo uongozi wa chuo hicho kupitia Makamu Mkuu wake Prof. Joseph Kuzilwa, umeamua kuvunja ukimya na sasa unasema taarifa hizo si za kweli na zinalenga kuupotosha umma.

Hadithi ya vyeti feki

Hii si mara ya kwanza kwa chuo hiki kilichokuwa kinara wa kutoa watendaji wengi mahiri serikalini kukumbwa na kashfa ya kuwa na walimu wasio na sifa.

Miaka michache iliyopita uliibuka mjadala katika mtandao uliokuwa ukijadili kuwepo kwa walimu wa aina hiyo chuoni hapo na hata wahitimu feki, wengine wakiwa wanasiasa.

Hata hivyo Kuzilwa, licha ya kukiri kuwa tatizo hili lilikuwepo zamani hususan wakati wa enzi za kilichokuwa Chuo cha Uongozi wa Maendeleo, kwa sasa anasema hakuna wahadhiri wa aina hiyo kama inavyosemwa na baadhi ya watu.

Akibainisha zaidi tatizo anasema hata wakati huo tatizo halikuwa walimu kuwa na vyeti feki bali lilikuwa wahusika kusoma na kupata shahada za uzamivu kutoka vyuo ambavyo havina ithibati au ithibati yake kutotambulika na mamlaka za kitaifa.

Anakiri kuwa wahadhiri wale walioshutumiwa licha ya kuwa na shahada za uzamili kutoka katika vyuo vinavyotambulika kimataifa, kwa makosa waliomba udahili wa kusoma shahada ya uzamivu katika vyuo ambavyo hawakujua hadhi yake kitaaluma.

"Mzumbe kiliwafadhili wahadhiri hawa kama ambavyo kilifanya kwa walimu wake wengine waliopata udahili katika vyuo vingine ndani na nje ya nchi katika kutekeleza mpango wake wa kuendeleza walimu," anasema.

"Ilionekana kuwa kwa kiasi kikubwa kutokea kwa tatizo hili kulichangiwa na kuzuka duniani kwa wimbi la mfumo wa masomo kwa njia ya masafa na njia ya mtandao ambapo mfumo wa ithibati yake haujakamilika."

Watuhumiwa washughulikiwa
Baada ya kuwepo kwa taarifa hizi Baraza la Ithibati la Elimu ya Juu, sasa inaitwa Kamisheni ya Vyuo Vikuu (TCU), mbali ya kuutahadharisha umma kuhusu kuwepo kwa vyuo visivyo na sifa vinavyotoa shahada ya uzamivu, liliuelekeza uongozi wa chuo kikuu Mzumbe kuwataka wahadhiri wale waombe udahili mpya katika vyuo vyenye sifa.

"Wahadhiri wote saba waliomba udahili katika vyuo vyenye ithibati inayotambulika. Kwa bahati mbaya wawili kati yao wametangulia mbele ya haki. Watano waliobakia wapo katika hatua inayoridhisha ya kukamilisha tafiti za tasnifu zao za shahada ya uzamivu na wanatarajia kuhitimu mwaka 2010", anaeleza

Aidha anapinga taarifa kuwa uongozi wa chuo uliwafutia au kuwanyang’anya sifa wahadhiri hawa kama ilivyotangazwa katika baadhi ya vyombo vya habari kwa kuwa kitaratibu Mzumbe haina uwezo wa kumnyang'anya mtu sifa ya taaluma ambayo haikumpa.

"Seneti ya Chuo Kikuu Mzumbe ina mamlaka ya kunyang'anya sifa ambayo Chuo Kikuu Mzumbe imetoa. Baraza la chuo liliagiza kuwa sifa za udaktari wa falsafa za wahadhiri hao zisitumike katika nyaraka na shughuli za chuo mpaka hapo wahusika watakapohitimu katika sifa hiyo katika udahili huu mpya"

Hadhi ya chuo
Miongoni mwa mambo yanayoelezwa kukipaka matope chuo hiki ni pamoja na kuwepo kwa taarifa kuwa chuo hiki hakikufuata taratibu kilipokuwa katika mchakato wa kukipandisha hadhi ya kuwa chuo kikuu.

