Kumbukizi ya Mapinduzi Yaliyofanyika Februari 24, 1966 Ili Kumng'oa Madarakani Rais Kwame Nkrumah wa Ghana

Jumanne Mwita

JF-Expert Member
Nov 18, 2014
424
1,044
"Ndugu Rais ninazo habari mbaya. Kumekuwa na Mapinduzi nchini Ghana."

"Unasema nini? Nkrumah aliuliza.
" Mapinduzi nchini Ghana. " akarudia balozi wa kichina.

Nkrumah alikuwa Peking .Hiyo ilikuwa tar 4 Februari, 1966, aliondoka Accra tar 21 Februari akiwa njiani kuelekea Hanoi mji mkuu wa Vietnam ,alikokaribishwa na Ho Chi Minh ambaye wakati huo alikuwa Rais wa Vietnam, wakati huo watu wa Vietnam walikuwa katikati ya vita vya ukombozi wakipambana na majeshi ya Marekani.

Nkrumah alikuwa na mapendekezo ya kumaliza vita hiyo, alikuwa mbali sana katika safari yake, mahali ambapo si rahisi kurudi Ghana kwa haraka. Balozi wa China aliendelea kumweleza Nkrumah mambo yaliyotokea kwa kadri ya habari zilivyowafikia toka Accra. Mnamo saa12 alfajiri ,alisema ,Afisa wa jeshi aitwaye Kotoka alitangaza katika redio ya Ghana kwamba jeshi na polisi vilikuwa vimechukua madaraka ya Serikali ya Ghana.

Mapinduzi hayo yalianza Usiku wa jumatano tarehe 23 Februari, 1966 wakati askari wapatao 600 waliokuwa na kambi yao Kumasi walipopewa amri kwenda Accra. Njiani walikutana na maafisa wawili, Afrifa na Kotoka. Afrifa alibakia akiongoza kikosi hicho na kotoka akarudi Accra kumweleza Harley ,kamishna wa Polisi juu ya mambo yalivyoendelea.

Wanajeshi waliambiwa kwamba Nkrumah alitaka kuwapeleka Vietnam kupigana vita na pia kwenda kupigana na walowezi wa Rhodesia , walisema ,ameondoka Ghana akiwa amechukua paundi milioni nane na hatarudi tena. Kwa hiyo ilikuwa ni wajibu wa jeshi sasa kuchukua madaraka ya Serikali ili kulinda usalama wa nchi na kuzuia uzorotaji wa uchumi.

Kotoka na askari 25 walikwenda haraka nyumbani kwa Mkuu wa majeshi Meja Jenerali Barwah. Barwah alikataa kuwaunga mkono na pia alikataa kusalim amri. Kotoka akampiga risasi ya kichwa tena kwa kumuua mbele ya mkewe na watoto wake. Askari saba pia waliokuwa zamu nao pia wakapigwa risasi na kuuawa.

Wakati Kotoka na askari wake wako kwa Barwah, askari na Polisi wengine waasi walikuwa wanawatia ndani viongozi maarufu wa Serikali na kukamata kiwanja cha ndege ,ofisi ya simu za nje ,kituo cha redio na barabara zote zinazoingia Accra. Wakati huo huo kikosi cha askari wa Accra kiliamriwa kuivamia Flagstaff House (Ikulu).

Hii haikuwa kazi rahisi kwasababu nyumba hiyo ya Rais Ilikuwa inalindwa na askari waaminifu wa kikosi cha ulinzi cha Rais. Askari hawa ingawa walizidiwa kwa wingi walipigana na askari waasi kishujaa, kwa muda hivi ilionekana kana kwamba wangeshinda, ukuta wa nje wa flagstaff House ulibomolewa lakini bado wakaendelea kupigana Hatimaye baada ya masaa kadhaa, askari watii ilibidi wakubali kushindwa. Wengi waliuawa na wengine walipigwa na kuchukuliwa mateka.

Askari waasi waliingia kila Chumba wakivunja madirisha na mapambo ya nyumba na kuharibu kumbukumbu za Serikali. Waliwasha Mwenge wa vitabu na makaratasi ya thamani kutoka ofisi ya Nkrumah, na kumwibia nguo na vitu vingine nyumbani mwake.
Mkewe na watoto wake watatu wadogo hawakudhurika, lakini walilazimishwa kuondoka Flagstaff house bila ya kuchukua kitu chochote kutoka humo ndani. Mama yake Nyaniba ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka themanini na karibu kipofu. Naye akalazimishwa kuondoka Flagstaff house ,aliambiwa kwa ujeuri arudi Kwenye kijiji chao cha Nkroful.

