Mfahamu Kwame Nkurumah

Sky Eclat

JF-Expert Member
Oct 17, 2012
57,595
215,276
220px-Kwame_Nkrumah_%28JFKWHP-AR6409-A%29.jpg


Alizaliwa mwaka 1909 mjini Nkrorful Ghana wakati huo ikiitwa Gold Coast. Hakuna aliyekuwa na elimu katika familia yake enzi hizo. Kwame ni jina wanalopewa watoto wa kiume wanaozaliwa Jumamosi katika mila za Ghana.

Baada ya elimu yake ya awali nchini Ghana mwaka 1935 Nkurumah alisafiri kwenda Pennsylvania USA ambako alisoma Batchelor of Arts, Batchelor of Theology na Masters of Science.

Mwaka 1945 alijiunga na London School of Economics kufanya PhD ya Anthropology

===================================================================

HUYU NDIYO KWAME NKRUMAH JABALI LA UKOMBOZI WA AFRIKA.

Kwa mamilioni ya watu ndani na nje ya Afrika, Kwame Nkrumah ndiye Afrika na Afrika ndiyo Kwame Nkrumah; Kwa Wakoloni na Mabeberu jina la Nkrumah ni laana kwao; kwa Masetla na Walowezi jina lake ni onyo kwamba siku zao zinahesabika; kwa Waafrika wanaokandamizwa kwa ukoloni na ubeberu wa kimataifa, jina lake ni pumzi ya matumaini, nyenzo ya uhuru, ushindi, udugu na usawa kwa wote”.
Ndivyo yalivyosomeka maneno ya bango moja mjini Accra, Ghana miaka ya 1960 wakati wa kilele cha harakati za Uhuru barani Afrika. Ghana ilipata uhuru Machi 6, 1957 chini ya Dakta Kwame Nkrumah kama Rais wa kwanza.

Lakini Nkrumah hakuridhika na uhuru wa nchi yake pekee, alisema: “Uhuru wa Ghana hautakuwa na maana kama nchi zingine za Kiafrika zitaendelea kuwa chini ya Utawala wa Kikoloni”, kuonesha jinsi mwanaharakati huyu alivyokuwa tayari kujitoa mhanga kwa ukombozi wa Bara zima la Afrika.
Mwaka mmoja tu baada ya uhuru wa Ghana, Nkrumah aliitisha Mkutano wa mataifa yote ya Afrika (All African People’s Conference) mjini Accra, Desemba 1958, kuzungumzia agenda ya harakati za uhuru, namna ya kulinda uhuru unaopatikana na kuendeleza mapinduzi ya Kiafrika. Kati ya waliohudhuria, baadhi yao ndio hao waliokuja kuwa viongozi wa nchi zao kufuatia uhuru.

Hao ni pamoja na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika); Dakta Hastings Kamuzu Banda (Nyazaland, baadaye kuitwa Malawi); Joshua Nkomo (Southern Rhodesia/Zimbabwe), Dakta Keneth Kaunda (Northern Rhodesia/Zambia) na Patrice Emery Lumumba (Congo Leopoldville/Zaire/DRC).
Wengine walikuwa ni Amilcar Cabral (Portuguese Guinea/Guinea Bissau); Holden Robert (Angola) na Tom Mboya (Kenya) aliyewakilisha Vyama vya Wafanyakazi na ambaye pia alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo.

Walihudhuria pia kwa “Mwaliko maalum”, wanaharakati kutoka Zanzibar: Abeid Amani Karume (Afro-Shirazi Party – ASP) na Ali Muhsin (Zanzibar Nationalist Party – ZNP). ASP na ZNP vilikuwa na ugomvi na uhasama mkubwa wa kisera na kimaono kiwango cha kuzuia meli ya uhuru kuong’oa nanga Visiwani.

Wakati ZNP kilichokuwa cha mrengo wa siasa za Kikomunisti na kiharakati zaidi (kwa msukumo wa Abdulrahman Babu kama Katibu Mkuu) kilitaka uhuru mara moja; ASP chenye siasa za kati chini ya Karume kilitaka agenda ya uhuru iahirishwe kwa muda (kauli yake ilikuwa “Uhuru Zuia”) kikihofia ZNP kuchukua nchi.

