Mfahamu Noureddine wa Genk kwa Samatta

Mfahamu Noureddine wa Genk kwa Samatta

aleesha

JF-Expert Member
Joined
Oct 17, 2016
Posts
834
Reaction score
1,213
Na Edo Kumwembe

NILIWASILI katika mji wa Genk jioni moja ya Mwezi Machi mwaka jana. Baridi ilikuwa inaondoka Ulaya lakini kwa ngozi iliyotoka Tanzania ni wazi kwamba baridi ilikuwa kali. Niliwasili katika kituo kikuu cha Treni cha Genk wakati jua likizama upande wa Magharibi.

Mji mdogo, mkimya, mpaka sasa una wakazi 65,000 tu. Wakazi wote wa Genk hawaujazi uwanja wa Old Trafford. Lakini ni mji uliopangiliwa vema na umetulia sana.

Mwenyeji wangu alikuwa Mbwana Samatta. Ndiye mtu ambaye nilikuwa namfuata katika mji wa Genk. Jioni ambayo nilifika Genk, Samatta alikuwa anafanya mazoezi na klabu yake ya Genk. Sikuweza kumpata katika simu.

Hata hivyo tayari alikuwa amenielekeza nifikie katika hotel inayoitwa M Hotel. Inatajwa kuwa hoteli bora zaidi kwa Genk. Udogo wa mji wa Genk umeruhusu hoteli chache sana za kiwango cha juu. Zipo tano tu. Nilipokwenda M hotel nikaambiwa imejaa.

Sikupata tabu sana kutafuta hoteli nyingine. Dada wa mapokezi katika hoteli ya M alipiga simu mbili tatu kwa hoteli nyingine za Genk akaniambia kuna nafasi imepatikana katika hoteli ya Atlantis. Ni hoteli nyingine ya kifahari.

Nilichukua taksi nikaenda hoteli ya Atlantis. Ilikuwa hoteli nzuri na ya kisasa sana ingawa haikuwa ya ghorofa. Mandhari yake yalikuwa tulivu na niliipenda. Vyumba vyake vilikuwa vya kisasa. Katika sehemu ya mapokezi nilimkuta msichana mrembo wa kizungu aliyejitambulisha kwa jina la Lydia.

Alinipatia chumba changu huku akionekana kuwa mchangamfu sana. Tulipiga stori nyingi za haraka haraka. Ghafla alitokea kijana mmoja wa Kiarabu ambaye alikuwa amevaa vazi la wapishi. Alitokea jikoni. Akaniuliza maswali ya hapa na pale katika sura iliyokuwa imevaa tabasamu kwa muda wote.

Nilipoacha mizigo yangu chumbani nilirudi haraka haraka kuongea na Lydia. Baadaye yule kijana wa Kiarabu ambaye nilikuja kujua jina lake kuwa ni Noureddin. Nadhani jina lake liliandikwa kwa mbwembwe za asili yao lakini kwa Kiswahili angeitwa Nurdin tu.

Noureddin akageuka kuwa mpishi wangu binafsi. Nilimuagiza aina ya chakula ambacho nilitaka anipikie. Alionekana kuwa mchangamfu zaidi ya Lydia. Hapo hapo pia alikuwa anahusika na kaunta na ndiye ambaye alikuwa ananiletea kinywaji kwa kasi kubwa pindi nikimuagiza.

Baadaye mimi na yeye tukahamia kaunta huku pia akihudumia wateja wengi. Aliniuliza kisa ambacho kilinipeleka Genk nikamwambia kuhusu Samatta. Akasema anamfahamu Samatta kwa sababu ujio wake ulitangazwa katika televisheni na redio za Ubelgiji.

Wakati wengi wa Genk ni mashabiki wa timu ya Genk. Ndio timu ambayo wanaifuatilia zaidi. Halikuwa jambo la kushangaza kwa Noureddin kufahamu ujio wa Samatta. Nilitegemea hilo.