Baadaye waasi walijaribu kumshawishi aseme kuwa Nkrumah hakuwa mwanae alikataa kusema uongo wa aina hiyo na kwa ushupavu alisema ataendelea kuishi mpaka mwanawe karudi Ghana.

Katika siku zilizofuata za Mapinduzi, Mawaziri wa CPP, viongozi wa chama na wanachama wapenzi wa Serikali ya CCP katika Ghana nzima walikamatwa na kutiwa nguvuni ,wengi waliteswa , wale waliopindua Serikali ya Ghana tarehe 24 Februari, 1966 walitangaza kwamba "hakukuwa na umwagaji damu" katika Mapinduzi hayo.
Ukweli ni kwamba kulikuwa na umwagaji damu ingawa haikujulikana kwa dhati ni watu wangapi walikufa au kujeruhiwa.

Huko Peking ,Nkrumah mara moja akavunja safari yake ya kwenda Hanoi na kuamrisha maafisa na askari wa Ghana warudi makambini kwao, katika tamshi lililotangazwa kwa waandishi wa magazeti Nkrumah alisema; 'Kufuatana na Katiba ya Ghana mimi ndiye Rais wa jamhuri ya Ghana na Mkuu wa majeshi. Narejea Ghana karibuni' Baadaye akapeleka simu ifuatayo kwa ofisi zote za ubalozi wa Ghana.

"Tulieni mkibaki makazini mwenu, Tumeni ujumbe wenu wote na taarifa zenu kwangu kupitia ofisi ya ubalozi wa Ghana mjini Peking na sio,Accra, mpaka hapo mtakapoamriwa vingine baadaye."

Lakini kila alivyozungumzia Mapinduzi hayo na viongozi wa Chama aliokuwa nao, Nkrumah alikatishwa tamaa kuona kwamba wengi waliogopa . kitu ambacho waliweza kufikiri ni ubinafsi wao, familia zao na mali zao, Lakini fikra za askari wa ulinzi 66 na maafisa wa ofisi yake zilikuwa tofauti, hawakuyakubali Mapinduzi hayo au uhaini waliofanyiwa wananchi wa Ghana, wao kama Nkrumah, walikuwa tayari kupambana na waasi

Wachina wakafanya mpango kwa Nkrumah kuondoka Peking kwa haraka iwezekanavyo ,Wakati huohuo alimaliza shughuli zake kama ilivyopangwa . Serikali ya China ilikuwa na imani kwamba Mapinduzi ya Ghana yalikuwa ni hitilafu ya muda tu. " wewe ni kijana " Waziri mkuu wa China, Chou En-Lai ,Alimwambia ' una miaka mingine arobaini mbele yako ".

Salaam za kuungwa mkono zilimiminika kwa Nkrumah kutoka pande zote za dunia . kati ya viongozi waliomuunga mkono Nkrumah wakati huo walikuwa ni pamoja na Sekou Toure wa Ghana, Gamel Abdul Naser wa Misri, Julius Nyerere wa Tanzania ,Milton Obote wa Uganda, Modibo Keita wa Mali, na Waziri Mkuu wa Sierra Leone, Albert Margai.

Katika ujumbe wake Rais Sekou Toure alisema kwamba ilikuwa muhimu kushambulia bila kuchelewa. alimkaribisha Nkrumah arudi haraka Guinea.

'Tunasubiri kwa hamu"
Nkrumah akaamua kukubali mwaliko wa Sekou Toure na wananchi wa Guinea, wachilia mbali kwamba Ghana na Guinea ziliungana mwaka 1958 ,Nkrumah alitaka kwenda kwenye nchi iliyo karibu na Ghana . katika barua yake ya tarehe 25, Februari, 1966.
Nkrumah alimwandikia Sekou Toure akisema;

'Ndugu mpenzi na Rais,

' Nimefurahi sana kupokea hii leo waraka wako ulioonyesha umoja na ushirikiano . Ni kweli ,kama usemavyo ,kwamba tukio hilo la Ghana ni njama za mabeberu ,ukoloni mamboleo na vibaraka wao katika Afrika. Na kwa kadiri ya ubeberu huu unavyozidi kukua .....wakitumia wahaini wanaohujumu lengo la Afrika kwa kupinga Uhuru wa ndugu zetu. Ni lazima tuongeze juhudi na kupigania kwa dhati utu wa watu wetu mpaka mtu wa mwisho kwasababu ya Umoja wa Afrika . inatia moyo kujua kwamba katika mapambano haya tumeweza kutegemea msaada na uelewano kwa viongozi wa Afrika, kama ulivyo.