"Taratibu zote za kisheria na kiithibati zilifuatwa katika kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe na hivyo ni Chuo Kikuu halali kinachotambulika na mamlaka husika za kitaifa na kimataifa", anatetea Kuzilwa na kusisitiza:

"Kusema kuwa chuo hiki hakikufuata utaratibu wakati wa kuanzishwa kwake kuwa Chuo Kikuu ni kudharau mamlaka za kitaifa na kimataifa ikiwamo Kamisheni ya Vyuo Vikuu (TCU) na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania"

Anasema walipata usajili wa muda baada ya kufanyika kwa tathmini ya awali na baadaye tathmini nyingine mbili zikafanyika na ilipofika mwaka 2006 walipewa usajili wa kudumu baada ya TCU kujiridhisha katika tathmini zao.

"Ilipofika mwaka 2006 tulipewa usajili wa kudumu baada ya TCU kujiridhisha katika tathmini zao na hata leo tuko tayari muda wowote kufanyiwa tathmini kuhusu uendeshwaji wa chuo chetu," anabainisha.

Ubora wa elimu na wahadhiri
Kwa sasa Mzumbe pamoja na uchanga wake kina wahadhiri 34 wenye sifa ya shahada ya juu ya falsafa walizosoma katika vyuo mbalimbali vya ndani na nje na vinavyotambulika.

Wahadhiri wengne 44 wana shahada za uzamili na sasa wapo katika hatua mbali mbali za masomo ya shahada ya falsafa.

Kuhusu ubora wa elimu anasema chuo chake kinazingatia ubora wa elimu inayoitoa kwa kutoa fursa za masomo yenye ubora na zinazoendana na mahitaji ya soko kwa Watanzania.

"Tunatambua kuwa kuwepo kwa wahadhirin wenye ujuzi wa kufundisha na waliopata elimu bora na yenye viwango vya juu ni njia mojawapo ya kufikia azma hii," anafafanua.

Anasema katika kutimiza azma ya kuongeza ubora wa programu zake chuo chake kinashiriki kikamilifu katika kuweka na kufuata mfumo wa ubora kama ulivyopitishwa na Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA). Hadi sasa kimeshafanyiwa ukaguzi mmoja wa nje.
 
Hivi, kwa nchi ilokua na chuo kikuu kimoja kwa miaka yote 30 ya uchanga wake (tena by choice, not by inability) tungetegemea nini?
Lazima kutakua na kizazi cha wasomi watakaofundishwa na wahadhiri wasiokua na qualifications za ngazi wanayofundisha!
Mfano mzuri ni hili swala la 'intern doctors' sasa hivi kupelekwa ktk hospitali ya mikoa/wilaya ambapo eti wanafundishwa kazi na watu wenye diploma /adv dip yaani clinical/ asst medical officers! Haiingii akilini, eh?



La
 
Mzumbe ina jina la chuo Kikuu lakini hata hadhi yake ile ya zamani ya kutoa Diploma imeshuka sana.
 
Mzumbe ina jina la chuo Kikuu lakini hata hadhi yake ile ya zamani ya kutoa Diploma imeshuka sana.


Mkuu Bongolander heshima mbele.
Makamu mkuu wa chuo Prof. Joseph Kuzilwa kajitahidi kujibu hoja zote kuhusiana na wahadhiri kusoma na kupata shahada za uzamivu kutoka vyuo ambavyo havina ithibati au ithibati yake kutotambulika na mamlaka za kitaifa.
Hii hoja kwamba chuo kikuu cha Mzumbe hakina hadhi nadhani ni hija mufilisi,tene mara nyingi inapendwa kutumiwa na wahitimu wa UDSM.
 
Mkuu Bongolander heshima mbele.
Makamu mkuu wa chuo Prof. Joseph Kuzilwa kajitahidi kujibu hoja zote kuhusiana na wahadhiri kusoma na kupata shahada za uzamivu kutoka vyuo ambavyo havina ithibati au ithibati yake kutotambulika na mamlaka za kitaifa.
Hii hoja kwamba chuo kikuu cha Mzumbe hakina hadhi nadhani ni hija mufilisi,tene mara nyingi inapendwa kutumiwa na wahitimu wa UDSM.

kwikwikwi tehetehe
Mkuu unavisa na wahitimu wa UDSM? mjisafishe kwanza!!!!! tehetehe
 
Wakuu nimesoma kwa kina ufafanuzi wa Profesa Kuzilwa, aidha niliisoma pia taarifa yake kwa waandishi wa habari.

