Mfumo wa uchaguzi zanzibar uwe kama israel


BongoTz

BongoTz

JF-Expert Member
Joined
Nov 3, 2006
Messages
272
Likes
2
Points
0
BongoTz

BongoTz

JF-Expert Member
Joined Nov 3, 2006
272 2 0
Na, Antar Sangali, Bagamoyo [www.bongotz.com]

Ili kuepuka utata na kuweka mazingira bora ya kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki visiwani, hatimaye kila pande kisiasa ziridhike na matokeo, kuna kila haja yalazima Zanzibar kuiga mfumo wa uchaguzi wa Israel.

Kimsingi chaguzi zote zilizofanyika Zanzibar toka mwaka 1957, 1961 , 1961,1963 na baadaye 1995 na 2000 : nidhahiri historia imekuwa ikijirudia kila miongo inavyozidi kupita katika siasa za Visiwa hivyo na kuibua malalamiko na shutuma toka upande mmoja wa siasa dhidi ya mwingine.

Nimejaribu kufanya tathmini na uchambuzi mwepesi kulingana historia ya chaguzi za Zanzibar na siasa zake na hatima yake nimegota mahali nafikiri ipo haja ya moja kwa moja nchi hiyo kufanya au kubadili aina ya mfumo wa uchaguzi wake kwa lengo la kuipatia Zanzibar utulivu na hatimaye kupunguza vuguvugu, joto na mukari wa kisiasa uliotanda.Kubwa linalohitajika ni katika kuandaa mazingira hayo ni lazima kufanyike marekebisho ya katiba ya nchi au sheria husika za uchaguzi na kubadili mfumo mzima wa uchaguzi .

Lakini kwa kubakia na katiba iliyopo ni kuendeleza malumbano yatakayopelekea siku moja Zanzibar yafumke mambo ambayo hakutakuwa na mzimaji au mzuiaji.

CCM inayotokana na chama cha ASP visiwani Zanzibar ni chama cha Waafrika waliolilia kujitawala kutokana na aina iliyowakumba ya ukandamizaji wa haki na uhuru wao wa kuweza kujiamulia mambo katika ardhi yao.Ama kwa hakika kundi kubwa la wafrika weusi tititi ndilo lililokuwa halina sauti na fursa pana katika zama za ukoloni visiwani humo.

Kundi hilo ndilo lililoongozwa na Hayati Abeid Aman Karume na kufanya Mapinduzi 1964. Hakuna awezae kusema ukandamizaji haukuwepo Zanzibar na kwa kusema hayakuwepo hayo mapinduzi ya '64. Ila swali tunalopaswa kuhoji ni kwamba: kwa nini Mapinduzi hayo yalifanyika?

ASP ilionekana kupata harubu nzito na kedi zilizofanana na takilifu wanazozipata CUF leo katika siasa za Zanzibar ambazo nazo ukizitazama zinatokana na mazingira ya kikatiba iliyopo ikiendana sambamba na mfumo wa uchaguzi wenyewe.

Nimeipitia katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na mtiririko wake katika mfumo wa uchaguzi nikilinganisha na Madaraka ya Serikali, Mamlaka ya Tume ya Uchaguzi na mipaka yake lakini kubwa nililobaini ni kujichomoza na kukomaa kwa utata usioweza kupata suluhu endapo kama hakutafanyika dhamira ya makusudi ya kubadili katiba iliyopo kwasasa.

Marekebisho ya sheria au Katiba ya Zanzibar yafanyike kwa kuzingatia histori ya Mapinduzi ya Januari 12 1964 kwa sababu Mapinduzi ni alama isiyofutika Visiwani humo na ni kazi kubwa kuzungumzia ukoloni bila ya kuyadurusu na kuyaheshimu Mapinduzi ya visiwa hivyo.

Mathalani, Katiba iliyopo katika sura ya Tatu inataja na kukinga haki za lazima na uhuru wa mtu binafsi katika vifungu toka cha 11 hadi 25, lakini utekelezaji wa yote unaonekana kupwaya kutokana na mazingira ya kisiasa na mfumo dhaifu wa uchaguzi.