Usiku ulipozidi kuwa mwingi nilienda zangu kulala nikimuacha Noureddin na wafanyakazi wengine wakihudumia wateja na wageni waliokuwa pale Baa. Nilikuwa nimechoka na niliacha ujumbe tu wa simu ya mkononi kwa Samatta kuwa nilikuwa nimefika Genk lakini sikufikia Hoteli M ambayo alikuwa amenielekeza na badala yake nilikuwa Hoteli ya Atlantis.

Asubuhi yake niliamka na kukutana na sura ya tabasamu ya Noureddin akiwa jikoni akiandaa chakula cha asubuhi kwa wateja. Lydia alikuwa pale pale mapokezi akiendelea kupiga kazi zake kama kawaida. Walionekana kuwa wachapakazi wazuri kama ilivyokuwa kwa wafanyakazi wengine.

Wakati nikipata mlo wa asubuhi Noureddin alikuja kukaa karibu yangu tukaanza maongezi mapya. Hapa ndipo Noureddin aliponiacha hoi. Nilimuuza zamu yake ilikuwa inaisha saa ngapi na angerudi tena hotelini lini.“Mimi sina zamu. Mimi ndiye mmiliki wa hoteli hii na yule Lydia pale mapokezi ni Mke wangu.” Nilibaki mdomo wazi. Ndiyo, mtu ambaye nilikuwa namuagiza anipikie chakula tangu jana usiku, mtu ambaye nilikuwa namtuma aniletee kinywaji, kumbe ndiye alikuwa mmiliki wa hoteli. Nilidhani alikuwa mpishi au Mfanyakazi wa kawaida!

Katika maongezi Noureddin ndipo aliponieleza kwamba yeye ni Mbelgiji lakini ana asili ya Morocco. Wazazi wake wanatoka katika jiji la Casablanca. Akanieleza jinsi ambavyo alianza biashara yake zamani akiwa kijana mdogo lakini mambo yake yakamnyookea vema. Akanieleza kuwa Lydia alikuwa ni msichana wa Kiitaliano na walifunga ndoa mwaka mmoja uliopita ingawa bado hawakubahatika kuwa na mtoto.

Sikutaka kumwambia lolote jinsi ambavyo matajiri wa Tanzania wasingeweza kuishi kama yeye anavyoishi. Kikubwa tulianza maongezi mengine kuhusu yeye kuja kutembea Tanzania. Akaniambia yeye na Lydia wanatamani sana kuja Zanzibar. Niliwaambia wasiwe na shaka, ningekuwa mwenyeji wao.

Saa nne ulikuwa muda ambao nilipanga kwenda kwa Samatta. Noureddin aliniambia angenipeleka tu kwa sababu mji wa Genk ulikuwa mdogo sana na yeye alikuwa anatazamia kuondoka muda huo kurudi nyumbani kupumzika. Kumbe yeye na Lydia wana chumba cha kupumzika hotelini na wana nyumba yao.

Ilipofika saa nne, mshangao mwingine ulikuwa unanisubiri. Ni kweli Noureddin alikuwa tajiri. Alinipeleka katika eneo la maegesho ya magari nikauona utajiri wake. Magari mawili ya kifahari yalikuwa yamefunikwa na Turubai. Moja lilikuwa lake, aina ya Audi New Model. Jingine lilikuwa la Lydia aina ya Mercedes Benz, toleo jipya.

Tukachukua Audi kwa ajili ya kunipeleka nyumbani kwa Samatta kupitia kwa anuani ambayo Samatta alikuwa amenipa. Ulikuwa mwendo wa dakika tano tu kutokea hotelini kwake. Yeye mwenyewe alikuwa na hamu kubwa ya kumuona Samatta. Alinisihi kama angeweza kupata nafasi ya kupiga picha na Samatta, lakini pia kubadilishana namba za simu.