Karume na Muhsin walipatanishwa na Nkrumah mwenyewe pamoja na Msaidizi wake George Padmore. Wawili hao wakaonywa kuepuka kuwa “Vita vya panzi” enzi hizo za harakati za uhuru. Mapatano hayo, yaliyopewa jina “The Accra Accord” kwa lengo la kuimarisha Umoja wa Kitaifa, ulikuwa “Mwafaka” wa kwanza kwa Siasa za mpasuko Zanzibar, japo haukudumu, ambapo leo uhasama huu umerithiwa na “CCM Zanzibar” na “CUF Zanbar” kwa misingi ile ile ya kale.

Nkrumah alikuwa Mwasisi wa wazo la kuundwa kwa Shirikisho la nchi za Afrika, wazo lililozaa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU, sasa AU). Lengo lilikuwa ni kuona Afrika inajizatiti katika kujenga uchumi huru na imara; kujitegemea na kuunda Jeshi kubwa, imara kuweza kukabiliana na uvamizi kutoka nje na ambalo lingetumika pia kwa harakati za ukombozi wa Afrika.

Ni kwa njia ipi na muundo upi Shirikisho la Afrika lingefikiwa, Nkrumah na Nyerere, majabali wawili wa Siasa za Afrika enzi hizo, walitofautiana. Wakati Nkrumah alitaka Afrika iungane mara moja bila kuchelewa kabla viongozi hawajaanza kunogewa na kulewa madaraka, Nyerere alitaka Muungano wa Afrika uanze kwa awamu na kikanda, kwa nchi chache kuungana kabla ya kufikia Muungano wa Afrika nzima.

Kwenye Mkutano wa Pili wa OAU mjini Cairo, Julai 1964, Nyerere na Nkrumah walishambuliana kwa maneno na ukinzani wa hoja nusura washikane mashati juu ya hilo, ugomvi uliopewa jina “The Great Encounter” (Pambano Kuu) ambapo hoja ya Nyerere ilishinda.

Afrika na Dunia nzima bado inajiuliza, ni yupi kati ya wawili hao alikuwa sahihi juu ya kufikia Shirikisho/Umoja wa Afrika, hasa tunaposhudia kwamba hadi leo, Afrika imeshindwa kuungana, huku miungano/jumuiya za Kikanda zikiibuka na kuvunjika haraka na kirahisi? Ni nani huyu, Mwanaharakati Kwame Nkrumah, mwenye kustahili kuitwa “Baba wa Uhuru” barani Afrika; jabali la siasa aliyeweza kusuguana mabega na Mwalimu Nyerere?

Chama cha kwanza cha kiharakati nchini Ghana kilianzishwa mwaka 1947, kikiitwa “The United Gold Coast Convention” (UGCC) chini ya Dakta Joseph Danquah, kilichoanza na hoja ya kubadili jina la nchi kutoka “Gold Coast” kuwa “Ghana” kabla hata ya uhuru. Kilimwajiri Dakta Nkrumah kama Katibu Mkuu ili kukipa nguvu, kwa kumwita kutoka Marekani na Uingereza alikoishi kwa miaka 12 na kujipatia shahada za juu katika uchumi, Sosholojia na falsafa.

Akiwa ng’ambo, Nkrumah alijikita katika kuwaunganisha watu weusi ugenini wajitambue na watambue haki zao na kusaidia uhuru wa Afrika. Ni Nkrumah na Weusi wengine wa nchi za Kikarebia, aliyeitisha Mkutano mkuu wa Kwanza wa watu Weusi duniani (Pan-Africanism Conference) mjini Manchester, mwaka 1945 kuzungumzia Mshikamano wa mtu mweusi.

Mwaka 1949, Nkrumah na Danquah walifarakana; Nkrumah akajiengua UGCC na kuanzisha Chama cha siasa za mrengo wa Ki-Karl Marx (Kikomunisti) cha ”Convention People’s Party” (CPP). Mwaka 1951, alishitakiwa na kufungwa miezi sita kwa makosa ya “uchochezi”, akaendelea kupigania uhuru akiwa kifungoni.