Tutazame mfano katika kifungu cha 51 kinatamka ya kwamba Madaraka ya Serikali ya Zanzibar yatakuwa mikononi mwa Rais na kwa mujibu wa katiba hii,ana weza kuyatekeleza mwenyewe moja kwa moja au kuwapa viongozi walio chini yake kutekeleza madaraka hayo. Chini ya misingi ya utawala bora na kuheshimu haki za Bianadamu ni vema madaraka ya Nchi kubaki mikononi mwa wananchi wenyewe kwa maana ya kuhimiza sauti na maamuzi ya umma, hususani uwajibikaji wa serikali kwa wananchi na kuifanya dola kuwa imara inayotii maamumuzi ya raia wapiga kura ambao ndio wajenga nchi.

Katika chaguzi zilizofanyika Zanzibar katika ukoloni uliokuwa ukikingwa na katiba ya Kiingereza kwa maslahi ya utawala wa Kisultan ni kiini cha Katiba ya Kiingereza na Katiba iliyoundwa baada ya Mapinduzi kujali sana na kutanguliza maslahi zaidi ya kisiasa kuliko ukweli wenye kuondosha utata husika au upana zaidi wa mipaka ya demokrasia haki na wajibu kwa raia.

Mkanganyiko katika katiba ya Zanzibar unazidi kutoa sura isiyo sawia ukikitazama kifungu cha 119 kwa mfano ambacho kina sema kuwa: kutakuwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ambayo itakuwa na wajumbe watakaoteuliwa na Rais. Lakini sehemu (d) inakataza kwamba Tume hiyo haitakuwa na Mjumbe ambaye ni Kiongozi wa Chama Cha Siasa lakini cha ajabu katika mazingira ya kufikia MUAFAKA, kifungu hiki kinaonekana kukiukwa na hatimaye Tume ikawa na wajumbe toka Vyama vya Siasa.

Mazingira haya kwa namna iliyo kubwa yameweza pia kujenga utata na ukorofi katika kutimiza matakwa ya sheria ya uchaguzi na kuifanya Tume kuwa na sura ya kisiasa kuliko Mamlaka na Madaraka ya Tume kisheria.

Wajerumani wana Katiba inayotoa sura za aina tatu sawia zilizo na uwazi katika kujali maslahi sahihi ya chama cha siasa, nafasi ya Mbunge mhusika na namna ambayo Mbunge anaweza kuona inafaa kulingana na wakati ulivyo. Wajarumani wenyewe wanaita Three Line Decision.

Katiba ya Zanzibar na katiba nyingi katika Bara la Afrika ni katiba zinazojali na kuainisha au kuweka mbele maslahi ya kisiasa kuliko utaifa, nafasi haba ya kidemokrasia ina ufinyu wa fursa kwa Mbunge aliyepigiwa kura kutokana na chama chake anachotoka na sauti yenye uzito kuheshimika toka kwa wapiga kura na kutopewa kwao uzito unaostahili.

Hili ni tatizo kuu la kimsingi ambalo kwa uchache wangu naona ni kiini mama cha kuzuka kwa hitilafu na kuibua mizozo ya kudumu katika Visiwa hivyo kwa kila chama kitakachotawala na kushika madaraka ya Visiwa hivyo vyenye zao la karafuu nyingi Barani Afrika.

Katiba ya Kiingereza katika Zanzibar ni wazi ilikuwa ikitazama zaidi ni vipi utawala wa kisultan utaendelea kubaki madarakani na jinsi gani vyama vya siasa vitatumika kumnusuru sultan hata kama endapo chama kimojawapo kitapata idhini na kubeba sauti ya wengi ilhali kisifikie haja ya kutawala na kupata madaraka.