" Najua kwamba lengo letu litafanikiwa na kwamba Iko siku Afrika itaungana kuwa huru bila kuingiliwa na mataifa ya nje .....
Niko Peking nikiwa Salama na mwenye afya nzuri, nami nimetuma mjumbe wangu akukabidhi salamu hizi kukujulisha mipango yangu ya kurudi Afrika haraka.
" Tutaonana Guinea hivi karibuni.

" Wako ndugu mpenzi.,

" Kwame Nkrumah "

Serikali ya kirusi ilipeleka ndege peking kumchukua Nkrumah na msafara wake na tarehe 28 Februari wakaondoa China, Hatua ya kwanza iliwafikisha Irkutsk, Siberia, Baadaye wakaruka hadi Moscow walikofika alfajiri tarehe 1 Machi . Kule wakapokelewa na viongozi wa kirusi. Siku nzima ilitumika kuzungumzia mipango ya baadaye na kuendelea hadi usiku wa manane wakati ndege ilipoondoka kwa safari ya kuelekea Guinea . Baada ya kusimama kwa muda mfupi kule Yugoslavia na Algeria ndege yao iliwasili Conakry. Ilikuwa mchana wa tarehe 2 Machi 1996.

Sekou Toure na kundi la watu wengi walijaa uwanjani kumkaribisha Nkrumah. Mara tu alipoteremka kwenye ndege mizinga 21 ikapigwa ,ishara ya kupokewa kwa Kiongozi wa nchi . Hiyo Ilikuwa ishara ya watu wa Guinea kumjulisha Nkrumah afahamu kwamba wao hawakuyatambua Mapinduzi hayo na kwamba Nkrumah bado ndiye Rais wa Ghana.

Siku iliyofuata uliitishwa Mkutano wa hadhara Kwenye uwanja wa Conakry ,Sekou Toure na Nkrumah Walizungushwa hapo uwanjani katika gari la wazi . watu walipiga makofi na kuwapungia vibendera na wakisema : " Nkrumah aendelee kuishi', ' Sekou Toure aendelee kuishi", na " ukoloni mamboleo utokomee".

Nkrumah alifurahi kuwako Guinea . Alijiona yuko nyumbani kwa vile alikuwa katika ardhi ya Afrika . lakini hakujitayarisha kusikia hotuba ya Sekou Toure siku hiyo. Kwani Sekou Toure aliwaambia watu kwamba Serikali na wananchi wa Guinea wameamua kumteua Nkrumah kuwa Mkuu wa nchi ya Guinea.

" Wahaini wa Ghana " alisema ," wamekosea kufikiria kwamba Nkrumah ni mwananchi wa Ghana tu"

Aliwaambia kwamba Nkrumah ni wa Afrika nzima ,na kwamba yeye Sekou Toure ,ataona fahari kufanya kazi chini yake, Sekou Toure alisema kwa lugha ya kifaransa ,na wakati ule Nkrumah hakujua vizuri lugha ya kifaransa ,na wakati ule Nkrumah hakujua vizuri lugha hiyo . Alijua Kutokana na shamra shamra na mayowe ya watu kwamba ametambulishwa kwao na kwamba tamko la maana limetolewa. Lakini haikuwa mpaka baadaye ndipo alipotambua Sekou Toure alikuwa amesema nini.

Nkrumah Alishangazwa sana, haijatokea kwa kiongozi wa nchi kuwahi kutangaza kwamba yuko tayari kumpisha utawala Kiongozi wa nchi nyingine. Hii iliutambulisha ulimwengu mzima kuwa ni nini wananchi wa Guinea walivyomfikiria Nkrumah ,na yote yale aliyoyafanya kwa ukombozi wa umoja wa Afrika . na kama Nkrumah alivyosema " hii ni hatua kubwa ya kuonyesha kwa vitendo lengo la Umoja wa Afrika ".

Nkrumah alimshukuru Sekou Toure na wananchi wa Guinea kwa kumkaribisha na kumuunga mkono . Lakini ,alisema ,angeweza tu kukubali kuwa Rais sawa na Sekou Toure . kwa hiyo ,alikubali wote wawe marais sawa wa Guinea.