Katika uchaguzi wa kwanza mwaka huo, ambapo aligombea akiwa jela, chama chake CPP, kilipata viti 34 kati ya viti 38 vya Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) na GCP cha Danquah kiliambulia viti vinne. Nkrumah mwenyewe katika Jimbo la Accra alipata kura 20,780 kati ya kura 23,122 zilizopigwa; mpinzani wake kutoka GCP alipata kura 2,342.

Habari za ushindi huo zilimfikia Nkrumah akiwa jela Februari 12, 1951; naye Gavana wa nchi hiyo, Aden Clarke, akalazimika kumtoa kifungoni siku hiyo na kumwomba aunde Serikali ya Mpito.
Julai 1953, huku akionesha dhahiri kupoteza subira, Nkrumah alishinikiza kuundwa kwa Serikali yenye madaraka kamili “bila kuchelewa”. Hata hivyo, ulizuka mtafaruku kati ya Nkrumah aliyetaka kujenga Taifa huru la kidemokrasia na la kisiasa, na Watawala wa kijadi (Machifu) waliotaka kubakia na madaraka yao ya wakati wa ukoloni; ghasia na machafuko yakazuka na nyumba ya Nkrumah ikashambuliwa kwa mabomu. Kwa kisingizio cha kutaka kupata matakwa sahihi ya wananchi, Serikali iliagiza ufanyike uchaguzi mwingine.

Licha ya ushindi mkubwa kwa mara ya pili kwenye uchaguzi wa mwaka 1954 kuelekea uhuru kamili, Serikali ya Uingereza ilikataa kutamka tarehe ya uhuru na badala yake ikatangaza uchaguzi mwingine kufanyika mwaka 1956. Katika uchaguzi huo, CCP kilipata kura 398,000 dhidi ya kura 299,000 za upinzani; na kwa viti vya LEGCO, kilipata viti 72 kati ya viti 104. Kwa matokeo hayo, Uingereza ikaridhia Ghana kupata uhuru Machi 6, 1957.

Mwandishi wa Kimarekani, John Gunther aliyekutana na Nkrumah siku ya uhuru anaelezea haiba ya kiongozi huyo katika Kitabu chake “Inside Africa”, ifuatavyo: “Mwendo, mwenendo na hisia (gesture) zake ni zenye mvuto, nguvu na utulivu wa kuhuisha; hana mikogo wala kauli tata za kutia chumvi”.
Nkrumah, akiwa bado kapera hadi Desemba 1957, maisha yake yalitawaliwa na siasa pekee kuliko vitu vingine; hakuwa mpenzi wa michezo, kinywaji, sigara wala starehe za aina yoyote.

Alikuwa mtu mpweke, mwenye fikra wa kuwaza na kuwazua nyakati zote na hakuamini wenzake na kwa nadra alitaka ushauri wao. Aliweza kuchanganyika na wanawake kwa urahisi lakini hakupenda kuhusiana nao kwa karibu, iwe kwa upendeleo maalum wa kivikundi au mmoja mmoja hivi kwamba kabla ya uhuru aliwahi kusema hakuwa na muda wa kuoa, hadi aliposhinikizwa na mfumo wa Serikali baada ya uhuru.

Bila kumjulisha mtu, lakini kwa shingo upande, na pengine kwa kushauriwa na aliyekuwa Rais wa Misri, Gamal Abdel Nasser; Nkrumah aliamua kuoa mke kutoka Misri; mwanamke ambaye hakuwahi kumsikia wala kukutana naye kabla ya hapo hadi siku alipoletwa Ghana siku ya kufunga ndoa, Desemba 30, 1957, iliyoshuhudiwa na watu wasiozidi 30.

Binti huyo wa Kimisri, Fathia Rizk, aliongea lugha ya Kiarabu pekee, na kidogo sana, Kifaransa kwa kubabia; wakati Nkrumah aliongea Kiingereza kufanya wanandoa hao kuhitaji wakalimani. Kwa nini Nkrumah alichagua ndoa baridi kama hiyo?