Mgawanyo wa majimbo baina ya kisiwa cha Unguja na Pemba ni utata wa msingi tokea enzi za ukoloni wa visiwa hivyo.Ili uweze kuwa mshidi wa Zanzibar ni lazima ukubalike kote Pemba na Unguja.Kwa Maana iliyo sahihi ni kwamba kisiwa cha Pemba kinaitegemea Unguja na Unguja inategemea Pemba hali kadhalika. Tatizo la kimsingi ni kwamba huwezi kupigiwa kura Pemba ikiwa wewe huna asili ya Pemba na kadhalika Unguja vivyohivyo, lakini pia huwezi kupata kura katika jimbo la Donge au Mkwajuni Kaskazini Unguja ikiwa asili ya uzawa wako ni Kusini Unguja huko Kizimkazi ima utoke Bwejuu.Kwa upande mwingine kuna Ukaskazini na Ukusini sembuse Upemba na Uunguja na katika makundi mengine wazanzibar wanajitaja na kujinasibu na kuwatenga wahamiaji (wakata maji) na wazalia.

Chaguzi za Zanzibar aghalab wakati ukiwadia ndizo zinazoamsha joto na kadhia ya kufikia mahali penye tishio la usalama na utulivu wa nchi,wabunge na wawakilishi ni nadra kuongozwa na utashi na maslahi ya kitaifa kuliko wanavyotanguliza misimamo ya sera za vyama vyao.

Hisia za ujimbo,ukabila na aina ya rangi ya mtu na mahali anapotoka husababishwa na mazingira ya mfumo wa uchaguzi kama nilivyosema awali kwamba ni kazi kuchaguliwa Chake Chake ikiwa wewe mgombea asili yako ni Bumbwini. Mfumo wa uchaguzi unaofanana na Israel ni wazi utafute dhana za majimbo,nguvu za siasa, asili ya mtu na zaidi kupuuzia itikadi za kisiasa ambazo ni kiini na chachu mbaya ya kumea kwa siasa za Zanzibar Historia inaoonyesha hata baada ya kupita Mapinduzi mwaka 1964 yalifumka makundi ndani ya ASP na wanamapinduzi wao kwa wao kupigana mapande kwamba fulani ni mzaliwa na mwingine ni makata maji, huyu mpemba na yule muunguja. Mgawanyo huu wenye asili na jadi unahiitaji kupatiwa dawa itakayotibu kansa hii Visiwani.

Israel wanafanya uchaguzi wenye uwakilishi wa moja kwa moja yaani Direct Proposational Represantation na wabunge wake hawatokani na majimbo ya uchaguzi bali wingi wa kura kinachopigiwa chama ndiko kunakotoa idadi ya wabunge au wawakilishi Bungeni na kisha Waziri Mkuu anathibitishwa na Bunge. Nchi ya Israel bila ya shaka wamezingatia siasa zao, chimbuko lake na uasili unaoambatana na Taifa lao hali ambayo inafanana kwa kiasi kikubwa na kisiwa cha Zanzibar kulingana na asili ya makundi ya kikabila ya kiitikadi, rangi na dini za watu wake.Zanzibar isitazamwe kama ni kisiwa kidogo lakini ni vyema ikatizamwa na kuhukumiwa kwa historia yake na asili ya visiwa hivyo.

Kabla na hata baada ya ujio wa wakoloni watu katika Zanzibar walipigana vita aidha vya kukataa kutawaliwa au kutumiwa na wakoloni kukinga utawala uliokuwa na nguvu kulingana na wakati. Nguvu hii sasa inaonekana kushikwa na walio katika madaraka kwa mana ya waliopindua na kundi kubwa la wanaopigania kutawala wana kundi kubwa pia lenye sauti na joto lilelile la siasa zama na zama.

Ni vema visiwani Zanzibar wananchi wapige kura bila ya kuwa na majimbo ya uchaguzi matokeo ya wingi wa kura katika vyama vya siasa yatoe idadi ya wabunge watakaoingia katika Baraza la Wawakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.Rais iwapo ameshinda kutokana na chama chake cha siasa Waziri Kiongozi na Mwanasheria Mkuu wathibishwe na Baraza la wawakilishi. Hali hii inaweza pia kutoa nafasi ya wazanzibar walio wengi ambao wanaishi nje ya nchi kuweza kupiga kura na kuchagua aina ya chama wanachokipenda kulingana na sera zake na hasa ukizingatia sasa watu wanatazama chama na ufanisi wa sera zake na utekekezaji wake katika kukuza uchumi,ustawi wa jamii na mendeeo kwa ujumla.

