Miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika1961: Rashid Mfaume Kawawa, Kenneth David Kaunda, Julius Kambarage Nyerere katika nyaraka za Sykes

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,266
MIAKA 60 YA UHURU WA TANGANYIKA1961: RASHID MFAUME KAWAWA, KENNETH DAVID KAUNDA NA JULIUS KAMBARAGE NYERERE NDANI YA NYARAKA ZA SYKES

Nimekutana na picha hiyo hapo chini kushoto Rashid Mfaume Kawawa, Kenneth David Kaunda na Julius Kambarage Nyerere.

Hii picha bila shaka ni ya miaka ya mwishoni 1950 au mwanzoni 1960.

Hii picha imenirudisha nyuma yapata miaka 30 sasa wakati nafanya utafiti wa historia ya TANU na Ally Sykes akanifungulia nyaraka zake ambazo kabla yangu hazikupata kuonekana na mtafiti yeyote.

Viongozi hawa niliowataja hapo juu wote nimewakuta katika nyaraka hizi.

Naamini msomaji wangu unaweza kuhisi vipi nilijihisi kukutana na hazina hii ya majina ya viongozi wakubwa katika historia ya Tanganyika.

Nakuomba uniruhusu nikushike mkono nikuingize katika dunia hii iliyokuwa ngeni kwangu nikukutanishe na mabingwa hawa wa siasa za Afrika katika miaka ile ya kupigania uhuru.

Nilipoanza kuandika kitabu changu ambacho naamini nyote mnakifahamu nilianza na maneno haya katika utangulizi:

''Ally Sykes ana barua ya mwaka 1954 iliyoandikwa kwa penseli kutoka kwa Zuberi Mtemvu kwenda kwake akimtaarifu juu ya mazungumzo aliyokuwanayo (Mtemvu) na Julius Nyerere kuhusu yeye na TANU; stakabadhi ya hundi ya posta toka kwa Ally Sykes kwenda kwa Japhet Kirilo wakati wa Mgogoro wa Ardhi ya Wameru; nakala ya barua isiyokuwa na tarehe kutoka TAA kwenda kwa Malkia Elizabeth iliyotiwa saini na viongozi wote wa TAA: Rais Julius Nyerere, Makamu wa Rais Abdulwahid Sykes, Katibu Mkuu Dome Okochi, Naibu Katibu Dossa Aziz, Mweka Hazina John Rupia, Naibu Mweka Hazina Ally Sykes ikimpongeza Malkia kwa kutawazwa.''

Ally Sykes ana barua ya mwaka 1952 kutoka kwa Rashid Mfaume Kawawa akiandika akiwa Bukoba kwenda kwa Ally Sykes ikimfahamisha juu ya hali ya siasa katika Kanda ya Ziwa; barua ya mwaka 1963 kutoka kwa Judith Listowel, Kenneth Kaunda, Julius Nyerere, Kasela Bantu, Chifu Thomas Marealle ...orodha haina mwisho.

Nipe rukhsa nimlete Kenneth Kaunda kama nilivyokutananae katika hizi Nyaraka za Sykes.

'Mwezi wa Novemba 1953 Ally Sykes alipokea barua kutoka kwa Kenneth Kaunda akimwalika kuhudhuria mkutano Lusaka.

Wakati ule ANC ilikuwa na manung'uniko kadhaa dhidi ya Waingereza na ilikuwa imeamua katika mapambano yake kutumia njia za amani.

Katika barua ambayo Kaunda alimpelekea Ally Sykes aliieleza kuwa watadai haki zao kwa njia za amani kwa namna kuwa hawatashirikiana na mtu yoyote katika shauri lolote litakalokuwa na madhara kwa maslahi ya Waafrika.''

Kila nilipokuwa nasoma nyaraka hizi ndiyo nilivyozidi kugubikwa na mshangao.

''Tarehe 12 Novemba, 1953 Ally Sykes alimwandikia barua Kaunda akimthibitishia kushiriki kwa Tanganyika African Government Servants Association (TAGSA) na TAA kwenye mkutano huo.

Ally Sykes alikuwa Katibu wa TAGSA.

Denis Phombeah na Bhoke Munanka, Katibu wa TAA Jimbo la Ziwa walikuwa wawakilishi wa TAA.

Mnamo tarehe 1 Desemba, Alexander Tobias alimwandikia barua Kamishina wa Kazi, Bennet akimuombea ruhusa Ally Sykes ahudhurie mkutano huo wa Lusaka.

Bennet alitoa rukhsa kwa Ally kuhudhuria mkutano ule ulioitishwa na Kaunda.

Munanka alinyimwa pasi ya kusafiria na serikali na kwa hivyo hakuweza kusafiri.

Ally Sykes na Phombeah baada ya kupewa ruhusa na serikali kuhudhuria mkutano huo waliondoka kwa ndege aina ya Dakota ya Central African Airways kwenda Lusaka kupitia Salisbury, Southern Rhodesia.''

Tuishie hapa.

Ally Sykes na Denis Phombeah walikamatwa uwanja wa ndege na hawakufika Lusaka.

Kwa kuhitiisha niruhusu nikufungulie jalada moja nililonikutanisha na Julius Kambarage Nyerere.

Nimemkuta Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika nyaraka hii: ''TANU memorandum to the United Nations Visiting Mission, 24th August, 1954.''

Katika barua hii kwenda UNO ndipo mimi kwa mara ya kwanza nimeiona sahihi ya Mwalimu nje ya noti tena baada ya uhuru mwaka wa 1961.

Picha ya pili ni moja ya Nyaraka za Sykes barua ya TAA kwa Malkia Elizabeth ikiwa na majina ya viongozi wote 1953, Ally Sykes na Denis Phombeah wakiwa Blantyre, baada ya kufukuzwa Salsbury, Southern Rhodesia.

Screenshot_20211206-040313_Facebook.jpg
 
Hawa wakina sykes wamekula sana neema za nchi hii,sykes waliyobakia sijui nao wanaendeleza legacy za mababu,baba zao

Ova
 
Back
Top Bottom