Tulipofika kwa Samatta nilimtambulisha Noureddin kwa Samatta. Bahati nzuri zaidi kwa Samatta ni kwamba Noureddin alimwambia kuwa asiwe na hofu kuhusu maisha ya Genk kwa vile yeye ni mwenyeji, lakini pia angempeleka katika misikiti ya Wamorocco na Waturuki kwa ajili ya kuswali.

Noureddin ni mtu wa msikitini kama ilivyo kwa Samatta.Kwa jinsi alivyokuwa, Samatta mwenyewe alikuwa anashangaa mtu kama Noureddin alivyoweza kumiliki hoteli ya Atlantis ambayo yeye pia anaifahamu.

Siku mbili baadaye nilihama hoteli ya Noureddin na kuhamia kwa Mbwana kwa ajili ya kufanya naye mahojiano yanayoendana na jinsi anavyoishi nyumbani kwake Genk. Hata hivyo, Noureddin ndiye ambaye alikuwa ananionyesha mji wa Genk.

Noureddin pia ndiye ambaye alinipitia kunipeleka uwanjani kutazama mechi ya Genk na Oastende katika uwanja wa Genk ambao upo nje kidogo ya mji. Aliniacha uwanjani akageuka kuendelea na shughuli zake za upishi katika hoteli yake anayoimiliki mwenyewe.

Siku ya kuondoka Genk, Samatta alikuwa bize mazoezini, Noureddin aliamua kunipeleka katika mji wa karibu na Genk unaoitwa Hasselt kwa sababu ni katika mji huo ndio kulikuwa na treni iliyokuwa inakwenda moja kwa moja mpaka katika uwanja wa ndege wa Brussels.

Kwanini nimekusimulia kuhusu Noureddin? Nimejifunza kitu kutoka kwake. Nimejifunza jinsi ambavyo bado kuna wanadamu wachache wameendelea kuishi kawaida licha ya Mwenyezi Mungu kubadilisha maisha yao.

Nimejifunza upendo na ukaribu kutoka kwa Noureddin. Mali, umaarufu na madaraka huwa tunaviacha duniani. Nimejifunza pia kuwa usimdharau mtu kwa jinsi ulivyomuona kwa mara ya kwanza. Kwangu kwa mara ya kwanza nilimuona Noureddin ni mpishi tu wa kawaida. Kumbe sio.

Mara nyingi huwa nachati na Noureddin kupitia katika Whatsapp huwa ananikumbusha kutenda mema. Mara ya mwisho nilimpa Samatta jezi ya Taifa Stars ampelekee Genk.

Huyo ndiye Noureddin wa Genk.

Tujifunze kuishi kama yeye!
 
Dah sidhani kama bongo hii walau yupo hata mmoja mwenye mali kama nurdin ila anaishi kama nurdin
 
Mara nyingi wengi wetu mali /utajiri vinakuwa vipo juu yetu sana na hatuvutiwi na hali za kibinaadam kama uungwana, ukarimu na utu ni kama tu 'Washamba' wa mali, hizi mali na hata madaraka hayatuongezei chochote ktk utu na ubinaadam wetu hii ina maana sisi bado ni jamii 'inayojitafuta' 'hatujakua' kwa viwango hivyo na hasa ktk ngazi ya 'utambuzi' na 'exposure'

Kwa ufupi tunapaswa sana kutafuta mali na hata madaraka lkn visiwe juu yetu na vikatu 'control'

Ndo maana tupo ktk jamii ukipata hata nafasi ya kazi sehemu na ukiwa muadilifu eti jamii ina kushangaa na kauli za huyu mjinga alikuwa au ana kazi lkn hajachangamka kabisa hapa wana maana 'uibe' yaani sehemu kubwa jamii yetu hatupeani mambo chanya kama kufanya kazi kwa bidii, kuwa waaminifu, kuwa na malengo na ku 'save' tupatacho nachelea kusema bado jamii yetu ipo 'backward' tunaishi kwa ramli zaidi
 
Back
Top Bottom