Kwa mujibu wa falsafa za Hayati Mwl. JK Nyerere, upinzani wa kweli utatokea ccm; Haikosi kwa maneno haya alimaanisha kwamba watakaoingia upinzani kwa wingi tokea ccm watauimarisha na kuupa nguvu. Hilo hufanywa na watu madhuti na sio wababaishaji au oili chafu kama tunavyotaka kuaminishwa. Mwl. hakusema makapi yatatoka ccm kuja upinzani bali wajenzi imara wa demokrasia ya kweli watatua upinzani na kuupa mwanzo mpya. Siku zote alionyesha kuichoka na kukerwa na ccm kama chama kinachonuka rushwa na kilichopoteza uelekeo na kutamani ipasuke vipande vipande watu watoke waende upinzani upatikane mwanga mpya. Sina hakika sana kama alimaanisha pia kwamba upinzani utachukua dola mara moja lakini ni wazi badiliko hilo ni taraja la kuleta uwiano wa kisiasa ndani ya nchi na kuondoa hodhi ya chama kimoja katika kuamua mustakabali wa nchi; wapinzani watapata madiwani zaidi, wabunge na hivyo kuwa sehemu kuu katika maamuzi muhimu ya nchi. Mimi binafsi sina chama cha siasa na kiujumla bado sijaona siasa za kufaa ndani ya nchi; hatuna dira ya taifa, vipaumbele wala maadili ya uongozi. Saisa bila nguzo hizi tatu katika katiba ya nchi ni vurugu mechi tu; hata akipatikana kiongozi msafi kiasi gani pale Ikulu bado ni shida tu, hakuna cha kumdhibiti asigeuke fisadi akiwa pale. Kwa maneno mengine, pamoja na nguvu ya upinzani kuongezeka bado hatujihakikishii jambo la maana sana katika mustakabali wa nchi yetu; wala haijalishi sana nani anakuja madarakani iwe upinzani au wabakie haohao mambo yatakuwa yaleyale tu; ni mvinyo uleule kwenye viriba vipya. Hata hivyo yafaa tusipuuze kabisa kejeli za oili chafu na makapi kwani ni heri nusu shari kuliko shari kamili. Haidhuru viriba vimekuwa vipya.