Katika muda wa miaka sita iliyofuata Nkrumah aliishi katika nyumba inayoelekea baharini ,iitwayo Villa Syli ,umbali wa maili moja kutoka katikati ya mji wa Conakry . kwa mbali upande wa Mashariki aliweza kuona Vilima vya Sierra Leone na upande wa mwingine aliona pwani ya Guinea Bissau. Wakati ule Guinea Bissau, ilikuwa bado ingali ni koloni la Wareno ,na vita vya ukombozi wao waliongozwa na Amilcar Cabral.

Cabral na wapigania Uhuru wengine kutoka sehemu zote za Afrika mara nyingi walimtembelea Nkrumah mjini Conakry. Walitumia masaa mengi kujadili sio tu matatizo yao binafsi , lakini masuala mengi yanayohusu ukombozi na umoja wa Afrika na mbinu za kukomesha aina zote za ukandamizaji .

Inasemekana kwamba wapigania Uhuru wengi zaidi walipitia Villa Syli kuliko walivyo Pitia Flagstaff House wakati Nkrumah Alipokuwa Ghana, baada ya wiki chache za kuwasili kwake Guinea ,Nkrumah aliweka ofisi na stesheni ya redio katika nyumba ya villa Syli, ili aweze kujua jinsi mambo yalivyokwenda huko Ghana na ulimwenguni kote, Kwa muda alikuwa akiwatangazia watu wa Ghana mara kwa mara .

" Maasi yaliyofanywa Ghana na baadhi ya maafisa wa jeshi na polisi hayakuwainua wananchi wa Ghana tu lakini pia Mapinduzi ya Afrika na umoja wa Uhuru wa bara letu " Alisema.
"Simameni imara mjitayarishe".

Wale wananchi 79 wa Ghana waliofuatana naye mpaka Guinea na wengine waliomfuata baadaye ,kila mmoja alipewa kazi ya kufanya . wale waliokuwa na ujuzi wa Polisi au jeshi walisaidiana na majeshi ya Guinea kutoa ulinzi wa Villa syli wale waliokuwa na ujuzi wa ukarani au uandishi walipewa kazi katika ofisi ya Nkrumah. Hakuna hata mmoja aliyekaa bila kazi . wote iliwabidi wahudhurie mafunzo ya kijeshi na kushirikiana katika majadiliano ya kisiasa. Nkrumah alitaka kila mmoja awe tayari katika pambano litakalofuata . kwani, alinuia kurudi Ghana kuendelea na kazi ya ukombozi na Umoja wa Afrika.

Alijifunza mbinu za upiganaji dhidi ya uasi ,na kushirikiana katika vikosi vya majeshi ya Guinea . Punde akawa mwenye shabaha mzuri sana. Alijifunza kuendesha gari Pamoja na masomo ya lugha ya kifaransa. Lakini muda wake mkubwa ulitumika kwenye kuandika vitabu. Wakati Mapinduzi yakitokea Ghana, vitabu vyake saba vilikuwa vimekwisha chapwa . alipokuwa Conakry aliandika vitabu sita zaidi. Kwanza alimaliza kuandika " challenges of Congo " kitabu ambacho kilionyesha jinsi mataifa ya kigeni yalivyoingilia katika utawala wa Kongo hata kusababisha kifo cha Patrice Lumumba na kuitisha Afrika yote huru . halafu akaandika " Handbook of Revolutionary Warfare" kitabu ambacho ni mwongozo kwa wapigania Uhuru wa Afrika. Mwaka huohuo ,Toleo la wapigania Uhuru la " Axioms" lilichapishwa hiki kilikuwa ni kitabu kidogo cha mfukoni kilichojaa sehemu muhimu za hotuba na maandishi yake.

Kikafuata "Dark Days in Ghana" kitabu kilichoeleza Mapinduzi ya Ghana ya mwaka 1966, Nkrumah alijadili sababu zilizoleta mapinduzi ,matokeo yake kwa Ghana ,na jinsi yalivyoingilia mapambano ya wagombea Uhuru katika sehemu nyingine za Afrika .