Erica Powell, mwanamama wa Kiingereza Msaidizi maalum wa Nkrumah, aliyeachiwa na Wakoloni kumsaidia kuweka sawa mambo ya utumishi na utawala (kama ambavyo tu Mwalimu Nyerere alivyopewa Mama Joan Wickens mwaka 1961) wakati wakiondoka, anamnukuu Nkrumah katika kitabu chake “Private Female Secretary in the Gold Coast”, akimwambia: “Erica, Je, wajua kwamba mimi ni mtu mpweke nisiye na rafiki wala makundi, na kwamba kwangu kilichomhimu ni Kazi tu?”

Aliwahi kumwambia (1965) pia kwamba, kitu ambacho angependa kufanya ni kujiuzulu Urais na kutumia muda wake wote kwa Umoja wa Afrika. Erica anakiri Nkrumah aliwahi kumtamkia pia kuwa, ikitokea kwamba ameoa, kwake suala la mke, watoto na mambo ya kifamilia kwa ujumla yasingekuwa masuala ya Kiserikali bali ya kibinafsi; akisema “ni hatari sana, na kwa kweli ni ubatili mtupu, kwa mke na familia kujiona kuwa sehemu ya utawala na Serikali”.

Nkrumah alimwambia Erica, ndoa haikumuondolea upweke, akasema: “Wajua Erica; sikutaka kuoa, wala sikuoa kwa kupenda ila kwa sababu ya Urais”. Erica hakuelewa, kwa nini mtu wa hadhi kubwa kama Nkrumah, mwenye elimu, akili na busara kubwa, aliamua kuoa msichana mdogo na ambaye hawakuelewana kwa kizuizi cha lugha. Hapa kulikuwa na mshabihiano uliofichika.

Ilitokea kwamba, Nkrumah alioa Misri si kwa bahati mbaya, kwa Rais mwanaharakati Kanali Nasser, mwenye siasa za mrengo wa Kikomunisti, aliyeingia madarakani kwa kupindua kijeshi Serikali ya Mfalme Farouk mwaka 1956. Nasser na Nkrumah, licha ya kuwa miongoni mwa waasisi wa OAU, walikuwa Waasisi pia wa Umoja wa Nchi zisizofungamana na upande wowote duniani (Non-aligned Movement – NAM), pamoja na Josef Bronz Tito (Yugoslavia) na Pandit Jawaharl Nethru (India). Wanne hao walikuwa pia wanamstari wa mbele wa kwanza na majabali dhidi ya ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo na ubeberu wa kimataifa.

Lakini pengine sababu kubwa zaidi kwa Nkrumah kumuoa binti huyo wa Kiarabu, ilikuwa ni kujaribu kuimarisha mshikamano wa Kiafrika (Pan-Africanism) kwa kujenga tafsiri mpya kwamba “Mwafrika” maana yake si “Mtu mweusi” pekee, bali ni “mzalendo yeyote mkazi wa Afrika mwenye mapenzi mema kwa Afrika”.

Mafanikio ya Nkrumah kisiasa hayakuwa bila mikwara kama anavyoelezea Genevova Marais, katika kitabu chake “Kwame Nkrumah As I knew Him” kwamba, “Kadri alivyopata mafanikio nchini, ndivyo alivyozidi kutowamini marafiki zake wa karibu, bila kujali jinsi walivyojitahidi kuonesha utii kwake. Kwa jinsi hii, alipoteza ushirikiano kiserikali na kubakia kuungwa mkono na Wana-CCP pekee, waliomwambia kile tu waliona angefurahi kusikia na kuacha mambo mengine yajiendee hovyo hivyo”. Kwanini?

Erica Powell anasema, tatizo la Nkrumah, na la madikteta wema wote (benevolent dictators) ni kwamba, “alikuwa hatabiriki; kwa haiba, aliweza kubadilika ghafla, akawa mkali kupindukia, asiyeambilika; lakini alikuwa mcheshi pia na mwenye kufikiria upya jambo akiona inafaa kufanya hivyo”.

Nkrumah alipinduliwa na Jeshi lake Februari 24, 1966 akiwa mjini Beijing, China akielekea Hanoi, Vietnam kama Kiongozi wa Kimataifa mwenye jukumu la kusuluhisha vita ya Vietnam, kati ya Vietnam na Marekani enzi hizo za vita baridi. Alirejea Afrika lakini si Ghana, bali kama mkimbizi uhamishoni nchini Guinea.