Nakumbuka alisema hatua zilichukuliwa mwaka 2005 na kuwa hao wahadhiri walipewa udahili upya university of Malawi na alilishangaa tamko la TCU.

Hapo wakuu nadhani tuwe more analytical, hisia zetu zisitupofushe macho isije ikatokea mtu akaanza kuuhoji upeo wetu wa kufikiri, kuchambua na kujenga hoja as a result credibility yetu ikapungua.

Mtu akisema chuo flani taaluma yake imeshuka tunatarajia atatupa vigezo alivyotumia mfano silabasi zake haziendani na mabadiliko ya dunia?,Hakina wahadhiri wa kutosha kwa standard zilizowekwa? Hakina maktaba inayokidhi vigezo? nakadhalika.

Nachelea kwamba mtu anaweza akatoka kuota ndoto na akaja akazimwaga hapa jamvini na wote tukaonekana tumetoka ndotoni.
 
Hii hoja kwamba chuo kikuu cha Mzumbe hakina hadhi nadhani ni hija mufilisi,tene mara nyingi inapendwa kutumiwa na wahitimu wa UDSM.

Wewe ndio unaleta hoja Mufilisi kabisa, una kigezo gani kuwa hoja hizi zinapenda kutumiwa na wahitimu wa UDSM?, ukiambiwa utoe ushahidi utakuwa hauna. Suala la Prof. Kuzilwa kujitetea ni hulka ya kila mkosaji, ulitaka akubali kuwa walifanya makosa?. Hakuna mtu hata kama alijua hivyo vyuo havina ithibati, ataweza kukiri hilo. Mwizi hawezi kukubali kaiba. Hata umeona mawaziri nao wanajitetea, kujitetea hakuhalalishi kosa kuwa sio kosa. Muhimu ni kufanya jitihada za kujikwamua kutoka katika hayo makosa, kama vile hao walioenda tena shule kutafuta PhD.

Mimi nadhani watu wanaokinyooshea vidole Chuo Kikuu cha Mzumbe wana nia njema, kile ni chuo chetu waTZ, na tunahitaji kiwe na wahadhiri walio bora ili kutoa wahitimu bora. Kukisema haimaanishi mtu ni mhitimu wa UDSM. Hata wa Mzumbe, SUA nk wana haki wakiona mabaya ya UDSM wayaseme.
 
Hii hoja kwamba chuo kikuu cha Mzumbe hakina hadhi nadhani ni hija mufilisi,tene mara nyingi inapendwa kutumiwa na wahitimu wa UDSM.

Mkuu Heshima mbele, Je unaweza kuthibitisha hili la wahitimu wa UDSM? Na kama ni kweli nini sababu hasa zinazokusudiwa maana sioni kama kuna sababu ya msingi hapa unless unithibitishie. Dhumuni langu katika mada hii ni kujua kile unachokifikiria na sio kupishana kwa maneno ni hoja tuu.
 
Wewe ndio unaleta hoja Mufilisi kabisa, una kigezo gani kuwa hoja hizi zinapenda kutumiwa na wahitimu wa UDSM?, ukiambiwa utoe ushahidi utakuwa hauna. Suala la Prof. Kuzilwa kujitetea ni hulka ya kila mkosaji, ulitaka akubali kuwa walifanya makosa?. Hakuna mtu hata kama alijua hivyo vyuo havina ithibati, ataweza kukiri hilo. Mwizi hawezi kukubali kaiba. Hata umeona mawaziri nao wanajitetea, kujitetea hakuhalalishi kosa kuwa sio kosa. Muhimu ni kufanya jitihada za kujikwamua kutoka katika hayo makosa, kama vile hao walioenda tena shule kutafuta PhD.

Mimi nadhani watu wanaokinyooshea vidole Chuo Kikuu cha Mzumbe wana nia njema, kile ni chuo chetu waTZ, na tunahitaji kiwe na wahadhiri walio bora ili kutoa wahitimu bora. Kukisema haimaanishi mtu ni mhitimu wa UDSM. Hata wa Mzumbe, SUA nk wana haki wakiona mabaya ya UDSM wayaseme.

Mkuu nakubaliana na wewe ILA USIKOMENTI KWA KUSIKIA , KOMENTI KWA VIGEZO, UKINYOOSHA KIDOLE NYOOSHA KWA VIGEZO, UKIFANYA HIVYO HAKUNA UBISHI tofauti na hivyo ni porojo.
 
Back
Top Bottom