Sheria mathalan ya ukaazi wa miaka mitano ni kinyume na haki za binadamu na haitoi picha nzuri wala sawia ya misingi ya demokrasia zaidi ya sheria hiyo kulenga kuinyanyasa ASP wakati wa ukoloni na sasa inaonekana kuifinya kambi nzima ya upinzania Zanzibar.

Mtanganyika anapiga kura katika Jamhuri ya Muungano Tanzania kwenye mikoa mathalan Shinyanga, Mwanza, Iringa, Pemba, Arusha kwa uhuru bila kizuizi na hoja ya ukaazi, iwe vipi fursa hii isipatikane katika Zanzibar?

Inashangaza sana mzanzibar ana haki ya kuwa Mbunge ,Mkuu wa Mkoa ,Mkuu wa Wilaya, Waziri na Rais katika Muungano ni kwanini mtanganyika asiwe hata mjumbe wa nyumba kumi katika Pemba au Unguja!?

Huu ni utata mzito na kama utazidi kuachiwa bila kukaliwa kitako ni wazi suluhu,utulivu na umoja wa kweli wa kitaifa katika Zanziabar vitabaki kuwa ndoto na kamwe hakutotoa taswira njema kwa mustakabali wa visiwa hivyo vyenye watu wenye kujinasibu kwa rangi, dini na asili zao kimsingi haitopatikana sumile ng'o.

Ni wazi bila ya kufanyika marekebisho ya katiba na sheria ya uchaguzi mazingira ya kisiasa huko Zanzibar yataendelea kuibuka katika kila wakati unapoanza au kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Kedi, hila na ghiliba na chungu za uchaguzi walianza kuzionja ASP na kuibuka kwa Mapinduzi ni matokeo ya ukandamizaji uliopita mipaka hivi kweli uchungu ule hauwaumi wapinzani wa leo na pengine wakafika mahali siku moja wakasema "tumechoka lolote na liwe" tazama hatari hiyo ijayo!!

Zanzibar ni sehemu ya Muungano, Rais Mkapa anamaliza muda wake madarakani, tayari wiki hii ameliaga rasmi Jeshi la Wananachi wa Tanzania (TPDF) kadhalika amezitembelea nchi kadhaa majirani kuziaga, bila shaka Mgombea ajae mwaka 2005 kulingana na upepo wa siasa za Tanzania na uanagenzi wa vyama vya upinzani ulipo Mhe Jakaya Kikwete nidhahiri atakikalia na kukirithi kiti cha enzi katika Ikulu ya Magogoni Dar es Salaam akipeperusha Bendera ta Taifa la Tanzania kwa miaka mitano ijayo huku Tausi wakiimba na kurukaruka kwenye bustani maridadi za ikulu hiyo aliyowahi kuishi Mzee Nyerere, Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa.

"JK" na serikali ya Muungano wanawajibu na haki ya kuyapatia matatizo na malalamiko katika mambo yanayohusu Muungano lakini kwa upande mwingine muundo wa Muungano wa serikali mbili ni kitu muafaka kwa sasa kutokana na historia na kudumu kwa Muungano huo na mchanganyiko wa damu za Watanganyika na Wazanzibar.

P.S. Makala hii ilirushwa hewani kwa mara ya kwanza na tovuti ya BongoTz October 24, 2005

Mungu ibariki Tanzania!
 
N

Ngekewa

JF-Expert Member
Joined
Jul 8, 2008
Messages
7,725
Likes
27
Points
145
N

Ngekewa

JF-Expert Member
Joined Jul 8, 2008
7,725 27 145
Matatizo ya wazanzibari yataamuliwa na wao wenyewe kikwete kazi yake itakuwa kupongeza tu
 
B

Bull

JF-Expert Member
Joined
Nov 4, 2008
Messages
984
Likes
0
Points
0
B

Bull

JF-Expert Member
Joined Nov 4, 2008
984 0 0
African problems need african solution, kwanini tuwaige waizraeli? wao mbona hawafikirii kuiga waafrika?
 

Forum statistics

Threads 1,251,234
Members 481,615
Posts 29,763,493