Mwalimu Nyerere alitaja sababu zenye ukakasi kidogo, juu ya kuangushwa kwa Nkrumah kuwa, “alifanya kosa kuruhusu rushwa na rushwa ikamlemea”. Je, ilikuwa rushwa pekee iliyomwondoa?
Kuanguka kwa Nkrumah hakukuja kwa sababu ya kukithiri kwa rushwa nchini Ghana, la hasha; wala si kwa sababu ya uongozi mbaya au kuharibika kwa uchumi. Nkrumah aliangushwa kwa kuthubutu kuchokoza ubeberu wa Kimataifa na kwa kutaka kuunganisha Afrika na nchi za dunia ya tatu kupambana na ubeberu huo.

Ndoto ya Nkrumah ya kuunda Shirikisho la Mataifa ya Afrika (United States of Africa) – “USA” mithili ya USA ya Marekani; kuunda ngome ya Kijeshi Afrika, mithili ya Umoja wa Kujihami Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) na kwa kujaribu kuinasua Afrika kutoka kwenye ushawishi wa Mataifa makubwa (Non-alignment) ilichangia pia.

Dalili zilijionesha mapema. Kuchapisha kwake kitabu, “Neo-Colonialism: The Highest stage of Imperialism” (Ukoloni Mamboleo: Hatua ya Juu kabisa ya Ubeberu) Oktoba 1965 kushambulia Ubeberu, kuliitia kichaa Marekani na kufuta msaada wa dola milioni 35 kwa Ghana. Miezi minne baadaye, akapinduliwa kwa msaada wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA).

Kanali A.A Afrifa aliyeongoza mapinduzi hayo, alielezea sababu hizo miezi mitano baadaye, katika kitabu chake “The Ghana Coup”, kuwa ni “ndoto za Nkrumah juu ya Pan-Africanism na Muungano wa Afrika; kuunga mkono ukombozi wa kitaifa nchini Kongo na kwingineko, na chuki bila sababu dhidi ya nchi rafiki zetu za Kimagharibi”.

Ni ukweli usiopingika, wala si uzushi, kwamba kupinduliwa kwa Nkrumah ulikuwa ushindi kwa ubeberu wa Kimataifa na ukoloni mamboleo Afrika. Kuanzia hapo, msukumo wa Afrika kuungana umetoweka, udikteta na uporaji wa rasimali za Afrika umetia fora; Afrika inazidi kudhoofika katika nyanja zote kuliko mwanzo; haina jeshi la pamoja la kujilinda wala kutetea uhuru wake ila kwa “msaada” kutoka nje. Afrika iko njia panda.
 
kimsingi nkurumah ndiye aliye mtia hofu nanihii asikubali kuundwa kwa umoja wa afrika kwani ilionekana yy nkurumah alistahili zaidi uongozi wa afrika ikiwa moja kuliko nanihii.
 
kwenye kikao kimoja huko kairo osagyefo alitukanana na nanihii kila mmoja akidai mwenzake katumwa na mabeberu kukwamisha mipango ya waafrika
 
mwisho wa siku, hata ww utaelewa tu, ninaamini mazingira hubadilika unacho kitegemea leo kesho hakipo.
Hata kama ulikuwa hujazaliwa enzi hizo, jaribu kujisomea historia ya Africa uifahamu vizuri. Achana na stori za vijiweni, umenisikia?
 
Hata kama ulikuwa hujazaliwa enzi hizo, jaribu kujisomea historia ya Africa uifahamu vizuri. Achana na stori za vijiweni, umenisikia?
suala la kuzaliwa toka lini likawa la muhimu kujua historia,tatizo ni waandishi wa historia wanaotanguliza njaa zao kama ww kupindisha ukweli kwani ukiwaambia watu kuwa kwenye hili suala hawa watu walipingana kunashida gani? mgonjwa kulikuwa na makundi mawili la freetown na monrovia kila kundi lilikuwa na kiongozi ingwa hawakuchaguliwa rasmi lkn waliyaongoza makundi haya kwa kujenga hoja kutetea maoni yao.
 
Back
Top Bottom