Alieleza maendeleo yaliyopatikana toka Ghana ipate Uhuru na jinsi mipango ya maendeleo iliyoanza kutoa matunda . wale waliopindua Serikali walisema " uongo mkubwa" waliosema kwamba Ghana ilibidi iokolewe kutokana na kuharibika kwa uchumi wake. Ni kweli kwamba kulikuwa na matatizo mengi ambayo yalikuwa bado kutatuliwa . Bei ya kakau ilianguka Vibaya sana. Kulikuwa na upungufu wa vitu vingine ,na kupunguza starehe za ubinafsi ili mipango ya ujamaa iweze kuendelea .

Haya na matatizo mengine yanazipata nchi nyingi ambazo zinataka kuendelea haraka na matatizo mengine .yanazipata nchi nyingi ambazo zinataka kuendelea haraka baada ya kutawaliwa na Wakoloni kwa muda mrefu . " Nimeandika , Nkrumah akasema ,kuhusu siku mbaya za Ghana " nikitumaini kwamba ukweli huo utasaidia kuficha mbinu za aina hii katika nchi huru za Afrika zinazoleta maendeleo

Miaka miwili baadaye ,Kukaja kitabu cha " Class struggle in Africa" kitabu kidogo cha maana Sana ambacho kimetolewa kwa niaba ya "Wakulima na wafanyakazi wa Afrika " Kitabu hiki kimeandikwa baada ya kutokea Mapinduzi kadhaa ya kijeshi katika Afrika. Mapinduzi ishirini na tano yalitokea kati ya januari 1963 na Desemba 1969 .Katika kitabu hiki Nkrumah akionyesha jinsi kilichokuwa na uhusiano mkubwa kati ya ukoloni mamboleo na waafrika waliopinga siasa ya ujamaa.

" jinsi uasi unavyoendelea kutumiwa kuwapinga waafrika " aliandika " Chama hakiwezi kufikia malengo yake bila ya kutumia mbinu zote za mapambano ya kisiasa ,pamoja na pambano la Mtutu wa bunduki " wakati anaandika vitabu hivi, Nkrumah pia alikuwa anajitayarisha kuandika vitabu vingine viwili ,kimoja juu ya Zimbabwe na kingine kingeitwa " Revolutionary Path" Hakupata nafasi ya kuvimaliza navyo vilipigwa chapa baada ya kufa kwake.

Vitabu alivyoandika Nkrumah na hotuba alizotoa kwa njia ya redio vilisaidia wananchi wa Ghana kupinga utawala wa kijeshi na Polisi ambao walichukua madaraka kwa nguvu baada ya Mapinduzi .
Serikali hii iliyojiita " National Liberation council " ( NLC) ilijaribu kuwazuia watu wasisikilize matangazo yake ya redio na redio nyingi zilikamatwa na Polisi . Lakini watu walisikiliza kwa siri na kupitisha maagizo ya Nkrumah.

Punde ,majaribio mengi yalifanywa kumkamata au kumuua Nkrumah. Usiku mmoja ,ilipokuwa giza nene, manowari ya ulinzi ya Guinea iligundua meli moja ya uvuvi karibu sana na Pwani ya villa Syli . Waliisimamisha na kuwakamata wale waliokuwemo ndani , Walionekana kwamba ni wahalifu walioachiwa kwa makusudi kutoka jela za Ghana na kutumwa wamkamate Nkrumah. Walikuwa wamrudishe Ghana ,akiwa hai au amekufa.

Lakini kila walivyo jaribu NLC hakuweza kumnyamazisha Nkrumah. Sauti yake kutoka Conakry iliendelea kusikia
" wafanyakazi na wakulima popote mlipo katika Ghana jitayarisheni kuanzia hivi sasa . Ni lazima muikomboe nchi yenu tena kama mlivyofanya wakati wa ukoloni wa mwingereza . shabaha yenu ni ya kihistoria, ni ujenzi wa Umoja katika Ghana na katika Afrika ya ujamaa, Wafanyakazi na wakulima wa Ghana msikate tamaa au kuogopa wakati ujao .Anzeni sasa. Mapambano yanaendelea.

Pichani chini ni Marais washiriki wa Guinea, Kwame Nkrumah na Sekou Toure wakisherehekea Sikukuu ya Mei Mosi pamoja na Umma wa Guinea katika uwanja wa Michezo wa Conakry tarehe 1 Mei mwaka 1967.
 
Nimepata elimu, sikujua kabisa huo mtanange! Muendelezo please!!
 
ebana eeh ikawaje muendelezo tafadhali kuna watu wamezifia nchi zao wameifia Africa msomwe milele vizazi hadi vizazi tusome ushujaa wenu
 
Back
Top Bottom