China ni nchi kubwa zaidi inayoendelea duniani, na ni nchi ya pili kwa ukubwa wa uchumi duniani, ikiifuata Marekani. Pamoja na maendeleo makubwa, China imekuwa mstari wa mbele kuzisaidia nchi nyingine zinazoendelea duniani, zikiwemo za Afrika, kujipatia maendeleo kwa njia na mazingira yanayoendana na nchi husika. China imefanya hivyo kwa njia mbalimbali, ikiwemo kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka nchi za Afrika, kuhamisha teknolojia bora na za kisasa za kilimo, na pia kuboresha miundombinu ya afya.
Asubuhi moja, Hama Moctar, mwenye umri wa miaka mitano, aliingia kwenye Hospitali Kuu ya Rufaa ya Niamey, mji mkuu wa Niger, kwa ajili ya kufuatilia matibabu yake, ikiwa ni siku 100 baada ya kufanyiwa upasuaji. Miguu yake, ambayo awali ilikuwa mifupi na imevunjika, sasa inamwezesha kutembea vizuri kwa kujiamini.
Miaka mitatu nyuma, mfupa wa paja lake la kushoto ulivunjika, na kufuatiwa na maambukizi ya vijidudu, na mguu wake ukawa mfupi kwa sentimita 10. Wakati madaktari wa huko wakisisitiza kuwa njia pekee ya kumwokoa ni kumkata mguu, Nong Jianbu, mtaalamu wa magonjwa kama hayo kutoka timu ya 24 ya madaktari wa China nchini Niger, alipendekeza njia nyingine, ambayo ni utaalamu wa Ilizarov. Kwa kutumia vifaa kutoka China na juhudi za pamoja, wataalamu wa upasuaji wa China na Niger walifanya upasuaji huo mgumu, na hii leo, miguu yote ya Moctar inalingana urefu na anaweza kutembea kwa uhuru bila ya matatizo yoyote.
Hospitali Kuu ya Rufaa ya Niamey, iliyojengwa na China mwaka 2016, ni moja ya hospitali kubwa zaidi katika kanda ya Afrika Magharibi, na ni ishara ya uhusiano wa pande mbili uliodumu kwa nusu karne. Tangu mwaka 1976, timu za madaktari wa China kutoka mkoa wa Guangxi Zhuang zimefanya kazi bila ya kuchoka nchini Niger, na kutoa mchango mkubwa sana katika mfumo wa afya wa nchi hiyo. Katika miaka iliyopita, madaktari wa China wamekabiliana na changamoto mbalimbali.
Wang Zhou, mjumbe wa timu ya 24 ya madaktari wa China nchini Niger, anakumbuka usiku mmoja wa mwezi Desemba mwaka 2024, ambapo mwanamke mmoja wa Niger, alipatwa na mshtuko wa moyo na kukimbizwa hospitali. Wang, wa kushirikiana na muuguzi anayeitwa Wen Lina, walichukua hatua za haraka wa kusafisha mishipa ya damu iliyokuwa imeziba. Kupitia upasuaji, walifanikiwa kuokoa maisha ya mwanamke huyo kwa wakati, jambo lililompa furaha sana Wang Zhou ambaye alisema, mafanikio katikati ya changamoto ni muujiza mkubwa.
Katika idara ya upasuaji wa uti wa mgongo, Li Xiaofeng naye alikabiliwa na hali kama hiyo, mwanamke mmoja wa miaka 50 aliyekuwa na uvimbe katika uti wake wa mgongo. Kutokana na ukosefu wa vifaa muhimu vya tiba na teknolojia katika hospitali za huko, wafanyakazi wa afya hawakuwa na imani kama wanaweza kufanya upasuaji huo. Li alikesha akisoma matokeo ya picha zake za kielektroniki na kushauriana na wataalamu walioko nchini China kupitia mtandao. Baada ya upasuaji uliochukua saa mbili, uvimbe huo uliondolewa. Li anasema, upasuaji huo ulikuwa kama kuweka uzi kwenye sindano katikati ya dhoruba ya mchanga, lakini kupona kwa mwanamke huyo kulifanya hatari zote kuwa na maana.
Tangu mwaka 1976, zaidi ya madaktari 750 wa China wametibu karibu wagonjwa milioni moja nchini Niger. Kiongozi wa timu ya 24 ya madaktari wa China nchini Niger, Zheng Zhida anasema, kila mgonjwa anayepona anaandika ukurasa mpya wa urafiki kati ya China na Afrika.
Mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo, Mamane Daou anasema, uhusiano kati ya China na Niger umezaa matunda, na kuongeza kuwa, timu ya madaktari wa China sio tu inapeleka madaktari wabobezi lakini pia inatoa vifaa muhimu vya matibabu. Anasema utaalamu wao na kujitolea kwao vinaheshimiwa sana, na kwamba hospitali hiyo kwa sasa inapokea wagonjwa kutoka nchi jirani za Mali na Burkina Faso.